Marko 6: Mwongozo wa Biblia

Wazo la Alfajiri/ Dhima: Yesu Kristo—alidharauliwa, alikataliwa/ Andiko Makini: Marko 6:1-6.

Marko 6:4–64 Yesu akawaambia, Nabii hakosi heshima, isipokuwa katika nchi yake mwenyewe, na kwa jamaa zake, na nyumbani mwake. 5 Wala hakuweza kufanya mwujiza wo wote huko, isipokuwa aliweka mikono yake juu ya wagonjwa wachache, akawaponya. 6 Akastaajabu kwa sababu ya kutokuamini kwao. Akazunguka-zunguka katika vile vijiji, akifundisha.

Utangulizi: Je, umewahi kudharauliwa, kukejeliwa, kushtakiwa, kukataliwa? Wakosoaji wakubwa wa maisha ya mwanadamu na kazi (au wito) wake ni wale walio karibu naye (yaani ndugu), wale ambao wamemfahamu siku zote. Yesu alipitia uzoefu kama huu (Mk 6:3). Katika sura hii, Yesu anaondoka Kapernaumu na kurudi kijijini Kwake, Nazareti. Utakumbuka kuwa Nazareti ilikuwa ni kama nyumbani hasa, kwa sababu alilelewa na kukuwa hapo kama mtoto/ kijana. Cha kushangaza ni kwamba watu wa kwao hawakumtambua kama Masihi: hawakukusanyika na kuja Kwake kama ilivyokuwa katika sehemu nyingine. Hakuna dalili kuwa alipata fursa ya kufundisha au kuwahubiria hadi siku ya Sabato, alipokwenda katika Sinagogi “kama ilivyokuwa desturi Yake” (Lk 4:16).

Hapa kuna maelezo ya jumla ya mistari sita ya kwanza katika Injili ya Marko 6 — Yesu alikuwa katika mji Wake, Nazareti (mstari wa 1-2); Wengine walianza kuhoji chanzo cha mamlaka Yake (mstari wa 2–3); Wengine walichukizwa Naye; Wengine walimchukulia tu kama mmoja wao (mstari wa 3-4); Wengine walizuia nguvu za Mungu (mstari wa 5); Wengine hawakuamini ukuu/ uungu Wake kabisa (mstari wa 6).

Maana ya Kiibada: Yesu hakukataliwa tu- alidharauliwa. Unakumbuka kile kilichosemwa kuhusu Yeye, yapata miaka 700 kabla ya kuzaliwa Kwake? Maandiko yalitabiri hivi: Alidharauliwa na kukataliwa na watu; Mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko; Na kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao, Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu (Isaya 53:3). Ni kwa njia gani leo tunaweza kumdharau Mwana wa Mungu? Kwa kupitia matendo yetu (kutotii), au kutoamini kwetu. Mtume Paulo katika Waebrania 6:4-6 anazungumzia “kumkanyaga” Mwana wa Mungu. Unajua, watu hukanyaga kile wasichokiheshimu, kutokukubaliana, au kuchukia. Muumini (Mkristo) anakanyaga chini ya miguu Mwana wa Mungu pale anapoasi dhidi Yake, au kukataa mapenzi Yake. Nini kinaweza kuwa kibaya zaidi kuliko hicho? Wapendwa, Mungu atusaidie ili tukapate kuwa wana na mabinti wa Mungu (Yohana 1:12); tukapate kuwa Watoto watiifu wa Mungu. Na hili ndilo ombi langu, la dhati kabisa kwa ajili yako asubuhi ya leo, katika jina la Yesu Kristo, Amina.

Sauti ya Injili: “Kwa hiyo vifungeni viuno vya nia zenu, na kuwa na kiasi; mkiitumainia kwa utimilifu ile neema mtakayoletewa katika ufunuo wake Yesu Kristo. Kama watoto wa kutii msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu; bali kama Yeye aliyewaita alivyo Mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote.” (1 Peter 1:13–15)

Iweni na Siku Njema: “Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia. Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu hata milele.” (1 John 2:16–17)

 

41-BSG-6K: MASWALI YA KUJADILI.

Mwongozo wa Kujifunza Biblia/ Marko 6, (41-BSG-6K)/ Maswali ya Majadiliano

[1] Huyu si mwana wa seremala, “Mwana wa Mariamu?” Kishazi “Mwana wa Mariamu” kinalenga/ kinamaanisha nini? Kwa nini waulize swali kama hili? (6:3) Je, ni sahihi kumwita Yesu, Mwana wa Mariamu? Vipi kuhusu wale wanaomuinua Maria (mama wa Mungu) katika sala/ ibada zao, je, ni sahihi kufanya hivyo?

[2] Katikamaeneo ya Kwao, Nazareti, Yesu alikabiliana na umati ambao ulishangaa jinsi alivyokuwa na nguvu sana katika Neno na kazi Yake, lakini cha kushangaza ni kwamaba hawakutaka kumwamini! Kwa kweli, alidharauliwa na kukataliwa. Je, kutoamini kwetu kunapunguza (ondoa) kile ambacho Mungu angeweza kutufanyia? Jadili (6:5–6)

[3] Katika mstari wa 7-11, Yesu aliwatuma wanafunzi Wake kufanya mambo yale yote aliyoyafanya: kuhubiri, kuwaponya wagonjwa, na kutoa pepo wachafu. Kama wanafunzi wa Kristo leo, tunawezaje kuwa na mamlaka juu ya mapepo, majini, ushirikina, n.k? (6:7)

[4] Kwa nini Yesu anawatuma wanafunzi, wawili wawili? (6:7–11) Kwa nini anawaamuru wasichukue chochote? (6:8) Kwa nini kutikisa mavumbi kutoka miguuni mwao? (6:11)

[5] Katika mstari wa 13, Yesu anawaamuru “kupaka mafuta wengi waliokuwa wagonjwa, na kuwaponya.” Rejea nyingine ya kupaka mafuta kwa ajili ya uponyaji inapatikana  katika Yakobo 5:14-15. Upako wenye mafuta ni taswira ya nini katika Biblia? Je, mafuta haya yalikuwa dawa pia katika siku hizo? Je, mafuta yanatibuje magonjwa? Au ni Imani tu (6:13)

[6] Kwa nini Herode alipenda kumsikiliza Yohana Mbatizaji, wakati Yohana alikosoa mwenendo wake wa maisha? (6:20) Je, kweli kuwa kiongozi huyu angetoa nusu ya ufalme wake kwa binti yake? (6:23)

[7] Nini cha ajabu sana kuhusu muujiza wa kuwalisha wanaume 5,000 (pamoja na wanawake na watoto) kwa “mikate mitano na samaki wawili” tu? (6:32–44) Je ni kanuni ipi ya Maisha twapaswa kujifunza hapa?

[8] “Naye [Yesu] aliposhuka mashuani, akaona mkutano mkuu, akawahurumia; kwa sababu walikuwa kama kondoo wasio na mchungaji” (aya ya 34). Ina maana gani kuwa umati ule ulikuwa kama “kondoo bila mchungaji?”

[9] Kama Yesu ni Mungu, kwa nini alihitaji kuomba? Kwanini kwenda faragani mlimani ili aombe? (6:46) Je kuna cha kujifunza hapa? (Linganisha Waebrania 5:7-8)

[10] Kwa nini Yesu alitembea juu ya maji? (6:48) Yesu alipoingia chomboni walimo wanafunzi, “upepo ukakoma; wakashangaa sana mioyoni mwao!” Maandiko yanasema.. “lakini mioyo yao ilikuwa mizito” Kwa nini? (6:52)

41-BSG-6M: DHAMBI ZA KUUNGAMA.

Mwongozo wa Kujifunza Biblia/ Marko 6, (41-BSG-6M)/ Orodha ya Dhambi za Kuepukwa/ Kuungama

[1] Kumpinga Kristo. Kristo alipitia upinzani wa aina mbalimabi toka pande zote, kwa mfano: upinzani wa Umati (Yohana 12:34-36); Familia Yake (Yohana 7: 2-9), Kizazi Chake (Mt 11:16–19; Lk 19:7), Herode (Mt 2:16; 14:1–13; Mk 6:14–29), watu wa Kwao, waNazareti (Mt 13:53–58; Mk 6:4–6), viongozi wa kidini (Mt 12:14; Mk 3:6; Lk 6:11; Yn 11:47-53), viongozi wa kisiasa/ serikali (Mt 2:13-14; Lk 13:31), lakini zaidi ya yote, alipingwa na Shetani (Mk 8:31–33; 34–38).

[2] Kushindwa Kutubu – “Wakatoka, wakahubiri kwamba watu watubu” (Marko 6:12)

[3] Uzinzi – Kuchukua mke wa ndugu yako ni dhambi. Yohana alimwambia Herode, “Si halali kwako kuwa na mke wa nduguyo.” Herode alimchukua Herodia, mkewe Filipo ndugu yake, na kumuoa (Mk 6:17-18).

[4] Usiue – Herode alimuuwa Yohana Mbatizaji. Maisha ni ya thamani sana mbele za Muumba! Je unakumbuka Amri ya Sita? USIUE! (Kutoka 20:13). Amri hii inajumuisha mambo mengi sana, ambayo  sitayajaja hapa.

[5] Kushindwa kuwa na Huruma: Yesu “aliposhuka mashuani, akaona mkutano mkuu, akawahurumia; kwa sababu walikuwa kama kondoo wasio na mchungaji.” (Mk 6:34). Ni mara ngapi umefanya matendo ya Huruma kwa wahitaji? Labda niseme tu kwa kifupi kuwa hautaweza kwenda Mbinguni ukipuuzia agizo hili. Soma Mathayo 25:41-43.

[6] Kushindwa kutoa shukrani kwa Baba kwa utunzaji WAKE wa ruzuku – “Akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama mbinguni, akashukuru, akaimega ile mikate, akawapa wanafunzi Wake wawaandikie; na wale samaki wawili akawagawia wote.” (Mk 6:41). Baba Mungu alisikia ombi hili, akaridhia, ndipo muujiza huu [Samaki wawili] ukalisha umati wote. Jambo la pili, tunapaswa kushukuru na kuomba kabla ya kula ili BWANA atakase hicho tulacho! Kuna wengi sana wemeshawekewa hata sumu, lakini Bwana akawaokoa! Usipuuzie ombi hili.

[7] Kutupa/ au Kutohifadhi vipande vilivyobakia — “Wakaokota vipande vilivyomegwa vya kuweza kujaza vikapu kumi na viwili; na vipande vya samaki pia.” (Marko 6:43) Hapa kuna fundisho Fulani: Hakika mkusanyiko wa vipande hivi hutufundisha mambo kadhaa — [a] Usitupe kutu kilichosalia, maana siku nyingine kinawezasaidia sehemu fulani; [b] Baraka za Mungu hazipaswi kupotea hovyo; [c] Mioyo yenye shukrani hutumia kikamilifu baraka za Mungu!

[8] Hofu, Ugumu wa Moyo -Wakati wanafunzi wasioamini walipomwona Kristo akitembea juu ya maji, walifadhaika – “Mara akasema nao, akawaambia, Changamkeni; ni Mimi, msiogope.” Maandiko yanaendelea kusema… “lakini mioyo yao ilikuwa mizito” (Mk 6:50, 52b)

Maonyo ya Adhabu ya Dhambi:Roho itendayo dhambi, ndiyo itakayokufa; mwana hatauchukua uovu wa baba yake, wala baba hatauchukua uovu wa mwanawe, haki yake mwenye haki itakuwa juu yake, na uovu wake mwenye uovu utakuwa juu yake. Lakini mtu mbaya akighairi, na kuacha dhambi zake zote alizozitenda, na kuzishika amri zangu zote, na kutenda yaliyo halali na haki, hakika ataishi, hatakufa” (Ezekieli 18: 20-21).

Wito wa Mungu wa Toba ya Kweli: “Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake Bwana” (Matendo 3:19).

Hitimisho: Hebu Bwana atusaidie kuepuka, kukemea, na kutubu Dhambi zilizotajwa hapo juu – “Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu. Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote. Tukisema kwamba hatukutenda dhambi, twamfanya Yeye kuwa mwongo wala neno lake halimo mwetu.” (1 Yohana 1: 8-10)

Bwana akubariki unapotafakari Neno Lake, Amina.