Hatari ya Kurudia Matapishi

Ibada ya Usiku.

HATARI YA KURUDIA MATAPISHI/ 20-BSG-26Y (Mithali 26:11; 2 Petro 2:22)

Wazo la Usiku linaloshabihiana na Mpango wa Usomaji wa Biblia wa leo: Mithali 26/ Andiko Msingi:Kama vile mbwa arudiavyo matapiko yake; Kadhalika mpumbavu afanya upumbavu tena” (Mithali 26:11). “Lakini imetukia kwao sawasawa na ile mithali ya kweli, Mbwa ameyarudia matapiko yake mwenyewe, na nguruwe aliyeoshwa amerudi kugaa-gaa matopeni.” (2 Petro 2:22)

TAFAKARI: Kwa Wayahudi, hakuna viumbe waliokuwa chini ya mbwa na nguruwe. “Katika nyakati za kibiblia, mbwa na nguruwe walikuwa wanyama waliodharauliwa sana (rej. Ayubu 30:1; Zab. 22:16; Mt. 7:6; Luka 16:21). Mbwa, kwa mfano, mara chache walitunzwa kama wanyama wa nyumbani kwa sababu kwa kawaida walikuwa nusu-mwitu –mara nyingi wachafu, wagonjwa, na hatari (cf. 1 Wafalme 14:11; 21:19, 23 – 24; Isaya 56:11; Ufunuo 22:15). Waliishi kwenye taka, na walikuwa tayari kula matapishi yao wenyewe. Si ajabu, basi, kwamba Wayahudi waliwadharau mbwa na kuwachukia. Nguruwe vile vile waliwakilisha uchafu, wakuwa wa mwisho katika nadharia ya unajisi kwa Wayahudi (cf. Luka 15:15 – 16). Hii ni hasa kwa sababu sheria ya Musa alitangaza kuwa wao ni najisi (Law. 11:7; Torati 14:8).” [John F. MacArthur Jr., 2 Peter and Jude, MacArthur New Testament Commentary, (Chicago: Moody Publishers, 2005), 108.]

MAANA YA KIIBADA: Methali ya kwanza imechukuliwa kutoka Mithali 26:11; ya pili pengine ilikuwa kauli maalumu katika karne ya kwanza. Maana ya Mithali zote hizi ni sawa: wale ambao wanarudia uovu baada ya kuwa wamesafishwa si bora kuliko mbwa wanaotapika na kurudia matapishi yao, au ngurue wanaosafishwa kisha kurudi kucheza katika matope. Wale ambao wana mfano wa utauwa bila badiliko la ndani la kiroho punde watarudi katika njia zao za zamani za maisha. Mbwa na nguruwe wanafanya kile wanayafanya kiasili; watu waovu watarudi katika uovu wao wa asili kwa dhambi na kwa hivyo kukumbana na hukumu ya Mungu. Kumbuka: itakuwa bora zaidi kwa mtu ambaye hakuwahi kumjua Yesu Kristo kuliko yule aliyemjua, kisha kiasi. Hukumu ya mwisho itakuwa mbaya zaidi, zaidi sana kwa watu kama hao.

HATUA YA MAAMUZI: Ni mwitikio gani unaodhani somo hili lingepaswa kutuhimiza kufanya? [1] Kama wakristo, hatupaswi kurudia matapishi (dhambi, dunia na anasa zake); [2] Hatupaswi kiacha njia ya haki na kutoka katika amri takatifu. Njia ya haki ni Yesu Kristo. Yeye ndiye amefanaya Mungu atuhesabu kuwa mwenye haki na kutukubali. Amri takatifu ni Neno la Mungu, yaani, amri zote za Mungu.

[3] Hatupaswi kuwa waasi, wakaidi kwa Mungu. Hukumu ya Mungu itakuwa kali na ya kutisha kwa wote ambao wajifanye kuwa na “mfano wa utauwa, lakini wakikana nguvu zake” (2 Timotheo 3:5). Watu hawa ni kama mbwa/nguruwe: kwa maana walirejea katika hali yao ya zamani ya maisha ya dhambi; hakukuwa na badiliko la dhati moyoni; asili yao ya uovu imebakia; hawakusalimisha maisha yao kwa Yesu Kristo.

Wapendwa, tusijidanganye: hukumu ya Mungu itakuwa kali kwa watu kama hawa. Sikiliza Maandiko yafuatayo tunapohitimisha:

  1. “Walakini nawaambieni, itakuwa rahisi Tiro na Sidoni kustahimili adhabu zao siku ya hukumu kuliko ninyi.” (Mt. 11:22)
  2. “Na hii ndiyo hukumu; ya kuwa nuru imekuja ulimwenguni, na watu wakapenda giza kuliko nuru; kwa maana matendo yao yalikuwa maovu.” (Yohana 3:19)
  • “Kwa maana imetupasa sisi sote kudhihirishwa mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ili kila mtu apokee ijara ya mambo aliyotenda kwa mwili, kadiri alivyotenda, kwamba ni mema au mabaya.” (2 Kor 5:10)
  • “Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja Nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo.” (Ufunuo 22:12)

Iweni na Usiku Mwema: “Angalieni, ndugu zangu, usiwe katika mmoja wenu moyo mbovu wa kutokuamini, kwa kujitenga na Mungu aliye hai. Lakini mwonyane kila siku, maadamu iitwapo leo; ili mmoja wenu asifanywe mgumu kwa udanganyifu wa dhambi.” (Waebrania 3:12-13)

Sauti ya Injili SDA/ Wazo la Usiku/ Mithali 1-31/ Mithali 26.