Zaburi 137: Mwongozo wa Biblia.

MWONGOZO WA IBADA.

Mwongozo wa Ibada unaoshabihiana na Mpango wa Usomaji wa Biblia wa leo: Zaburi 137/ Neno Kuu: “Shauku ya Sayuni katika nchi ya Ugeni”/ 19-BSG-137A: (Zaburi 137:1-9)/ Wimbo: “Niimbe Pendo Lake” (NZK # 31)

UCHUNGUZI: Watu wa Yuda wapelekwa uhamishoni Babeli (angalia 1 Nya. 9:1; 2 Nya. 36:1-21; Zab 137:1-9; Dan 1:1-7)

TAFAKARI: “Zab. 137 imeitwa Wimbo wa Mateka. Huonesha Waisraeli katika nchi ya uhamisho. Waimbaji wao mashuhuri wapo kimya, mabwana  wao wanawakejeli, wakitaka wapige matari yao na kuimba moja ya nyimbo za Sayuni. Mioyo ya wafungwa ni nzito. Dokezo la wazi katika Zaburi hii ni ule ambao kamwe haushindwi kutoa huruma ya msomaji kwa wafungwa wenye shida na wenye kuvunjika mioyo.” (SDA BC 3:922). Sura hii ina sehemu tatu tofauti: kuomboleza hali ya uhamisho, (aya. 1-4); furaha juu ya Yerusalemu (aya. 5-6); mwisho, wito wa hukumu ya Mungu juu ya Babeli, (aya. 7-9).

MAANA YA IBADA: “Waisraeli walikuwa wameweka matumaini yao juu ya ukuu wa kilimwengu. Toka wakati wa kuwasili kwao katika nchi ya Kanaani, waliondoka kwenye amri za Mungu, na kufuata njia za mataifa. Ilikuwa kazi bure kwamba Mungu aliwatumia maonyo kwa manabii Wake. Walipata mateso ya ukandamizwaji na udhalilishwaji wa taifa lisilomjua Mungu.” (The Desire of Ages, p. 28).

SAUTI YA INJILI: Sehemu hii imeandikwa kana kwamba Mungu anaongea moja kwa moja nawe—kwa sababu hufanya hivyo. Je, Bwana ananiambia nini asubuhi ya leo? Mwanangu, endapo utadumu kuwa mwaminifu Kwangu; endapo utatembea na Mimi kama Henoko alivyotembea, basi Mimi nitakamilisha lengo Langu katika maisha yako: “Kama mkikubali na kutii mtakula mema ya nchi; bali kama mkikataa na kuasi mtaangamizwa kwa upanga; maana kinywa cha Bwana kimenena haya.” (Isaya 1:19-20)

SHAUKU YANGU LEO: Ninataka kuwa mtiifu, mfuasi mwaminifu wa Yesu Kristo, na kujifunza kutokana na makosa ya watu wa Yuda. Ninataka kutubu dhambi zangu zote na kumwomba Bwana anisafishe, na kunitumia kwa huduma Yake.

Iweni na Siku yenye Baraka: “Na masikio yako yatasikia neno nyuma yako, likisema, “Njia ni hii, ifuateni;” mgeukapo kwenda mkono wa kulia, na mgeukapo kwenda mkono wa kushoto.” (Isaya 30:21)