Hulka ya Shetani.

HULKA YA SHETANI.

Mwongozo wa Kujifunza Biblia/ Fundisho kuhusu Malaika: Shetani/ 76-014 (Yohana 8:44)/ Andiko Msingi: “Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo.” (Yohana 8:44)

Malengo: Kusudi la somo hili ni kujibu swali hili: Je Biblia inasema nini kuhusu hulka ya Shetani?

Vipengele vya Somo:

 1. Asili ya Hulka Yake
 2. Ushahidi wa Hulka Yake
 3. Tabia za Hulka Yake
 4. Nasaba za Hulka Yake
 5. Uwezo wa Shetani wa Uratibishaji

Maelezo ya Ufunguzi: “Endapo mtu huyakubali Maandiko kama ufunuo kutoka kwa Mungu, badala ya rekodi tu ya mawazo ya mwanadamu kuhusu Mungu, basi uhalisia wa Shetani hauwezi kukanwa. Shetani hakuibuka kama kiumbe-nafsi; alikuwepo na alitenda kazi tangu mwanzo kabisa hadi vitabu vya mwisho vya ufunuo wa Mungu. Vitabu saba ya Agano la Kale hufundisha kuhusu uhalisia wake (Mwanzo, 1 Nyakati, Ayubu, Zaburi, Isaya, Ezekieli, Zekaria). Kila mwandishi wa Agano Jipya alithibitisha kuhusu uhalisia na utendaji wake. Fundisho la Kristo pia huafiki na kuthibitisha uwepo na utendaji wa Shetani. Katika aya ishirini na tano kati ya ishirini na tisa katika Injili ambazo humzungumzia Shetani, Bwana wetu anazumgumza. Katika baadhi ya aya hizo hakuna mashaka kwamba Kristo anelekeza fundisho Lake dhidi ya kutojua ama dhana potofu za umati kuhusu Shetani kwa sababu ya imani ya uwili ya Uajemi.” [Charles Caldwell Ryrie, Basic Theology: A Popular Systematic Guide to Understanding Biblical Truth, (Chicago, IL: Moody Press, 1999), 156–157].

ASILI YA HULKA YAKE.

[1] Yeye ni Kiumbe— Ezekieli 28:15 hutamka bayana kwamba Shetani aliumbwa. Hii ina maana kwamba hana hulka zilizo za Mungu pekee, kama vile uenevu, ujalali, na utaalifu. Japo ni kiumbe mwenye uwezo mkubwa, ana mipaka ya kiumbe. Na kwa vile ni kiumbe, lazima awajibike kwa Muumbaji wake.

[2] Yeye ni Nafsi-Pepo— Shetani ni akidamu/ngazi ya malaika wanaoitwa makerubi (Eze. 28:14). Ila shaka ndiye malaika wa juu zaidi aliyeumbwa (v. 12).

[3] Yeye ni Kiongozi wa Malaika Walioanguka— Shetani anaweza kuitwa mkuu wa malaika wote waovu.

[4] Ana Uwezo Mkuu— Hata katika hali yake ya sasa ya anguko, angali na uwezo mkubwa (japo chini ya uradhi wa Mungu). Hivyo anaitwa mungu wa ulimwengu huu na mkuu wa uwezo wa anga (2 Kor. 4:4; Efe. 2:2).

 • “Mkuu wa uwezo wa anga. Shetani sasa ni “mkuu wa ulimwengu huu,” na hadi pale Bwana atakapomtupa nje (Yohana 12:31) ataendelea kutawala. Uwezo (au mamlaka) wa anga pengine hurejelea jeshi la Shetani la pepo wa wachafu wanaostakimu angani. Paulo ana wazo hili katika Waefeso 6:12, anapoonya juu ya “majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.” Katika zama za sasa yeye na jeshi lake la pepo wabaya humdhibiti, hushinikiza, na kumtawala kila mtu ambaye hajaokoka. Yeye ni unasifishaji wa mauti ya kiroho kwa sababu yeye ni unasifishaji wa uasi dhidi ya Mungu—na ndivyo ulivyo mfumo aliouvumbua.” [John F. MacArthur Jr., Ephesians, MacArthur New Testament Commentary, (Chicago: Moody Press, 1986), 56].

[5] Yeye Si Mtaalifu— “Kama walivyo malaika wote, wasioanguka na walioanguka, Shetani ni kiumbe aliyeumbwa na Mungu kupitia Yesu Kristo Mwana wa Milele (Yohana 1:3; Kol. 1:16–17). Aliumbwa akiwa na maarifa na fadhila maridhawa (Eze. 28:11–19), naye alikuwa mkuu zaidi miongoni mwa malaika (28:12), lakini hakuumbwa na uwezo usio na ukomo au kama mwenye maarifa ya kila kitu. Hana ujalali wala utaalifu. Kwamba anakosa utaalifu huonekana katika Mathayo 24:36, ambako Yesu huzungumzia ujio wa pili: “Walakini habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana, ila Baba.” (cf. Marko 13:32).”

“Dhambi kuu ya Shetani ilikuwa katika kiburi ya ukuu akitamani kufanana na Mungu (Isa. 14:12–14), na katika mengi atendayo huiga uwezo na matendo ya Mungu, lakini hawezi kulingana nayo au kuyazidi. Uwezo na wadhifa wake katika uumbaji ni wa pekee lakini una mipaka. Shetani halingani na Mungu na wala hatendi nje ya utawala na mipango ya Mungu. Shetani ni kiumbe junubu ambaye, katika kila sifa na tendo, yuko chini ya Mungu.” [H. Wayne House and Timothy J. Demy, Answers to Common Questions about Angels & Demons, (Grand Rapids, MI: Kregel Publications, 2011), 46].

USHAHIDI WA HULKA YAKE.

[1] Yeye ni Nafsi Halisi – Shetani ni nafsi na ana hulka. Shetani anatajwa kama nafsi katika Agano la Kale na Agano Jipya.

 • Katika Ayubu 1:7, Bwana akamwuliza Shetani, Umetoka wapi wewe?
 • Zingatia kwamba Kristo alitumia viwakilishi vya nafsi katika kuzungumza naye, akimwakifia hulka Shetani. Mathayo 4:1–111 Kisha Yesu alipandishwa na Roho nyikani, ili ajaribiwe na Ibilisi. 2 Akafunga siku arobaini mchana na usiku, mwisho akaona njaa. 3 Mjaribu akamjia akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, amuru kwamba mawe haya yawe mikate. 4 Naye akajibu akasema, Imeandikwa, Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu. 5 Kisha Ibilisi akamchukua mpaka mji mtakatifu, akamweka juu ya kinara cha hekalu, 6 akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu jitupe chini; kwa maana imeandikwa, Atakuagizia malaika Zake; Na mikononi mwao watakuchukua; Usije ukajikwaa mguu Wako katika jiwe. 7 Yesu akamwambia [yeye], Tena imeandikwa, Usimjaribu Bwana Mungu wako. 8 Kisha Ibilisi akamchukua mpaka mlima mrefu mno, akamwonesha milki zote za ulimwengu, na fahari yake, 10 Ndipo Yesu alipomwambia, Nenda zako, Shetani; kwa maana imeandikwa, Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu Yeye peke yake. 11 Kisha Ibilisi akamwacha; na tazama, wakaja malaika wakamtumikia.

NASABA ZA HULKA YAKE.

Kama walivyo malaika wengine, Shetani anabainishwa kuwa na nasaba za hulka:

[1] Ana Werevu – Japo dhambi imepotosha hekima yake asilia, Shetani angali kiumbe mwenye maarifa makubwa ulimwenguni. Pamoja na maarifa yake asilia aliyopewa wakati wa uumbaji, amepata maarifa mengi ya uzoefu katika vita vyake dhidi ya Mungu na mwanadamu katika zama zote baada ya anguko lake.

 • Huonesha Werevu-–“Lakini nachelea; kama yule nyoka alivyomdanganya Hawa kwa hila yake, asije akawaharibu fikira zenu, mkauacha unyofu na usafi kwa Kristo.” (2 Wakorintho 11:3)
 • Alikuwa akitambua kikamilifu kuhusu udhaifu wa Petro—“[Bwana] Akasema, Simoni, Simoni, tazama, Shetani amewataka ninyi apate kuwapepeta kama vile ngano.” (Luka 22:31)
 • Alikuwa akitambua kikamilifu, mfano, juu ya nguvu ya Ayubu— Ayubu 1:6–126 Ilikuwa, siku moja ambayo hao wana wa Mungu walikwenda kujihudhurisha mbele ya Bwana, Shetani naye akaenda kati yao. 7 Bwana akamwuliza Shetani, Umetoka wapi wewe? Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Natoka katika kuzunguka-zunguka duniani, na katika kutembea huku na huku humo. 8 Kisha Bwana akamwuliza Shetani, Je! Umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Kwa kuwa hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na mwelekevu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu. 9 Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Je! Huyo Ayubu yuamcha Bwana bure? 10 Wewe hukumzingira kwa ukigo pande zote, pamoja na nyumba yake, na vitu vyote alivyo navyo? Kazi za mikono yake umezibarikia, nayo mali yake imeongezeka katika nchi. 11 Lakini nyosha mkono Wako sasa, uyaguse hayo yote aliyo nayo, naye atakukufuru mbele ya uso Wako. 12 Bwana akamwambia Shetani, Tazama, yote aliyo nayo yamo katika uwezo wako; lakini usinyoshe mkono wako juu yake yeye mwenyewe. Basi Shetani akatoka mbele ya uso wa Bwana.
 • Ayubu 2:1–71 Tena kulikuwa na siku hao wana wa Mungu walipokwenda kujihudhurisha mbele ya Bwana, Shetani naye akaenda kati yao, ili kujihudhurisha mbele ya Bwana. 2 Bwana akamwuliza Shetani, Umetoka wapi? Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Natoka katika kuzunguka-zunguka duniani, na katika kutembea huku na huku humo. 3 Bwana akamwuliza Shetani, Je! Umemwangalia huyo mtumishi Wangu Ayubu? Kwa kuwa hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na mwelekevu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu; naye hata sasa anashikamana na utimilifu wake, ujapokuwa ulinichochea juu yake, ili nimwangamize pasipokuwa na sababu. 4 Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Ngozi kwa ngozi, naam, yote aliyo nayo mtu atayatoa kwa ajili ya uhai wake. 5 Lakini sasa nyosha mkono Wako, uuguse mfupa wake na nyama yake, naye atakukufuru mbele ya uso Wako. 6 Bwana akamwambia Shetani, Tazama, yeye yumo mkononi mwako; lakini tunza tu uhai wake. 7 Basi Shetani akatoka mbele ya uso wa Bwana, akampiga Ayubu na majipu mabaya tangu wayo wa mguu hata utosi wa kichwa.

[2] Ana Hisia.

 • Shauku – Ana malengo fulani; kuna mambo anayohitaji kuona yanatimizwa. “[Bwana] Akasema, Simoni, Simoni, tazama, Shetani amewataka ninyi apate kuwapepeta kama vile ngano.” (Luka 22:31) “Shetani alitaka kumseta Simon Petro na wanafunzi wengine kama vile punje za ngano. Alitarajia kupata tu makapi ili ayapeperushe. Lakini Yesu alimhakikishia Petro kwamba japo imani yake ingetetereka, isingeangamizwa, maana alisema, “lakini nimekuombea wewe ili imani yako isitindike; nawe utakapoongoka waimarishe ndugu zako.” (Luke, Life Application Bible Commentary, uk. 503).
 • Kiburi – Katika kuelezea sifa za shemasi, Paulo anaorodhesha vizuizi vifuatavyo: “Wala asiwe mtu aliyeongoka karibu, asije akajivuna akaanguka katika hukumu ya Ibilisi.” (1 Timotheo 3:6)
 • Kiburi – Kiburi ilikuwa dhambi #1 iliyosababisha anguko la Lusifa. Kwa sababu ya uzuri wake, hekima, na hadhi ya juu (zaidi ya malaika wote) alipata ushaufu: “Wewe ulikuwa kerubi mwenye kutiwa mafuta afunikaye; Nami nalikuweka hata ukawa juu ya mlima mtakatifu wa Mungu, umetembea huko na huko kati ya mawe ya moto. Ulikuwa mkamilifu katika njia zako tangu siku ile ulipoumbwa, hata uovu ulipoonekana ndani yako. (Ezekieli 28:14–15)
 • Ghadabu Kuu – “Kwa hiyo shangilieni, enyi mbingu, nanyi mkaao humo. Ole wa nchi na bahari! Kwa maana yule Ibilisi ameshuka kwenu mwenye ghadhabu nyingi, akijua ya kuwa ana wakati mchache tu.” (Ufunuo 12:12)
 • ZINGATIA: Shetani ana hasira sana kwa sababu ya kushindwa kwake. “Badala ya kupata majuto na huzuni dhidi ya uovu, alijitumbukiza zaidi na zaidi katika udhalimu. Huendelea mbele kwa uhasama mpya na shadidi katika juhudi zake za kulitesa kanisa la Mungu aliye hai” (SDA BC 7:811). Ndiyo maana tunaaswa “kuwa na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wetu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze.” (1 Petro 5:8)

[3] Huonesha Hisia: HASIRA—“Joka akamkasirikia yule mwanamke, akaenda zake afanye vita juu ya wazao wake waliosalia, wazishikao amri za Mungu, na kuwa na ushuhuda wa Yesu; naye akasimama juu ya mchanga wa bahari.” (Ufunuo 12:17)

 • Maandiko yanasema, Joka alikasirika! Sikiza, Shetani hakupata mafanikio katika jitihada yake ya kumgharikisha mwanamke kwenye mafuriko ya mateso (pia hujulikana kama Zama za Giza). Hivyo juhudi yake maalum inaelekezwa dhidi ya masalia ya uzao wa mwanamke. Katika jaribu la kuliangamiza kanisa la Kikristo, juhudi turufu ya Shetani katika mwelekeo huu haujakamilika bado, mipango ingali ikiendelea, naye ataendeleza mipango hiyo miovu (mateso) katika wakati ujao (Kwa Usomaji wa Ziada: angalia Ufunuo 13:11-17; 16:12-16)
 • Shetani ana HASIRA hususan dhidi ya wale waitunzao Sabato (Amri ya Nne). “Wale wanaoiheshimu Sabato ya Biblia watashutumiwa kuwa maadui wa sheria na utaratibu, na kuwa wanavunja vizuizi vya kimaadili vya jamii, kwamba wanasababisha vurug na upotofu, na kuitisha hukumu za Mungu duniani. Uadilifu wao makini utapingwa kuwa ufidhuli, ukaidi, na kudharau mamlaka. Watashutumiwa kuiasi serikali. Wachungaji wanaokana sharti la sheria ya kiungu watawasilisha mimbarini wajibu wa kusalimisha utii katika mamlaka za kiraia kama zilivyoakifishwa na Mungu. Katika kumbi za sheria na mabaraza ya haki, watunza-amri watawasilishwa vibaya na kuhukumiwa. Visingizio vya uongo vitabandikwa kwenye maneno yao; uzushi wa kutisha utapachikwa kwenye nia zao.” (The Great Controversy Between Christ and Satan, uk. 592).

[4] Ana Utashi – “Kuwa na utashi kuhusu kitu fulani” ni kujaribu kusababisha jambo litokee au mtu fulani atende jambo kutokana na nguvu tu za mawazo, azma, au shauku ya mtu husika.

 • Shetani ana utashi mkubwa na amekusudia kwa dhati
 • Ana malengo mahususi ulimwenguni na hujitahidi kuyatimiza kwa kila namna iwezekanayo
 • Katika somo letu lililopita tuliona jinsi Lusifa anavyoonesha kwamba ana utashi
 • Je unazikumbuka zile “Nita” tano mashuhuri za Lusifa kutoka Isa. 14:13–14:
  • Nitapanda mpaka mbinguni
  • Nitakiinua kiti changu juu kuliko nyota za Mungu
  • Nami nitaketi juu ya mlima wa mkutano
  • Nitapaa kupita vimo vya mawingu
  • Nitafanana na Yeye Aliye juu.
 • Wakati ule Paulo akimwelekeza Timotheo jinsi ya kushughulika na Wakristo wapogofu (waliorudi nyuma), alisema kuwa mpole, ila thabiti, “wapate tena fahamu zao, na kutoka katika mtego wa Ibilisi, ambao hao wametegwa naye, hata kuyafanya mapenzi yake.” (2 Timotheo 2:26)

[5] Ana Kumbukumbu – Mara nyingi tunakumbushwa jinsi Yesu alivyoyajibu majaribu ya Shetani pale jangwani kwa Maandiko (Mathayo 4). Lakini zingatia kwamba Shetani naye alitumia Maandiko!

 • Katika jaribu la pili, Ibilisi alimnukulia Kristo Zaburi 91:11-12. Hivi ndivyo Shetani alimwambia Yesu: “Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu jitupe chini; kwa maana imeandikwa, Atakuagizia malaika Zake; Na mikononi mwao watakuchukua; Usije ukajikwaa mguu Wako katika jiwe.” (Mathayo 4:6)
 • Hakika aliondoa kabisa andiko hili kwenye muktadha wake na kulipindua. Aliondoa maneno – “Wakulinde katika njia Zako zote.” Haya hapa maandiko rasmi: “Kwa kuwa atakuagizia malaika Zake Wakulinde katika njia Zako zote. Mikononi mwao watakuchukua, Usije ukajikwaa mguu Wako katika jiwe.” (Zaburi 91:11–12)

Huu hapa mfano mwingine—ibara ifuatayo hujadili kuhusu pepo wachafu, hawa huwatendea Shetani kazi. Wao ni malaika walioanguka. Wazo tunalojaribu kuthibitisha ni hili: wana kumbukumbu.

 • “Naye alipofika ng’ambo, katika nchi ya Wagerasi, watu wawili wenye pepo walikutana Naye, wanatoka makaburini, wakali mno, hata mtu asiweze kuipitia njia ile. Na tazama, wakapiga kelele, wakisema, Tuna nini Nawe, Mwana wa Mungu? Je! Umekuja kututesa kabla ya muhula wetu?” (Mathayo 8:28–29) “Ni bayana, hata pepo wachafu siyo tu kwamba hutambua uungu wa Yesu, lakini pia walijua ulikuwepo muda ulioteuliwa na Mungu kwa ajili ya hukumu yao Naye angekuwa hakimu wao. Eskatolojia yao ilikuwa na taarifa sahihi, lakini ni jambo moja kuujua ukweli, na ni lingine kabisa kuupenda (cf. Yakobo 2:19).” [John MacArthur Jr., Ed., The MacArthur Study Bible, electronic ed., (Nashville, TN: Word Pub., 1997), 1407].

Katika Ufunuo 12, tunasoma—“Kwa hiyo shangilieni, enyi mbingu, nanyi mkaao humo. Ole wa nchi na bahari! Kwa maana yule Ibilisi ameshuka kwenu mwenye ghadhabu nyingi, akijua ya kuwa ana wakati mchache tu.” (Ufunuo 12:12)

 • Shetani anajua kwamba ana wakati mchache! Alijuaje hili? Kwa sababu ana akili, ana kumbukumbu nzuri, anakumbuka mambo yenye umuhimu mkubwa kwake. Alijifunza Unabii wa Biblia (kabla hatujazaliwa); anaelewa vizuri sana Matukio ya Siku za Mwisho (Mat 24, Luka 3, nk.)
 • Wapendwa, Shetani anajua vizuri sana kwamba ujio wa Kristo u karibu. Ilhali akijua kwamba wakati wake ni mchache, Shetani huzidisha juhudi zake dhidi ya Mungu, anazidisha mashambulizi yake dhidi ya jamii ya wanadamu, hususan masalia, “hao wazishikao amri za Mungu, na imani ya Yesu.” (Ufu. 14:12)

UWEZO WA SHETANI WA URATIBISHAJI.

Ili kufanikiwa katika vita vyovyote, unahitaji kujua udhaifu wa wapinzani, silaha zao, na uwezo wa uratibishaji. Tunahitaji kuelewa uwezo fanidi wa uratibishaji wa Shetani, kwa sababu tunashughulika na adui halisi—Shetani, Hasidi wetu. Shetani ana uwezo mkubwa wa uratibishaji.

Kwanza, Biblia huzungumzia masinagogi, mafundisho, na mafumbo.

 • “Basi Roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani.” (1 Timotheo 4:1)
 • “Naijua dhiki yako na umaskini wako, (lakini u tajiri) najua na matukano ya hao wasemao ya kuwa ni Wayahudi, nao sio, bali ni sinagogi la Shetani.” (Ufunuo 2:9)
 • “Lakini nawaambia ninyi wengine mlioko Thiatira, wo wote wasio na mafundisho hayo, wasiozijua fumbo za Shetani, kama vile wasemavyo, Sitaweka juu yenu mzigo mwingine.” (Ufunuo 2:24) 
 • ZINGATIA: Tutajadili mambo haya 3 (masinagogi ya Shetani, mafundisho, na mafumbo) katika masomo yajayo.

Hebu Zingatia Uwezo wa Uratibishaji wa Shetani katika Maandiko Yafuatayo:

[1] Shetani ndiye kwa urakibu alimweka shaibu Ayubu wa Agano la Kale kwenye majaribu ya moto katika jaribu la kumwangamiza (Angalia Ayubu 1 – 2).

[2] Shetani ndiye aliyepanga na kuongoza uasi wa kwanza dhidi ya Mungu. Uwezo wake wa uratibishaji ulithibitishwa pale alipowashawishi theluthi ya malaika wa mbinguni wajiunge naye.

 • “Na mkia wake wakokota theluthi ya nyota za mbinguni, na kuziangusha katika nchi” (Ufu. 12:4a) Toleo la Biblia la NKJV linasema “mkia wake ulivuta theluthi ya nyota za mbinguni.”
 • Neno kokota katika andiko hili hutokana na neno la Kiyunani suro, lenye maana ya “kuvuta, kukokota, gurugusha, kuburuta, au kubeba kitu fulani.” Pia linapatikana katika Matendo 14:19 pale mwili wa Paulo baada ya kuzimia ulipoburutwa nje ya mji wa Listra na maadui wake. Hivyo, Lusifa aliweza kuwaburuta chini kutoka kwenye hadhi yao tukufu theluthi ya malaika. Waliangushwa na nguvu danganyifu ya Shetani nao wakatupwa nje pamoja naye (Yuda 1:6; 2 Petro 2:4)

[3] Shetani ndiye atakayechochea haraka za Sheria ya Kitaifa ya Jumapili. Atawashtaki na kuwatesa wasabilifu watunza-Sabato. Maandiko huwabainisha kama —“hao wazishikao amri za Mungu, na imani ya Yesu.” (Ufu. 14:12). Anafanya hivi kwa kuunganisha majeshi pamoja na Mnyama wa Nchi Kavu na Mnyama wa Baharini wa Ufu. 13. (Kwa ajili ya usomaji mpana zaidi, angalia Ufu. 12, 13, 14, 17, 18)

[4] Shetani ndiye ataratibu na kuongoza uasi wa mwisho dhidi ya Mungu– baada ya miaka 1000, Shetani ataachiliwa huru kutoka kifungoni kwa “muda mchache.” (Ufu. 20:3). Katika jaribu lake la kuipinga serikali ya Mungu “atatoka kuwadanganya mataifa walio katika pembe nne za nchi” (Ufu. 20:8).

[5] Shetani ndiye atakayejaribu kuushambulia mji wa Mungu. Katika udanganyifu wake wa mwisho, Shetani atatafuta kuwatia shime waovu juu ya kuuteka kwa nguvu ufalme wa Mungu. Ilhali akiyakusanya mataifa ya ulimwengu, atawaongoza dhidi ya mji huu mpendwa (Ufu. 20:8-9). “Waovu waliokataa kikaidi kuingia kwenye Mji wa Mungu kupitia hisani za upatanisho wa kafara ya Kristo, sasa wanaazimu kujipatia fursa ya kuingia na kutawala mashambulizi na vita.” (Questions on Doctrine, uk. 505)

MAANA YA KIIBADA: Harmagedoni. “Wakawakusanya hata mahali paitwapo kwa Kiebrania, Har-Magedoni. Na huyo wa saba akakimimina kitasa chake juu ya anga. Sauti kuu ikatoka katika hekalu, katika kile kiti cha enzi, ikisema, Imekwisha kuwa.(Ufunuo 16:16–17)

Kwa sababu ya uwezo wake wa uratibishaji, Shetani atawashawishi tawala za kidini na hadinifu/za kilimwengu na kuwakusanya kwenye mahali paitwapo kwa Kiebrania “Harmagedoni” —- “Mlima wa Megido.” Maelezo ya kina ya mahali hapa yataongezwa kwenye masomo yajayo.

“Tawala za kidini na hadinifu/za kidunia zote zimeungana na kuratibishwa kuwa jeshi moja chini ya uongozi wa utatu wa kishetani kwa ajili ya vita vya siku kuu ya Mungu Mwenyezi. Hii hutukumbusha andiko katika Zaburi 2:2: “Wafalme wa dunia wanajipanga, Na wakuu wanafanya shauri pamoja, Juu ya Bwana, Na juu ya Masihi Wake.” Vita vya Harmagedoni huakisi pambano lijulikanalo sana kwenye Mlima Karmeli kati ya nabii Eliya na manabii wa Baali (1 Wafalme 18). Suala hili lililosuluhishwa kabisa mara moja kwenye Mlima Karmeli lilipaswa kumtambulisha Mungu wa kweli: “Bwana akiwa ndiye Mungu, mfuateni; bali ikiwa Baali ni Mungu, haya! Mfuateni yeye.” (1 Wafalme 18:21).”

“Suala hilohilo litasuluhishwa katika onesho kuu la vita vya Harmagedoni: Je utatu wa kweli au utatu bandia wa kishetani unapaswa kufuatwa na kuabudiwa? Hatimaye vita vitasuluhisha tatizo aliloanzisha Shetani hapo mwanzo: Je nani aliye mtawala halali wa ulimwengu? Hii huonesha zaidi kwamba vita vya mwisho vya Harmagedoni siyo vita vya kijeshi bali vya kiroho—vita kwa ajili ya kuteka akili za watu. Hitimisho lake litakuwa kama vile vya pambano la Karmeli katika wakati wa Eliya pale watu waliokusanyika Mlimani Karmeli walipotambua kwamba “Bwana ndiye Mungu, Bwana ndiye Mungu.” (1 Wafalme 18:39).” [Ranko Stefanovic, Revelation of Jesus Christ: Commentary on the Book of Revelation, Second Edition., (Berrien Springs, MI: Andrews University Press, 2009), 502–503].

SAUTI YA INJILI: Wapendwa, pambano la kutisha liko mbele yetu. Tunakaribia vita vya Harmagedoni. Shetani na jeshi lake la uovu (mamlaka na tawala za dunia) wako katika upinzani mkali dhidi ya Mungu wa mbinguni. Hivyo, wamejawa chuki dhidi ya wote wamtumikiao Bwana katika roho na kweli; wale wanaosimama pamoja na Yesu katika Mlima Sayuni; wale wamfuatao Mwanakondoo kila aendako (Ufu. 14:4); “hao wazishikao amri za Mungu, na imani ya Yesu.” (Ufu. 14:12).

Hivi karibuni sana, vita kuu vya mwisho kati ya wema na uovu, vitapiganwa. Shetani atawaweka wengi kwenye vifungo vya gereza. Wengi watauawa kwa ajili ya imani yao. Hakuna sababu ya kutaharuki, kwa sababu Kristo alitahadharisha kuhusu mambo haya: “Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili Yangu. Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu.” (Mathayo 5:11–12) “Usiogope mambo yatakayokupata; tazama, huyo Ibilisi atawatupa baadhi yenu gerezani ili mjaribiwe, nanyi mtakuwa na dhiki siku kumi. Uwe mwaminifu hata kufa, Nami nitakupa taji ya uzima.” (Ufunuo 2:10)

Je “Sauti ya Injili” leo ni ipi? Hii hapa, Kristo anazungumza, sikiza kwa makini. Anasema, “Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake.” (Ufunuo 16:15) Wapendwa, tunapaswa kuwa makini na kujihadhari vinginevyo tutadanganywa na Shetani. Tunapaswa kudumisha mavazi yetu yawe safi, yaani, tuendelee kuwa waaminifu kwa Mungu, tukiwa thabiti katika imani na tabia, tukishika amri Zake, na kujihudhurisha ili tuvikwe haki Yake.

HATUA YA MAAMUZI: Ni mwitikio gani unaodhani sura hii ingepaswa kutuhimiza kufanya? [1] Soma Biblia kwa bidii; [2] Jifunze somo kuhusu Shetani—mtambue adui; [3] Tubu dhambi zako; [4] Jihadhari—juu ya mafundisho potofu; [5] Jiandae kuteseka kwa ajili ya Kristo kama ipo haja; [6] Wapashe wengine habari kuhusu Pambano Kuu (vita visivyoonekana), na hitaji la kuwa tayari kwa ajili ya Yesu sasa kabla hujachelewa sana! Bwana akubariki.

 • “Watu wa Mungu hawana budi kusikia ushuhuda thabiti, makini kwa ajili ya ukweli, ukifunua makusudi ya Mungu kwa ushahidi wa kalamu na sauti. Sehemu moja baada ya nyingine wanapaswa kutangaza ujumbe wa Neno la Mungu, wakiwaamsha wanaume na wanawake waitambue kweli…
 • Kuna uhalisia katika mafundisho imara. Siyo kama mvuke, utowekao. Nuru haina budu kuangaza kutoka kwenye Neno la Mungu. Mungu huwaita watu Wake wamkaribie Yeye. Hebu yeyote asiingilie kati Yake na watu Wake. Kristo anabisha mlangoni mwa moyo, akitafuta kuingia. Je utamruhusu? [This Day with God, uk. 308].

Uwe na Siku Yenye Baraka: “Kesheni basi (zingatieni kwa makini, chukueni tahadhari na iweni amilifu), kwa maana hamjui ni siku ipi (ama karibu au mbali) atakayokuja Bwana wenu… Kwa sababu hiyo ninyi nanyi jiwekeni tayari; kwa kuwa katika saa msiyodhani Mwana wa Adamu yuaja.” (Mathayo 24:42, 44, AMP)

Sauti ya Injili/ Mwongozo wa Kujifunza Biblia/ Fundisho kuhusu Malaika: Shetani/ Somo # 14.