Mhubiri 2: Mwongozo wa Biblia

21-BSG-2A: MWONGOZO WA IBADA

Mwongozo wa Ibada Unaoshabihiana na “Mpango wa Usomaji Biblia” wa leo: Mhubiri 2/ Dhima: Anasa na Usabilifu wa Kilimwengu/ 21-BSG-2A, (Mhubiri 2:1)/ Wimbo: “Earthly pleasures vainly call me; I would be like Jesus” (SDAH 311)

UCHUNGUZI: Anasa ya Kidunia na Ubatili wa Furaha ya Hawaa– (Mhu. 2:1, 10-11; Mit. 23:5; Yak. 4:14).

TAFAKARI: Ujumbe wa Mhubiri 2:1-3 ni rahisi sana: Anasa ya kidunia inashindwa kutosheleza kabisa moyo wa mwanadamu! Waovu hutafuta furaha katika anasa za kidunia—burudani, ngono, pombe, dawa za kulevya, michezo, sinema, michezo ya video, nk. Hitimisho la Sulemani lilikuwa hivi: yote ni ubatili. Vilithibitika kuwa havina maana—haviridhishi, havidumu, wala kukaa kwa muda. “Nilisema moyoni mwangu, ‘Njoo sasa, nitakujaribu kwa anasa; jifurahishe.’ Lakini tazama, haya nayo yalikuwa ubatili.” (Mhubiri 2:1, ESV). Sulemani alitafuta raha kupitia burudani na kicheko: haya pia yalikuwa upumbavu na hayakuridhisha; pia kupitia divai (pombe, dawa za kulevya) na kuendekeza hawaa: tena haya nayo yakawa upuuzi—mtindo wa maisha ya kijinga, ya mwili, ya upumbavu, ya yaliyopotezwa—haswa wakati wa kutafuta hekima (v. 2).

MAANA YA KIIBADA: Anasa ni ushawishi wenye nguvu sana! Watu wengi wameanguka kuifuata. Kwa bahati mbaya, hata miongoni mwa wachungaji—wale waliowakifishwa/tengwa kwa ajili ya kazi ya Mungu—baadhi wamesalimisha kila kitu cha thamani kwenye madhabahu ya anasa: uzinzi, pombe, dawa za kulevya, nk. Anasa ni ushawishi wenye sumu. Hakika ni tamu kuionja, lakini athari yake hufisha. Jihadharini nayo, ewe mhubiri! Jihadhari nayo, ewe mwamini! Jihadharini nayo enyi “masalia”—walinzi wa ukuta wa Sayuni. “Yafikirini yaliyo juu, siyo yaliyo katika nchi. Kwa maana mlikufa, na uhai wenu umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu.” (Wakolosai 3:2–3)

SAUTI YA INJILI: Sehemu hii imeandikwa kana kwamba Mungu anazungumza nawe moja kwa moja — kwa sababu anafanya hivyo. Je Bwana ananiambia nini asubuhi ya leo? Mwanangu, raha ya kweli hupatikana katika mambo ya Mungu: kwa kunijua na kunitii. Kaa mbali na anasa za Kidunia! Anasa za kidunia ni hatari: ni “anasa za dhambi kwa muda kitambo,” lakini mwisho, huleta mauti – “Iko njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu, Lakini mwisho wake ni njia za mauti.” (Mithali 14:12) Ninakualika ukae ndani Yangu, uzishike amri Zangu na Nitakidhi mahitaji ya roho yako (Zaburi 23:1-3; 16:11) na kukupa matamanio ya moyo wako (Zaburi 37:4).

SHAUKU YANGU: Kwa neema ya Mungu, ninataka kutafuta furaha na raha ya kweli inayopatikana tu kwa Bwana Yesu Kristo.

Uwe na Siku Yenye Baraka: “Utanijulisha njia ya uzima; Mbele za uso Wako ziko furaha tele; Na katika mkono Wako wa kuume Mna mema ya milele.” (Zaburi 16:11)

21-BSG-2B: MWONGOZO WA MAOMBI

Mwongozo wa Maombi Unaoshabihiana na “Mpango wa Usomaji Biblia” wa leo: Mhubiri 2/ Dhima: Anasa na Usabilifu wa Kilimwengu/ 21-BSG-2B, (Mhubiri 2:1)/ Wimbo: “Now, dear Lord, as we pray, Take our hearts and minds far away” (SDAH 671)

Shabaha: Usiruhusu anasa za kidunia, ufahirishi (materialism) na endekezaji anasa vikuvuruge kutoka kwa mambo ya Mungu.

Andiko Msingi: “Basi, jiangalieni, mioyo yenu isije ikalemewa na ulafi, na ulevi, na masumbufu ya maisha haya; siku ile ikawajia ghafula, kama mtego unasavyo.” (Luka 21:34)

Maelezo ya Ufunguzi: Mhubiri 2 huendeleza dhima ya Mhubiri 1. Sulemani akiombolezea ubatili na utaabishi wa maisha. Hakuna kinachoridhisha. “Ni maombolezo ya mtu asiye na Yesu Kristo. Ni maombolezo ya mtu ambaye huona tu maisha haya na siyo uzima wa milele.” (John G. Butler). “Yesu aliwaambia wafuasi Wake wawe waangalifu wasiruhusu majaribu au hofu za maisha haya kuwavuruga wasikeshe na kuwa tayari kwa ajili ya kurudi Kwake. (Angalia Luka 12: 13-31, 35-48; 17: 26-37 ambapo Yesu alionya dhidi ya ufahirishi na uendekezaji anasa.) Siku hiyo itakuja bila kutarajia, na itamjia kila mtu—hakuna ubaguzi. Hakutakuwa na nafasi ya toba ya dakika ya mwisho au kujadiliana. Chaguo ambalo kila mtu ameshafanya litaamua hatima yake ya milele.” [Bruce B. Barton, David Veerman, Linda Chaffee Taylor, and Grant R. Osborne, Luke, Life Application Bible Commentary, (Wheaton, IL: Tyndale House Publishers, 1997), 484].

Tunapokuja kwenye Kipindi cha Maombi cha leo, unaweza kumwomba Bwana akusaidie kushinda majaribu ya starehe za kidunia, ufahirishi na kuendekeza anasa? Badala yake, hivi unaweza kujikabidhi kwa Mungu na kujikita katika ‘vitu vya juu’ (Bwana Yesu) na maandalizi muhimu yanayohitajika haraka kwa kurudi Kwake haraka?

Maadili ya Kukuza: Imani, Maombi, Tumaini, Kutafuta kwanza ufalme wa Mungu na Haki Yake.

Dhambi za Kuepuka/Kuungama: Kukosa kutambua utupu katika maisha yote (bila Yesu Kristo -Yohana 10:10); Ufahirishi: kujitahidi “kupata ulimwengu wote” wakati unapoteza roho yako (Marko 8:36); Kutegemea kile kipatikanacho katika ulimwengu.

Jambo la Kumshukuru Mungu Kwalo: “Mkono wa Mungu”–Kudra (2:24); “Mungu humpa yeye aliyemridhia hekima na maarifa na furaha” (2:26); mdhambi, Mungu humpatia kazi ya “kukusanya na kututa” – ili ampatie yule aliye mwema mbele ya Mungu (2:26).

Watu wa Kuombewa: Waombee watu wote (haswa waovu) ili waokolewe na kupata ujuzi wa Ukweli (1 Tim 2: 4); Omba kwa wale wote walioghubikwa vitu vya Ulimwengu huu: waongolewe na kuwa tayari kwa kurudi kwa Kristo hivi karibuni.

Masuala ya Kuombea: Omba Mwongozo wa Kujifunza Biblia juu ya Mhubiri (maandalizi, kusoma, na wokovu); Uraibu (ulevi / dawa za kulevya); Maandalizi ya Kifo na Kufa; Furaha ya kweli ya Haki; Ushindi juu ya anasa za kidunia, ufahirishi wa mali na kuendekeza nafsi; Ufahamu kwamba mafanikio yote ya mwanadamu na hekima ni bure, ubatili, hutoweka upesi (kama hazikujengwa kwa Bwana Yesu Kristo).

Ahadi ya Leo: “Maneno Yako yalionekana, nami nikayala; na maneno Yako yalikuwa ni furaha kwangu, na shangwe ya moyo wangu; maana nimeitwa kwa jina Lako, Ee Bwana, Mungu wa majeshi.” (Yeremia 15:16) “Bali utafuteni kwanza ufalme Wake, na haki Yake; na hayo yote mtazidishiwa.” (Mathayo 6:33)

 HATUA YA MAAMUZI: Chukua muda wa kuomba, kukiri na kutubu dhambi zilizoorodheshwa hapo juu. Ikiwa unayo Mahitaji ya Kuombea, tafadhali yaandike hapa chini, na mtu fulani atayaombea.

SALA: Sasa, Bwana mpendwa, tunapoomba, chukua mioyo yetu na akili zetu mbali; kutoka kwa mgandamizo wa ulimwengu pande zote, hadi Kiti cha Enzi Chako ambapo neema ni kuu. Hebu maisha yetu yabadilishwe na upendo Wako. Nafsi zetu ziburudishwe kutoka juu. Kwa wakati huu, hebu watu kila mahali, wajiunge nasi sasa tunapokuja Kwako katika maombi. Amina.