Zaburi 141: Mwongozo wa Biblia.

19-BSG-141A: MWONGOZO WA IBADA

Mwongozo wa Ibada unaoshabihiana na Mpango wa Usomaji wa Biblia wa leo: Zaburi 141/ Somo: Ombi la Ukombozi dhidi ya Maadui/19-BSG-141A, (Zaburi 141:1-10)/ Wimbo: Popote na Yesu naweza kwenda! (NK 133)

UCHUNGUZI: Ombi la Ukombozi dhidi ya Maadui (Soma 2 Wafalme 19:9-11; 2 Nya. 14:11; Zab 17:8-9; 35:4)

TAFAKARI: Zaburi hizi mbili (140-141) zinahusiana na zote mbili hutumia misamiati inayofanana — moyo, ulimi, mikono, mitego, wenye haki, nk. Adui alikuwa anamuwinda Daudi tena, na alihitaji ukombozi wa haraka (aya. 1). Mandari ya Zaburi hii ni wakati Daudi alipokuwa katika pango: wakati alikimbia toka kwa Sauli hadi jangwa la Engaddi na kujificha katika pango hilo kwa ajili ya usalama wake mwenyewe (1 Sam. 24).

Hapa kuna vipengele vya ombi la Daudi: [a] anasihi kwamba ombi lake lipae mbinguni kama uvumba (aya. 2); [b] anasihi kuokolewa toka katika dhambi ya ulimi (aya. 3); [c] anasihi kuokolewa toka katika dhambi za mawazo na matendo (aya. 4); [d] anasihi ili apate kukemewa, kurekebishwa, kwa ukosoaji wa haki (aya. 5). Sala ya Daudi pia inalenga juu ya matendo ya waovu, (aya. 6-7) — [e] aliendelea kuwaombea maadui zake na alitamani kuona siku ambayo Mungu angewahukumu na kumdhihirisaha (Zab 138:8; 140:12).

MAANA YA KIIBADA: Mimi nitaendelea kusonga Mbele kwa Imani! (Zab. 140:8-10). “Kukaza macho kwa Bwana asiyeonekana kunamaanisha kuishi kwa imani katika Neno Lake (Isa. 45:22; Ebr. 12:1 – 2). Mungu alimpaka mafuta Daudi kuwa mfalme wa Israeli na hakuna chochote isipokuwa uasi wa Daudi mwenyewe ungeweza kuvuruga mpango huo. Tofauti na Petro alipokuwa akitembea juu ya maji katika dhoruba, Daudi hakuondoa macho yake ya imani mbali na Bwana (Mt. 14:22-33). Mungu alikuwa kimbilio la Daudi na asingeweza kufa hadi kazi yake ilipomalizika. Endapo Daudi angekuwa na wasiwasi juu ya hila na mitego ya siri ambayo adui aliiweka, angepooza kwa hofu; lakini badala yake, alijitolea kwa Bwana na kutembea salama katika uwanja wa vita.” [Warren W. Wiersbe, Be Exultant, “Be” Commentary Series, 1st ed., (Colorado Springs, CO: Cook Communications Ministries, 2004), 202].

SAUTI YA INJILI: Kipengele hiki kimeandikwa kana kwamba Mungu ndiye anaongea nawe moja kwa moja—kwa sababu Yeye hufanya hivyo! Je Bwana ananiambia nini asubuhi ya leo? Mwanangu; Shetani yu kazini mchana na usiku kwa sababu “anajua ya kuwa ana wakati mchache tu” (Ufu. 12:12); hivyo, daima anataka kukuangamiza (1 Pet. 5:8). “Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; Mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele.”(Yohana 10:10). Shetani anataka kuharibu maisha yako, ushuhuda wako, wito wako, huduma yako, familia yako, n.k. Maombi ndiyo silaha bora zaidi dhidi ya Shetani, majaribu, na uovu (Efeso. 6:18). Kumbuka kwamba Shetani daima huweka mitego kwa ajili yako, lakini Nakualika unitegemee Mimi kwa ushindi: “Neema Yangu yakutosha; maana uweza Wangu hutimilika katika udhaifu” (2 Kor. 12:9). Nina mpango mzuri kwa ajili yako! Je, utaniamini, utanitii, na kudumu kuliita Jina Langu?

SHAUKU YANGU LEO: Kwa neema ya Bwana, nataka [1] kumlilia kwa msaada wa haraka (aya. 1-2); [2] kumsihi Bwana anikinge na watu waovu (aya. 3-5a); [3] kuomba dhidi ya uovu (aya. 5b-7); [4] nitaelekeza macho yangu kwa Bwana, na kupiga simu mbinguni (aya. 8-10).

Iweni Na Siku Yenye Baraka: “Macho yangu yanakuelekea Wewe, MUNGU BWANA, Nimekukimbilia Wewe, usiniache nafsi yangu. Unilinde na mtego walionitegea, na matanzi yao watendao maovu. Wabaya na waanguke katika nyavu zao wenyewe, Pindi mimi ninapopita salama.” (Zaburi 141:8-10)