Roho wa Baba yenu.

Ibada ya Alfajiri/ Dhima: Roho Mtakatifu.

Majina Yanayotumika kwa Roho Mtakatifu/ 79B-003, (Mathayo 10:20)/ Aya Kuu: “Kwa kuwa si ninyi msemao, bali ni Roho wa Baba yenu asemaye ndani yenu.” (Mathayo 10:20)

TAFAKARI: Mathayo sura ya 10 inajadili mambo yafuatayo: Mitume kumi na wawili (1-4); Kutumwa kwa Thenashara (5-15); Kristo anaonya juu ya mateso yajayo (16-26); Yesu anafundisha kumcha Mungu (27-30); Tunapaswa kuungama Kristo mbele ya wanadamu (32-33); Injili ya Kristo huleta mgawanyiko (34-38); Kikombe cha maji baridi (40-42).

Katika sura hii, Kristo anaonya kwamba maadui wa Mungu watawachukia wanafunzi Wake. Kuna makundi manne yaliyoorodheshwa hapa: (a) Mateso ya kidini—watawekwa mikononi mwa mahakama na kupigwa katika masinagogi, (Mt. 10:16 -17); (b) Mateso ya kisiasa — wataitwa mbele ya magavana na wafalme; hii itawapa nafasi ya kushuhudia, (Mt. 10:18); (c) Mateso ya kifamilia –- watu wa familia zao wataisaliti, (Mt. 10:21); (d) Mateso ya jumla— kila mtu atawachukia kwa sababu ya utii wao kwa Kristo, (Mt. 10:22-23).

MAANA YA KIIBADA: “Yesu aliwaambia wanafunzi kwamba wakati (si” kama “) wakikamatwa na kukabidhiwa kwa mamlaka, hawapaswi kuwa na wasiwasi juu ya nini cha kusema katika utetezi wao. Wazo la kuletwa mbele ya watawala wa Mataifa liliogopesha Myahudi ye yote, lakini Yesu aliwaonya wanafunzi wake wasiogope. Kile kinachopaswa kusemwa kitapewa kwenu wakati huo—Roho wa Mungu angeongea kupitia kwao.” [Bruce B. Barton, Matthew, Life Application Bible Commentary, (Wheaton, IL: Tyndale House Publishers, 1996), 207].

SAUTI YA INJILI: Mtume Paulo anasema, “Naam, na wote wapendao kuishi maisha ya utauwa katika Kristo Yesu wataudhiwa” (2 Timotheo 3:12). Wapendwa, mateso yanakuja kwa watu wa Mungu. Katika lile hubiri la Mlimani, Kristo anasema: “Heri wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki; Maana ufalme wa mbinguni ni wao. Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili Yangu.” (Mt. 5:10-11).

Hii ndiyo habari njema: Roho wa Mungu atatusaidia! Hatuna sababu yoyote ya kuwa na uwoga au wasiwasi, kwa sababu Roho atatupa maneno sahihi ya kusema au kujibu! Roho Mtakatifu atakuwa “Wakili Mtetezi”- akituletea msaada uliyo karibu.

Ujumbe wa leo ni Rahisi Sana: Usiogope! Kwanini? Kwa sababu una Mtetezi, Mwalimu, Mshauri, naam, Msaidizi. Sikiliza Sauti ya Bwana Yesu tunapohitimisha somo hili: “Lakini hapo watakapowapeleka, msifikiri-fikiri jinsi mtakavyosema; maana mtapewa saa ile mtakayosema. Kwa kuwa si ninyi msemao, bali ni Roho wa Baba yenu asemaye ndani yenu.” (Mathayo 10:19-20)

UWE NA ALFAJIRI NJEMA: “Bwana akamwambia [Musa], Ni nani aliyekifanya kinywa cha mwanadamu? Au ni nani afanyaye mtu kuwa bubu au kiziwi, au mwenye kuona, au kuwa kipofu? Si mimi, Bwana? Basi sasa, enenda, Nami nitakuwa pamoja na kinywa chako, na kukufundisha utakalolinena.” (Kutoka 4:11-12)

Sauti ya Injili/ “Njoo Roho Mtukufu”/ Mawazo Mafupi ya Kiibada/ Roho Mtakatifu/ Wazo la # 3/

Mwitikio Wetu:

Nyimbo Za Kikristo, No. 41: Roho Mtakatifu.

[1] Roho Mtakatifu, Kiongozi amini; Utushike mkono, Tulio wasafiri; Utupe kusikia Sauti ya upole: “Msafiri, fuata, Naongoza nyumbani.”

[2] Wewe ndiwe rafiki, Msaada karibu; Tusiache shakani, Na tukiwa gizani; Utupe kasikia sauti ya upole: “Msafiri, fuata, Naongoza nyumbani.”

[3] Siku zetu za kazi, Zikiwa zimekwisha; Wala hatuna tama, ila mbingu na sala; Utupe kusikia Sauti ya upole: “Msafiri fuata, Naongoza nyumbani.”