Baba Sina Msaada!

Ibada ya Alfajiri/ Kipindi: “Anza na Bwana!”

BABA SINA MSAADA! (NZ # 143)

Baba sina msaada ila Kwako pekee, Kama kwangu ungefichwa, nifanyeje Baba?

Sasa hivi naamini, Yesu alikufa, Aliimwaga damu yake, nitoke dhambini.

Naamini Mwana wako, nipe nguvu Zako, Nijazie mahitaji, katika saa hii.

Ni furaha gani kwangu, kukuona uso, Nijue sauti Yako, nipate neema.

INJILI KATIKA WIMBO/NZK # 143, Baba Sina Msaada!/ Maadili ya Kukuza: Imani, Toba, Utii, Unyenyekevu.

Dondoo za Kiibada katika Kipindi cha “Anza na Bwana” (Tafakari ya Wimbo # 143)/ Andiko Kuu: “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.” (Yohana 3:16)

[1] Sisi tu wadhambi, wanyonge, wasiojiweza. Mara nyingi kwa sababu ya kiburi tunafikiri kuwa sisi ni matajiri, tusiyo na haja ya kitu; lakini hatujui kuwa tu wanyonge, wenye mashaka, maskini, vipofu, na uchi (Uf. 3:17). Wapendwa, pasipo msaada wa Mungu hatuwezi chochote! —- Kristo anatukumbusha akisema, “pasipo Mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote” (Yohana 15:5). Mtume Paulo anasema “Nayaweza mambo yote katika Yeye anitiaye nguvu.(Wafilipi 4:13). Musa, mtumishi wa Bwana anatukumbusha jambo moja muhimu sana; ni ahadi kwa wote wamtegemeao Bwana. Sikiliza — “Bwana, Yeye ndiye atakayekutangulia, atakuwa pamoja nawe, hatakupungukia wala kukuacha; usiogope wala usifadhaike.” (Torati 31:8).

[2] Je unamwamini Yesu Kristo? Wapendwa, Yesu alikubali kubeba adhabu yetu na kulipa gharama ya dhambi zetu ili kwamba tusipotee. Neno “asipotee” katika andiko letu kuu (Yohana 3:16) halimaanishi kifo cha kimwili, kwani sisi sote tutakufa hatimaye. Hapa linahusu kupotea milele. Wale wanaopokea injili ya Mungu na kumwamini  Yesu Kristo, “Mwanawe pekee” watapokea njia mbadala: maisha mapya ambayo Yesu alinunua kwa ajili yetu — uzima wa milele na Mungu katika Paradiso Yake.

[3] Katika ubeti wa tatu, tunakumbushwa juu ya furaha isiyo kifani Yesu atakaporudi. Furaha hii inahusu washindi dhidi ya dhambi — “Katika siku hiyo watasema, Tazama, huyu ndiye Mungu wetu, Ndiye tuliyemngoja atusaidie; Huyu ndiye Bwana tuliyemngoja, Na tushangilie na kuufurahia wokovu Wake.” (Isaya 25:9). Wadhambi “watatupwa katika giza la nje, ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.” (Mt 8:12). Kwaya ya Kurasini SDA wana wimbo mmoja unasema “Kiwewe kiwewe, chenye kutisha…” Bwana atakapotokea angani (linganisha hofu ya wadhambi katika Ufunuo 6:15-17). Wapendwa, tunapaswa kukata shauri sasa, kabla hatujachelewa.

Je ni shauku yako kuuona uso wa Bwana siku moja? Je umajiandaa kuisikia sauti Yake, parapanda itakapolia? Sikiliza maneno ya Kristo tunapohitimisha: “Msistaajabie maneno hayo; kwa maana saa yaja, ambayo watu wote waliomo makaburini wataisikia sauti Yake. Nao watatoka; wale waliofanya mema kwa ufufuo wa uzima, na wale waliotenda mabaya kwa ufufuo wa hukumu.” (Yohana 5:28-29). Mpendwa, Je utakuwa upande upi katika siku hiyo?

HATUA YA MAAMUZI: Ni mwitikio gani unaodhani wimbo huu ungepaswa kutuhimiza kufanya? Mwamini Yesu! Angalia tena kibwagizo: “Sasa hivi naamini, Yesu alikufa; Aliimwaga damu Yake, nitoke dhambini.” Wapendwa, damu ya Yesu Kristo ni ya thamani kuliko kitu chochote: Ni damu iokoayo; Ni damu itutakasayo; Ni damu itupayo msamaha wa dhambi; Ni damu inayotupatia Uzima wa Milele. Mwamini Yesu leo, nawe utaokoka.

SAUTI YA INJILI: “Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka.” (Warumi 10:9)

Iweni na Siku Yenye Baraka! “Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa.” (Marko 16:16)