Sifa za Mwanamke Bora.

Ibada ya Usiku/ Sifa Za Mwanamke Bora/ 20-BSG-31Y (Mithali 31:10 -31)

Wazo la Usiku linaloshabihiana na Mpango wa Usomaji wa Biblia wa leo: Mithali 31/ Dhima: Mwanamke Mwenye Ushawishi/ Andiko Msingi:Mke mwema, ni nani awezaye kumwona? Maana kima chake chapita kima cha marijani. Moyo wa mumewe humwamini, Wala hatakosa kupata mapato.” (Mithali 31:10-11)/ Wimbo: “Vitu vyote ni sawa panapo Pendo.”

Methali 31 bila shaka hunukuliwa na kutumiwa na wahubiri wengi sana hususan Siku ya Wakinamama (Mother’s Day) kuliko kifungu kingine chochote katika Maandiko Matakatifu. Methali hii huelezea Mwanamke Mwema ambaye huongoza nyumba yake kwa uadilifu, nidhamu, na kipaji. Mke na Mama huyu ni kiongozi, si kwa sababu anajaribu kuwa, lakini kwa sababu yeye hujitambua. Naomba tutafakari kwa kifupi sana wasifu wake:

Sifa Zake: Yeye ni Mwaminifu (aya. 11); Yeye ana ushawishi chanya (aya. 12); Yeye ni mfanyakazi shupavu (aya. 13, 14, 19, 24-27); Yeye ni Mpangaji—‘planner’ (aya. 21-22); Yeye ni kinga kwa familia yake (aya. 27).

Mafanikio Yake: Yeye hukidhi mahitaji ya nyumbani kwake (aya. 15); Yeye huwekeza kwa ajili ya familia yake (aya. 16); Yeye huvaa vizuri: Hupendeza (aya. 17); Yeye humsaidia Mume wake kuwa na mafanikio (aya. 23).

Mitazamo Yake: Mhangaikaji (aya. 13); Mwenye Afya (aya. 18); Mwenye Huruma (aya. 20); Asiye na Ubinafsi (aya. 20); Mwenye Hekima (aya. 25); Mwenye Ukarimu (aya. 25).

Sifa Atakazopata: Kutoka kwa Familia yake (aya. 28); Kutoka kwa Mume wake (aya. 28-29); Kutoka kwa Neno la Mungu (aya. 30); naKutokana na Kazi yake (aya. 31).

DONDOO ZA KIIBADA: Leo wanaume wengi wanahitaji mchumba/ mke mwenye sifa kama hizi. Kuna wanawake wengi ambao hawajishugulishi kabisa, kisa baba (mume) ana kazi nzuri; tena wanadai kuwekewa wasaidizi wa ndani (yaani, house girl). Si mbaya kufanya hivyo, lakini hoja yangu kuu ni hii: wanawake wengi wanasahau wajibu wao katika familia zao. Ndoa nyingi zimevunjilka kwa sababu ya kutozingatia na kupuuza sifa/ majukumu ya “Mwanamke Bora.”

Mpendwa unayesoma “Wazo hili la Usiku,” hebu ukapate kubadilika na kuwa “Mwanamke Bora.” Lakini pia, ikumbukwe kuwa “Mke mwema hutoka kwa Bwana.” Naomba sana wababa msichoke kuwafundisha wake zenu jumbe za sura hii, lakizi zaidi ya yote, wapendeni sana wake zenu, msameheane pale mmoja wenu anapojikwaa, mkishiriki ibada na kuomba pamoja kama familia, n.k. Wapendwa mkifanya hivyo, hakika nyumba zenu zitabarikiwa, na ndoa zenu zitadumu milele.

Iweni na Usiku Mwema: “Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake; ili makusudi alitakase na kulisafisha kwa maji katika neno; apate kujiletea Kanisa tukufu, lisilo na ila wala kunyanzi wala lo lote kama hayo; bali liwe takatifu lisilo na mawaa. Vivyo hivyo imewapasa waume nao kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe.” (Waefeso 5:25-28).