Roho Ya Mungu.

Ibada ya Alfajiri/ Dhima: Roho Mtakatifu/ Roho Ya Mungu.

Majina Yanayotumika kwa Roho Mtakatifu: “Roho Ya Mungu”/ 79B-001 (Mwanzo 1:1-2)/ Aya Kuu: “Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi. Nayo nchi ilikuwa ukiwa, tena utupu, na giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji; Roho ya Mungu ikatulia juu ya uso wa maji.” (Mwanzo 1:1-2).

Tafakari: Kuna Mungu mmoja katika nafsi tatu, yaani, Baba, Mwana, na Roho. Neno la Bwana linatukumbusha likisema: “Sikiza, Ee Israeli; Bwana, Mungu wetu, Bwana ndiye mmoja.” (Torati 4:6).

Mungu Roho mtakatifu alihusika katika kazi ya uumbaji. Ni jambo la muhimu sana kuelewa kwamba kazi ya Roho Mtakatifu ni ya kihistoria na makini sana katika asili ya mwanadamu. Mungu Roho Mtakatifu — ambaye aliiongoza Biblia — anaonekana juu ya ukurasa wake wa kwanza kabisa. Yeye ndiye muasisi wa mwanga na uzuri wote katikati ya ulimwengu uliokuwa na giza.

Maana ya Kiibada: “Mungu akasema, Iwe nuru; ikawa nuru.” (Mwa. 1:3). Mungu Roho Mtakatifu aliyeleta mwangaza [Nuru] kwenye ulimwengu wa giza, bado leo aweza kuleta Nuru katika maisha ya kila muumini. Je utamruhusu afanye hivyo?

Sauti ya Injili: “Kwa kuwa Mungu, aliyesema, Nuru itang’aa toka gizani, ndiye aliyeng’aa mioyoni mwetu, atupe nuru ya elimu ya utukufu wa Mungu katika uso wa Yesu Kristo.” (2 Wakorintho 4:6)

Alfajiri Njema: 8 Kwa maana zamani ninyi mlikuwa giza, bali sasa mmekuwa nuru katika Bwana; enendeni kama watoto wa nuru, 9 kwa kuwa tunda la nuru ni katika wema wote na haki na kweli; 10 mkihakiki ni nini impendezayo Bwana. 11 Wala msishirikiane na matendo yasiyozaa ya giza, bali myakemee.” (Waefeso 5:8-11)

Sauti ya Injili/ Dondoo Fupi kuhusu Roho Mtakatifu: “Roho Ya Mungu”/ Wazo la 1.

Mwitikio Wetu: Nyimbo Za Kikristo, No. 41: ROHO MTAKATIFU.

[1] Roho Mtakatifu, Kiongozi amini; Utushike mkono, Tulio wasafiri; Utupe kusikia Sauti ya upole: “Msafiri, fuata, Naongoza nyumbani.”

[2] Wewe ndiwe rafiki, Msaada karibu; Tusiache shakani, Na tukiwa gizani; Utupe kasikia sauti ya upole: “Msafiri, fuata, Naongoza nyumbani.”

[3] Siku zetu za kazi, Zikiwa zimekwisha; Wala hatuna tama ila mbingu na sala; Utupe kusikia Sauti ya upole: “Msafiri fuata, Naongoza nyumbani.”