Sabato katika Mwanzo.

SABATO KATIKA MWANZO

Mwongozo wa Kujifunza Biblia/ Siku Iliyosahauliwa: Sabato ya Siku ya Saba/ 86-003 (Mwanzo 2:1–3)/ Andiko Msingi:Basi mbingu na nchi zikamalizika, na jeshi lake lote. Na siku ya saba Mungu alimaliza kazi Yake yote aliyoifanya; akastarehe siku ya saba, akaacha kufanya kazi Yake yote aliyoifanya. Mungu akaibarikia siku ya saba, akaitakasa kwa sababu katika siku hiyo Mungu alistarehe, akaacha kufanya kazi Yake yote aliyoiumba na kuifanya.” (Mwanzo 2:1–3)

Malengo ya Somo: Kuchanganua maandiko kuhusu Sabato katika mfululizo yanavyojitokeza katika Pentatuku. Leo, tutaenda kuzingatia Sabato katika Mwanzo, kisha, tutaona katika Kutoka, Walawi, Hesabu, na Kumbukumbu la Torati..

Rejea za Sabato katika Pentatuku:

 1. Sabato katika Mwanzo 2:1-3.
 2. Sabato katika Kutoka 5:5.
 3. Sabato katika Kutoka 16.
 4. Sabato katika Kutoka 20:8–11.
 5. Sabato katika Kutoka 23:12.
 6. Sabato katika Kutoka 31:13–17.
 7. Sabato katika Walawi 19:3, 30; 26:2.
 8. Sabato katika Walawi 25:2–6.
 9. Sabato katika Hesabu 15:32–36.
 10. Sabato katika Hesabu 28:9-10.
 11. Sabato katika Kumbukumbu 5:12–15.

Maelezo ya Ufunguzi.: Mojawapo ya kweli za kina zaidi kwenye Biblia ni kwamba pale Edeni, katika ulimwengu mkamilifu ulioumbwa na Mungu mkamilifu, “siku ya saba” ilitengwa mbali na siku zingine za juma na kufanywa kuwatakatifu. Huo ndio umbali wa kale, na jinsi gani Sabato ya siku ya saba ilivyo ya msingi. Kutokana na mtazamo wa ulimwengu huu, huwezi kwenda mbali zaidi ya hapo. Hivyo basi, katika Sabato tunashughulika na mojawapo ya kweli za kibibilia za asili na msingi zaidi.

MASWALI NA MAJIBU

[1] Sabato iliasisiwa na nani? Sabato iliasisiwa na Mungu Muumbaji. “Maana, kwa siku sita Bwana alifanya mbingu, na nchi, na bahari, na vyote vilivyomo, akastarehe siku ya saba; kwa hiyo Bwana akaibarikia siku ya Sabato akaitakasa.” (Kutoka 20:11)

[2] Kwa mujibu wa Biblia, nani aliyeumba vitu vyote? Yesu Kristo.

 • Waebrania 1:1–21 Mungu, ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi, 2 mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika Mwana, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa Yeye aliufanya ulimwengu.
 • Yohana 1:1–3 1 Hapo mwanzo alikuwepo Neno, Naye Neno alikuwa kwa Mungu, Naye Neno alikuwa Mungu. 2 Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu. 3 Vyote vilifanyika kwa Huyo; wala pasipo Yeye hakikufanyika chochote kilichofanyika.
 • Wakolosai 1:16–1716 Kwa kuwa katika Yeye vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na vilivyo juu ya nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana; ikiwa ni vitu vya enzi, au usultani, au enzi, au mamlaka; vitu vyote viliumbwa kwa njia Yake, na kwa ajili Yake. 17 Naye amekuwako kabla ya vitu vyote, na vitu vyote hushikana katika Yeye.

[3] Nani, basi, aliyeasisi Sabato? Yesu Kristo. Kwa vile vitu vyote viliumbwa na Kristo, lazima Sabato nayo iliasisiwa na Kristo.

[4] Je wakati gani Sabato iliasisiwa? Sabato iliasisiwa wakati wa uumbaji (Angalia Mwa. 2:1-3; Kut. 20:11). “Wakati ule misingi ya dunia ilipowekwa, wakati ule nyota za asubuhi zilipoimba pamoja kwa furaha, na wana wote wa Mungu walipopaza sauti kwa furaha, hapo ndipo ulipowekwa msingi wa Sabato. Ayubu 38:6, 7; Mwanzo 2:1–3. Ni sahihi taasisi hii iweze kudai ustahivu wetu; iliasisiwa bila mamlaka yoyote ya mwanadamu na haikujengwa katika mapokeo yoyote ya kibinadamu; ilianzishwa na Mzee wa Siku na kuamriwa kwa neno Lake la milele.” (The Great Controversy between Christ and Satan, uk. 455).

[5] Zingatia mara ngapi kirai “siku ya saba” kimerudiwa katika Mwanzo 2:1–3. Je kuna uwezekano wa umuhimu gani wa mrudio huo?

Basi mbingu na nchi zikamalizika, na jeshi lake lote. Na siku ya saba Mungu alimaliza kazi Yake yote aliyoifanya; akastarehe siku ya saba, akaacha kufanya kazi Yake yote aliyoifanya. Mungu akaibarikia siku ya saba, akaitakasa kwa sababu katika siku hiyo Mungu alistarehe, akaacha kufanya kazi Yake yote aliyoiumba na kuifanya.” (Mwanzo 2:1–3).

Katika Mwanzo 2:1–3 “siku ya saba” imetajwa mara tatu. Hii husisitiza hali ya pekee sana ya Sabato ya siku ya saba na kwa namna bayana huitenga mbali na siku zingine za juma.

Kisahihi Wenham anadadavua kwamba “kutajwa mara tatu kwa siku ya saba, kila wakati katika sentensi ya maneno saba ya Kiebrania, huvutia usikivu kwenye silika mahususi ya Sabato. Kwa jinsi hii muundo na maudhui husisitiza upekee wa siku ya saba.” (Wenham, Genesis, vol. 1 of Word Biblical Commentary, 7).

Zingatia: Kutajwa mara tatu kwa ‘siku ya saba’ kunapaswa daima kutukumbusha kwamba Mungu hakuifanya siku ya kwanza kuwa siku maalum ya juma (kama wadaivyo wengine) au siku nyingineyo. Baraka maalum ni kwa ajili ya ‘siku ya saba’ na wala siyo nyingineyo.

[6] Je hatua gani ya kwanza iliyofanywa katika kuiasisi Sabato? Kupumzika katika siku ya saba ya kwanza ya wakati (Mwa. 2:1-3).

Kitenzi “akapumzika,” shabath, kimsingi humaanisha “kukoma” kazi au shughuli (angalia Mwa. 8:22; Ayubu 32:1; nk.). Kama ambavyo mjenzi mwanadamu akamilishavyo kazi yake baada ya kusanifu katika ubora wake, na hivyo hukoma kuendelea kuiboresha, halikadhalika katika dhana ya juu zaidi Mungu alikamilisha uumbaji wa ulimwengu kwa kukoma kusanifu chochote kipya, kisha ‘akapumzika.’ Mungu hakupumzika kwa sababu alikuwa anahitaji kufanya hivyo (angalia Isa. 40:28). Kwa hiyo, pumziko la Mungu halikutokana na uchovu wala mavune, bali kukoma kufanya shughuli ya awali.” (SDA BC 1:220).

[7] Je siku ya saba ilikuwa siku ya pumziko ya nani na kwa nini? Siku ya pumziko ya Bwana. “Kwa maana Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa Sabato.” (Mathayo 12:8) “Basi Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa Sabato pia.” (Marko 2:28)

Sabato hutumika pia kama siku ya kuzaliwa ya jamii ya wanadamu, sawa na vile siku ambapo kila mmoja wetu alizaliwa huwa siku yake ya kuzaliwa.

Zingatia: Japo mwanadamu aliumbwa katika siku ya sita, mara tu baada ya siku hiyo, Sabato ikawadia, hivyo Sabato huanza wakati wa machweo Ijumaa (siku ya sita inapoisha), hadi machweo Jumamosi (siku ya saba). Angalia Nehemia 13:19.

“Mungu akaiita nuru Mchana, na giza akaliita Usiku. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku moja.” (Mwanzo 1:5)

Kauli halisi “ikawa jioni (pamoja na saa zilizofuatia za usiku hiyo), ikawa asubuhi (pamoja na saa zilizofuatia za usiku hiyo), siku moja” ni bayana kwamba ni maelezo juu ya siku ya kinajimu, yaani, siku yenye kipindi cha saa 24. Ni sawa na muundo changamani “jioni na asubuhi” ya Kiebrania inayokuja baadaye katika Dan. 8:14, ambao toleo la KJV umefasiri kama “siku,” hapa ukimaanisha siku za kinabii, na ule wa neno la Kiyunani la Paulo, nuchthemeron, lifasiriwalo kama “kuchwa kucha” (2 Kor. 11:25). Hivyo Waebrania, ambao kamwe hawakutilia mashaka maana ya maneno haya, waliinza siku wakati wa machweo na kuimaliza katika kipindi kilichofuata cha machweo (Law. 23:32; Kumb. 16:6). Zaidi sana, lugha ya amri ya nne haiachi uvuli wowote wa mashaka kwamba jioni na asubuhi ya rekodi ya uumbaji ni vipengele vijenzi vya siku ya kidunia. [Francis D. Nichol, Ed., The Seventh-Day Adventist Bible Commentary, (Review and Herald Publishing Association, 1978), 1:210].

Kwa Kielelezo: Mtu anapozaliwa katika siku fulani, siku hiyo huwa siku yake ya kuzaliwa. Hivyo, Mungu alipopumzika katika siku ya saba, siku hiyo ikawa siku Yake ya pumziko au siku ya Sabato. Hivyo, lazima daima siku ya saba iwe siku ya Mungu ya Sabato. Je unaweza kubadili siku yako ya kuzaliwa kutoka siku uliyozaliwa kwenda siku nyingineyo? Hapana. Halikadhalika huwezi kubadili siku ya Mungu ya pumziko kwenda katika siku ambayo hakupumzika.

Hivyo siku ya saba bado ingali siku ya Sabato ya Mungu. Katika Ezekieli 20:12, Bwana hudai siku hii kuwa Yake: “Tena naliwapa Sabato Zangu.” Katika Kut. 31:13, Yehova anasema “Hakika mtazishika Sabato Zangu.”

Wazo la Msingi ni Hili: Wapendwa, Sabato ya siku ya saba siyo siku yako, hapana! Ni siku ya Bwana. Huwezi kuachana nayo kama upendavyo. Huwezi kuthubutu kuhoji utakatifu wake, wala kuubadili. Kufanya hivyo kutakusababishia ghadhabu ya Mungu, hukumu, na adhabu kali (linganisha Ebr. 10:26-29)

Kwa Usomaji Zaidi: Angalia lugha iliyotumiwa katika maandiko yafuatayo — (Kut. 16:29; 20:8-11; 31:13; 35:2; Law. 23:3, 24, 32, 39; 25:4; Kumb. 5:12-15; Neh. 9:14; Isa. 58:13; Marko 2:27-28; Eze. 20:20)

[8] Ni hatua gani ya pili katika kuasisi Sabato? Na hilo lilifanyia nini Sabato? Kuibariki, yaani, kuiheshimu siku hiyo na kuifanya iwe takatifu zaidi ya siku zinginezo (Mwa. 2:3; Kut. 20:11).

Mwanzo 2:3 hudai kwamba Muumbaji “akaibariki” siku ya saba, kama ambavyo alikuwa amewabariki wanyama na mwanadamu katika siku iliyoitangulia (Mwa. 1:22, 28). Mungu hurejelea baraka hii ya Sabato katika amri ya nne ya Dekalojia, daima ikiunganisha Sabato ya uumbaji na Sabato ya kila juma.

[9] Je Sabato iliasisiwa kwa ajili ya jamii yote ya wanadamu au Wayahudi pekee? Neno “mwanadamu” katika Marko 2:27 kwa Kiyunani ni anthrōpos, ambalo kimsingi humaanisha, “mtu,” istilahi jenasi inayojumuisha wanaume, wanawake, na watoto (angalia katika Marko 6:44). “Jamii ya wanadamu” huakisi maana ya anthrōpos kwa usahihi zaidi. Sabato ilikusudiwa na kuakidhishwa na Muumbaji mwenye upendo kwa ajili ya ustawi wa mwanadamu: wanadamu wote, siyo Wayahudi tu.

“Kitendo hiki cha kuibariki siku ya saba na kuitangaza kuwa takatifu kilifanyika kwa maslahi ya jamii ya wanadamu, ambao siku ya Sabato iliasisiwa kwa faida yao. Sabato ya siku ya saba ya kila juma mara nyingi imetambulika kama taasisi ya zama za Kiyahudi, lakini Rekodi Iliyovuviwa huibainisha kuwa iliasisiwa zaidi ya milenia mbili kabla ya kuzaliwa Mwisraeli wa kwanza (mzao wa Yakobo-Israeli). Zaidi ya hapo tuna maneno ya Yesu yakidai, “Sabato ilifanyika kwa ajili ya mwanadamu” (Mark 2:27), ambayo huonesha wazi kwamba taasisi hii haikuakidhishwa kwa ajili ya Wayahudi pekee bali jamii yote ya wanadamu pia.” (The Seventh-Day Adventist Bible Commentary, 1:221).

[10] Ipi hatua ya nne katika uasisi wa Sabato, na ilikuwa na maana gani? Utakasaji wa siku ya saba; yaani, kuitenga kwa kusudi takatifu, au kuamuru itakaswe (Mwa. 2:1-3; Kut. 20:11).

“Kitendo cha utakaso kilijumuisha kuitangaza siku hiyo kuwa takatifu, au kuwa imetengwa kwa makusudi matakatifu. Kama ilivyokuwa hapo baadaye Mlimani Sinai ilipotakaswa (Kut. 19:23), au, kwa muda huo, kuvishwa utakatifu kama makao ya Mungu, na kama Haruni na wanawe walivyotakaswa, au kutaufishwa, kwenye wadhifa wa kikuhani (Kut. 29:44), na kama vile mwaka wa jubilii ulivyotakaswa, au kusabilishwa, kwa kusudi la dini (Law. 25:10), halikadhalika hapa siku ya saba ilitakaswa, na kwa jinsi hiyo kutangazwa kuwa siku takatifu.” (The Seventh-Day Adventist Bible Commentary, 1:220–221).

[11] Ni zipi miongoni mwa hatua hizi zilifanya siku ya saba kuwa Sabato? Kitendo cha Mungu kupumzika katika siku ya saba kiliifanya kuwa Sabato, maana tayari ilikuwa Sabato hapo alipoibariki; hivyo kila siku ya saba imekuwa Sabato ya Bwana tangu uumbaji.

[12] Ni sababu ipi pekee ambayo Mungu amewahi kubainisha kwa ajili ya kuibariki na kuitakasa Sabato? Alipumzika katika siku hiyo, na kwa vile alipumzika katika siku hiyo wakati wa uumbaji, lazima basi kwamba aliibariki na kuitakasa wakati wa uumbaji pale pumziko lilipomalizika; hivyo Sabato iliasisiwa wakati wa uumbaji.

[13] Ni vidokezo gani huthibitisha kwamba Muumbaji, Yesu Kristo, ndiye aliasisi Sabato? Sabato inaitwa “Sabato ya Bwana” (Ex. 20:10); “Sabato Zangu” (Kut. 31:13); “Siku Yangu takatifu” (Isaya 58:13); “Mwana wa Adamu ni Bwana wa Sabato” (Mark 2:28).

[14] Je ingetajwa kwa jina gani endapo ingeasisiwa na mtu fulani? Kama Sabato ingeasisiwa na mtu au watu au taifa fulani, basi ingebeba jina la mwasisi husika. Lakini kwa vile iliasisiwa na Muumbaji, hubeba sahihi na cheo Chake.

MAANA YA KIIBADA: “Ikumbuke siku ya Sabato uitakase. Siku sita fanya kazi, utende mambo yako yote; lakini siku ya saba ni Sabato ya Bwana, Mungu wako, siku hiyo usifanye kazi yoyote, wewe, wala mwana wako, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala mjakazi wako, wala mnyama wako wa kufuga, wala mgeni aliye ndani ya malango yako. Maana, kwa siku sita Bwana alifanya mbingu, na nchi, na bahari, na vyote vilivyomo, akastarehe siku ya saba; kwa hiyo Bwana akaibarikia siku ya Sabato akaitakasa.” (Kutoka 20:8–11)

Kumbuka. “Neno hili halifanyi amri ya nne iwe muhimu zaidi kuliko zingine tisa. Zote zina umuhimu sawa. Kukiuka moja ni kukiuka zote (Yakobo 2:8–11). Lakini amri ya Sabato hutukumbusha kwamba Sabato ya siku ya saba, kama pumziko teule ya Mungu kwa ajili ya mwanadamu, hurejelea mwanzo hasa wa historia ya mwanadamu na ni kipengele husika cha juma la uumbaji (Mwa. 2:1–3; PP 336). Hoja kwamba Sabato iliwasilishwa mara ya kwanza kwa mwanadamu pale Sinai haina msingi wowote kabisa (Marko 2:27; PP 80, 258). Kwa namna binafsi Sabato huja kama ukumbusho kwamba katikati ya mahangaiko mengi ya maisha hatupaswi kumsahau Mungu. Kuingia kikamilifu katika utashi wa Sabato ni kupata awani ya thamani katika kutii sehemu iliyosalia katika Dekalojia. Zingatio na usabilifu maalum ulioelekezwa kwenye siku hii ya pumziko kwa Mungu na kwa vitu vyenye thamani ya milele hutupatia nguvu ya akiba kwa ushindi dhidi ya maovu ambayo kwayo tunaonywa katika amri zingine. Sabato imelinganishwa vyema na daraja lililokingamwa katika maji-mafuriko ya kimaisha, ambapo juu yake tunaweza kupita hadi ufukweni ng’ambo ya pili, kiunganishi kati ya dunia na mbinu, mfano wa siku ya milele ambapo wale walio waaminifu kwa Mungu watavaa milele vazi halidi la utakatifu na furaha.” [Francis D. Nichol, Ed., The Seventh-Day Adventist Bible Commentary, (Review and Herald Publishing Association, 1978), 1:604].

HATUA YA MAAMUZI: Ni mwitikio gani unaodhani sura hii ingepaswa kutuhimiza kufanya? “Ikumbuke siku ya Sabato uitakase.”

“Sabato hutupatia wito wa kujitoakatika shughuli za kawaida za kimwili na kuelekeza akili na moyo katika mambo matakatifu. Waisraeli waliusiwa kuitumia kwa ajili ya mikusanyiko takatifu (Law. 23:3). Vitabu vya Injili huthibitha kwamba ilitumiwa hivyo na Kristo na mitume (Luka 4:16; Matendo 17:2; 18:4; nk.), na kwamba ingepaswa budi kuendelea kuadhimishwa na Wakristo baada ya kukamilishwa kwa huduma ya Kristo duniani (Mat. 24:20).

Ukweli kwamba bado Sabato itaadhimishwa katika nchi mpya kama siku ya ibada (Isa. 66:23) ni dokezo dhahiri kwamba kamwe Mungu hakukusudia uadhimishaji husika uhamishiwe siku nyingine. Sabato ya kila juma ni kumbukumbu ya uumbaji, ikimkumbusha mwanadamu kila juma kuhusu uwezo wa Mungu wa uumbaji na kiasi gani anachowiwa na Muumbaji na Mpaji mwenye rehema. Kuikataa Sabato ni kumkataa Muumbaji, na hufungua mlango mpana kwa ajili ya kila namna ya nadharia za uongo. “[Sabato] ni ushuhuda wa daima juu ya uwepo Wake na ukumbusho wa ukuu Wake, hekima Yake, na upendo Wake. Endapo Sabato ingeadhimishwa kwa utakatifu wakati wote, kamwe asingekuwepo mkana-Mungu au mwabudu-sanamu” (PP 336).” [SDA BC 1:221].

SHAUKU YANGU LEO: Chagua Kisanduku kinachoakiasi uamuzi wako leo:

 • Nataka kujifunza zaidi kuhusu Sabato.
 • Nataka kuwashirikisha wengine ukweli kuhusu Sabato.
 • Nataka kushika amri zote za Mungu, ikiwa ni pamoja na Sabato
 • Ni shauku yangu ya kumtii Bwana kwa kuidumisha Siku Yake (Sabato ya siku ya saba) kuwa takatifu, Kut. 20:8.

Uwe na Siku Yenye Baraka: “Tena naliwapa Sabato Zangu, ziwe ishara kati ya Mimi na wao, wapate kujua ya kuwa Mimi, Bwana, Ndimi niwatakasaye. (Ezekieli 20:12)

Sauti ya Injili/ Mwongozo wa Kujifunza Biblia/ Mafundisho Makuu/ Sabato katika Maandiko na Historia/ Somo # 3.