Dhambi na Anguko la Shetani

DHAMBI NA ANGUKO LA SHETANI

Mwongozo wa Kujifunza Biblia/ Fundisho kuhusu Malaika: Shetani/ 76-013 (Isaya 14:13–15)/ Andiko Msingi: “Nawe ulisema moyoni mwako, Nitapanda mpaka mbinguni, Nitakiinua kiti changu juu kuliko nyota za Mungu; Nami nitaketi juu ya mlima wa mkutano, Katika pande za mwisho za kaskazini. Nitapaa kupita vimo vya mawingu, Nitafanana na Yeye Aliye juu. Lakini utashushwa mpaka kuzimu; Mpaka pande za mwisho za shimo.” (Isaya 14:13–15)

Malengo: Katika somo hili tunadurusu wadhifa wa awali wa Lusifa, na kuchunguza dhambi na anguko la kimaadili la Lusifa. Katika masomo yajayo, kwa neema ya Mungu, tutaangalia juu ya hulka, shughuli, na vita kubwa zaidi ya kilimwengu kati ya Kristo na Shetani: Pambano Kuu.

Vipengele vya Somo:

 1. Maswali ya Msingi
 2. Dhambi ya Shetani: Kiburi.
 3. Dhambi ya Shetani: Ubinafsi
 4. Dhambi ya Shetani: Udhalimu
 5. Matokeo ya Anguko la Shetani
 6. Kushindwa kwa Shetani
 7. Maana ya Kiibada (Wakati wa Kuchagua)

Maelezo ya Ufunguzi: “Picha katika Isaya 14:1–23 ni ufalme wenye nguvu ambao kiburi chake kiliuletea uangamivu. Hiki ndicho kilichomtokea Belshaza pale Dario Mmedi alipoikamata Babeli mnamo mwaka 539 K.K. (Dan. 5). Isaya anaelezea kufika kwa mfalme huko sheoli, makao ya wafu, ambako utajiri, utukufu, na mamlaka ya mfalme yalitoweka. Wafalme wafu walio tayari huko sheoli walisimama kumpata heshima (Isa. 14:9), lakini yote yalikuwa dhihaka. Mauti ni msawazishaji; hakuna wafalme katika ulimwengu wa wafu. “Lusifa” (v. 12) ni neno la Kilatini lenye maana ya “nyota ya asubuhi” na hupendekeza kwamba utukufu wa mfalme huyu haukudumu muda mrefu.”

“Nabii aliona katika tukio hili kitu fulani cha kina zaidi kuliko kushindwa kwa ufalme. Katika anguko la ufalme wa Babeli, aliona kushindwa kwa Shetani, “mkuu wa ulimwengu huu,” anayetafuta kuwatia nguvu na kuwahamasisha viongozi wa mataifa (Yohana 12:31; Efe. 2:1–3). Danieli 10:20 huonesha kwamba Shetani amewafawidhi “wakuu” (malaika walioanguka) kwa mataifa mbalimbali ili kuwashawishi viongozi watende kinyume na mapenzi ya Mungu.”

“Mkuu zaidi miongoni mwa malaika wa Mungu alijaribu kujitwalia enzi ya Mungu na kujichukulia ibada iliyo stahiki ya Mungu pekee (Mat. 4:8–10).” [Warren W. Wiersbe, Be Comforted, “Be” Commentary Series, (Wheaton, IL: Victor Books, 1996), 45–46].

Muhtasari wa Biblia kuhusu Pambano Kuu (Seh. 1).

MUHTASARI/MASWALI YA MSINGI

[1] Kristo anamzungumziaje Shetani hapo mwanzo? (Yohana 8:44).

 1. Alikuwa muuaji tangu mwanzo
 2. Ukweli haukuwa ndani yake
 3. Lugha-asilia ya Shetani ni udanganyifu
 4. Shetani ni baba wa uongo

[2] Isaya anamzungumziaje Shetani hapo mwanzo? (Isa. 14:12–15).

 1. Shetani amekuwa na enzi tangu mwanzo
 2. Shetani alitamani kujitwalia enzi ya Mungu
 3. Shetani alitamani kuwa Mungu: “Nifanana na Yeye Aliye juu.”
 4. Matokeo: Shetani alianguka kutoka mbinguni
 5. Alishusha hadi kwenye nchi
 6. Alidhoofisha mataifa
 7. Atashusha chini hadi Sheoli, kwenye vina vya chini kabisa vya Kuzimu

[3] Ezekieli anamzungumziaje Shetani hapo mwanzo? (Eze. 28:12–19).

 1. Wakati fulani alikuwa kielelezo/muhuri wa ukamilifu
 2. Alikuwa amejaa hekima na mkamilifu katika uzuri
 3. Alikuwa Edeni, bustani ya Mungu
 4. Alikuwa amefunikwa na “kila kito cha thamani”
 5. Alikuwa kerubi mpwa-mafuta afunikaye
 6. Alikuwa kwenye mlima mtakatifu wa Mungu
 7. Alitembea huku na huko kati ya mawe ya moto
 8. Alihudumu katika enzi ya Mungu (Patakatifu)
 9. Akiwa kerubi mlinzi, alikuwa akisimamia Sheria ya Mungu
 10. Alikuwa na kiburi kwa sababu ya uzuri wake
 11. Alikuwa mwovu na kueneza uzushi (dhidi ya Mungu)
 12. Alitupwa kutoka kwenye nafasi yake kama kerubi mlinzi kwenye enzi ya Mungu
 13. Aliingia Bustani ya Edeni duniani

[4] Yohana anamzungumziaje Shetani hapo mwanzo? (Ufu. 12:1–17).

 1. Aliwashawishi malaika wengi kuja upande wake (Ufu. 12:4–10).
 2. Shetani na malaika wake walipigana dhidi ya Kristo (Mikaeli) na malaika Wake huko mbinguni
 3. Shetani na malaika wake walipoteza nafasi yao mbinguni (cf. Yuda 6, 9)
 4. Shetani amekuwa akitenda dhambi tangu mwanzo (1 Yohana 3:8).

[5] Musa anamzungumziaje Shetani baada ya kutupwa kutoka mbinguni? (Mwa. 3:1–6).

 1. Shetani alimshawishi Hawa, naye anatajwa kama nyoka mwenye hila.
 2. Hii huthibitishwa kwa kirai “nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani” Ufu. 12:9).
 3. Hawa alidanganywa, siyo Adamu (1 Tim. 2:14).
 4. Shetani alisababisha mashaka katika Neno la Mungu, hivyo kupelekea anguko la wanadamu.

DHAMBI YA SHETANI: KIBURI

[1] Nini chanzo cha kiburi cha Lusifa? Uzuri na hekima yake.

Lusifa alikuwa adinati zaidi miongoni mwa malaika wote lakini alitumia vibaya uzuri wake. Uzuri wake alipewa kwa kusudi ili kukidhi nafasi yake ya “kerubi afunikaye” (Eze. 28:14). Somo: Mungu anapotukirimia uzuri Wake maalum, hulka, talanta, sifa, nk., tunapaswa kutafuta kwa nini na hivyo kutumia sifa hizo kumhimidi Mungu.

Uzuri wa Lusifa na hekima yake vilimpatia kiburi – alikoma kufurahia ukamilifu wa Mungu na alianza kupendezewa na ukamilifu wake mwenyewe, aliopewa na Mungu. Yesu hakufanya hivi, “Nimemweka Bwana mbele yangu daima” (Zab. 16:8).

Wapendwa, Mungu huwashutumu watu wenye kiburi (1 Tim. 3:6). Yeye “huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema.” (1 Petro 5:5). Yeye humchukia mtu mwenye kiburi, kwa sababu kiburi huhafifisha utukufu wa Mungu, na kumletea mtu huyo uangamivu — “Kiburi hutangulia uangamivu; Na roho yenye kutakabari hutangulia maanguko.” (Mithali 16:18).

Wapendwa, hatuna budi kutupa chini “mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii Kristo” (2 Wakorintho 10:5).

Sikiliza Biblia toleo lijulikanalo kama Amplified Bible: “Kadiri ambavyo sisi tunapinga hoja na nadharia na fikra na kila kitu cha kiburi na kilicho juu kijiinuacho dhidi ya maarifa ya kweli ya Mungu; na kuongoza kila wazo na kila kusudi kiwa mateka katika kumtii Kristo (Masihi, Mpakwa-Mafuta)” (2 Wakorintho 10:5, AMP). Ni wazi, Lusifa hakufanya hivi. Lakini tunaweza kufanya vyema zaidi!!

DHAMBI YA SHETANI: UBINAFSI

[2] Je nini matokeo ya kiburi chake? Shauku ya ubinafsi.

Katika Isa. 14:12–14, Shetani anazungumza “nita” mara tano ambayo hudhihirisha shauku zake za kibinafsi: “Jinsi ulivyoanguka kutoka mbinguni, Ewe nyota ya alfajiri, mwana wa asubuhi! Jinsi ulivyokatwa kabisa, Ewe uliyewaangusha mataifa! Nawe ulisema moyoni mwako, Nitapanda mpaka mbinguni, Nitakiinua kiti changu juu kuliko nyota za Mungu; Nami nitaketi juu ya mlima wa mkutano, Katika pande za mwisho za kaskazini. Nitapaa kupita vimo vya mawingu, Nitafanana na Yeye Aliye juu.” (Isaya 14:12–14)

 1. Nitapanda mpaka mbinguni. Akiwa kama kerubi mlinzi afunikaye, Shetani alikuwa na fursa ya kuingia mbinguni. Tuliona kwamba alikuwa akihudumu katika Patakatifu Mno (walimokuwamo makerubi). “Kupanda mpaka mbinguni” huonesha shauku yake ya kuhodhi na kustakimu mbinguni katika usawa pamoja na Mungu.
 • Nitakiinua kiti changu juu kuliko nyota za Mungu. Hii huweza kuwa na maana ya mambo mawili– (a) “Nyota” hurejelea malaika (Ayubu 38:7; Yuda 13; Ufu. 12:3–4; (b) “Nyota” hurejelea magimba yang’aayo angani. Katika kila namba/fasiri la neno “nyota,” ni dhahiri kwamba Shetani alitamani kutawala uumbaji wote wa Mungu. Alikusudia kupanda juu zaidi, kumshinda Mungu, na kuanzisha enzi yake!
 • Nami nitaketi juu ya mlima wa mkutano, Katika pande za mwisho za kaskazini. Hii huonesha shauku ya Shetani ya kutawala ulimweng kama inavyodhaniwa kwamba ilifanywa na baraza la miungu ya Babeli. Alikusudia kuketi juu ya mlima wa mamlaka ya ulimwengu.
 • Nitapaa kupita vimo vya mawingu. Alitaka utukufu uliokuwa stahiki ya Mungu tu (mara nyingi mawingi yanahusianishwa na uwepo wa Mungu, (angalia Kut. 16:10; Isa. 19:1).
 • Nitafanana na Yeye Aliye juu. Hapa mfano-bandia wa Shetani ni bayana kabisa. Kuna ufanano wa kushangaza kati ya lugha hii na ile iliyotumiwa katika 2 Wathesalonike 2:4, kuhusu mpinga-Kristo: “yule mpingamizi, ajiinuaye nafsi yake juu ya kila kiitwacho Mungu ama kuabudiwa; hata yeye mwenyewe kuketi katika hekalu la Mungu, akijionyesha nafsi yake kana kwamba yeye ndiye Mungu.” (2 Wathesalonike 2:4) Hii ndiyo sababu vita kati ya Kristo na Shetani ni binafsi—kwa vile kiumbe (Shetani) anataka kujitwalia mamlaka ya Muumbaji wake (Kristo) na kumnyang’anya utukufu, heshima, na ibada ambavyo ni stahiki Yake. “Kufanana na Yeye Aliye juu,” ni kutamani kuwa– siyo kama Mungu—bali kuwa Mungu! Hivi ndivyo Lusifa alivyokuwa mpumbavu.

DHAMBI YA SHETANI: UDHALIMU

[3] Nini kilichotokea wakati akitafakari haya yote? Udhalimu ulipatikana ndani yake.

 • Ulikuwa mkamilifu katika njia zako tangu siku ile ulipoumbwa, hata uovu ulipoonekana ndani yako. Kwa wingi wa uchuuzi wako watu walikujaza udhalimu ndani yako, nawe umetenda dhambi; kwa sababu hiyo nimekutoa kwa nguvu katika mlima wa Mungu, kama kitu kilicho najisi; Nami nimekuangamiza, Ewe kerubi ufunikaye, utoke katika mawe hayo ya moto. (Ezekieli 28:15–16)

“Huko mbinguni kerubi afunikaye katika enzi ya Mungu aliumbwa na aliendelea kuwa mkamilifu hadi uovu ulipoonekana ndani yake, naye akaanza kumkashfu Mungu. Alifukuzwa kutoka kwenye mlima wa enzi wa Mungu kwa sababu ya kiburi (uasi, Isa. 14:15–17). Kiburi chake hudhihirishwa katika Isaya 14:13–14… Kerubi mwasi huyu huko mbinguni alitaka kuwa kama Mungu ili kuichukua nafasi Yake.” [Norman R. Gulley, Systematic Theology: God as Trinity, (Berrien Springs, MI: Andrews University Press, 2011), 497].

[4] Udhalimu ni nini? Kabla ya kulijibu swali hili, hebu zingatia Swali la Moyoni lifuatalo: Je kuna viwango vya dhambi? Je Mungu huona dhambi zote kuwa sawa? Kwa maneno mengine, dhambi moja siyo mbaya kuliko nyingine, ndivyo?

 • Kiwango #1 (DHAMBI): Dhambi humaanisha “kukosa lengo” na ni lugha ya jumla kwa ajili ya kutofikia kiwango cha Mungu. Warumi 3:23 inasema, “wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu.” Dhambi inaweza kuwa ya makusudi au siyo ya makusudi (Hesabu 15:27). Dhambi siyo tu kufanya kitu fulani kibaya, bali pia ni kushindwa kufanya jambo sahihi (Yakobo 4:17).
 • Kiwango #2 (MAKOSA): Makosa humaanisha kukaidi kwa kusudi au kukiuka amri kwa kudhamiria. Daudi alikuwa akizungumzia aina hii ya dhambi alipoandika, “Heri aliyesamehewa dhambi, Na kusitiriwa makosa yake.” (Zaburi 32:1). Makosa yanahusiana na ukiukaji, ikiwa na maana uhalifu wa sheria kwa makusudi. Tumepewa sheria ili kutuonesha kosa lilivyo (Wagalatia 3:19).
 • Kiwango #3 (UDHALIMU):  Udhalimu ni upotoshaji wa kweli na mwenendo pindifu unaofikiria na kupanga kutenda dhambi. Udhalimu ni mienendo ya asili inayotusukuma kurudia kutenda dhambi na kunajisi tabia. Mienendo hii potofu bila shaka huweza kurithishwa kizazi hadi kizazi.
 • Mika 2:1 inasema, “Ole wao wakusudiao mambo maovu, na kutenda mabaya vitandani mwao.” Usengenyaji, kashfa, kulaani, na ukosoaji ni udhalimu. Yakobo 3:6 inasema, “Nao ulimi ni moto; ule ulimwengu wa uovu.” Maneno mengi tuyasemayo yanaweza kusababisha mizizi ya udhalimu kustawi.

[5] Je udhalimu husababisha nini? Udhalimu husababisha uasi, kukosa hofu ya Mungu, huba zisizo za asili, na nia potofu (Warumi 1:28-32). “Kwani kuasi ni kama dhambi ya uchawi, Na ukaidi ni kama ukafiri na vinyago; Kwa kuwa umelikataa neno la Bwana, Yeye naye amekukataa wewe usiwe mfalme.” (1 Samweli 15:23, AMP)

UASI WA SHETANI

Huu hapa muhtasari mfupi wa kile ambacho tumejifunza hadi hapa:

 1. Shetani alitaka kufanana na Mungu
 2. Alitaka kuwa na nguvu kama Mungu
 3. Alitaka kujitwalia mamlaka na ufalme wa Mungu
 4. Alitaka kuabudiwa, haki ambayo iliyo halali kwa Mungu pekee
 5. Alitaka kutumia mamlaka na kuutawala ulimwengu
 6. Dhambi yake ilikuwa upinzani mchaa dhidi ya utawala na mamlaka ya Mungu
 7. Alitamani kufanana na Mungu katika wadhifa, nguvu, na utukufu, lakini siyo kitabia
 8. Alitamani kujipatia akrama ambayo jeshi la malaika walimpatia Mungu
 9. Ilhali akiwa kiumbe, alitafuta kujipatia heshima iliyokuwa stahiki ya Muumbaji tu
 10. Alikusudia moyoni mwake “kufanana na Yeye Aliye Juu” (Muumbaji, Mmiliki na Mtawala wa mbingu na dunia) (Mwa. 14:19; Zab. 83:18).
 11. Badala ya kutafuta kumfanya Mungu awe turufu katika hisia za jeshi la malaika, alijitafutia nafasi ya kwanza katika fikra zao (SDA BC 4:171).

Kifupi, Lusifa alikusudia kumshusha chini ya enzi Yake Mwenyezi Mungu na kumhawilisha kwa nafsi yake mwenyewe. Kwa maneno mengine, kiumbe anapanga, anafikiria na kujaribu kumwangusha Muumbaji. Hili halijawahi kusikiwa kamwe!!!

Uasi wa Lusifa:

 1. Aliasi mamlaka ya Mungu
 2. Alijaribu kuangusha ufalme wa Mungu
 3. Alijitahidi sana, lakini uasi wake haukuwa na mafanikio
 4. Uasi huu, kama ambavyo tumeona hapo juu, ulitajwa kuwa ni “udhalimu” (uhalifu), Eze. 28:15, na “dhambi” (uasi wa sheria ya Mungu), Eze. 28:16.

ZINGATIA: Katika uasi huu, Shetani alizindua ufalme ili kushindana na ufalme wa Mungu.

MATOKEO YA UASI WA LUSIFA

[1] Hakuwa tena “Lusifa” (nyota ya asubuhi) bali “Shetani” (hasidi)—Hakuwa tena mwakisi wa utukufu wa Mungu bali mpinzani mkuu wa ufalme wa ufalme wa Mungu, makusudi Yake, nia Yake na watu wa Mungu.

[2] Shetani aliachiwa hekima (Eze. 28:17), hata hivyo, ilikuwa hekima potofu. Sasa hekima yake ilitumika kueneza uovu na wala siyo wema.

[3] Shetani alikuwa mdhambi wa kwanza—Alikuwa wa kwanza miongoni mwa viumbe wa Mungu kupinga mamlaka ya Mungu. Yeye, ilhali akiwa mdhambi wa kwanza, akawa “baba” wa wadhambi, (Yohana 8:44). “(Laki) atendaye dhambi (ahusishaye na mienendo ya uovu) ni wa Ibilisi (huiga tabia yake kutoka kwa yule mwovu); kwa kuwa Ibilisi hutenda dhambi (amekiuka sheria ya kiungu) tangu mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa (alionekana), ili azivunje (aharibu, alegeze, na kusambaratisha) kazi (ambazo amefanya) Ibilisi.” (1 Yohana 3:8, AMP)

[4] Alinajisi hekalu la Mungu kwa wingi wa udhalimu wake (Eze. 28:18)

[5] Kupitia mfano wake mbaya wa uovu na ushawishi mbaya, Shetani alisababisha anguko la theluthi ya malaika. — “Kwa maana ikiwa Mungu hakuwaachilia malaika waliokosa, bali aliwatupa shimoni, akawatia katika vifungo vya giza, walindwe hata ije hukumu.” (2 Petro 2:4) “Na mkia wake wakokota theluthi ya nyota za mbinguni, na kuziangusha katika nchi.” (Ufu. 12:4)

[6] Shetani alitupwa kama “kitu kilicho najisi” kutoka kwenye mlima wa Mungu(Eze. 28:16)—alifukuzwa kutoka kwenye wadhifa wake/nafasi yake. Badala yake, aliruhusiwa kudumisha mamlaka yake ya utawala juu ya walaika walioanguka (Mat. 12:24).

Kuhusu anguko la Lusifa, Kristo anasema: “Nilimwona Shetani, akianguka kutoka mbinguni kama umeme.” (Luka 10:18)

[7] Shetani alishutumiwa na kuhukumiwa kwa ajili ya kuangamizwa—dhambi huleta hatia, hukumu, na adhabu.

Shetani alipotenda dhambi, mambo matatu yalitokea: alitangazwa kuwa na hatia (Eze. 28:16); alihukumiwa (1 Tim. 3:6), naye aliandikiwa adhabu ya kuangamizwa: “Nimetokeza moto kutoka ndani yako, nao umekuteketeza, Nami nimekufanya kuwa majivu juu ya nchi, machoni pa watu wote wakutazamao.” (Eze. 28:18)

 • Uangamivu wa mwisho wa kudumu wa kerubi huyu aliyeanguka umetabiriwa katika lugha ya Kiebrania “hali timilifu kinabii”—njeo ya wakati uliopita imetumika kuonesha tukio la wakati ujao kana kwamba tayari limetokea kwa sababu ni hakika kabisa kwamba litatokea.” [Jon L. Dybdahl, Ed., Andrews Study Bible Notes, (Berrien Springs, MI: Andrews University Press, 2010), 1078].

Kitabu cha Ufunuo kinasema: “Na yule Ibilisi, mwenye kuwadanganya, akatupwa katika ziwa la moto na kiberiti, alimo yule mnyama na yule nabii wa uongo. Nao watateswa mchana na usiku hata milele na milele.(Ufunuo 20:10)

ZINGATIA: Hukumu ya Shetani itatekelezwa mara moja baada ya utawala wa Kristo wa Milenia.

KUSHINDWA KWA SHETANI

Sikiza wapendwa, kushindwa kwa Shetani kulishangiliwa mbinguni baada (siyo kabla), lakini baada ya tukio la msalaba. Wakati ule ambapo Mikaeli (Yesu Kristo) alipokufa msalabani, na kutamka maneno “IMEKWISHA,” hakika yote yalikuwa yameisha kwa Ibilisi. Alikuwa ameshinda vita kwa kiwango kikubwa! Hii ndiyo sababu kwaya ya mbinguni ilisikika ikiimba kwa ushindi: “Nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema, Sasa kumekuwa wokovu, na nguvu, na ufalme wa Mungu wetu, na mamlaka ya Kristo Wake; kwa maana ametupwa chini mshitaki wa ndugu zetu, yeye awashitakiye mbele za Mungu wetu, mchana na usiku. (Ufunuo 12:10)

Hata hivyo, ufalme wa Shetani ungalipo kwa muda kitambo. Pale Mikaeli atakapokuja mara ya pili, atawatuma malaika watakaomtupa Shetani “kuzimu, akamfunga, akatia muhuri juu yake, asipate kuwadanganya mataifa tena, hata ile miaka elfu itimie; na baada ya hayo yapasa afunguliwe muda mchache.” (Ufunuo 20:3)

Mikaeli atakapokuja mara ya pili, mwishoni mwa miaka 1000, uwepo wa Shetani (kama tujuavyo) utakuwa umefikia mwisho. “Na yule Ibilisi, mwenye kuwadanganya, akatupwa katika ziwa la moto na kiberiti, alimo yule mnyama na yule nabii wa uongo. Nao watateswa mchana na usiku hata milele na milele.” (Ufunuo 20:10)

Habari njema hizi hapa: hivi karibuni sana Yesu Kristo atawaweka maadui Wake wote chini ya miguu Yake na kuhudhurisha kwa Baba uumbaji uliokombolewa, ambaye tangu wakati huo na kuendelea atatawala kwa uturufu usiopingwa. “Hapo ndipo mwisho, atakapompa Mungu Baba ufalme Wake; atakapobatilisha utawala wote, na mamlaka yote, na nguvu. Maana sharti amiliki Yeye, hata awaweke maadui Wake wote chini ya miguu Yake. Adui wa mwisho atakayebatilishwa ni mauti.” (1 Wakorintho 15:24–6)

MAANA YA KIIBADA: Kwa nini Mungu asingeweza kufanya kingine zaidi? Kwa nini Kristo hakumpatia Lusifa muda zaidi ili kutubu? — “Ulikuwa mkamilifu katika njia zako tangu siku ile ulipoumbwa, hata uovu ulipoonekana ndani yako. Kwa wingi wa uchuuzi wako watu walikujaza udhalimu ndani yako, nawe umetenda dhambi; kwa sababu hiyo nimekutoa kwa nguvu katika mlima wa Mungu, kama kitu kilicho najisi; Nami nimekuangamiza, Ewe kerubi ufunikaye, utoke katika mawe hayo ya moto.” (Ezekieli 28:15–16)

“Hapakuwepo tumaini lolote la ukombozi kwa wale waliokuwa wameshuhudia na kufurahia utukufu mkuu usioelezeka wa mbinguni, na waliokuwa wameona usajifu mkuu wa Mungu, na, katika uwepo wa utukufu wote huu, walikuwa wamemwasi. Hayakuwepo maonesho yoyote mapya na ya ajabu ya nguvu taalifu ya Mungu ambayo yangeweza kuwagusa kwa kina sana wale ambao tayari walikuwa wamepata uzoefu huo. Kama waliweza kuasi katika uwepo hasa wa utukufu usioelezeka, wasingeweza kuwekwa katika hali bora zaidi ili kuthibitishwa. Haikuwepo nguvu ya ziada, wala havikuwepo vimo virefu zaidi na vina vya utukufu halidi ili kutiisha mashaka yao ya husuda na manung’uniko ya uasi.” (SDA BC 4:1163)

SAUTI YA INJILI: Wapendwa, Mungu hatavumilia dhambi milele. Hakuruhusu vurugu, uovu na dhambi mbinguni. Pale rehema ya Lusifa ilipoisha, alitupwa (alifukuzwa) kutoka kwenye maskani ya mbinguni. Vilevile, Mungu hatavumilia dhambi wakati wote kwa kizazi hiki cha siku za mwisho. Lazima tutubu sasa na kumtii. Roho anasihi na kila mmoja wetu akisema: “chagueni hivi leo mtakayemtumikia” (Yoshua 24:15).

Mlango wa rehema bado ungali umefunguliwa, na Yesu Kristo bado angali pale juu — (katika Patakatifu mbinguni) – akiomba na kufanya upatanisho kwa ajili ya kila mmoja wetu, ili tuamke kutoka usingizini mwetu, kutoka kwenye njia zetu za uovu, kutubu na kumkubali Yeye kama Bwana na Mwokozi wetu

Kipindi hiki cha rehema (kama ilivyokuwa katika siku za Nuhu, Luka 17: 28-32) hivi karibuni kitafikia mwisho, maana Kristo akiondoka Patakatifu hapatakuwepo tena Mpatanishi, au Mwombezi. Anapotamka maneno haya “Imekwisha!” (Ufu. 16:17), kwa kweli itakuwa imekwisha! Yote yatakuwa yamekwisha! Utakuwa umechelewa sana!

Punde ulimwengu wote utasikia maneno haya: “Mwenye kudhulumu na azidi kudhulumu; na mwenye uchafu na azidi kuwa mchafu; na mwenye haki na azidi kufanya haki; na mtakatifu na azidi kutakaswa.” (Ufunuo 22:11). Tutasikia tarumbeta ya Malaika mkuu; Mfalme Yesu ataonekana mawinguni ili kuwachukua wateule Wake nyumbani; lakini waovu wataangamia pamoja na Ibilisi. Na kisha —- “Ndipo kutakapokuwa na kilio na kusaga meno” (Luka 13:28).

Wapendwa, muda ni sasa! Sikiza maneno ya Kristo wakati tunapofunga: “Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake.” (Ufunuo 16:15)

HATUA YA MAAMUZI: Ni mwitikio gani unaodhani sura hii ingepaswa kutuhimiza kufanya? Wakati wa kuchagua. Vita kati ya Kristo na Shetani ni halisi. Wapendwa, nadhani hili ni somo la Biblia muhimu sana maishani mwako. Kuna vita halisi vya kiroho kwa kila mmoja wetu, kila dakika, kila siku moja. Kuna pande mbili! Kuna viongozi wawili! Kuna njia mbili tu za kupita! Habari njema ni hii: tunajua kwamba wale walio katika Kristo Yesu hatimaye hushinda vita na kuishi milele pamoja Naye mbinguni. Wale wasiofanya hivyo watakufa (angamia) pamoja na Shetani na malaika wake waovu.

Kwa vile tuko katika mada ya kuchagua, hebu tufunge na kisa cha Wapotevu Wawili katika kirai: “Maana umesema moyoni mwako”

[1] Mfano wa kwanza ni Lusifa (Isa. 14:12) Moyo wake ulikuwa umejaa kiburi na ujeuri. Hivyo “alikusudia moyoni mwake” kuwa kama Mungu. Matokeo: alianguka na kupoteza wadhifa wake/hadhi yake kuu mbinguni.

[2] Mfano wa pili ni mwana mpotevu aliyetubu na kurejea, ambaye moyo wake ulijaa unyenyekevu, baada ya kutafakari kuhusu uasi wake. Sikiza alichosema: “Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena; nifanye kama mmoja wa watumishi wako.” (Luka 15:18–19) Nasi tunakumbuka kisa chote: alikaribishwa nyumbani kwenye familia ya Mungu, akasamehewa, akakumbatiwa! Hiki ndicho hasa anachohitaji Mungu kwa kila mmoja wetu.

Je utakuwa kuwa mnyenyekevu na kusamehewa, au utakuwa na kiburi kama Lusifa na kuangamia? Unataka kuwa kwenye kundi gani leo? Ni uchaguzi wako! Hebu Mungu atusaidie kuchagua kwa busara kabla hatujachelewa! Amina.

Uwe na Siku Yenye Baraka: “Malaika wa saba akapiga baragumu, pakawa na sauti kuu katika mbingu, zikisema, Ufalme wa dunia umekwisha kuwa ufalme wa Bwana wetu na wa Kristo Wake, Naye atamiliki hata milele na milele.” (Ufunuo 11:15)

Sauti ya Injili/ Mwongozo wa Kujifunza Biblia/ Fundisho kuhusu Malaika: Shetani/ Somo # 13.