Roho Mtakatifu ni Nani?

ROHO MTAKATIFU NI NANI?

Roho Mtakatifu ni Nani? / 79-001 (Matendo 2:1–2)/ Mwongozo wa Kujifunza Biblia/ Dibaji ya Numatolojia: (Fundisho kuhusu Roho Mtakatifu)/ Andiko Msingi: “Hata ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja. Kukaja ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi.” (Matendo 2:1–2)

Malengo: Kusudi la somo hili ni kuwasilisha muhtasari juu ya mada ya Roho Mtakatifu.

DHIMA: ROHO MTAKATIFU.

Katika mfululizo huu tutazingatia dhima zifuatazo:

 1. Upako wa Roho Mtakatifu
 2. Ubatizo wa/kwa Roho Mtakatifu
 3. Kufuru dhidi ya Roho Mtakatifu
 4. Usadikisho wa Roho Mtakatifu
 5. Maandamo Maradufu ya Roho Mtakatifu
 6. Ubainishaji wa Roho Mtakatifu
 7. Uungu wa Roho Mtakatifu
 8. Kujazwa Roho Mtakatifu
 9. Matunda ya Roho Mtakatifu
 10. Mungu Roho Mtakatifu (Uungu)
 11. Uongozi wa Roho Mtakatifu
 12. Moyo na Roho Mtakatifu
 13. Roho Mtakatifu na Uhakikisho
 14. Roho Mtakatifu na Utume
 15. Roho Mtakatifu na Amani
 16. Roho Mtakatifu na Sifa
 17. Roho Mtakatifu na Maombi
 18. Roho Mtakatifu na Kuhubiri
 19. Roho Mtakatifu na Uongofu
 20. Roho Mtakatifu na Utakaso
 21. Roho Mtakatifu na Maandiko
 22. Roho Mtakatifu kama Mshauri
 23. Roho Mtakatifu kama Mwalimu
 24. Roho Mtakatifu katika Agano la Kale
 25. Roho Mtakatifu Kanisani
 26. Roho Mtakatifu Mpaji wa Uzima
 27. Roho Mtakatifu, Kazi Ulimwenguni
 28. Roho Mtakatifu Kukaa Ndani Mtu
 29. Furaha ya Roho Mtakatifu
 30. Pentekoste na Roho Mtakatifu
 31. Hulka ya Roho Mtakatifu
 32. Nguvu ya Roho Mtakatifu
 33. Uwepo wa Roho Mtakatifu
 34. Ahadi ya Roho Mtakatifu
 35. Kutiwa Muhiri na Roho Mtakatifu
 36. Uturufu wa Roho Mtakatifu
 37. Karama za Kiroho na Roho Mtakatifu
 38. Vyeo na Majina ya Roho Mtakatifu
 39. Dhambi Isiyosameheka
 40. Upepo—Taashira za Roho Mtakatifu
 41. Hekima ya Roho Mtakatifu
 42. Ushuhuda wa Roho Mtakatifu

Somo # 1:

ROHO MTAKATIFU NI NANI?

Maswali ya Moyoni: [1] Roho Mtakatifu ni nani? [2] Anafananaje? [3] Anafanya nini? [4] Yuko wapi? [5] Kwa nini tujifunze kuhusu Roho Mtakatifu?

Maelezo ya Ufunguzi: Pengine Roho Mtakatifu ndiye mshirika wa Utatu anayeeleweka kwa uchache zaidi. Miongoni mwa visasili na dhana potofu zinazoenezwa, Yeye amebainishwa kama nguvu, mzimu, au huenda nafsi duni au mbadala wa mungu. Wakati fulani anatatanishwa, akiwasilishwa kama umbile linalojitokeza wakati fulani. Hakuna lolote zaidi ya hili ambalo lingekuwa mbali na ukweli. Roho Mtakatifu ni Mungu. Ni muhimu sana kwa mwanafunzi yeyote wa Biblia kujua Mungu Roho Mtakatifu ni nani; kujifunza jinsi ya kuhusiana Naye; kujifunza jinsi ya kujua kumwabudu; na kufahamu jinsi ya kumdhihirisha.

Utangulizi: Katika somo letu juu ya Fundisho la Mungu, tulijifunza kwamba wapo washirika watatu katika Uungu (Utatu)—Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu. Hii hapa durusu ya haraka: tuliona kwamba Roho Mtakatifu ni nafsi; tuliona kwamba Roho Mtakatifu ni Mungu.

Katika somo hili tutamtambulisha Roho Mtakatifu katika namna tofauti kabisa. Badala ya kutumbukia katika kina kirefu mwishoni, tutaambaa kwenye maji mafupi, kisha tutasonga kwenye kina zaidi. Tutajaribu kuelewa nini maana ya Roho Mtakatifu kana kwamba hatukujua lolote.

NJIA YA KUMTAMBULISHA ROHO

Kuna njia chache wezekani za kumtambulisha Roho

[1] Tunaweza kuanza na Agano la Kale. Roho wa Mungu ametajwa katika Mwanzo 1– “Nayo nchi ilikuwa ukiwa, tena utupu, na giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji; Roho ya Mungu ikatulia (akiambaa, akistakiri) juu ya uso wa maji.” (Mwanzo 1:2, AMP)

Kuna rejea zingine mbalimbali kuhusu Roho Mtakatifu katika Agano la Kale, mfano;

 • “Na Roho ya Bwana atakaa juu Yake, Roho ya hekima na ufahamu, Roho ya shauri na uweza, Roho ya maarifa na ya kumcha Bwana.” (Isaya 11:2)
 • Roho wa Bwana MUNGU i juu Yangu, Kwa sababu BWANA ameniwakfisha Niwahubiri maskini habari njema; Amenituma niwagange waliovunjika moyo, Niwatangazie mateka uhuru, Na kuwafungulia gereza hao waliofungwa” (Isaya 61:1)

[2] Tunaweza kuanza na Injili Shabihi. Injili Shabihi ni Mathayo, Marko na Luka. Zinaitwa hivyo kwa sababu kiwango kikubwa cha ufanano miongoni mwa maandishi yao.

Rejea ya kwanza kuhusu Roho Mtakatifu katika Agano Jipya ni Mathayo 1:18, 20; Luka 1:35

 • Kuzaliwa kwake Yesu Kristo kulikuwa hivi. Mariamu mama Yake alipokuwa ameposwa na Yusufu, kabla hawajakaribiana, alionekana ana mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu.” (Mathayo 1:18)
 • “Basi alipokuwa akifikiri hayo, tazama, malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto, akisema, Yusufu, mwana wa Daudi, usihofu kumchukua Mariamu mkeo, maana mimba yake ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu. (Mathayo 1:20)
 • “Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu.” (Luka 1:35)

Kwa Usomaji Zaidi: Tazama jinsi Injili Shabihi zinahusianisha ubatizo wa Yesu na kushuka kwa Roho Mtakatifu kama huwa (Soma Mathayo 3:16; Marko 1:10; Luka 3:22).

[3] Tunaweza kuanza na Kitabu cha Matendo. Matendo sura ya pili huanza kwa namna hii: “Hata ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja. Kukaja ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi.” (Matendo 2:1–2)

Luka, aliyeandika Matendo, miongoni mwa waandishi wote wa Injili Shahibi, alikuwa na mengi ya kusema kuhusu Roho Mtakatifu. Baada ya kuambia kungojea pale Yerusalemu, Roho Mtakatifu alishuka Siku ya Pentekoste (Matendo 2). Huu ndio wakati ambapo wanafunzi walielewa kikamilifu Roho Mtakatifu alikuwa nani. Huduma Yake ya wokovu ilitambulika miongoni mwao. Waliungana pamoja kama watu wamoja katika kusudi na utume (uinjilisti). Walielewa sababu kwa nini Yesu alikuwa amekufa msalabani. Hata hivyo, Yesu alikuwa amewatambulisha kuhusu Roho Mtakatifu hapo awali.

“Je matokeo ya kumwagwa Roho yalikuwa nini katika Siku ya Pentekoste? Habari njema za Mwokozi aliyefufuka zilipelekwa maeneo ya mbali kabisa katika ulimwengu uliokaliwa na watu. Kadiri wanafunzi walipotangaza ujumbe wa neema ikomboayo, mioyo ilijisalimisha chini ya nguvu ya ujumbe huu. Kanisa lilishuhudia waongofu wakimiminika kwake kutoka pande zote. Wapogofu (waliorudi nyuma), waliongolewa upya. Wadhambi waliungana na waumini katika kutafuta lulu yenye thamani kuu. Baadhi waliokuwa wapinzani wa injili wakali zaidi wakati watetezi wake.” (The Acts of the Apostles, uk. 48).

[4] Tunaweza kuanza na Mtume Paulo. Paulo, katika nyaraka zake, kwa namna bayana zaidi hufasili injili na hutusaidia kuelewa Agano Jipya kwa ujumla wake.

Yesu alitambulisha mada ya Roho Mtakatifu katika Yohana 14, akidai kwamba “angemwomba Baba, Naye atawapa Msaidizi mwingine (Mshauri, Msaidizi, Mwombezi, Mtetezi, Mwimarishaji, na Mbadala), ili akae nanyi hata milele” (Yohana 14:16, AMP)

Hata mapema zaidi katika sura husika, Kristo alisema hili: “Hata bado nikali ninayo mengi ya kuwaambia, lakini hamwezi kuyastahimili hivi sasa.” (Yohana 16:12) “Yalikuwepo mambo mengi kuhusu kazi ya Roho na uimarishaji wa dini ambayo yangesemwa. Yesu alikuwa amewapatia mdokezo; alikuwa amewawasilishia mafundisho makuu ya mfumo husika, lakini alikuwa hakuwapatia maelezo ya kina. Haya yalikuwa mambo ambayo hawakuweza kustahimili. Bado walikuwa wamejaa hisia za chuki za Kiyahudi, na hawakuwa wamejiandaa kwa ajili ya maendelea kamili ya mipango Yake.” (Albert Barnes’ Notes on the Whole Bible)

Lakini Paulo alianzia pale Yesu alipoishia (Yohana 16:12). Paulo aliendeleza kila ambacho Yesu alisema kingekuwa zaidi ya ustahimilifu wa wanafunzi kwa wakati huo.

[5] Vitabu vya Agano Jipya. Vitabu vingine vya Agano Jipya humrejelea Roho lakini ndani yao huchukuliwa kwamba tayari msomaji anajua kitu fulani kuhusu Roho Mtakatifu.

Hii hapa mifano michache:

 • “Mungu naye akishuhudu pamoja nao kwa ishara na ajabu na nguvu za namna nyingi, na kwa magawanyo ya Roho Mtakatifu, kama alivyopenda Mwenyewe.” (Waebrania 2:4)
 • “Kwa hiyo, kama anenavyo Roho Mtakatifu, Leo, kama mtaisikia sauti Yake” (Waebrania 3:7)
 • “Kwa maana [haiwezekani] hao waliokwisha kupewa nuru, na kukionja kipawa cha mbinguni, na kufanywa washirika wa Roho Mtakatifu (Waebrania 6:4)
 • “Basi si zaidi damu yake Kristo, ambaye kwamba kwa Roho wa milele alijitoa nafsi Yake kwa Mungu kuwa sadaka isiyo na mawaa, itawasafisha dhamiri zenu na matendo mafu, mpate kumwabudu Mungu aliye hai?” (Waebrania 9:14)
 • “Mwaonaje? Haikumpasa adhabu iliyo kubwa zaidi mtu yule aliyemkanyaga Mwana wa Mungu, na kuihesabu damu ya agano aliyotakaswa kwayo kuwa ni kitu ovyo, na kumfanyia jeuri Roho wa neema?(Waebrania 10:29)
 • “Au mwadhani ya kwamba maandiko yasema bure? Huyo Roho akaaye ndani yetu hututamani kiasi cha kuona wivu?” (Yakobo 4:5)
 • “Kama vile Mungu Baba alivyotangulia kuwajua katika kutakaswa na Roho, hata mkapata kutii na kununyiziwa damu ya Yesu Kristo. Neema na amani na ziongezwe kwenu.” (1 Petro 1:2)
 • “Kwa maana Kristo naye aliteswa mara moja kwa ajili ya dhambi, mwenye haki kwa ajili yao wasio haki, ili atulete kwa Mungu; mwili Wake akauawa, bali Roho Yake akahuishwa (1 Petro 3:18)
 • “Mkilaumiwa kwa ajili ya jina la Kristo ni heri yenu; kwa kuwa Roho wa utukufu na wa Mungu anawakalia.” (1 Petro 4:14)
 • “Maana unabii haukuletwa popote kwa mapenzi ya mwanadamu; bali wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu, wakiongozwa na Roho Mtakatifu.(2 Petro 1:21)
 • “Bali ninyi, wapenzi, mkijijenga juu ya imani yenu iliyo takatifu sana, na kuomba katika Roho Mtakatifu” (Yuda 20)

MAANA YA KIIBADA: “Nami nitamwomba Baba, Naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele; ndiye Roho wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, Naye atakuwa ndani yenu.(Yohana 14:16–17)

 • “Katika aya ya 15 Yesu alikuwa amezungumza kuhusu upendo wa wanafunzi Kwake; hapa aliwadhihirishia upendo Wake. Kwa kuzingatia kazi Yake ya upatanisho kama Kuhani wao Mkuu, Yesu aliahidi kumwomba Baba kuwatumia watu Wake Msaidizi mwingine—Roho Mtakatifu. Paraklētos (Msaidizi) ni istilahi ambayo maana yake haiwezi kutoshelezwa kwa neno lolote moja. Kimsingi humaanisha “aliyeitwa ili kusaidia kando ya” na hubeba dhana ya msaidizi, mfariji, mshauri, mnasihi, mpatanishi, mhimizaji, na wakili (wakili mtetezi).” [John F. MacArthur Jr., John 12–21, MacArthur New Testament Commentary, (Chicago, IL: Moody Publishers, 2008), 112].

Wapendwa, Roho Mtakatifu ni Mungu. Kinyume na itikadi/imani zingine, Biblia hufundisha wazi kwamba kuna Mungu Roho Mtakatifu. Ana hulka, nyadhifa za kiungu na stahiki, kama ilivyo kwa Baba na Mwana. Katika somo letu lijalo tutaangalia vitu hivi kwa upana zaidi).

Dua ileile aliyoomba Kristo kwa Baba –“Nami nitamwomba Baba” – bado analiomba leo. Siyo kwamba Baba angetutumia Roho Mtakatifu (kwa sababu tayari ametumwa), bali kwamba, tuweze kumkiri na kumtambua kwamba yuko hapa kwa ajili yetu: kwa ajili ya manufaa yetu, baraka zetu, wokovu wetu, uzima wetu wa milele.

Wakati akingali nao, Yesu alikuwa kwa wanafunzi Wake mshauri, mwongozi, rafiki; lakini sasa alikuwa akiondoka. Ilikuwa muhimu basi kuwatumia Yule ambaye angekuwa “msaidizi kando” yao. “Mfariji ambaye Kristo aliahidi kumtuma baada ya kupaa mbinguni, Roho katika utimilifu wote wa Uungu, akidhihirisha uwezo wa neema ya kiungu kwa wote wanaopokea na kuamini katika Kristo kama Mwokozi binafsi.” (Evangelism, uk. 615).

Wapendwa, Roho wa Mungu yuko kwa ajili yetu. Yeye ni msaidizi, mfariji, mshauri, mnasihi, mpatanishi, mhimizaji, na mtetezi wetu mkuu. Sikiza sasa: anakuombea, hata wakati ukitafakari somo hili. Hataki doa lolote la dhambi ndani yako. Anatamani uweze kuungama na kutubu dhambi zako, na kumpokea Yesu Kristo kama Bwana na Mwokozi wako. Anatamani uweze kuokolewa na kuupata uzima wa milele. Je utamsikiliza Yeye sasa?

HATUA YA MAAMUZI: Ni mwitikio gani unaodhani Somo hili ingepaswa kutuhimiza kufanya?  [1] Amini kwamba Mungu alitutumia “Msaidizi mwingine” ili awe pamoja nasi milele; [2] Amini kwamba Yeye ni “Roho wa kweli,’ ikiwa na maana kwamba atatuongoza katika kweli yote (16:13); [3] Mkubali Yeye; jisalimishe Kwake sasa Naye atakudhihirishia mambo ya Mungu.

MAAMUZI YANGU LEO.

Weka tiki kwenye kisanduku sahihi kinachoakisi uamuzi wako leo:

 • Naamini kwamba Roho Mtakatifu ni Mungu.
 • Yeye ni wa milele (Ebr. 9:14).
 • Yeye ni Mwenevu (Zab. 139:7–13).
 • Yeye ni Mtaalifu (1 Kor. 2:10).
 • Yeye ni Jalali (Luka 1:35; Rum. 15:19).
 • Yeye ni Mfariji wangu (Matendo 9:31; 2 Cor 1:3).
 • Yeye ni Mtakasaji wangu (Eze. 37:28; Rum. 15:16).
 • Hunisaidia katika udhaifu wangu (Rum. 8:26-27)
 • Ananiombea na kunifanyia upatanisho (Rum. 8:26-27)
 • Yeye ni Rafiki, Muumbaji, Mungu, Mkombozi wangu. Nasalimisha maisha yangu Kwake.

WIMBO WA KUFUNGA:  – Roho Mtakatifu, Kiongozi Amini. (NZK #41)

1. Roho Mtakatifu, Kiongozi Amini; Utushike Mkono Tulio Wasafiri. [Utupe Kusikia Sauti Ya Upole; “Msafiri Fuata, Naongoza Nyumbani].”

2. Wewe Ndiwe Rafiki, Msaada Karibu; Tusiache Shakani; Na Tukiwa Gizani; [Utupe Kusikia Sauti Ya Upole; “Msafiri Fuata, Naongoza Nyumbani].”

3. Siku Zetu Za Kazi, Zikiwa Zimekwisha, Wala Hatuna Tamaa Ila Mbingu Na Sala; [Utupe Kusikia Sauti Ya Upole; “Msafiri Fuata, Naongoza Nyumbani].”

Iweni na Siku Yenye Baraka: “Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho Mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa. Na yeye aichunguzaye mioyo aijua nia ya Roho ilivyo, kwa kuwa huwaombea watakatifu kama apendavyo Mungu.” (Warumi 8:26–27)

Sauti ya Injili/ Mwongozo wa Kujifunza Biblia/ Mafundisho Makuu/ Dibaji ya Numatolojia: (Fundisho kuhusu Roho Mtakatifu)/ Somo # 1