Zaburi 140: Mwongozo wa Biblia.

MWONGOZO WA IBADA.

Mwongozo wa Ibada unaoshabihiana na Mpango wa Usomaji wa Biblia wa leo: Zaburi 140/ Ee Bwana, uniokoe na mtu mbaya /19-BSG-139A, (Zaburi 140:1-13)/ Wimbo: Njiani huniongoza Yesu wangu Mwokozi (NK # 155)

UCHUNGUZI: Kashfa ni dhambi na imekatazwa katika Biblia (Soma Yer. 9:4-6; Ezekieli 22:9; Mk. 7:21-23; Mt. 15:19-20; Rumi 1:29-31; 2 Kor. 12:20; 2 Tim 3:2-4)

TAFAKARI: Zab. 140 ni sala kwa ajili ya kuokolewa toka kwa maadui wa vurugu na hila (2-4); kwa ajili ya hifadhi dhidi ya mitego yao waliyoweka (5-6). Hapa tunaona onyesho la imani ya mtunga zaburi katika Bwana: Yeye hatampa asiye haki tamaa zake, wala kufanikisha hila zake. Daudi anasihi kwamba hila mbaya za waovu zisitimizwe, (7-8).  Ana imani kwamba hukumu ya Mungu itawashinda waovu (9-11), na kwamba kusudi la wenye haki litathibitishwa (12-13).

“Zaburi hii iliandikwa na David wakati akikabiliwa vikali na maadui wengi. Hawa wapinzani walidhamiria kumuangamiza; hawangeweza kustahimili kwamba mwana wa Yese anapaswa kuwa na upendeleo kwa Mungu, na kwamba atakuja kwenye kiti cha enzi; basi wakawa wanaweka vikwazo, na kashfa za kila namna. Walifasiri vibaya matendo yake, waliwakilisha vibaya nia yake; walitema sumu mbaya toka katika vinywa vyao, na wakati huo huo, walisema wao kwa wao, “endapo tutaweza kumwongoza kutenda mabaya, kama tunaweza, kwa namna moja au nyingine, kwa kumtega katika hotuba yake, au katika tabia yake binafsi, au katika vitendo vyake vya umma, basi tutakuwa na silaha ambayo kwayo tunaweza kumpiga.” [C. H. Spurgeon, The Metropolitan Tabernacle Pulpit Sermons, 1897, 43, 349].

MAANA YA KIIBADA: Nini cha kufanya wakati unakabiliwa na kashfa, majeshi ya uovu, watu wenye vurugu, na watoao sumu katika ndimi zao? [1] Mlilie Bwana ili akukomboe. Yeyey huweza kukulinda toka katika mikono ya waovu na mipango yao miovu (Zab. 140:1-5). [2] amalilie Bwana akurehemu (Zab. 140:6-8). [3] Omba uovu dhidi yako na vurugu zote za maadui zisimamishwe na kupatiwa haki (Zab. 140:9 – 11). [4] Kuwa na imani katika ukombozi wa Mungu (Zab. 140:12-13).

Wapendwa, tunaweza kumwamini Mungu kuwa atahukumu kwa haki na hatimaye kulipa/ kuadhibu kila udhalimu. Je, tunapaswa kuomba hukumu ya Mungu iwaangukie wenye dhambi, (Zab. 140:10)? Je, ni haki kuomba kulipiza kisasi, (Zab 58:6-8)? La Hasha! Sikiliza mpendwa, Uchungu au moyo usio samehe waweza kuharibu roho zetu (Mt. 6:14 – 15; Ebr 12:14 – 15). Badala yake, tunapaswa kuwa huru na hisia kama hizo na hata kujaribu kupenda na kuomba kwa ajili ya maadui zetu. Je unakumbuka maelekezo ambayo Kristo alitupatia? “Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi, ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni” (Mt. 5:44-45).

SAUTI YA INJILI: Kipengele hiki kimeandikwa kana kwamba Mungu ndiye anaongea nawe moja kwa moja —kwa sababu hufanya hivyo. Bwana ananiambia nini asubuhi ya leo? Mwanangu, Mimi ndiye kimbilio lako. “Nitakulinda na mikono ya mtu asiye haki; na kukuhifadhi na mtu wa jeuri” (Zaburi 140:4). Hauna sababu yoyote ya kuogopa. Ndiyo, wakati mwingine, utapitia majaribu mazito; utazungukwa na waovu, lakini unapaswa kufahamu hili: Mimi nitakuwa pamoja nawe. Niamini Mimi na tii sheria Zangu.

SHAUKU YANGU LEO: Nataka kutoa shukrani kwa Jina Takatifu la Mungu; na kuishi katika uwepo Wake (Zab. 140:13).

Uwe Na Siku Yenye Baraka: “Tazama, Mungu ndiye wokovu wangu; Nitatumaini wala sitaogopa; Maana Bwana YEHOVA ni nguvu zangu na wimbo wangu; Naye amekuwa wokovu wangu.” (Isaya 12:2)

Sauti ya Injili/ Mwongozo wa Biblia/ Zaburi 1-150/ 19-BSG-139 (Zaburi 139)/ 21 Juni, 2020.