Uasi: Kuacha Imani

Ibada ya Alfajiri/ 81-GCR-A001, (Isaya 1:2-5)/ Dhambi ya Kuepuka & Kuungama: Mwongozo wa Ungamo na Toba.

Dhambi dhidi ya Mungu:

KUACHA IMANI BAADA YA KUIJUA KWELI.

Isaya 1:2-5 2 Sikieni, enyi mbingu, tega sikio, Ee nchi, kwa maana Bwana amenena; Nimewalisha watoto na kuwalea, nao wameniasi 3 Ng’ombe amjua bwana wake, Na punda ajua kibanda cha bwana wake; Bali Israeli hajui, watu wangu hawafikiri. 4 Ole wake, taifa lenye dhambi, watu wanaochukua mzigo wa uovu, wazao wa watenda mabaya, watoto wanaoharibu; wamemwacha Bwana, wamemdharau yeye aliye Mtakatifu wa Israeli, wamefarakana naye na kurudi nyuma. 5 Mbona mnataka kupigwa hata sasa, hata mkazidi kuasi? Kichwa chote ni kigonjwa, moyo wote umezimia.

Israeli (Yuda) walitelekeza imani yao baada ya kujua ukweli — (kumjua Yehova). Hapa kuna orodha ya sababu zilizofanya Yuda awe chini ya adhabu ya Mungu. Sababu hizi ndizo zilipelekea Yuda kuzungukwa na maadui wengi—Kwanza, walidharau heshima waliyopewa na Mungu kama taifa teule na kumuasi Mungu (1:2); walikosa busara, hekima na utambuzi (1:3); uchafuzi wa dhambi uliongezeka katika nchi (1:4a); waliachana na Yehova (1:4b); walimdharau Yeye aliye Mtakatifu wa Israeli (1:4c); walichagua njia ya uovu (1:4d); na walikusudiia kuendelea katika njia ya ovu (1:5).

Dhambi ya Uasi ni ya kwanza kabisa kati ya maneno matano muhimu yahusuyo dhambi katika sura hii (Isaya 1:2, 4, 13). Mungu aliwaonesha watu hawa fadhila maalumu. Alielezea rehema Zake katika kuwaleta kutoka utumwa wa Misri; na juu ya hili, alidai Utiifu na Upendo (Kutoka 20:1-3). Lakini badala yake alipata nini? Uasi! Israeli walimtelekeza BWANA Mungu, wakamuacha na kuasi sharia Zake.

Kijihoji Nafsi: Je, tumekuwa kama Yuda? Je tumekuwa taifa lenye dhambi, watu wanaochukua mzigo wa uovu, wazao wa watenda mabaya, watoto wanaoharibu? Je tumemwacha Bwana? Je tumemdharau Yeye aliye Mtakatifu wa Israeli? Je tumefarakana Naye na kurudi nyuma?

Dhambi za Kuepuka/Kuungama: Ukengeufu; kumsahau Bwana; Uasi dhidi ya Mungu: njia yake au neno lake; Kumkataa; Kushindwa au kukataa kuitikia upendo na miongozo Yake.

Hatua ya Mamuzi: Chukua muda wa kujichunguza mwenyewe: Je, umeona dhambi yoyote maalum iliyoorodheshwa hapa katika maisha yako? Kama ndiyo; Ungama na Kutubu mara moja. Kumbuka, “dhambi ambazo bado hazijatubiwa na kuachwa hazitasamehewa, na kufutwa kutoka kwenye vitabu vya kumbukumbu, lakini zitasimama kama ushahidi dhidi ya mdhambi katika siku ya Mungu [Siku ya Hukumu]” (The Faith I Live By, uk. 211). Chukua muda sasa kujiombea na ikiwezekana omba kwa ajili ya mtu mwingine ambaye bado hajapata ushindi dhidi ya dhambi hizi. Bwana Akubariki Sana!

Mwaliko: “Basi, kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, nami nitamkiri mbele za Baba yangu aliye mbinguni.” (Mathayo 10:32)

Uwe Na Siku Yenye Baraka: “Haya, njoni, tusemezane, asema Bwana. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu. Kama mkikubali na kutii mtakula mema ya nchi; bali kama mkikataa na kuasi mtaangamizwa kwa upanga; maana kinywa cha Bwana kimenena haya.” (Isaya 1:18-20)