Imani Yetu (We Believe)

IMANI YETU

Tunaamini kwamba Biblia ni neno la Mungu na kwamba “kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki” (2 Timotheo 3:16)

Tunaamini kwamba Yesu Kristo ni Mungu. Pamoja na kwamba Yeye ni Mungu, alijinyenyekeza, akaacha utukufu, akazaliwa kama mwanadamu, akafa kifo cha aibu – msalabani, ili atupatanishe na Mungu. “Alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; 8 tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba. 9 Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; 10 ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; 11 na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO ni BWANA, kwa utukufu wa MUNGU BABA.” (Wafilipi 2:7-11)

Tunaamini kwamba “mshahara wa dhambi ni mauti” (mauti ya pili); lakini Bwana asifiwe, kwa sababu ya Msalaba, Yesu Kristo amekuwa Mbadala wetu, na ametupatia uzima: “bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu.” (Warumi 6:23).

Tunaamini kwamba “tumeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zetu,” bali “ni kipawa cha Mungu; wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu” (Waefeso 2:8-9).

Tunaamini kwamba Amri Kumi za Mungu hazijabadilika, ziko palepale (Kutoka 20:3-17). Tunampenda Yesu kwa sababu Yeye alitupenda kwanza. Kwa sababu ya upendo huu mkuu, tunapaswa kumpenda na kumtii, hii inamaanisha kutii Amri Zake zote, ikiwemo amri ya Nne (Sabato); “Mkinipenda, mtazishika amri Zangu” (Yohana 14:15). Japo hatuokolewi kwa matendo yetu; tunapaswa kukumbuka pia kwamba: “Imani pasipo matendo imekufa” (Yakobo 2:26). Kwa kuwa tunampenda Yesu, tutaendelea kufanya uamuzi wa busara, kwa kutii Amri Zake, kila wakati, kutubu na kuachana na dhambi, na kumchagua Yewe daima.

Tunaamini kwamba ni jukumu letu kushiriki mwito mtakatifu wa Yesu Kristo, katika mchakato wa Injili kote ulimwenguni. “19 Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; 20 na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, Mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.” (Mathayo 28:19-20)

Tunaamini kwamba Unabii unaonyesha dhahiri kwamba Kristo yu mlangoni (Mathayo 24:32-51); hivyo twapaswa kujiweka tayari siku zote, katika “sala zote na maombi, tukisali kila wakati katika Roho” (Waefeso 6:8); tukikesha na kuomba kwa kadiri tuonavyo Siku ile kuwa inakaribia” (Waebrania 10:25)


 

Sauti Ya Injili SDA © 2017