Sabato katika Kutoka

Mwongozo wa Kujifunza Biblia/ Siku Iliyosahauliwa: Sabato ya Siku ya Saba/ 86-004, (Kutoka 31:13)/ Andiko Msingi: “Kisha, nena wewe na wana wa Israeli, na kuwaambia, Hakika mtazishika Sabato Zangu, kwa kuwa ni ishara kati ya Mimi na ninyi katika vizazi vyenu vyote; ili mpate kujua ya kuwa Mimi ndimi Bwana niwatakasaye ninyi.” (Kutoka 31:13)

Malengo ya Somo: Kuchanganua maandiko kuhusu Sabato katika mfululizo yanavyojitokeza katika Pentatuku. Leo, tutazingatia Sabato katika Kutoka, kisha, tutaona katika Walawi, Hesabu, na Kumbukumbu.

Vipengele vya Somo:

 1. Sabato katika Kutoka 5:5.
 2. Sabato katika Kutoka 16.
 3. Sabato katika Kutoka 20:8–11.
 4. Sabato katika Kutoka 23:12.
 5. Sabato katika Kutoka 31:13–17.

Maelezo ya Ufunguzi.: Katika Kutoka, amri ya 4 hutuhimiza “kuikumbuka” — Sabato ya siku ya saba– kabla ya kutuhimiza kufanya lolote. Kile tunachopaswa kukumbuka hubainisha maana ya Sabato. Mungu huitenga Sabato pamoja na utakatifu Wake, uwepo Wake, uaminifu Wake, kazi Yake kwa niaba yetu, baraka Zake za agano kwetu — kabla ya kutajwa kokote kwa mwitikio wa kibinadamu. Nimesikia wengi sana wakisema kwamba Sabato ni kipimo cha utii wetu kwa Mungu, na hilo ni kweli (angalia Ufu. 12:17; 13:16-17; 14:6-11, 12, nk.)  Hata hivyo, Sabato pia ni ishara ya uaminifu wa Mungu kwetu. “Yeye aliyeanza kazi njema mioyoni mwenu ataimaliza hata siku ya Kristo Yesu” (Wafilipi 1:6). Katika Ufunuo 2:10, Bwana anasema: “Usiogope mambo yatakayokupata; tazama, huyo Ibilisi atawatupa baadhi yenu gerezani ili mjaribiwe, nanyi mtakuwa na dhiki siku kumi. Uwe mwaminifu hata kufa, Nami nitakupa taji ya uzima.” Nakumbuka katika matukio mawili tofauti nilipopoteza ajira yangu kwa sababu ya Sabato, niliteseka saba, lakini Mungu alinikumbuka na kunikirimia. Ee Bwana, jinsi ulivyo mkuu uaminifu Wako!

[1] Sabato katika Kutoka 5:5

Katika Kutoka 5, tunaona ukinzani kati ya Bwana na Farao. Tunaona tukio la kwanza Musa alipokabiliana na Farao ili kutaka ruhusa kwa ajili ya Waebrania kwenda kumwabudu Bwana. “Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Wape watu Wangu ruhusa waende, ili kunifanyia sikukuu jangwani.” (v. 1).

Swali balagha la Farao: “Bwana ni nani?” haina budi kueleweka kama upinzani mchaa (wa moja kwa moja) dhidi ya Mungu. “Farao akasema, Bwana ni nani, hata niisikilize sauti Yake, na kuwapa Israeli ruhusa waende zao? Mimi simjui Bwana, wala sitawapa Israeli ruhusa waende zao.” (v. 2). Mfalme alikataa ombi la Musa. Jibu la Farao ni bainifu na kweli—hamjui Yehova. Yapo mengi yanayoweza kusemwa kuhusu aya hii ya Maandiko, lakini kwa kusudi la somo hili, wazo kuu ni hili:

 • Kutoka 5:5 ina istilahi ya Sabato katika kauli, “Kisha Farao akasema, Tazameni, watu wa nchi sasa ni wengi, nanyi mnawapumzisha (šābaṯ), wasichukue mizigo yao.” (Kutoka 5:5). Ilhali siku ya saba ya juma haikutajwa kwa namna mahususi, muktadha halani hudokeza kwamba pumziko hili lilikuwa na umuhimu wa kidini.
 • “Ombi lililowasilishwa mbele ya Farao lilikuwa la kimantiki. Waisraeli wasingeweza kutoa kafara za wanyama wao Wamisri wakiwepo bila kuchochea mlipuko wa uhasama wa kidini, kwa vile miongoni mwa wanyama ambao wangechinjwa walikuwemo baadhi ambao Wamisri waliwastahi kuwa wasalihi, na hivyo wasingepaswa kuuliwa kwa namana yoyote ile. Ili kuepuka hatari hii, lazima karamu ya Waisraeli ifanyikie ng’ambo ya mipaka ya Misri, jangwani.” (SDA BC 1:519)

[2] Mana & Sabato katika Kutoka 16

Basi ikawa siku ya sita wakaokota kile chakula sehemu maradufu, kila mtu pishi mbili; na wazee wote wa mkutano wakaenda na kumwambia Musa. Akawaambia, Ndilo neno alilonena Bwana, Kesho ni starehe takatifu, Sabato takatifu kwa Bwana; okeni mtakachooka, na kutokosa mtakachotokosa; na hicho kitakachowasalia jiwekeeni kilindwe hata asubuhi. Basi wakakiweka hata asubuhi, kama Musa alivyowaagiza; nacho hakikutoa uvundo wala kuingia mabuu. Musa akasema, Haya, kuleni hiki leo; kwa kuwa leo ni Sabato ya Bwana; leo hamtakiona nje barani. Siku sita mtaokota; lakini siku ya saba ni Sabato, siku hiyo hakitapatikana.” (Kutoka 16:22–26)

Muktadha wa sura hii ni ukirimiwaji wa Mana kwa wana wa Israeli katika Jangwa la Sini, wiki mbili kabla hawajafika Mlima Sinai. Yapo mambo mawili muhimu ambayo hayana budi kukumbuka katika sura hii – (1) Mlo Maalumu (Kut. 16:1–22, 31–36. Licha ya ulalamikaji daima wa Waisraeli, Bwana aliwatumia kware ili wawale jioni na kuwakirimia kila siku mkate (“mana”) kutoka mbinguni; (2) Siku Maalumu (Kut. 16:23–30). Musa anawaambia watu waishike siku ya Sabato, siku ya pumziko kila juma.

Kwa mujibu wa Kutoka 16:5, katika siku ya sita Waisraeli walipaswa kukusanyika na kuleta “maradufu ya kiwango wakusanyacho kila siku.” Baadaye katika sura hii wanaarifiwa kwamba katika siku ya saba hakuna mana yoyote ambayo ingeonekana (Kut. 16: 25-26). Kinachoshangaza sana ni hiki: Mana ambayo ingekusanywa katika kila moja ya siku zingine ingevunda usiku, lakini ile iliyokusanywa katika siku ya sita ingedumu kuwa tamu na salidi (Kut. 16:19–24). Katika siku ya saba baadhi ya watu wakatoka kwenda kondeni kutafuta mana wasione chochote (Kut. 16:27). Jibu la Mungu lilikuwa, “Mtakataa kuyashika maagizo Yangu na sheria Zangu hata lini?” (Kutoka 16:28) “Angalieni, kwa kuwa Bwana amewapa ninyi hiyo Sabato, kwa sababu hii huwapa siku ya sita chakula cha siku mbili; kaeni kila mtu mahali pake, mtu awaye yote asiondoke mahali pake kwa siku ya saba.” (Kutoka 16:29) Zingatia: Muundo huu wa maneno huwasilisha dokezo bayana kwamba tayari Sabato ilikuwa ikijulikana kwa Waisraeli.

Masomo Amali ya Sabato:

 • “Mungu anaagiza kwamba siku Yake takatifu itunzwe kwa heshima kuu sasa kama ilivyokuwa wakati wa Israeli. Amri waliyopewa Waebrania inapaswa kuchukuliwa na Wakristo wote kama agizo la Yehova kwao. Siku kabla ya Sabato inapaswa ifanywe kuwa siku ya maandalio, ili kila kitu kiwe tayari kwa ajili ya saa zake takatifu. Kwa namna yoyote ile shughuli zetu binafsi hazipaswi kuruhusiwa kuingilia saa takatifu. Mungu ameagiza kwamba wagonjwa na wanaoteseka wahudumiwe; kazi inayohitajika ili kuwafanya wajisikie kufarijika ni kazi ya rehema, na wala siyo uvunjaji wa Sabato; lakini kazi zote zisizo za lazima zinapasa kuepukwa. Watu wengi kwa uzembe huahirisha hadi mwanzo wa Sabato mambo madogomadogo ambayo wangeweza kufanya katika siku ya maandalio. Hali halipaswi kuwa hivyo. Kazi ambayo imepuuzwa hadi wakati wa kuanza kwa Sabato inapaswa ibaki bila kutendwa hadi Sabato ipite. Hatua hii inaweza kusaidia kumbukumbu za hawa wasiojali, na kuwafanya kuwa waangalifu ili kutenda kazi zao wenyewe katika siku sita za kazi.
 • “Kila juma wakati wa safari yao ndefu jangwani Waisraeli walishuhudia miujiza mitatu, iliyokusudiwa kushawishi akili zao kuhusu utakatifu wa Sabato: maradufu ya chakula ilimwagwa kwa siku ya sita, na hakikuwepo kabisa katika siku ya saba, na sehemu iliyohitajika kwa ajili ya Sabato ilihifadhiwa kuwa tamu na safi, wakati ambapo kama kiasi chochote kingetunzwa katika nyakati zingine kilioza na hakikufaa kutumika.
 • “Katika mazingira yanayohusiana na ukirimiwaji wa chakula hiki, tunapata ushahidi thabiti kwamba Sabato haikuanzishwa, kama wengi wanavyodai, wakati sheria ilitangazwa pale Sinai. Kabla Waisraeli hawajafika Sinai walitambua kuwa Sabato ilikuwa sharti la lazima juu yao. Kwa kutakiwa kukusanya kila siku ya Ijumaa mara mbili ya kiwango cha chakula chao cha kawaida katika kujiandaa na Sabato, ambapo kisingeanguka kabisa, hali ya utakatifu wa siku hiyo ya pumziko ilisisitizwa daima katika fikra zao. Na ilipotokea kwamba baadhi ya watu wametoka katika siku ya Sabato ili kukusanya chakula chao, Bwana aliuliza, “Mtakataa kuyashika maagizo Yangu na sheria Zangu hata lini?” (Patriarchs and Prophets, uk. 296–297).

[3] Sabato katika Kutoka 20:8–11.

“Ikumbuke siku ya Sabato uitakase. Siku sita fanya kazi, utende mambo yako yote; lakini siku ya saba ni Sabato ya Bwana, Mungu wako, siku hiyo usifanye kazi yoyote, wewe, wala mwana wako, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala mjakazi wako, wala mnyama wako wa kufuga, wala mgeni aliye ndani ya malango yako. Maana, kwa siku sita Bwana alifanya mbingu, na nchi, na bahari, na vyote vilivyomo, akastarehe siku ya saba; kwa hiyo Bwana akaibarikia siku ya Sabato akaitakasa.” (Kutoka 20:8–11)

“Kutoka 20 hubainisha Amri Kumi ambazo Mungu alimpatia Musa pale Sinai. Katika sheria hii, amri ya nne hupambanua kwamba kazi inapaswa kufanywa kwa siku sita na kwamba siku ya saba inapaswa kuadhimishwa kama siku ya pumziko. Msingi wa agizo hili ni kwamba “kwa siku sita Bwana alifanya mbingu, na nchi, na bahari, na vyote vilivyomo, akastarehe siku ya saba; kwa hiyo Bwana akaibarikia siku ya Sabato akaitakasa” (aya ya 11).

Lugha iliyotumiwa hapa ni muhtasari wa maudhui ya Mwanzo 2:2, 3, bila kuacha mashaka yoyote kwamba 20:11 hulenga kwenye Sabato ya uumbaji. Jambo muhimu pia ni kwamba amri ya Sabato huonekana ndani ya sheria ya amri kumi, ambayo ni kiini cha agano la Mungu. Kwamba sheria hii ya amri kumi ilikuwa bainifu, ilhali sheria zingine za Pentatuku zikiwa nyongeza au ufafanuzi, ni dhahiri kutokana na kauli katika Kumbukumbu 5:22 kwamba kwenye Amri Kumi hizi Mungu “wala hakuongeza neno”—yaani, Dekalojia ilikuwa mfumo kamili kwa yenyewe.

Zaidi, msingi wa agano unaobainishwa katika Kutoka 20 kwa ajili ya utunzaji wa Amri Kumi, ikiwa ni pamoja na amri ya Sabato, ni historia ya ukombozi, au kisahihi zaidi, ukombozi wa kiungu hasa. Wana wa Israeli walikuwa wamekuja katika uhusiano wa agano pamoja na Yehova (angalia Kut. 19). Kisha katika dibaji na utangulizi wa kihistoria wa Dekalojia, Mungu anatamka kipengele kikuu katika ukombozi ambao Waisraeli walikuwa wamepitia: “Mimi (Yehova) ni Bwana, Mungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa.” (Kut. 20:2). Waisraeli walikuwa wamekombolewa kutoka utumwani, na wema huu wa awali wa Yehova uliweka msingi kwa ajili ya uhusiano wa agano ambapo Waisraeli wangepaswa kuwa watii kwa amri za Mungu.

Nyakati fulani Sabato na dhana ya agano la Mungu kimsingi vilisawiana (linganisha Kut. 31:16). Zaidi ya yoyote miongoni mwa amri tisa ya Dekalojia, Sabato iliweka tofauti bayana inayowatenga watu wa Mungu mbali na yeyote na wote ambao hawakumtumikia Yehova. Hivyo kwa namna halisi sana imejumuishwa katika maana halisi ya uhusiano wa agano pamoja na Mungu, maana iliwatambulisha Israeli kama watu katika ushirika pamoja na Muumbaji na Mkombozi wao.

Zaidi ya hapo, amri ya Sabato ndiyo pekee kwenye Dekalojia yenye alama tatu za utofautishi za muhuri: jina, wadhifa, na himaya ya mhusika au mfumo wa yule ambaye mamlaka yake huwakilishwa na mhuri huo. Hivyo amri ya Sabato inaweza kuchukuliwa kama mhuri wa Dekalojia. (Angalia pia mjadala wa Sabato kama “ishara” kuhusiana na Kutoka 31:13–17 na Ezekieli 20:12, 20.) Amri ya Sabato ni bainifu siyo tu kuwa na vitu vitatu muhimu kwenye mhuri, bali pia kwa kutumia utangulizi wa pekee, neno “IKUMBUKE.” Neno hili linaweza kubeba dhana kadhaa: kuikumbuka Sabato kama taasisi ambayo tayari imepewa heshima ya wakati; kuikumbuka, kwa sababu inaweza kuwepo hatari ya kuisahau; na kuikumbuka kwa mtazamo ujao, kwa sababu Sabato ni kiini muhimu kwa uzoefu endelevu wa agano. Licha ya dhana yoyote ya kina ambayo neno hili linaweza kuwa nayo katika muktadha wa kauli ya awali pale Sinai, jambo moja ni hakika: neno “ikumbuke” ni msisitizo kama utangulizi hapa, na hutumika kutoa mwito maalumu kwenye amri ya Sabato.” [Raoul Dederen, Handbook of Seventh-Day Adventist Theology, Commentary Reference Series, electronic ed., (Hagerstown, MD: Review and Herald Publishing Association, 2001), 12:496].

[4] Sabato katika Kutoka 23:12.

Sheria za Sabato (Kutoka 23:10–19).

 • Sehemu ya mwisho ya sheria katika Kitabu cha Agano hubainisha sikukuu za kidini ambazo zingepaswa kuadhimishwa katika Israeli ya zamani. Hii ni kalenda salidi (takatifu) ya kale zaidi katika Biblia. Kizio cha msingi cha kalenda hii ni uadhimishaji wa Sabato ya kila juma (23:10–13). Kilichofungashwa na kujengwa kwenye Sabato ni sikukuu tatu za mahujaji za kitaifa ambazo Israeli ilipaswa kusherehekea kila mwaka.

23:10–11. ‘Utapanda mbegu katika nchi yako muda wa miaka sita na kuyavuna maongeo yake; lakini mwaka wa saba utaiacha nchi ipumzike na kutulia; hao maskini miongoni mwa watu wako wapate kula; na hicho watakachosaza wao, wapate kula wanyama wa kondeni. Utafanya vivyo katika shamba lako la mizabibu, na katika shamba lako la mizeituni.’

 • Hapa huanza ufafanuzi wa Musa wa Amri ya Nne, agizo la Sabato lipatikanalo katika Kutoka 20:8–11. Matumizi mojawapo ya agizo hilo ni kwamba Waebrania wanapaswa kuanzisha mfumo wa miaka saba wa kupumzisha ardhi katika suala la kilimo. Maelezo zaidi ya kina ya agizo hili yanapatikana katika Walawi 25:1–7, 18–22. Zipo sababu mbili za ardhi kupewa Sabato, kwa mujibu wa andiko hili: kwanza kabisa ni, hisanijamii, kiasi kwamba wale ambao hawakuwa na urithi au wahitaji waweze kupata chakula. Ni kile ambacho Kaufman hukiita ‘mfumo wa ustawi wa jamii kwa ajili ya maskini.’ Sheria ni kwa ajili pia ya manufaa ya uhaimwitu, kiasi kwamba wanyama wanaweza kupata chakula.
 • Haiwezekani kwamba Israeli yote ilisheherekea Sabato ya nchi katika mwaka uleule mmoja. Pengine kulikuwa na mzunguko ili ardhi fulani ipumzishwe kila mwaka, lakini sehemu nyingine kubwa ililimwa. Hivyo, maskini wangeweza kukusanya chakula kila mwaka, siyo tu mara moja katika miaka saba.

23:12. ‘Siku sita utafanya kazi yako, na siku ya saba utapumzika; ili kwamba ng’ombe wako na punda wako wapate kupumzika, kisha mwana wa mjakazi wako na mgeni wapate kuburudika.’

 • Wakati ambapo aya ya 10–11 ardhi inapewa pumziko kila miaka saba, jamii ya wanadamu imepewa pumziko la kila siku saba. Jambo kipindi cha wakati ni tofauti, mfumo wa Sabato ni uleule. Pamoja na hilo, makundi mawili yaliyofaidi pumziko la nchi, wahitaji na wanyama, hupata mishabihiano katika mtumishi na mgeni, kwa upande mmoja, na ng’ombe na punda, kwa upande mwingine, katika sheria ya sasa.
 • Kitenzi badala ya ‘kuacha’ katika Kiebrania ni shābat, ambapo hudahiliwa neno ‘Sabato.’ Hubeba dhana ya kukoma na kusitisha shughuli za kazi za kawaida na za kila siku. Wanadamu pia ‘wataburudishwa’ katika siku hii. Hicho ni kitenzi cha nadra katika Kiebrania (kilichotumiwa mara tatu tu). Katika Kutoka 31:17 Mungu anatajwa kwamba ‘alistarehe’ katika siku ya saba ya uumbaji kwa sababu ya pumziko Lake. Hivyo, kazi na pumziko la Mungu katika uumbaji hutumika kama kielelezo kwa ajili ya kazi na pumziko la mwanadamu kila juma.” [John D. Currid, A Study Commentary on Exodus: Exodus 19–40, EP Study Commentary, (Darlington, England; Carlisle, PA: Evangelical Press, 2001), 2:117–118].

[5] Sabato katika Kutoka 31:13–17.

Kisha, nena wewe na wana wa Israeli, na kuwaambia, Hakika mtazishika Sabato Zangu, kwa kuwa ni ishara kati ya Mimi na ninyi katika vizazi vyenu vyote; ili mpate kujua ya kuwa Mimi ndimi Bwana niwatakasaye ninyi. Basi mtaishika hiyo Sabato; kwa kuwa ni takatifu kwenu; kila mtu atakayeitia unajisi hakika yake atauawa; kwa kuwa kila mtu afanyaye kazi katika siku hiyo, nafsi hiyo itakatiliwa mbali na watu wake. Kazi itafanywa siku sita; lakini siku ya saba ni Sabato ya kustarehe kabisa, takatifu kwa Bwana; kila mtu atakayefanya kazi yo yote katika siku ya Sabato, hakika yake atauawa. Kwa ajili ya hayo wana wa Israeli wataishika Sabato, kuiangalia sana hiyo Sabato katika vizazi vyao vyote, ni agano la milele. Ni ishara kati ya mimi na wana wa Israeli milele; kwani kwa siku sita Bwana alifanya mbingu na nchi, akastarehe kwa siku ya saba na kupumzika.” (Kutoka 31:13–17)

 • Katika Kutoka 31:13–17 tunapata kauli sawa kabisa na zile katika Mwanzo 2:2–3 na Kutoka 20:11, ila pamoja na vipengele kadhaa vilivyoongezwa. 1. Utunzaji wa Sabato ya Mungu ni ishara, siyo tu ya Uumbaji (aya ya 17), bali pia ya kuwatakasa watu Wake (aya ya 13). 2. Uhusiano wa agano, mapema ilibainishwa katika muktadha wa Dekalojia (sura ya 19 na 20), sasa hutumiwa wazi kwenye Sabato na hutajwa kama “agano la milele” (aya ya 16). 3. Adhabu ya mauti inatamkwa dhidi ya unajisi wa Sabato (aya ya 14, 15). 4. Istilahi ya msisitizo šabbaṯ šabbāṯôn, “sabato ya pumziko makini,” hutumiwa kwa mara ya kwanza (aya ya 15). 5. Katika kurejelea Sabato ya Uumbaji, kauli husika huzungumzia siyo tu Mungu akipumzika, kama ilivyo katika Mwanzo 2:2, 3 na Kutoka 20:8–11, bali pia huongeza kwamba Mungu “alistarehe” (aya ya 17), bila shaka siyo kwa maana ya urejeshaji dhidi ya uchovu, bali kama burudiko zuri kufuatia, na kwa sababu ya, Mungu kukamilisha kazi Yake katika kuhuluku Uumbaji mkamilifu.
 • Matumizi ya neno “ishara” katika aya ya 13 ni bayana. Ishara ni kitu fulani kinacholenga mbali na chenyewe ili kudhihirisha uhalisia adhimu zaidi. Kuhusiana na Sabato, uhalisia huo ni wa namna mbili: Sabato hutupatia uhakikisho wa daima kuhusu Mungu kuwatakasa watu Wake(aya ya 13), na hutumika kama ukumbusho endelevu juu ya sifa ya Mungu wa Uumbaji (aya ya 17). Katika vipengele hivi viwili, utunzaji wa Sabato ndio unaoipatia ufanisi kama ishara (aya ya 13, 16). [Raoul Dederen, Handbook of Seventh-Day Adventist Theology, Commentary Reference Series, electronic ed., (Hagerstown, MD: Review and Herald Publishing Association, 2001), 12:497].
 • “Dokezo la mwisho kuhusu ujenzi wa maskani takatifu na sheria za kikuhani ni agizo linalohusiana na Sabato. Vyote hufikia kilele katika Sabato. Kama ambavyo Matthew Henry anadokeza, sababu ambapo vyote huishia hapa ni ‘kwa vile uadhimishaji wa Sabato kwa kweli ni upindo na ukingo wa sheria yote.’ Agizo la Sabato huonekana hapa pia kwa kusudi halisia zaidi: ili Waebrania wasijihusishe kujenga maskani katika siku ya Sabato ili kuikalimisha mapema. Ujenzi wa mahali pa ibada katika siku ya ibada ungekuwa dhambi kubwa.” [John D. Currid, A Study Commentary on Exodus: Exodus 19–40, EP Study Commentary, (Darlington, England; Carlisle, PA: Evangelical Press, 2001), 2:264].

[6] Sabato katika Kutoka 34:21

“Utafanya kazi siku sita, lakini katika siku ya saba utapumzika; wakati wa kulima mashamba, na wakati wa kuvuna pia, utapumzika (siku ya Sabato).” (Kutoka 34:21, AMP)

 • Nomino “Sabato” halijitokezi kwenye andiko hili, lakini “Sabato ya siku ya saba” huoneshwa wazi na kitenzi cha maneno mawili ya “kupumzika” ni šābaṯ.
 • Katika uchumi wa kilimo Sabato ilipaswa kutunza kwa uaminifu wakati majira mawili muhimu zaidi katika kazi: “wakati wa kulima” na “wakati wa mavuno.”
 • Hii husisitiza utakatifu mkuu ambao kwao Mungu alikuwa ameakifishia siku hii. Nyakati za kulima na zile za kuvuna yalikuwa majira ya majaribu makubwa zaidi katika kukiuka Sabato.

“Sheria ya Sabato sasa inahitimishwa kifupi (angalia maelezo ya ufafanuzi kuhusu Kut. 20:8–11 na 23:12). Majira mawili yanatajwa kwa namna mahususi kuhusu kukoma kwa kazi katika Sabato: ‘wakati wa kulima’ na ‘wakati wa mavuno. Hizi ni nyakati mbili za shughuli nyingi zaidi katika kalenda ya kilimo na, hivyo, hata huingia chini ya vizuizi vya sheria ya Sabato. Pamoja nayo, istilahi mbili husika zitumiwapo pamoja katika Agano la Kale ni nahau ya kalenda nzima ya mwaka (angalia Mwa. 45:6; 1 Sam. 8:12). Kufuatia hilo, Waebrania wanazuiwa kufanya kazi katika Sabato yoyote mwaka mzima. Hakuna simile.” [John D. Currid, A Study Commentary on Exodus: Exodus 19–40, EP Study Commentary, (Darlington, England; Carlisle, PA: Evangelical Press, 2001), 2:318].

[7] Sabato katika Kutoka 35:2-3

Kutoka 35:1–31 Musa akakutanisha mkutano wote wa wana wa Israeli, na kuwaambia, Maneno aliyoyausia Bwana ni haya, kwamba myafanye. 2 Fanyeni kazi siku sita, lakini siku ya saba itakuwa siku takatifu kwenu; ni Sabato ya kustarehe kabisa kwa Bwana; mtu awaye yote atakayefanya kazi yoyote katika siku hiyo atauawa. 3 Hamtawasha moto katika nyumba zenu kwa siku ya Sabato.”

 • Mkutano wote. Waisraeli sasa walikuwa tayari kuanza ujenzi na kusimika maskani iliyokuwa imepangwa (sura ya 25–31) but delayed because of their apostasy (sura ya 32; PP 343) na hitaji la kufanya upya agano (sura ya 33, 34). Kwa vile huu ulikuwa mradi ambapo watu wote kimsingi walikuwa na maslahi nao na walijihusisha nao kwa sababu ya sadaka zao (sura ya 25:2–7) na juhuzi zao (angalia sura ya 28:3; 35:10, 25; 36:4; 39:42), Mungu “aliwakusanya” “pamoja” kwa ajili ya maelekezo ya awali.
 • Siku sita. Waebrania walipaswa kuhusishwa katika shughuli takatifu na wasingepaswa kudhani kwamba hii ilikuwa simile ya kufanya kazi katika siku ya Sabato. Lakini hawakupaswa kuruhusu hali takatifu ya kazi yao kuwadanganya kiasi cha kupuuza uadhimishaji mtakatifu wa siku husika au kukanyaga muda wakati mtakatifu bila kujali. Hapa kuna somo makini kwa ajili ya wachungaji na wengine wafanyao kazi ya Mungu katika siku ya Bwana. Ujenzi wa maskani takatifu, pamoja na stadi na vifaa mbalimbali vilivyohitajika vilikuwa kazi ya kidunia, na hivyo haikuwa shughuli sahihi ya siku takatifu ya Mungu. [Francis D. Nichol, Ed., The Seventh-Day Adventist Bible Commentary, (Review and Herald Publishing Association, 1978), 1:679].

Sehemu mbili za kwanza za sura hii hujadili Maagizo ya Sabato (vv. 1-3) na Vifaa vya Maskani (vv. 4-19). “Kabla ya ujenzi hasa wa maskani kufanyika, Mungu anawasilisha maagizo mawili ya awali kupitia Musa. Ile ya kwanza inahusiana na Sabato, na ya pili inahusu michango inayohitajika kwa ajili ya mradi wa ujenzi.

Maagizo ya kujenga maskani yaliishia katika amri ya Sabato (angalia ufafanuzi katika Kut. 31:12–17). Sasa ujenzi halisi wa patakatifu huanza na amri ya Sabato. Kwa kweli, andiko la sasa ni, kwa sehemu kubwa, mrudio wa lile la 31:15. Hutumika kama himizo la dibaji: Waebrania hawaruhusiwi kufanya kazi siku ya Sabato, hata katika ujenzi wa maskani takatifu!

Nyongeza moja huonekana hapa ambayo haikuwepo katika agizo la awali. Waisraeli walizuiwa wasiwashe mioto katika ‘maskani yao’ katika siku ya Sabato. Nomino hii mara nyingi ina maana pana zaidi kuliko ‘nyumba’ tu—mara nyingi hutumiwa kuhusu ‘himaya/wilaya/maeneo ya makazi katika nchi’ (Mwa. 10:30; 27:39; Kut. 10:23). Na hivyo wazo la msingi ni kwamba Waebrania hawapawi kuwasha mioto katika mastakimu yao siku ya Sabato. Moto, kwa kweli, ulikuwa muhimu kwa kazi za aina mbalimbali zilizohusianana ujenzi wa maskani, kama vile shughuli za vyuma. Tena, Waebrania hawakuruhusiwa kufanya kazi ya ujenzi wa maskani siku ya Sabato.” [John D. Currid, A Study Commentary on Exodus: Exodus 19–40, EP Study Commentary, (Darlington, England; Carlisle, PA: Evangelical Press, 2001), 2:327–328].

MAANA YA KIIBADA: “Sabato hutuelekeza hapo awali kwenye ulimwengu kamilifu (Mwa. 1:31; 2:1–3), na hutukumbusha wakatiambapo Muumbaji kwa mara nyingine tena “atafanya yote kuwa mapya” (Ufu. 21:5). Pia ni ukumbusho kwamba Mungu yu tayari kurejesha ndani ya mioyo na maisha yetu sura Yake Mwenyewe kama ilivyokuwa hapo mwanzo (Mwa. 1:26, 27). Yule aingiaye katika utashi halisi wa uadhimishaji wa Sabato kwa jinsi hiyo atafuzu kupokea muhuri wa Mungu, ambao ni utambuzi wa kiungu kwamba tabia Yake imeakisiwa kikamilifu maishani (Eze. 20:20). Ni fursa yetu ya furaha mara moja kila juma kusahau kila kitu kinachotukumbusha juu ya ulimwengu huu wa dhambi na “kukumbuka” mambo yale yanayotuvuta kuja karibu na Mungu. Sabato kwetu inaweza kuwa patakatifu fulani katika jangwa la ulimwengu huu, ambapo kwa muda kitambo tunaweza kuwa huru dhidi ya shughuli zake na kuingia, kwa namna hiyo, katika furaha za mbinguni. Kama pumziko la Sabato lilitamanika kwa viumbe wasio na dhambi pale Paradiso (Mwa. 2:1–3), ni muhimu mara ngapi zaidi kwa halifa (watu wenye hali/asili ya kufa) wakosea wanaojiandaa kuingia tena katika maskani yaliyobarikiwa!” [Francis D. Nichol, Ed., The Seventh-Day Adventist Bible Commentary, (Review and Herald Publishing Association, 1978), 1:604].

HATUA YA MAAMUZI: Ni mwitikio gani unaodhani sura hii ingepaswa kutuhimiza kufanya? “Ikumbuke siku ya Sabato uitakase.”

[1] Tunapaswa kuifikiria Sabato kwa juma zima na kufanya maandalizi husika ili kuiadhimisha kwa jinsi impendezavyo Mungu.

[2] Kama jinsi ambavyo Mungu “alistarehe siku ya saba, akaacha kufanya kazi Yake yote aliyoifanya” (Mwa. 2:2), halikadhalika sisi tunapaswa kuwa na pumziko, na “kukoka” kufanya kazi yetu! Hatupaswi kujihusisha katika kazi ya kidunia isiyohitajika! Hatupaswi kujihusisha katika shughuli za kidunia katika siku ya Sabato.

[3] Siku ya Sabato haina budi kutumiwa katika tafakari ya kidinii, usomaji wa neno, ibada, huduma kwa Mungu, na matendo ya rehema/wema kwa wanadamu wenzetu (angalia Isa. 58).

 1. Kufungua vifungo vya uovu,
 2. Kutua mizigo mizito,
 3. Kuwaweka huru walioteswa,
 4. Kuvunja kila nira ya utumwa, mateso, nk,
 5. Kumgawia mkate wako mtu mwenye njaa,
 6. Kumletea nyumbani mwako maskini aliyetengwa,
 7. Kumvika aliye uchi,
 8. Kuwahudumia wagonjwa, waliojeruhiwa, na walemavu, nk,
 9. Kuwatembelea yatima na wajane katika taabu yao (Yakobo 1:27).

Zingatia: Mambo haya hayana budi kufanywa siyo tu katika Sabato, bali saa zote, 24/7.

[4] Sabato pia hutupatia fursa ya pumziko la kimwili. Kipengele hiki cha Sabato kina umuhimu wa pekee kwa mwanadamu katika hali yake ya dhambi, ambapo lazima ajipatie riziki yake kwa jasho la uso wake (Mwa. 3:17–19).

Sabato ni msawazishaji mkuu, mwekaji huru dhidi ya vitowianifu katika muundo wa kijamii. Zingatia kauli ya katazo katika amri hii: lazima wote wakome kufanya kazi yoyote katika siku ya Sabato: “wewe, wala mwana wako, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala mjakazi wako.” Hata wanyama wa kufuga, pamoja na wageni wowote nyumbani, wanajumuishwa (Kut. 20:8-11). Wapendwa, Mungu humaanisha asemacho; ana anasema anachomaanisha! Wengi wamekosa baraka za kiungu kwa kutotii amri ya Sabato.

Wazo moja zaidi: Yesu (aliye Mwasisi wa Sabato) alipumzika katika Sabato hata wakati wa mauti Yake! (angalia Mat 27:57-61; Luka 23:50-56)

Naye [Yusufu wa Arimathaya] akanunua sanda ya kitani, akamtelemsha, akamfungia ile sanda, akamweka katika kaburi lililochongwa mwambani; akavingirisha jiwe mbele ya mlango wa kaburi (Marko 15:46).

“Hatimaye Yesu alikuwa katika pumziko. Siku ndefu ya fedheha na mateso ilikuwa imeisha. Kadiri miali ya mwili ya jua la machweo iliposindikiza Sabato, Mwana wa Mungu alilala kwa utulivu kwenye kaburi la Yusufu. Kazi Yake ikiwa imemalizika, mikono Yake ikiwa imekunjwa kwa amani, alipumzika katika nyakati takatifu za siku ya Sabato…. Sasa Yesu alipumzika dhidi ya kazi ya ukombozi; na japo yalikuwepo majonzi miongoni mwa wale waliompenda duniani, hata hivyo ilikuwepo furaha mbinguni.” (The Desire of Ages, uk. 769).

SHAUKU YANGU LEO. Chagua Kisanduku kinachoakiasi uamuzi wako leo:

 • Nataka kujifunza zaidi kuhusu Sabato
 •  Nataka kuwashirikisha wengine ukweli kuhus Sabato
 • Nataka kushika amri zote za Mungu, ikiwa ni pamoja na Sabato
 • Ni shauku yangu ya kumtii Bwana kwa kuidumisha Siku Yake (Sabato ya siku ya saba) kuwa takatifu, Kut. 20:8.

Moreover, also I gave them My Sabbaths to be a sign between Me and them, that they might understand and realize that I am the Lord who sanctifies them [niwatengaye na kuwaweka kando].” (Ezekieli 20:12, AMP)

Sauti ya Injili/ Mwongozo wa Kujifunza Biblia/ Mafundisho Makuu/ Sabato ya siku ya saba/ Somo # 4.