Zaburi 139: Mwongozo wa Biblia

Zaburi 139: Mwongozo wa Ibada

Mwongozo wa Ibada unaoshabihiana na Mpango wa Usomaji wa Biblia wa leo: Zaburi 139/ Maarifa, Kudura, na Uwepo wa Mungu /19-BSG-139A, (Zaburi 139:1-24)/ Wimbo: Muumbaji Mfalme, vitu vyote Vyako (NK # 9)

UCHUNGUZI: Nguvu isiyo na kikomo ya Mungu (soma Mwa. 17:1; 18:14; 1 Nya. 29:11; 2 Nya. 20:6; Ayubu 9:12; 42:2; Isa 40:12; 43:13; Yer 32:17-19, 27; Ufunuo 1:8; 11:17; 19:6)

TAFAKARI: Mada ya Zaburi 139 ni Maarifa yasiyopimika, Kudura, na Uwepo wa Mungu. Kwanza, Maarifa Yake yasiyochunguzika. Mungu anajua kila kitu kuhusu sisi: kile tunachofanya (Zab. 139:1-3); kile tunachofikiri (Zab. 139:2), na kile tunachosema (Zab. 139:4-6).

Pili, Uwepo Wake. Mungu ana uwezo wa kuwa “kila mahali” kwa wakati mmoja. Wapendwa, Mungu anauwezo wa kuwa – katika pembe nne za nchi (Uf. 7:1)— kwa wakati mmoja. Basi aishangazi kugundua kwamba Yeye huweza kusikia sala, maombi, na dua zote (katika wakati halisi) na kuyajibu ipasavyo. Yeye yu kila mahali — Yuko juu mbinguni (Zab. 139:7-8); Yu kuzimu (Zab. 139:8); Anaweza kupatikana hata katika “pande za mwisho za bahari” (Zab 139:9-10); Giza na Nuru, vyote ni sawasawa mbele Zake (Zab 139:11-12), hakuna sehemu yoyote tunayoweza kujificha asituone. Je unakumbuka kisa cha Yona cha kujificha? Hatima yake ilikuwa nini?

Tatu, Mungu ni Muweza wa Yote: Yeye hutujua kabla hatujazaliwa; Yeye hutunga na hupangilia miili yetu michanga ndani ya tumbo za mama zetu (Zab. 139:13-15); Yeye hujua ratiba ya kila siku katika uhai/ maisha yetu — kabla hatujazaliwa (139:16); Yeye hutunza kikamilifu kumbukumbu za maisha yetu ya kila siku katika kitabu Chake (Zab. 139:16); Yeye hufikiria mipango ya ajabu na “fikira Zake zina thamani nyingi sana kwetu” (Zab. 139:17-18).

MAANA YA KIIBADA: Kuna masomo mengi sana katika Zaburi hii, lakini mambo makuu ni haya: Kuwa na Ufahamu—Mungu anakujua kwa undani sana (aya. 1-6); Kumbuka hili— Huwezi kuepuka au kujificha kutoka kwenye uwepo wa Mungu (aya. 7-12); Kuwa na Shukrani — Mungu alikuumba, kuwa mnyenyekevu mbele Zake (aya. 13-18); Kuwa Macho — ondoka/ kimbia toka kwa jamii ya waovu (aya. 19-22); Kuwa na Toba — Mlilie Bwana akuchunguze, aujue moyo wako; akujaribu, ayajue mawazo yako (aya. 23-24). Katika kitabu cha Waebrania, tunakumbushwa kuweka kando “kila mzigo mzito, na dhambi ile ituzingayo kwa upesi” (Ebr. 12:1-2). Aya mbili za mwisho zinajikita kwenye uchunguzi wa kina wa kiungu; ni kama sampuli ndogo ya mgonjwa (damu) inavyowekwa chini ya hadubini (katika maabara) kabla ya daktari kuweza kuagiza tiba bora iwezekanayo kutibu mgonjwa/ ugonjwa husika. Wapendwa habari njema ni hii: Tiba tayari inapatikana, nayo ni hii– “damu ya Yesu Kristo.” Je, uko tayari kuingia katika maabara ya kiungu ili uchunguzwe na kutua mzigo wako wa dhambi? Natumai utafanya hivyo (Isa. 1:18).

SAUTI YA INJILI: Kipengele hiki kimeandikwa kana kwamba Mungu ndiye anaongea nawe moja kwa moja —kwa sababu hufanya hivyo. Bwana ananiambia nini asubuhi ya leo? Mwanangu, kama kuna fundisho lolote hapa, Zaburi hii inapaswa kukufundisha/ kukukumbusha Mimi ni nani. Mimi ni BWANA MUNGU wako, Muumba wa Mbingu na Nchi, ikimaanisha nimekuumba wewe. Je, upo tayari kuwa mnyenyekevu, mtiifu, kuniita Mimi, na kunitegemea kwa mambo yako yote? Sikiliza ahadi hii: “Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho” (Yeremia 29:11-12).

SHAUKU YANGU LEO: Nataka kutambua dhambi zote (tabia za uovu) katika maisha yangu; Nataka kukiri na kupeleka dhambi hizo kwa Bwana; Nakata shauri kumtegemea Bwana ili Yeye ndiye aongoze maisha yangu; mwisho, nataka kumsihi Bwana “aniongoze katika njia ya milele,” Amina.

Uwe Na Siku Yenye Baraka: “Ee Mungu, unichunguze, uujue moyo wangu, Unijaribu, uyajue mawazo yangu; Uone kama iko njia iletayo majuto ndani yangu, Ukaniongoze katika njia ya milele.” (Zab. 139:23-24).

Sauti ya Injili/ Mwongozo wa Biblia/ Zaburi 1-150/ 19-BSG-139 (Zaburi 139)/ 20 Juni, 2020.