Sabato, Utangulizi.

SABATO, UTANGULIZI.

Mwongozo wa Kujifunza Biblia/ Siku Iliyosahaulika: Sabato ya siku ya saba/ 86-001, (Kutoka 20:8)/ Andiko Msingi: “Na katika mashindano watasimama ili kuamua; wataamua sawasawa na hukumu Zangu; nao watazishika sheria Zangu, na amri Zangu, katika sikukuu Zangu zote zilizoamriwa; nao watazitakasa Sabato Zangu.” (Ezekieli 44:24)

Malengo: Kusudi la somo hili ni kutambulisha mada kuhusu Sabato na kusisitiza mambo 13 halisi na rahisi ya kufikria kwenye mada hii adhimu.

Maelezo ya Ufunguzi: Je siku gani ni Sabato? Pengine Sabato ya siku ya saba ndiyo mada yenye ukinzani mkuu zaidi miongoni mwa Wakristo leo. Baadhi ya Wakristo hawatambui kwamba Sabato ya Mungu ya siku ya saba ni Jumamosi. Baadhi hukiri ukweli huu lakini kwa namna fulani wanasita kulipokea fundisho hili.

Biblia hutuambia kwenye kitabu cha Danieli kwamba “utawala katili” ungekuja na kuazimu kubadili sheria za Mungu, na ndivyo ulivyofanya—Sabato ya siku ya saba ikawa sabato ya siku ya kwanza bila ukubali wa Mungu. Kitabu cha Danieli pia kinarejelea badiliko hili la sheria ya Mungu lililotendwa na “utawala wa mpinga-Kristo” kuwa sawa na kuyafikia majeshi ya mbinguni na “kukanyagisha patakatifu pa mbinguni” (Dan 8:13).

Tunapata maneno hayo yakitumiwa katika Waebrania sura ya kumi katika kurejelea dhambi ya kusudi. “Maana, kama tukifanya dhambi kusudi baada ya kuupokea ujuzi wa ile kweli, haibaki tena dhabihu kwa ajili ya dhambi; bali kuna kuitazamia hukumu yenye kutisha, na ukali wa moto ulio tayari kuwala wao wapingao. Mtu aliyeidharau sheria ya Musa hufa pasipo huruma, kwa neno la mashahidi wawili au watatu. Mwaonaje? Haikumpasa adhabu iliyo kubwa zaidi mtu yule aliyemkanyaga Mwana wa Mungu, na kuihesabu damu ya agano aliyotakaswa kwayo kuwa ni kitu ovyo, na kumfanyia jeuri Roho wa neema?” (Waebrania 10:26–29)

Wapendwa, andiko hili hutuonya kwamba haibaki tena dhabihu ya kwa ajili ya dhambi, na kuendelea na dhambi ya kusudi ni kumkanyagia chini Mwana wa Mungu na kuihesabu kazi ya kristo msalabani kama kitu ovyo licha ya kuwa chini ya neema. Kupuuza amri ya Sabato kwa kudhamiria ni “kumkanyagia chini Mwana wa Mungu” kwa vile Yeye ni Bwana wa Sabato. Hili ni onyo tunalopaswa kulizingatia kwa dhati!

Badiliko la siku ya Sabato lilikuja kwa takriban mamia ya miaka. Pia lilisababisha vifo vya mamilioni ya Wakristo waaminifu waliopoteza maisha yao kwa kutii amri ya Mungu. Huu ni ukweli mwingine ambao Wakristo wengi hawautambui. (Tutakuza/thibitisha wazo hili kwenye masomo yajayo).

DONDOO ZA MSINGI:

[1] Je Sabato ni siku gani ya juma? Siku ya saba (angalia Kut. 20:8)

Sabato (šǎb·bāṯ): —1. Sabato, yaani, siku ya saba ya juma, hujulikana kwenye tamaduni nyingi kama “Jumamosi,” siku muhimu iliyowakifishwa kwa ajili ya pumziko na ibada (Kut. 16:23); 2. juma, yaani, jumla ya siku saba (Law. 23:15); 3. sabato, kipindi cha pumziko, yaani, kipindi cha wakati kwa ajili ya pumziko, ambacho huweza au pengine isiwe siku ya saba ya juma, yenye kujikita katika hili kama kipindi cha pumziko (Law. 16:31; 23:32; 25:2, 4,6, 8; 26:34, 35, 43; 2 Nya. 36:21) [James Swanson, Dictionary of Biblical Languages with Semantic Domains: Hebrew (Old Testament), 1997].

[2] Nini maana ya neno “Sabato?” Sabato ni “udahilishaji wa neno la Kiebrania lenye maana ya “kukoma” au “kuhulu.” Sabato ilikuwa siku (tangu Ijumaa machweo hadi Jumamosi machweo katika wakati ule wa Yesu) muda ambapo kazi ya kawaida ilikoma. Maandiko yanaeleza kwamba Mungu aliwapatia watu Wake Sabato kama fursa ya kumtumikia, na kuwa ukumbusho wa kweli kuu mbili kwenye Biblia—uumbaji na ukombozi.” [Walter A. Elwell and Barry J. Beitzel, Baker encyclopedia of the Bible, 1988, 2, 1874].

[3] Ni virai gani vya Biblia vinavyohusiana na neno ‘Sabato?’

  1. Mwaka wa Sabato: Mwaka ambapo mashamba yaliachwa yenyewe ili kupumzika katika kuadhimisha Sabato kwa ajili ya nchi. Ilifanyika kila mwaka wa saba.
  • Siku baada ya Sabato: Jumapili –siku ambapo kuhani alipaswa kuleta sadaka ya miganda mbele ya Mungu (Law. 23:11, 15). Pia, Kristo alifufuka katika siku hii (siku ya kwanza ya juma).
  • Siku kabla ya Sabato: Ijumaa — siku ambapo maandalizi kwa ajili ya Sabato hufanyika. Kristo alisulubiwa katika siku hii (siku ya sita ya juma).
  • Sabato za Miaka: Mwaka wa saba ambapo mtumwa Mwebrania alipaswa kuachiliwa huru. (Pia angalia mada husiani kama vile –Mwaka wa Jubilii, Mwaka wa Maachilio, Maachilio, Sabato za Miaka, Majuma ya Miaka)

KWELI 13 ZA BIBLIA KUHUSU SABATO.

[1] Neno lililofasiriwa “akapumzika” kwenye Biblia zetu za Kiingereza katika Mwanzo 2:3 kwa kweli ni “shabbath” katika Kiebrania na humaanisha Sabato. “Jumamosi” huitwa Sabato katika zaidi ya lugha 105 vilevile kama ilivyotajwa wakati wa uumbaji. Hii hurejelea Babeli katika Mwanzo 11 ambapo Jumamosi ilitambulika kama siku ya Sabato na ilijulikana kama jina hasa la siku husika. Katika Kiingereza tuna jina la kipagani ambalo ni Jumamosi.

[2] Siku ya Pumziko: Baada ya kufanya kazi kwa siku sita za juma katika kuiumba dunia hii, Mungu alipumzika katika siku ya Sabato (Mwanzo 2:1-3). Hii ilitia muhuri siku hiyo kama siku ya Mungu ya pumziko, au siku ya Sabato, kwa vile siku ya Sabato humaanisha siku ya pumziko.

  • Kielelezo: Mtu anapozaliwa katika siku fulani, siku hiyo huwa siku yake ya kuzaliwa. Hivyo, Mungu alipopumzika katika siku ya Sabato, siku hiyo ikawa siku Yake ya pumziko au siku ya Sabato. Hivyo, lazima daima siku ya saba iwe siku ya Mungu ya Sabato. Je unaweza kubadili siku yako ya kuzaliwa kutoka siku uliyozaliwa kwenda siku nyingineyo? Hapana. Halikadhalika huwezi kubadili siku ya Mungu ya pumziko kwenda katika siku ambayo hakupumzika. Hivyo siku ya saba bado ingali siku ya Sabato ya Mungu.

[3] Taasisi ya Sabato: Mungu ndiye mwasisi wa Sabato. Sabato iliumbwa na Mungu (Mwa. 2:3); ikabarikiwa na Mungu (Mwa. 2:3); ikatakaswa na Mungu (Kut. 20:11); misingi ya kuasisiwa kwake (Mwa. 2:2, 3; Kut. 20:11).

Tangu mwanzo siku ya saba iliadhimishwa kama Sabato, ikiwa takatifu kwa Mungu (Kut. 20:9–11); na “ilifanyika kwa ajili ya mwanadamu” (Marko 2:27). Zingatia: Sabato ilifanyika kabla ya anguko, hivyo siyo “mfano” – maana mifano iliingizwa baada ya anguko. Sababu pekee ambayo hufanya tuwe na siku ya saba ya juma ni kwamba Mungu aliweka wakati wa uumbaji kwa ajili ya kusudi hili moja tu.

[4] Ni kumbukumbu ya uumbaji (Kutoka 20:11; 31:17): Kila wakati tunapopumzika katika siku ya saba, kama alivyofanya Mungu wakati wa uumbaji, tunakumbuka tukio hilo kuu. Mungu anatuonya kwamba utawala katili ungeazimu kubadili sheria Yake na hili lilifanywa na Kanisa kwa kubadili Sabato kwenda Jumapili na kwa damu ya mamilioni ya watakatifu (Danieli 7:25). Yesu anasema ilifanyika kwa ajili ya mwanadamu (Marko 2:27), yaani, kwa ajili ya jamaa, kwa vile neno mwanadamu hapa halina mipaka; hivyo kwa ajili ya Mataifa pamoja na Myahudi.

[5] Sabato haiwezi kuwa taasisi ya Kiyahudi — (kama wengi wadaivyo) –maana ilifanyika miaka 2,300 kama ya kuwepo hata Myahudi mmoja! Kwa kweli, kamwe Biblia haiiti kuwa ni “Sabato ya Kiyahudi,” bali daima “Sabato ya Bwana Mungu wako.” Watu wanapaswa kujihadhari jinsi wanavyoinyanyapaa siku takatifu ya Mungu ya pumziko. Sabato ilikabidhiwa kwa Adamu, kiongozi wa jamii ya wanadamu (Marko 2:27; Mwanzo 2:1-3)

[6] Ni sehemu ya Sheria Kumi za Mungu kabla ya Sinai. Mungu aliwajaribu wanawe ili kuona kama wangeshika amri Zake. Jinsi gani Mungu aliwajaribu? Kwa kuona endapo wangeshika Sabato ya siku ya saba (Kutoka 16:4-30). Kisha Mungu akaiweka kwenye moyo wa sheria Yake ya maadili (Kutoka 20:1-17). Kwa nini Mungu aliiweka hapo kama haikuwa sawa na amri zingine tisa, ambazo wote hukiri kuwa hazibadiliki?

Sabato ya siku ya saba iliamuriwa kwa sauti ya Mungu aliye hai (Kumb. 4:12–13); halafu akaiandika amri hiyo kwa chanda Chake Mwenyewe (Kutoka 31:18); akaichongea kwenye jiwe la kudumu ikionesha asili yake ya kutoharibika (Kumb. 5:22); ilihifadhiwa kwa utakatifu ndani ya Sanduku la Agano katika Patakatifu pa Patakatifu (Kumb. 10:5)

[7] Athari za Kukiuka Sabato: Mungu aliwaangamiza Waisraeli jangwani kwa sababu waliinajisi Sabato (Ezekieli 20:12-13); amri hii ni ishara ya Mungu wa kweli ambayo kwayo tunapaswa kumjua Yeye dhidi ya miungu ya uongo (Ezekieli 20:20); aliiangamiza Yerusalemu kwa ajili kuikiuka (Yeremia 17:27); aliwapeleka Waisraeli katika utumwa wa Babeli kwa kuikiuka (Nehemia 13:18).

[8] Baraka za Sabato: Mungu ameahidi kuwabariki wote wanaoishika Sabato (Isaya 56:2, 6); anatamani tuiite Sabato Yake kuwa siku ya “furaha” (Isaya 58:13); ametangaza baraka maalum kwa Mataifa wote wanaoishika (Isaya 56:2, 6).

[9] Urejeshwaji wa Sabato: Baada ya Sabato takatifu kukanyagiwa chini kwa “vizazi vingi,” haina budi kurejeshwa katika siku za mwisho (Isaya 58:12-13)

[10] Kristo na Sabato: Yesu alikuwa/na bado angali “Bwana wa Sabato” (Marko 2:28) –yaani, huipenda na kuilinda, kama ambavyo mume ni bwana wa mkewe, kwa ajili ya kumpenda na kumtunza. Yesu alipokuja, alishika siku ya saba maisha yake yote (Luka 4:16; Yohana 15:10); hivyo, alifuata mfano wa Baba Yake wakati wa uumbaji. Hivi hatupaswi kuufuata mfano wa Baba pamoja na Mwanawe?

[11] Siku ya saba ni Sabato ya Bwana (Angalia Ufunuo 1:10; Marko 2:28; Isaya 58:13; Kutoka 20:10). Badala ya kuibatilisha Sabato, Yesu alifundisha jinsi ya kuadhimishwa (Mathayo 12:1-13); aliwafundisha wanafunzi Wake kwamba hawapaswi kufanya lolote katika siku ya Sabato ambalo “si halali” (Mathayo 12:12); aliwaagiza mitume Wake kwamba Sabato ingetunzwa hata miaka arobaini baada ya ufufuo Wake (Mathayo 24:20)

[12] Hakuna siku nyingineyo imewahi kutakaswa kama siku ya pumziko. Sabato huanza Ijuma wakati wa machweo hadi Jumamosi machweo (angalia Mwanzo 2:1-3; Kutoka 20:8-11; Isaya 58:13-14; 56:1-8; Matendo 17:2; Matendo 18:4, 11; Luka 4:16; Marko 2:27-28; Mathayo 12:10-12; Waebrania 4:1-11; Mwanzo 1:5, 13-14; Nehemia 13:19)

[13] Utakatifu wa Jumapili kama siku “mpya” ya ibada haina msingi wowote kabisa wa Biblia. Mimi siyo tajiri kiasi hicho, lakini nimejiandaa kuweka ahadi hii: Nipatie andiko moja tu la Biblia ambalo hubainisha wazi kwamba Mungu amebatilisha amri ya nne (Sabato ya siku ya saba) na badala yake akaweka amri “mpya” ya kuiadhimisha Jumatatu (siku ya kwanza ya juma) kama siku mpya ya ibada, nami nitakupatia Dola 100 za Kimarekani. Nimejiandaa kukuandikia cheki leo.

ZINGATIA: Kuna taarifa nyingi zaidi ambazo tutatukuleteeni kadiri tunaposafiri katika mfululizo huu. Hii ilikuwa seti sampuli tu ya taarifa kwa ajili ya kutumika kama utangulizi wa mada hii makini.

MAANA YA KIIBADA: Sabato, miongoni mwa mambo mengine, ni ishara ya utakaso. Sabato ni sishara ya uwezo wa Mungu ubadilishao, ishara ya utakatifu au utakaso.

Bwana alitamka, “Kisha, nena wewe na wana wa Israeli, na kuwaambia, Hakika mtazishika Sabato Zangu, kwa kuwa ni ishara kati ya Mimi na ninyi katika vizazi vyenu vyote; ili mpate kujua ya kuwa Mimi ndimi Bwana niwatakasaye (niwatengaye kwa kusudi Langu) ninyi).” (Kutoka 31:13, AMP) “Zitakaseni (zitengeni na kuzidumisha katika utakatifu) Sabato Zangu; zitakuwa ishara kati ya Mimi na ninyi, mpate kujua ya kuwa Mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.” (Ezekieli 20:20, AMP)

Sabato, kwa hivyo wapendwa, pia ni ishara ya Mungu kama Mtakasaji. Kama ambavyo watu wanatakaswa kwa damu ya Kristo (Ebr. 13:12), Sabato pia ni ishara ya muumini kuikubali damu Yake kwa ajili ya msamaha wa dhambi.

HATUA YA MAAMUZI: Ni mwitikio gani unaodhani somo hili lingepaswa kutuhimiza kufanya? “Ikumbuke siku ya Sabato uitakase.”

Wapendwa, miongoni mwa amri zote, Mungu aliichagua hii ya nne: Sabato, na kutuagiza (jamii yote ya wanadamu, siyo Wayahudi tu) “kuikumbuka” Sabato, kwa sababu alijua kwamba siku moja watu wangejaribu kuipuuza, kuiharibu, kuisahau, na hatimaye kuikanyagia chini. Sabato ni muhimu leo kama ilivyokuwa pale Edeni. Sabato hutumika kama ishara kati ya Mungu na watu Wake (Eze. 20:8). Amri ya Sabato itakuwa kigezo cha maamuzi katika vita vikuu zaidi kati ya Kristo na Shetani (Ufu. 12:17; 13) mara tu kabla Yesu hajarejea tena. Leo, Mungu anamwita kila mmoja wetu “azishike amri” na kuwa na “imani ya Yesu” (Ufu. 14:12) – hiyo inahusisha utii wa amri ya nne!

Kama ambavyo Mungu ametenga siku ya Sabato kwa ajili ya kusudi takatifu, halikadhalika amewatenga watu Wake kwa ajili ya kusudi takatifu—ili wawe mashuhuda Wake maalum. Ushirika wao pamoja Naye katika siku hii hupelekea utakatifu; wanajifunza kutotegemea rasilimali zao wenyewe bali kumtegemea Mungu, awatakasaye. Je utakuwa radhi leo ili kutakaswa na Bwana? Lakini, kwanza, hivi utaitii amri hii: “Ikumbuke siku ya Sabato uitakase.” (Kutoka 20:8). Udumishe katika utakatifu, nawe utabarikiwa! Amina.

Uwe na Siku Yenye Baraka: “Tena naliwapa Sabato Zangu, ziwe ishara kati ya Mimi na wao, wapate kujua ya kuwa Mimi, Bwana, Ndimi niwatakasaye [niwatengaye na kuwaweka kando].” (Ezekieli 20:12, AMP)

Sauti ya Injili/ Mwongozo wa Kujifunza Biblia/ Mafundisho Makuu/ Sabato ya siku ya saba/ Somo # 1.