Asili ya Upendo

Wazo la Usiku/ Asili Ya Upendo/ 133A-001, (1 Yohana 4:7-8)

Maneno ya Ufunguzi: Maandiko Matakatifu hutoa uelewa wa chanzo, tabia na thamani ya upendo, kulingana na asili na matendo ya Mungu. Mungu ndiye chanzo cha upendo. Pasipo Yeye, hakuna upendo. Tabia Yake ni upendo. 1Yohana 4:7-8; 1Th 3:12; 2Ti 1:7; 1 Yohana 4:16, 19

Mtume Yohana akiandika kuhusu mada hii nyeti anasema hivi: “Wapenzi, na mpendane; kwa kuwa pendo latoka kwa Mungu, na kila apendaye amezaliwa na Mungu, naye anamjua Mungu. Yeye asiyependa, hakumjua Mungu, kwa maana Mungu ni Upendo.” (1 Yohana 4:7-8)

“Yohana alirudia wito wake kwa Wakristo (marafiki zake wapendwa) kuendelea kupendana (ona pia 3:10-18, 23). Mungu ni Pendo (4:8). Yeye ndiye chanzo cha upendo wote; kwa hivyo, upendo unatoka kwa Mungu. Yesu Kristo, aliyetuma kutoka kwa Mungu Baba, alijivika upendo na kudhihirisha upendo huo katika maisha Yake hapa duniani. Kiasili upendo kama huo haupo kwa mwanadamu. Hatukuzaliwa nao, wala hatuwezi kujifunza [pasipo Yeye]. Waumini hupokea upendo wa Mungu kwa njia ya Roho Mtakatifu.” [Bruce B. Barton and Grant R. Osborne, 1, 2 & 3 John, Life Application Bible Commentary, (Wheaton, IL: Tyndale House, 1998), 90].

Wapendwa, yatupasa kuwa na shauku ya kujifunza maana halisi ya Upendo wa Mungu; kujifunza Tabia Yake ya Upendo; na kisha kuakisi tabia hiyo katika maisha yetu ya kila siku.

Hatua ya Maamuzi: Mapenzi ya Mungu ni nini kwangu? Pendaneni Ninyi kwa Ninyi! Sikiliza mwito wa Kristo: “Amri mpya nawapa, Mpendane. Kama vile Nilivyowapenda ninyi, Nanyi mpendane vivyo hivyo. Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi Wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi.” (Yohana 13:34-35).

Angalizo: Katika mwendelezo huu (kila siku usiku, kwa Neema ya Mungu) tutaangalia Mada zifuatazo: Asili ya upendo; Upendo wa Mungu; Upendo wa Yesu Kristo; Upendo & Roho Mtakatifu; Upendo kwa Mungu; Upendo kwa Watu Wengine; Upendo katika Mahusiano; Upendo na Ulimwengu; Upendo na Maadui; Dhana potofu kuhusu Upendo.

Usiku Mwema: “Sisi twapenda kwa maana Yeye alitupenda sisi kwanza.” (1 Yohana 4:19).