Mithali 8: Mwongozo wa Biblia

Mithali 8: Mwongozo wa Ibada

Ibada ya Alfajiri/ Dhima: Chagua Hekima juu ya kitu chochote/ 20-BSG-8A, (Mithali 8:1-36)/ Andiko Muhimu: “Je! Hekima halii? Ufahamu hatoi sauti yake? Juu ya mahali palipoinuka karibu na njia, Penye njia panda, ndipo asimamapo.” (Mithali 8:1-2)/ Wimbo: Yesu akwita, akwita wewe (NK 101) [Mtunzi: Fanny Crosby].

UCHUNGUZI: Wito wa Mungu kwa wenye dhambi — Yeyote Atakaye na Aje (Isa. 2:5; 45:22; 55:1; Mt 11:28-30; 22:2-4; Lk 14:17; Yoh. 6:37; 7:37; Ufu. 22:17)

TAFAKARI: Methali sura ya 8-9 ni kilele cha kila kitu ambacho baba amekuwa akimfundisha mwanawe katika sura saba za awali. Katika sura hii tunaona mwito wa kusikia hekima (aya. 1 – 5); Kusikiliza thamani kubwa ya hekima (aya. 6 – 9); Kuchagua hekima juu ya fedha na dhahabu (aya. 10 – 21); Kujua asili na chanzo cha hekima (aya. 22 – 31); mwisho, kusikiliza ombi la hekima na ahadi zake za masharti (aya. 32 – 36).

Hekima inayofundishwa katika Biblia si hekima ya ulimwengu! Haiwezi kupatikana mashuleni, au toka kwenye vitabu vya elimu, wazazi, au walimu, La Hasha. Hekima iliyo kuu ni ile itokayo kwa Mungu, na tunawezaipata tu kwa njia ya maarifa na utii wa Neno Lake. Sura hii inatualika kutafakari juu ya njia ya Hekima — Bwana wetu Yesu Kristo, “hekima ya Mungu” (1 Kor. 1:24, 30). Kumbuka, maisha ya dhambi (njia pana) huelekeza upotevuni, lakini maisha tele yanapatikana ndani ya hekima ya Mungu (Mithali 2:6; Ayubu 11:6).

MAANA YA IBADA: “Hekima husimama katika njia panda ya milele… Kuna hatua maalum ambapo barabara ya uharibifu na njia ya uzima hukutana — makutano halisi. Barabara kuu kwenda jehanamu na barabara kuu ya mbinguni hukutana Kalivari. Pale, msalabani, hekima huimba wimbo wake wa furaha. Kwa sauti na ushindi anatangaza habari yake njema — habari njema ya injili: Yesu alikufa, na akazikwa, na akafufuka tena siku ya tatu (1 Cor. 15:3-4). Alitengeneza njia iendayo mbinguni. Kuna matumaini! Kuna wokovu! Hekima huangaza nuru, hupeperusha bendera, huinua ishara ya kuelekeza watu kwenye barabara hii.” (Proverbs, The Preacher’s Outline & Sermon Bible, p. 133).

SAUTI YA INJILI: Kipengele hiki kimeandikwa kana kwamba Mungu anaongea nawe moja kwa moja –kwa sababu hufanya hivyo. Je Bwana ananiambia nini asubuhi ya leo? Mwanangu, barabara ya Hekima (Yesu Kristo) itakupatia si tu safari bora, lakini pia mwisho mwema wa safari. Ni hakika kuwa barabara hii si nyepesi – inahitaji kujikana nafsi, unyenyekevu, utakatifu. Wakati mweingine ina mateso, maudhi, fedheha, n.k. – lakini ni “njia salama” na bora zaidi. Ukichagua njia Yangu — njia ya Hekima, Ninaahidi kuwa pamoja nawe: kamwe hautasafiri peke yako! (Mt 28:20; Ebr 13:5). Njia ya hekima sio tu njia iendayo uzimani, bali ni njia ya uzima — Uzima wa Milele! Je, ungependa kuingia katika mlango mwembamba? Ninakusubiri!

Shauku Yangu Leo: Kwa neema ya Mungu, ninataka kuchagua hekima, ninataka kumchagua Yesu Kristo, njia pekee itakayonipeleka kwa Baba.

Iweni na Alfajiri Njema: “Ingieni kwa kupitia mlango ulio mwembamba; maana mlango ni mpana, na njia ni pana iendayo upotevuni, nao ni wengi waingiao kwa mlango huo. Bali mlango ni mwembamba, na njia imesonga iendayo uzimani, nao waionao ni wachache.” (Mathayo 7:13-14).