Sabato Katika Kumbukumbu.

Mwongozo wa Kujifunza Biblia/ Siku Iliyosahauliwa: Sabato ya Siku ya Saba/ 86-007/ Andiko Msingi: “Ishike siku ya Sabato uitakase, kama Bwana, Mungu wako, alivyokuamuru.” (Kumbukumbu 5:12)

Malengo ya Somo: Kuchanganua maandiko kuhusu Sabato katika mfululizo yanavyojitokeza katika Pentatuku. Leo, tutazingatia Sabato katika Kumbukumbu. Kwenye masomo yaliyotanguliwa, tumeona mada ya Sabato katika Mwanzo, Kutoka, Walawi, na Hesabu.

Maelezo ya Ufunguzi: Andiko hili (Kumb. 5:12–15) hubainisha rejea ya mwisho kwenye Pentatuku kuhusu Sabato. Hapa Musa anasisitiza amri ya Sabato katika maneno sawa na yale katika Kutoka 20:8–11. Japo Wakristo wengi wanafahamu vyema amri ya Sabato kama inavyoelezewa katika kitabu cha Kutoka, Bwana aliwasilisha tena (pamoja na amri zingine zote) katika kitabu cha Kumbukumbu. Kinachoshangaza ni kwamba, japo amri hii huonekana katika lugha husika shabihi sana, lugha hiyo siyo sawa kabisa. Zaidi ya hapo, amri katika Kumbukumbu imeambatishwa na msukumo mwingine, usioonekana katika Kutoka. Badala ya rejea kuhusu Sabato ya Uumbaji, mantiki ya kuadhimisha Sabato ni tukio la Mungu kuwaokoa Waisraeli kutoka utumwani Misri (Kumb. 5:15).

MASWALI YA MSINGI.

[1] Soma Kutoka 20:8–11. Linganisha na Kumbukumbu 5:12–15.

 • Kutoka 20:8–118 “Ikumbuke siku ya Sabato uitakase. 10 Siku sita fanya kazi, utende mambo yako yote; 11 Maana, kwa siku sita Bwana alifanya mbingu, na nchi, na bahari, na vyote vilivyomo, akastarehe siku ya saba; kwa hiyo Bwana akaibarikia siku ya Sabato akaitakasa.
 • Kumbukumbu 5:12–1512 ‘Ishike siku ya Sabato uitakase, kama Bwana, Mungu wako, alivyokuamuru. 13 Siku sita fanya kazi, utende mambo yako yote; 14 lakini siku ya saba ni Sabato ya Bwana, Mungu wako; siku hiyo usifanye kazi yoyote, wewe, wala mwanao, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala mjakazi wako, wala ng’ombe wako, wala punda wako, wala mnyama wako yeyote, wala mgeni aliye ndani ya malango yako, ili mtumwa wako na mjakazi wako wapumzike vilevile kama wewe. 15 Nawe utakumbuka ya kuwa wewe ulikuwa mtumwa katika nchi ya Misri, na ya kuwa Bwana, Mungu wako, alikutoa huko kwa mkono wenye nguvu, na mkono ulionyoshwa; kwa sababu hiyo Bwana, Mungu wako, alikuamuru uishike Sabato.

[2] Je ni mifanano ipi iliyopo baina ya maandiko haya mawili?

 • Ingawa mengi ni sawa baina yao, kuna kipengele na msisitizo mpya. Ilhali amri zote mbili huzungumzia watumwa kupumzika siku ya Sabato, Kumbukumbu huenda mbali zaidi kiasi cha kusisitiza wazo hilo. Andiko husomeka kwamba wanapaswa kuishika Sabato ili “ili mtumwa wako na mjakazi wako wapumzike vilevile kama wewe.” (Kumb. 5:14.
 • “Katika Israeli ya zamani ingelikuwa kwa mkuu wa kaya pamoja na familia yake jirani kuadhimisha Sabato ilhali familia nzima iliendelea kama kawaida. Ili kuzuia hili, kwa namna mahususi amri hii huwaorodhesha wengine katika kizio cha uchumi ili kujumuishwa kwenye hisani hiyo: watoto (waume na wake), watumishi (waume na wake), wanyama wa mizigo (ng’ombe na punda), na watu wote wa nje waishio mjini kwa muda. Kishazi cha utashi kilichoongezwa husisitiza kwamba katika haki yao ya kupata pumziko la Sabato hawa wote walikuwa sawa na mwenye nyumba; Sabato ilikuwa tunu kwa wote. Katika kuhimiza “sikukuu” kwenye kumbukumbu ya Israeli juu ya uzoefu wao huko Misri (v. 15), Musa hutoa wito wa mwenendo wa huruma kwa wale walio chini ya mamlaka ya mwenye nyumba. Kwa namna walivyowatendea watoto, watumishi, wanyama, na wageni, wakuu wa kaya walipaswa kuzingatia haki adhimu ya sheria za Yehova zilizodhihirishwa (Kumb. 4:8).” [Daniel I. Block, The NIV Application Commentary: Deuteronomy, ed. Terry Muck, (Grand Rapids, MI: Zondervan, 2012), 164].

[3] Ni tofauti gani uzionazo kati ya rekodi hizi mbili kuhusu amri hii?

 • “Amri hii hutofautiana katika maneno dhidi ya Amri ya Nne iliyodhihirishwa pale Sinai (Kut. 20:8–11). Neno la kwanza hasa ni tofauti: pale Sinai ilikuwa ‘ikumbuke’ bali hapa ni ‘ishike.’ Miundo yote miwili ni kihalida fusili (infinitive absolutes), na hutumika katika dhana shurti msisitizo. Vitenzi hivyo viwili vinaweza kuwa sawa, lakini kitenzi ‘ishike’ (Kiebrania, shamar) kina dhana amilifu zaidi kuhusu utii. Kitenzi hiki kwa kawaida pia hutumiwa ili kuwaagiza Israeli kutii na kusherehekea sikukuu zake (mfano, Law. 26:2). Msingi wa kalenda ya Kiebrania ni Sabato (angalia Law. 23)—iko katika kiini na msingi hasa wa sherehe za kidini za Israeli.”
 • “Aya ya 12 ya andiko la sasa huongeza maneno, ‘kadiri ambavyo Yehova, Mungu wenu, amewaamuru.’ Nyongeza hii hurejea uwasilishwaji wa kwanza wa Dekalojia pale Sinai na, kwa hiyo, isingejumuishwa katika ufunuo wa awali.”
 • “Tofauti kuu kati ya maelezo hayo mawili ni aya ya mwisho kwenye amri husika. Wakati ambapo katika Kutoka mantiki kwa ajili ya Sabato ni uumbaji, hapa ni matendo makuu ya Mungu ya ukombozi ya kuwaokoa watu Wake kutoka kwenye udhalimu wa Misri. Kihalisia, hizi hazikosi kutoafikiana, bali hukamilishana. Kumbukumbu haibatilishi Kutoka; husisitiza tu sababu nyingine kwa ajili ya amri ya Sabato. Sabato huwashiria uwekwaji huru kutoka kwenye udhalimu na, kwa namna mmoja, uundwaji aliofanya Mungu kwa ajili ya kusudi Lake Mwenyewe.” [John D. Currid, A Study Commentary on Deuteronomy, EP Study Commentary, (Darlington, England; Webster, New York: Evangelical Press, 2006), 138–139].

[4] Kwa tofauti hizo katika rekodi hizi mbili za amri hii ni muhimu?

 • Sabato ilipoasisiwa mara ya kwanza, ilikusudiwa kuwa kumbukumbu ya Uumbaji katika ulimwengu usioanguka. Haikuhusiana na watumishi au wajakazi na hakika haikuhusiana na kuwa utumwani Misri, penyewe pakiwa alama ya utumwa wa dhambi, na ukombozi kutoka kwenye utumwa huo.
 • Kipengele kipya hiki, basi, kilikuwa kimeongezwa kwenye amri baada ya Anguko; yaani, amri ya awali ilikuzwa ili kujumuisha kitu fulani ambacho awali haikuwa nacho.
 • Hivyo, kama ilivyotambuliwa awali, Sabato ilikuwa alama ya Uumbaji; baada ya dhambi, ilikuwa alama ya Uumbaji na Ukombozi, ambayo yenyewe ni aina ya uumbaji mpya (2 Kor. 5:17, Gal. 6:15, Ufu. 21:1). Uumbaji na Ukombozi vinahusiana kwa karibu katika Biblia; ni Mungu Muumbaji pekee ndiye angeweza kuwa Mungu Mkombozi, na tunazo sifa hizi mbili katika Yesu (angalia Yohana 1:1–14). Matoleo yote mawili ya amri husika huonesha kwamba Sabato ya siku ya saba ni ishara ya kazi ya Yesu, Muumbaji na Mkombozi wetu.

[5] Je kuna uhusiano gani kati ya Sabato na upatanisho wa Kristo pale msalabani?

 • “Katika Kumbukumbu 5:15, Sabato ya siku ya saba husherehekea kazi ya Kristo iliyokamilika ya ukombozi wa Israeli kutoka Misri. Kwa sababu Kristo alipumzika kaburini kwa mujibu wa amri ya Sabato (Luka 23:54–24:1), mtu angeweza kusema kwamba Sabato ya siku ya saba ilisherehekea kazi ya Kristo ya kafara ya upatanisho iliyokamilika pale msalabani. Hivyo Sabato ya siku ya saba husherehekea tunu ya Kristo ya uumbaji, ukombozi, na wokovu. Sabato ni ishara ya watu wa Mungu katika kila kizazi. Ni siku iliyotengwa kwa ajili ya watu waliotengwa. “Tena naliwapa Sabato Zangu, ziwe ishara kati ya Mimi na wao, wapate kujua ya kuwa Mimi, Bwana, Ndimi niwatakasaye.” (Eze. 20:12). Wakristo hupata katika kila mmoja ya kazi hizi za Kristo zilizokamilika sababu za kusherehekea Sabato kwa kupumzika katika siku ya saba aliyoichagua Kristo. Hivyo, uadhimishaji wa Sabato ya siku ya saba ni wajibu wa Kikristo.” [Norman R. Gulley, Systematic Theology: Creation, Christ, Salvation, (Berrien Springs, MI: Andrews University Press, 2012), 61].

MAANA YA KIIBADA: “Ukombozi wao kutoka Misri uliunda sababu ya nyongeza kwa nini Waisraeli wangepaswa kuistahi Sabato, hata hivyo maneno hasa ya amri ya nne yenyewe hurejelea asili ya Sabato katika uumbaji (Kut. 20:8–11) kama sababu kwa ajili ya amri hapa ya “kuishika Sabato na kuitakasa.” Inapaswa kukumbukwa kwamba namna Mungu alivyotamka Amri Kumi pale Sinai ni ile iliyowasilishwa katika Kut. 20, siyo katika Kumb. 5. Kama jina lake linavyodokeza, kitabu cha Kumbukumbu ni mrudio wa sheria kadhaa zilizowasilishwa kwa Israeli pale Sinai, pamoja na maelezo ya nyongeza kutoka kwa Musa katika jitihada za kuwahimiza watu kuhusu umuhimu wa kutii kwa uaminifu yote waliyokuwa wameamuriwa kufanya. Endapo kutajwa kwa ukombozi kutoka Misri katika kuhusiana na amri ya nne kukichukuliwa kwamba huwekea mipaka uadhimishaji wake, kikanuni, kwa wale waliokombolewa hivyo—Waisraeli halisi—basi kanuni za Amri Kumi kijumla ni kwa ajili ya Wayahudi pekee, maana hapa (Kumb. 5:6) na katika Kut. 20:2 Mungu aliwasilisha sheria Yake kwa msingi wa ukweli kwamba alikuwa amewatoa nchi ya Misri.”

“Kama ambavyo Israeli halisi walikombolewa kutoka utumwani Misri bondage, vivyohivyo watu wa Mungu leo wamewekwa huru kutoka katika utumwa wa dhambi (Rum. 6:16–18). Hivyo Sabato kwa Mkristo huwa kumbukumbu siyo tu ya uumbaji bali pia uumbaji mpya wa sura ya Mungu moyoni na akilini mwa mtu huyo (angalia katika Kumb. 5:8). Hivyo Sabato ni “ishara” ya utakaso (Eze. 20:12)—ya ukombozi pamoja na uumbaji.” [Francis D. Nichol, Ed., The Seventh-Day Adventist Bible Commentary, (Review and Herald Publishing Association, 1978), 1:972].

HATUA YA MAAMUZI: Ni mwitikio gani unaodhani sura hii ingepaswa kutuhimiza kufanya? “Wewe ulikuwa mtumwa katika nchi ya Misri” (Kumb. 5:15)

[1] Kila tendo la Mungu kwa niaba yetu huunda sababu kwa nini tunapaswa “kuikumbuka.” Ikumbuke, iadhimishe, ishike siku ya Sabato, itakase! Tafakari juu ya ukweli wa Sabato; mtambue Mungu kama Muumbaji na Mkombozi; mwisho, thamini upendo na hisani Yake.

[2] Ni kusudi la Mungu kwamba katika siku ya Sabato chochote kinachoingilia ushirika mchaa na binafsi kati ya kiumbe na Muumbaji wake kinapaswa kuwekwa kando.

[3] Siku ya Sabato ni siku ambapo ni fursa yetu ya furaha kumfahamu vyema Baba yetu wa mbinguni, ambaye kwa kumjua ni uzima wa milele (Yohana 17:3).

[4] Kumbuka kwamba kumjua Mungu ni kumpenda Yeye (angalia 1 Yohana 4:8), kumheshimu, na kuthamini ushahidi mbalimbali wa wema Wake kama Baba (Rum. 1:21). Kristo anasema: “Kama (kweli) mnanipenda Mimi, mtazishika (tii) amri Zangu.” (Yohana 14:15, AMP). Wapendwa, kama kweli unampenda Bwana, utashika Sabato ya siku ya saba kuwa siku takatifu.

[5] Kama ambavyo Mungu aliwakomboa Israeli kutoka utumwani Misri, vilevile ametuweka huru, sote tumwaminio, kutoka katika utumwa wa dhambi (angalia Rum. 6:16–18). Wapendwa, upuuzaji wowote wa amri ya Sabato ya siku ya saba, baada ya mtu kuujua ukweli kikamilifu, ni dhambi. Tumeitwa kutii sheria ya Mungu. Uasi husababisha mauti, hata mauti ya milele! (Rum. 6:23). “Dhambi inapokuwa bwana wetu, hatuna nguvu yoyote isipokuwa kutenda kile inachotuamuru. Tunakuwa watumwa wa dhambi, ambayo hupelekea mauti. Lakini tunapochagua kumtii Yule aliyetuumba, na hivyo tukawa watumwa wa utii Kwake, tutagundua kwamba huo ni utumwani uletao haki. Kuna chaguzi mbili kuu na wala hakuna uwanja wa kati. Hivi ni kama alivyosema Yesu, “Hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili” (Mathayo 6:24). [Bruce B. Barton, David Veerman, and Neil S. Wilson, Romans, Life Application Bible Commentary, (Wheaton, IL: Tyndale House Publishers, 1992), 124].

MASWALI HALISIA MOYONI:

[1] Ni aina gani ya utumwa ambao Kristo ameahidi kutuweka huru dhidi yake? Utumwa wa dhambi.

 1. “Ole wangu, maskini mimi! Ni nani atakayeniokoa na mwili huu wa mauti?” (Warumi 7:24)
 2. “Wakiwaahidia uhuru, nao wenyewe ni watumwa wa uharibifu, maana mtu akishindwa na mtu huwa mtumwa wa mtu yule.” (2 Petro 2:19)
 3. “Wapate tena fahamu zao, na kutoka katika mtego wa Ibilisi, ambao hao wametegwa naye, hata kuyafanya mapenzi yake.” (2 Timotheo 2:26)
 4. “Yesu akawajibu, Amin, amin, nawaambia, Kila atendaye dhambi ni mtumwa wa dhambi.” (Yohana 8:34)
 5. “Basi, kwa kuwa watoto wameshiriki damu na mwili, Yeye naye vivyo hivyo alishiriki yayo hayo, ili kwa njia ya mauti amharibu Yeye aliyekuwa na nguvu za mauti, yaani, Ibilisi” (Waebrania 2:14)
 6. “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, Nami nitawapumzisha. Jitieni nira Yangu, mjifunze Kwangu; kwa kuwa Mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu.” (Mathayo 11:28–29)

[2] Je Mungu huondoa dhambi zetu tunapotubu? Ndiyo. Lakini kwa namna gani?

 1. Kwa kufanya upatanisho kwa ajili ya dhambi zetu (Ebr. 2:17);
 2. Kwa kutusamehe dhambi zetu (Mik. 7:18; 1 Yn. 1:9);
 3. Kwa kutufutia madeni (Mat 6:12);
 4. Kwa kufunika dhambi zetu (Zab. 32:1; 85:2);
 5. Kwa kuzitwaa dhambi zetu (Zab. 103:12);
 6. Kwa kutozikumbuka dhambi zetu tena (Isa 43:25).

[3] Ni ahadi zipi za msamaha tulizonazo katika Yesu? “Ni nani aliye Mungu kama Wewe, mwenye kusamehe uovu, na kuliachilia kosa la watu wa urithi Wake waliosalia? Hashiki hasira Yake milele, kwa maana Yeye hufurahia rehema.” (Mika 7:18) “Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote.” (1 Yohana 1:9)

[4] Jinsi gani unaweza kujifunza kudai ahadi hizi na kisha kumruhusu Bwana azifanye kuwa halisi maishani mwako? “Yeye awezaye kuwalinda ninyi msijikwae, na kuwasimamisha mbele ya utukufu Wake bila mawaa katika furaha kuu; Yeye aliye Mungu pekee, Mwokozi wetu kwa Yesu Kristo Bwana wetu; utukufu una Yeye, na ukuu, na uwezo, na nguvu, tangu milele, na sasa, na hata milele. Amina.” (Yuda 24–25)

SHAUKU YANGU LEO. Chagua Kisanduku kinachoakiasi uamuzi wako leo:

 • Nataka kutubu na kumwomba Bwana anisamehe kwa kuivunja Sabato
 • Nataka kujifunza zaidi kuhusu Sabato
 •  Nataka kuwashirikisha wengine ukweli kuhus Sabato
 • Nataka kushika amri zote za Mungu, ikiwa ni pamoja na Sabato
 • Ni shauku yangu ya kumtii Bwana kwa kuidumisha Siku Yake (Sabato ya siku ya saba) kuwa takatifu, Kut. 20:8.

“Tena naliwapa Sabato Zangu, ziwe ishara kati ya Mimi na wao, wapate kujua ya kuwa Mimi, Bwana, Ndimi niwatakasaye [niwatengaye na kuwaweka kando].” (Ezekieli 20:12, AMP)

Sauti ya Injili/ Mwongozo wa Kujifunza Biblia/ Mafundisho Makuu/ Sabato ya siku ya saba/ Somo # 7.