Onyo Kuhusu Kujisifu.

Wazo la Usiku linaloshabihiana na Mpango wa Usomaji wa Biblia wa leo: Mithali 27/ Andiko Msingi: “Usijisifu kwa ajili ya kesho; Kwa maana hujui yatakayozaliwa na siku moja. Mwingine na akusifu wala si kinywa chako mwenyewe” (Mithali 27:1-2a)/ Wimbo: “Nina haja nawe kila saa; Hawezi mwingine kunifaa” [Mtunzi: Annie S. Hawks (1872)]

UCHUNGUZI: Kujisifu kumekatazwa katika Maandiko Matakatifu (Soma Mithali 27:1; Zab 10:2-6; 12:3-4; 52:1; 94:4; Hab. 1:10-11; Warumi 1:29-30; 2 Tim. 3:1-2; 1 Yohana 2:16)

TAFAKARI: Neno kujisifu lina maana gani? Kiburi cha majivuno, kujizungumzia kibinafsi kuhusu mafanikio yako, mali, au uwezo. Kujisifu ni dhambi, na sura hii huanza kwa kushughulikia suala la kujisifu—lazima tujihadhari na ujasiri uliokithiri kuhusu kesho kwa sababu hakuna ajuaye kesho!

Je, yatupasa kufanya nini kuhusu mipango yetu ya baadaye? “Kwanza, methali hii haikatazi kupanga au kuandaa mambo yajayo. Si vibaya kurasimu ajenda au kuishi kwa ratiba. Methali ya kisasa inaeleza kwa busara kwamba wale ambao wanashindwa kupanga, hupanga kushindwa. Hata mchwa wanapongezwa  katika Methali kwa ajili ya kuhifadhi chakula katika maandalizi ya majira ya baridi (Mithali 6:6-8; 30:25).

Pili, Mithali hii hushutumu kujiaminishia (mambo ya) wakati ujao. Ni dhambi kuchukulia kesho kirahisi na kutenda kana kwamba tuna uwezo wa kudhibiti siku na matukio ya maisha yetu. Hatuna uwezo huo. Ni Mungu pekee anaweza kuelekeza siku zijazo. Mipango Yake, si yetu, hatimaye itashinda (Mithali 16:9; 19:21; Yer. 10:23). Yesu alifunza kwamba tunapaswa kuishi ‘siku moja’ kwa kuzingatia neema ya Mungu na uongozi wake katika siku hiyo (Mt. 6:33 – 34). Lazima tujihadhari tusijekuwa kama tajiri mpumbavu ambaye Yesu alizumgumzia. Alifanya mipango yake yote ya siku za usoni na alikuwa na uhakika kwamba mipango hiyo ingeweza kutimia. Alishindwa kumwamini Mungu katika maisha na kukumbuka kwamba kifo kingeweza kumzuia kukamilisha ajenda yake (Luk. 12:16 – 21).” [Leadership Ministries Worldwide, Proverbs, The Preacher’s Outline & Sermon Bible, (Chattanooga, TN: Leadership Ministries Worldwide, 2012), 404].

MAANA YA KIIBADA: wakati tunapofanya mipango yetu, tunapaswa kumtumaini Bwana na kusihi “Mapenzi Yako Yatimizwe!” Ni lazima tujiwasilishe kwa Mungu na kutoa mipango yetu yote chini ya uangalizi Wake. Maandiko yanasema hivi — “Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe; Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako.” (Mithali 3:5-6)

Sehemu ya andiko (Yakobo 4:15) la Mtume Yakobo (tazama hapo chini) hujumuisha mambo matatu muhimu ya maisha ambayo yatafanya mipango yetu kwenda sawasawa: 1. Mungu yu katika udhibiti — “Bwana akipenda” (4:15); 2. Maisha ni zawadi ya kila siku — “tutakuwa hai” (4:15); 3. Kwenda kwetu na kutenda kwetu lazima zizingatie hoja mbili za kwanza akilini. Kwa hiyo, wapenzi, wakati wa kupanga mipango yetu ya baadaye, miradi, kazi, n.k., hebu tumkabidhi Bwana na kuacha vyote chini ya utegemezi Wake kwa kuwa Yeye hujua na kutegemeza mipango ya baadaye – maana Yeye ni Alfa na Omega.  Hebu sikia Sauti ya Bwana (Sauti ya Injili) tunapohitimisha — “Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho.” (Yeremia 29:11)

Iweni na Usiku Mwema: “Walakini hamjui yatakayokuwako kesho. Uzima wenu ni nini? Maana ninyi ni mvuke uonekanao kwa kitambo, kisha hutoweka. Badala ya kusema, “Bwana akipenda, tutakuwa hai na kufanya hivi au hivi.” Lakini sasa mwajisifu katika majivuno yenu; kujisifu kote kwa namna hii ni kubaya” (Yakobo 4:14-16)

Sauti ya Injili SDA/ Wazo la Usiku/ Mithali 1-31/ Mithali 27