Mithali 29: Mwongozo wa Biblia

Mithali 29: Vifungu Sambamba.

20-BSG-29I (Mithali 29).

NUKUU ZA AGANO LA KALE NA VIDOKEZO KATIKA AGANO JIPYA.

Malengo: Kuchunguza nukuu za Agano la Kale na Vidokezo katika Agano Jipya/ Mawazo Makuu: 1. Ukahaba: Kutapanya mali kwa Uasherati; 2. Onyo kuhusu Kiburi (Kujiinua); 3. Wito wa Unyenyekevu (Kujishusha).

[1] UKAHABA: KUTAPANYA MALI.

Mithali 29 (Mithali 29:3// Luka 15:13).

“Apendaye hekima humfurahisha babaye; Bali ashikamanaye na makahaba hutapanya mali.” (Mithali 29:3) “Akasema, Mtu mmoja alikuwa na wana wawili; yule mdogo akamwambia babaye, Baba, nipe sehemu ya mali inayoniangukia. Akawagawia vitu vyake. Hata baada ya siku si nyingi, yule mdogo akakusanya vyote, akasafiri kwenda nchi ya mbali; akatapanya mali zake huko kwa maisha ya uasherati (Luka 15:11-13)

Fundisho: Kuna mengi sana ya kujifunza katika kisa cha Mwana Mpotevu, lakini nitasema mache hapa: wababa na vijana wengi leo “wanatapanya mali/ fedha zao kwa maisha ya uasherati.” Utakuta mtu mzima ana kazi nzuri tu, lakini mwisho wa mwezi mshahara wake hauonekani. Mke wake na watoto nyumbani wanateseka, hali “makahaba zake” wanaponda mali zake. Baba wa watu hana maendeleo yoyote: hajajenga, hana miradi, hana njozi ya kuwekeza. Kazi yake ni kuranda-randa na wanawake. Wapendwa, tubadilike, mbali na kuwa uasherati ni dhambi, tabia hii imeshafilisi familia nyingi.

Hatua ya Maamuzi: We baba/ we kaka uliyezama katika dhambi hii, jirudi. Kiri dhambi hii kwa Mungu na kwa mkeo wa ndoa – “mke wa ujana wako.” Achana na vimada/ makahaba: watakufilisi. Jambo la pili, Tubu, mlilie Bwana akusamehe na kukupa ushindi dhidi ya dhambi hii. Nakuhakikishia hili: Utaona mibaraka ya Bwana katika familia yako, na utapata Amani itokayo kwa Bwana.

Ahadi: “Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote.” (1 Yohana 1:9).

[2] KIBURI (KUJIINUA).

Mithali 29 (Mithali 29:23//Mathayo 23:12)

“Kiburi cha mtu kitamshusha; Bali mwenye roho ya unyenyekevu ataheshimiwa.” (Mithali 29:23)

Wapendwa, Mungu huchukia kiburi na kujiinua. Mungu hunyenyekeza wenye kiburi. Sikiliza nukuu hii — “Hakuna nafasi ya juu sana ambayo Mungu hawezi kuikomesha. Hakuna udhalilishwaji mkubwa sana amabao Mungu hawezi kunyanyua wanyenyekevu ili kufurahia utajiri mkuu. Bwana hufanya kazi ya kunyenyekeza kiburi cha mwanadamu katika ye yote atakayepatikana nacho, ili kwamba wanadamu waweze kujifunza kukuza roho ya utiifu wa kweli kwa mapenzi Yake.” (The Publishing Ministry, p. 134).

Agizo: “Bwana MUNGU asema hivi; Kiondoe kilemba, ivue taji; haya hayatakuwa tena kama yalivyo; kikweze kilicho chini, kakishushe kilichoinuka.” (Ezekieli 21:26)

Ahadi: “Hapo watakapokuangusha, utasema, Kuna kuinuka tena; Naye mnyenyekevu Mungu atamwokoa.” (Ayubu 22:29).

[3] UNYENYEKEVU (KUJISHUSHA).

Mithali 29 (Mithali 29:23//Mathayo 23:12)

“Kiburi cha mtu kitamshusha; Bali mwenye roho ya unyenyekevu ataheshimiwa.” (Mithali 29:23)

“Wala msiitwe viongozi; maana kiongozi wenu ni Mmoja, naye ndiye Kristo. Naye aliye mkubwa wenu atakuwa mtumishi wenu. Na ye yote atakayejikweza, atadhiliwa; na ye yote atakayejidhili, atakwezwa.” (Mathayo 23:10-12)

Fundisho: (Kuhusu Viongozi wa Kanisa). Kuna viongozi wengi makanisani wanaofikiri nyadhifa walizopewa zinawafanye wawe na kiburi na kujikweza. Mara fulani hujiona wako juu kuliko waumini. Lakini hili si fundisho la Biblia, naam, fundisho la Yesu Kristo.

Mtume Petro aliwashauri wazee wa Kanisa: “Lichungeni kundi la Mungu lililo kwenu, na kulisimamia, si kwa kulazimishwa, bali kwa hiari kama Mungu atakavyo; si kwa kutaka fedha ya aibu, bali kwa moyo. Wala si kama wajifanyao mabwana juu ya mitaa yao, bali kwa kujifanya vielelezo kwa lile kundi. (1 Pet. 5:2-3).

Kama viongozi wa kanisa, au huduma mbalimbali za Injili, hatupaswi kabisa kujiinua, badala yake, yatupasa kuhudumu kwa unyenyekevu— “tutapokea taji ya utukufu, ile isiyokauka” siku ile Yesu Kristo, “Mchungaji Mkuu atakapodhihirishwa” (aya ya 4).

Kwa viongozi wote wa Kanisa, vijana kwa wazee, Petro alitoa maonyo yafuatayo: “Vivyo hivyo ninyi vijana, watiini wazee. Naam, ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa sababu Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema. (1 Pet. 5:5).

DONDOO ZA KIIBADA KUHUSU UNYENYEKEVU:

  1. “Heri walio maskini wa roho; Maana ufalme wa mbinguni ni wao.” (Mathayo5:3)
  • [Yesu] akasema: Amin, nawaambia, “Msipoongoka na kuwa kama vitoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni. Basi, ye yote ajinyenyekeshaye mwenyewe kama mtoto huyu, huyo ndiye aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni.” (Mathayo18:3-4)
  • “Ingawa Bwana yuko juu, amwona mnyenyekevu, Naye amjua mwenye kujivuna tokea mbali.” (Zaburi 138:6)
  • “Msitende neno lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake. Kila mtu asiangalie mambo yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mambo ya wengine.” (Wafilipi 2:3-4)

Hatua ya Maamuzi. Tufanye nini basi na somo hili?“Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake.” (1 Pet 5:6).

Iweni na Siku Njema: “Maana yeye aliye juu, aliyetukuka, akaaye milele; ambaye jina lake ni Mtakatifu; asema hivi; Nakaa Mimi mahali palipoinuka, palipo patakatifu; tena pamoja na yeye aliye na roho iliyotubu na kunyenyekea, ili kuzifufua roho za wanyenyekevu, na kuifufua mioyo yao waliotubu.” (Isaya 57:15).

Sauti ya Injili SDA/ Mwongozo wa Biblia/ Vifungu Sambamba/ Mithali 29/