Hali ya Asili ya Shetani.

Mwongozo wa Kujifunza Biblia/ Fundisho kuhusu Malaika: Shetani/ 76-012 (Ezekieli 28:14-15)/ Andiko Msingi: “Wewe ulikuwa kerubi mwenye kutiwa mafuta afunikaye; Nami nalikuweka hata ukawa juu ya mlima mtakatifu wa Mungu, umetembea huko na huko kati ya mawe ya moto. Ulikuwa mkamilifu katika njia zako tangu siku ile ulipoumbwa, hata uovu ulipoonekana ndani yako.” (Ezekieli 28:14–15)

Malengo: Katika somo hili tunachunguza asili, wadhifa, na anguko la kimaadili la Lusifa. Katika somo linalofuata, tutaangalia kuhusu dhambi ya Lusifa.

Vipengele vya Somo:

 1. Dibaji ya Ezekieli 28:12-19.
 2. Shetani au Mfalme wa Tiro?
 3. Maswali ya Msingi (Patakatifu).
 4. Hali Asilia ya Shetani
 5. Wadhifa wa Juu wa Lusifa (Nyongeza)
 6. Maana ya Kiibada.

Maelezo ya Ufunguzi: Mara nyingi maswali ya namna mbili huulizwa kuhusu Shetani: “Kwa nini Mungu alimwumba Ibilisi, na kwa nini Mungu hamwangamizi?” Jibu rahisi kwa maswali haya yangekuwa: “Hakufanya hivyo, na Atamwangamiza!”

DIBAJI YA EZEKIELI 28:12-19.

Maandiko mawili ya AK ni muhimu sana katika kuelewa asili, wadhifa, na anguko la kimaadili la Lusifa (Isa. 14:4–21; Eze. 28:12–19). Hebu tuanze kwa kuangalia chimbuko la Lusifa na anguko lake kama inavyobainishwa na nabii Ezekieli.

Katika kitabu chake, Ezekieli anatabiri ujio wa hukumu kwa mji mwovu wa Tiro katika sura ya 26, 27 na sehemu ya kwanza ya sura ya 28. Tayari hii imetimizwa, maana mji huo ulishambuliwa na Nebukadneza mnamo mwaka 573 K.K. na baadaye kuangamizwa na Aleksanda mnamo mwaka 332 K.K. Lakini katika aya ya 12-19 ya Ezekieli 28, nabii anaenda ng’ambo ya mandhari ya duniani akitamka hukumu kwa mfalme (au mkuu) wa Tiro katika wakati huo (ambaye jina lake lilikuwa Ithabaali II). Ezekieli anatuelezea uumbaji na hukumu ya kiumbe mwovu na katili asiye mwanadamu ambaye jina lake tunagundua baadaye kuwa Lusifa.

Mara nyingi Mungu hutumia njia ya mbadala—yaani, humzungumzia Shetani kupitia mhusika mwingine. Mfano, katika Mwanzo 3, Mungu alimtamkia Ibilisi hukumu kwa kumsemesha nyoka. Mfano mwingine ni katika Mathayo 16:23, pale Yesu alipomkemea Shetani ilhali akizungumza na Simoni Petro.

Katika Ezekieli 28 Mungu alimtumia mfalme (mkuu) wa Tiro ili kuwasilisha unabii mpana zaidi– kwa kweli, kumfikia Ibilisi. “Mwanadamu, umfanyie maombolezo mfalme wa Tiro, umwambie, Bwana MUNGU asema hivi; Wewe wakitia muhuri kipimo, umejaa hekima, na ukamilifu wa uzuri.” (Ezekieli 28:12)

SHETANI au MFALME WA TIRO?

[1] Je Mfalme wa Tiro ni nani? Je andiko hili huzungumzia nini? Kuna mijadala mingi leo kuhusu endapo Ezekieli 28:11–19 inamzungumzia Shetania au la. Swali ni kwamba, hivi Ezekieli ilihusu kiongozi mwanadamu halisi kihistoria, au ilikuwa pia na kiumbe mwingine mkubwa zaidi, Shetani?

“Aya ya 11–19, japo imewasilishwa kama maombolezo juu ya mfalme wa Tiro, kwa nadra huweza kuishia kwa mkuu wa Tiro kimatumizi. Taashira husika hutaabadi (hupita) kwa mbali sana rejea husika mahalia kiasi kwamba maelezo kama “kinyume shadidi” hushindwa kujibu maswali yaliyoundwa endapo matumizi mahalia yote yakiavizwa kwenye andiko hili.”

“Kauli ifuatayo huonekana kipekee kuwa ngumu kuiaviza kwa “mfalme wa Tiro” yeyote halisi: (1) “Ulikuwa ndani ya Adeni, bustani ya Mungu,” v. 13; (2) “Wewe ulikuwa kerubi mwenye kutiwa mafuta afunikaye; Nami nalikuweka hata ukawa juu ya mlima mtakatifu wa Mungu,” v. 14; (3) “Ulikuwa mkamilifu katika njia zako tangu siku ile ulipoumbwa, hata uovu ulipoonekana ndani yako,” v. 15; (4) “nimekutoa kwa nguvu katika mlima wa Mungu, kama kitu kilicho najisi; nami nimekuangamiza, Ewe kerubi ufunikaye,” v. 16.”

“Inaonekana kwamba wakati Ezekieli akitazama tabia na shughuli za mfalme halisi wa Tiro katika njozi, Uvuvio uliinua pazia kati ya vinavyoonekana na visivyoonekana naye nabii huyu aliruhusiwa kuona kiumbe asiyeonekana lakini mwenye nguvu kuu ambaye mfalme wa Tiro alimtumikia. Halikadhalika, Isaya alikuwa ameruhusiwa kuona fauka/ng’ambo ya mfalme halisi wa Babeli (sura ya 14:4) kwa Shetani, ambaye tabia na sera zake alizitekeleza mfalme wa Babeli (vs. 12–16).”

“Hivyo inaonekana kuwa rahisi zaidi kuzingatia andiko husika kwamba linahama kutoka katika unabii juu ya mkuu wa Tiro hadi sasa historia ya yule ambaye hakika alikuwa mfalme halisi wa Tiro, Shetani mwenyewe.  Linapoeleweka hivyo, andiko hili hutupatia historia ya asili, wadhifa wa awali, na anguko la malaika ambaye baadaye alikuja kujulikana kama Ibilisi na Shetani. Mbali na andiko hili na lile katika Isa. 14:12–14, tungeachwa bila kisa kamili kimantiki kuhusu chanzo, hali ya awali, na sababu za anguko la mkuu wa uovu. Rejea za AJ kwa kiumbe huyu (Luka 4:5, 6; 10:18; Yohana 8:44; 1 Yohana 3:8; 2 Petro 2:4; Yuda 6; Ufu. 12:7–9; nk.), japo ni patanifu na unabii huu wa kale, kwa zenyewe hazitupatii historia kamili.” [Francis D. Nichol, Ed., The Seventh-Day Adventist Bible Commentary, (Review and Herald Publishing Association, 1977), 4:675].

MASWALI YA MSINGI.

[1] Je kuna Patakatifu mbinguni? Ndiyo.

 • “Basi, katika hayo tunayosema, neno lililo kuu ndilo hili: Tunaye kuhani mkuu wa namna hii, aliyeketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Ukuu mbinguni, mhudumu wa patakatifu, na wa ile hema ya kweli, ambayo Bwana aliiweka wala si mwanadamu.” (Waebrania 8:1–2)

[2] Hivi Patakatifu duniani palikuwa “nakala ile ya kweli” mbinguni? Ndiyo.

 • “Kwa sababu Kristo hakuingia katika patakatifu palipofanyika kwa mikono, ndio mfano wa patakatifu halisi; bali aliingia mbinguni hasa, aonekane sasa usoni pa Mungu kwa ajili yetu.” (Waebrania 9:24)
 • “Nao na wanifanyie patakatifu; ili nipate kukaa kati yao. Sawasawa na haya yote nikuonyeshayo, mfano wa maskani, na mfano wa vyombo vyake vyote, ndivyo mtakavyovifanya.” (Kutoka 25:8–9)
 • “Watumikiao mfano na kivuli cha mambo ya mbinguni, kama Musa alivyoagizwa na Mungu, alipokuwa tayari kuifanya ile hema; maana asema, Angalia ukavifanye vitu vyote kwa mfano ule uliooneshwa katika mlima.” (Waebrania 8:5)
 • “Ambayo ndiyo mfano wa wakati huu uliopo sasa; wakati huo sadaka na dhabihu zinatolewa, zisizoweza kwa jinsi ya dhambi kumkamilisha mtu aabuduye.” (Waebrania 9:9)

[3] Wadhifa wa Shetani mbinguni ulikuwa nini? Alikuwa kerubi mwenye upako afunikaye.

[4] Alihudumu wapi? Alihudumu kwenye Mlima wa Mungu.

[5] Mlima wa Mungu ni nini? Patakatifu, Hekalu, Maskani.

 • “Utawaingiza, na kuwapanda katika mlima wa urithi Wako, Mahali pale ulipojifanyia, Ee Bwana, ili upakae, Pale patakatifu ulipopaweka imara, Bwana, kwa mikono Yako.” (Kutoka 15:17)
 • “Lakini itakuwa katika siku za mwisho, ya kwamba mlima wa nyumba ya Bwana utawekwa imara juu ya milima, nao utainuliwa juu ya vilima; na watu wa mataifa watauendea makundi makundi. Na mataifa mengi watakwenda na kusema, Njoni, twende juu mlimani kwa Bwana, na nyumbani kwa Mungu wa Yakobo; Naye atatufundisha njia Zake, nasi tutakwenda katika mapito Yake; kwa maana katika Sayuni itatoka sheria, na neno la Bwana litatoka Yerusalemu.” (Mika 4:1–2)
 • “Kisha nikaona, na tazama, huyo Mwanakondoo amesimama juu ya mlima Sayuni, na watu mia na arobaini na nne elfu pamoja Naye, wenye jina Lake na jina la Baba Yake limeandikwa katika vipaji vya nyuso zao.” (Ufunuo 14:1)

[6] Je ni mahali gani afanyapo kazi kerubi afunikaye? Patakatifu pa Patakatifu.

 • “Nami nitaonana nawe hapo, na kuzungumza nawe pale nilipo juu ya kiti cha rehema, katikati ya hayo makerubi mawili yaliyo juu ya sanduku la ushuhuda, katika mambo yote nitakayokuagiza kwa ajili ya wana wa Israeli.” (Kutoka 25:22)

[7] Walikuwa wakifanya nini hapo? “Kwa maana makerubi yalinyosha mbawa zao, juu ya mahali pa sanduku, makerubi yakalifunika lile sanduku na miti yake kwa juu.” (1 Wafalme 8:7)

[8] Nini kilikuwemo ndani ya Sanduku la Agano? Sheria ya Mungu – (Amri 10).

[9] Yohana wa Ufunuo aliporuhusiwa kuona mandhari ya hekalu la Mungu mbinguni, aliona nini? “sanduku la agano Lake.” Sanduku la Agano ni kiini cha njozi husika.

 • “Kisha Hekalu la Mungu lililoko mbinguni likafunguliwa, na sanduku la agano Lake likaonekana ndani ya hekalu Lake. Kukawa na umeme, na sauti, na radi, na tetemeko la nchi, na mvua ya mawe nyingi sana.” (Ufunuo 11:19)

[10] Nini kilichokuwemo kwenye Sanduku la Agano? Sheria ya Mungu – (Amri 10).

Tafadhali zingatia yafuatayo:

 • Katika patakatifu pa mfano (duniani), Sanduku la Aganolilikuwa mahali patakatifu mno, palipokuwa kiini cha huduma ya Siku ya Upatanisho kama siku ya hukumu ya mfano.
 • Sanduku la Agano katika patakatifu pa mfano lilikuwa hifadhi ya Amri Kumi, sheria ya Mungu ya maadili isiyobadilika kwa wanadamu wa vizazi vyote. Hakuna mtu amwaminiye Mungu katika nyakati za Wayahudi ambaye angefikiria sanduku la agano bila dhamiri yake kupata utambuzi mara moja kuhusu Amri Kumi.
 • Shetani alihudumu katika mlima mtakatifu wa Mungu (patakatifu). Kwa namna mahususi alihudumu katika Patakatifu Mno pa hekalu la mbinguni kama malaika afunikaye sanduku la agano la Mungu.

[11] Nini kilichohusianishwa na uwepo wa Mungu? Moto.

 • “Ndipo akakwea juu, Musa, na haruni, na Nadabu, na Abihu, na watu sabini miongoni mwa wazee wa Israeli; wakamwona Mungu wa Israeli; chini ya miguu yake palikuwa na kama sakafu iliyofanyizwa kwa yakuti samawi, kama zile mbingu zenyewe kwa usafi wake.” (Kutoka 24:9–10)
 • “Na huo utukufu wa Bwana ukakaa juu ya mlima wa Sinai; lile wingu likaufunikiza siku sita; na siku ya saba akamwita Musa toka kati ya lile wingu. Na kuonekana kwake ule utukufu wa Bwana kulikuwa kama moto uteketezao, juu ya mlima machoni pa wana wa Israeli.” (Kutoka 24:16–17)

HALI YA ASILI YA SHETANI.

 • Ezekieli 28:12–1712 “Mwanadamu, umfanyie maombolezo mfalme wa Tiro, umwambie, Bwana MUNGU asema hivi; Wewe wakitia muhuri kipimo, umejaa hekima, na ukamilifu wa uzuri. 13 Ulikuwa ndani ya Adeni, bustani ya Mungu; kila jiwe la thamani lilikuwa kifuniko chako, akiki, na yakuti manjano, na almasi, na zabarajadi, na shohamu, na yaspi, na yakuti samawi, na zumaridi, na baharamani, na dhahabu; kazi ya matari yako na filimbi zako ilikuwa ndani yako; katika siku ya kuumbwa kwako zilitengenezwa tayari. 14 Wewe ulikuwa kerubi mwenye kutiwa mafuta afunikaye; Nami nalikuweka hata ukawa juu ya mlima mtakatifu wa Mungu, umetembea huko na huko kati ya mawe ya moto. 15 Ulikuwa mkamilifu katika njia zako tangu siku ile ulipoumbwa, hata uovu ulipoonekana ndani yako. 16 Kwa wingi wa uchuuzi wako watu walikujaza udhalimu ndani yako, nawe umetenda dhambi; kwa sababu hiyo nimekutoa kwa nguvu katika mlima wa Mungu, kama kitu kilicho najisi; Nami nimekuangamiza, Ewe kerubi ufunikaye, utoke katika mawe hayo ya moto. 17 Moyo wako uliinuka kwa sababu ya uzuri wako; umeiharibu hekima yako kwa sababu ya mwangaza wako; nimekutupa chini, nimekulaza mbele ya wafalme, wapate kukutazama.”

Hebu tuzingatie maelezo machache ya kina, au virai msingi katika andiko hili kuhusu Lusifa:

[1] Alikuwa muhuri wa ukamilifu (v. 12).

 • KJV inasema–“Wewe ndiye utiaye muhuri jumla ya ukamilifu.”
 • Kitu kinatiwa muhuri kinapokuwa kimekamilika (Danieli 9:24).
 • “Jumla” hubeba dhana ya kipimo kamili cha uzuri, kutokana na mzizi wa Kiebrania, “kupima.”
 • “Mihuri ilitumika kama nembo za mamlaka na uhalali. Kumiliki muhuri wa aali/mkuu ilikuwa ishara ya heshima kubwa, ikiashiria kwamba mhusika alikuwa amekaimishwa kusaini nyaraka kwa niaba yake.” (Block)

[2] Alikuwa amejaa hekima na ukamilifu katika uzuri (v. 12).

 • Alikuwa muhuri wa ukamilifu.
 • Hivyo huyu alikuwa kiumbe avidadi na mwenye mng’ao zaidi miongoni mwa waliowahi kuishi.
 • Neno “kamilifu” ndilo neno husika lililotumiwa kuelezea kafara kamilifu katika patakatifu.

[3] Alikuwa Edeni, bustani ya Mungu (v.13)

 • Neno Edeni humaanisha “taanusi/inayofurahisha.”
 • Ni bustani gani ambayo Ezekieli huitaja hapa? Bustani ya mbinguni.
 • Edeni hapa huzungumziwa “katika maana yake kubwa zaidi kama maskani ya Mungu. Muktadha huonesha kwamba Lusifa bado alikuwa hajaanguka. Uumbaji wa dunia yetu, kustakimishwa kwa wazazi wetu wa kwanza pale Edeni, vilitokea baada ya anguko lake.” (SDA BC 4:675–676).

[4] Alikuwa amefunikwa kwa “kila kito cha thamani:” akiki, yakuti manjano, almasi, zabarajadi, shohamu, yaspi, yakuti samawi, zumaridi, baharamani, dhahabu.

 • Vito tisa miongoni mwa kumi na mbili katika kifuko cha kifuani cha kuhani mkuu vimetajwa hapa.
 • Kwa Kujifunza Zaidi, soma Kut. 28:17-30, ambayo hushabihiana na Kut. 39:10-13.
 • Mtume Yohana katika njozi ya mawe ya msingi ya Yerusalemu mpya, hutumia taswira hiyohiyo (Ufu. 21:19-20).

[5] Ustadi wa “matari na filimbi” uliandaliwa kwa ajili yake, siku alipoumbwa.

 • Dkt. J. Dwight Pentecost anaadika: Ala za muziki vilikusudiwa hapo awali kuwa njia ya kumsifu na kumwabudu Mungu. Haikuwa lazima kwa Lusifa kujifunza kutumia ala za muziki ili kumsifu Mungu. Kama unapenda, alikuwa ameumbiwa ala ya muziki ndani yake, au, alikuwa ala ya muziki yeye mwenyewe! Hivyo ndivyo alivyomaanisha nabii aliposema, “kazi ya matari yako na filimbi zako….” Lusifa, kwa sababu ya uzuri wake, alifanya kile ambacho ala ya muziki ingefanya mikononi mwa mwanamuziki mahiri– kuibua zaburi ya sifa kwa ajili ya utukufu wa Mungu. Lusifa hakuwa na sababu ya kumtafuta mtu fulani ili kutumia ala ya muziki ili aweze kuimba doksolojia– yeye mwenyewe alikuwa doksolojia. (Your Adversary, the Devil, uk. 16)

[6] Alikuwa kerubi mwenye upako na afunikaye (v. 14)

 • Kwa ajili ya utambulisho, utume, na sifa za makerubi angalia Somo # 8.
 • Kerubi (wingi makerubi) ni malaika wa “ndani kabisa” wanaomkaribia Mungu zaidi na kulinda utakatifu Wake.

[7] Alikuwa kwenye mlima mtakatifu wa Mungu (v. 14)

 • Je mlima mtakatifu wa Mungu ni nini? Patakatifu (angalia hapo juu)

[8] Alitembea huku na huko katikati ya mawe ya moto (v. 14).

 • Hadhi yake ya awali ilikuwa ipi? 
 • Alitembea huku na huko kati ya mawe ya moto (Eze. 28:14)

[9] Je “mawe haya ya moto” huweza kuwa nini? Amri 10.

 • “Mlima wa Sinai wote pia ukatoa moshi, kwa sababu Bwana alishuka katika moto; na ule moshi wake ukapanda juu kama moshi wa tanuu, mlima wote ukatetemeka sana.” (Kutoka 19:18)
 • “Hapo Bwana alipokuwa amekwisha zungumza na Musa katika mlima wa Sinai, akampa hizo mbao mbili za ushuhuda, mbao mbili za mawe, zilizoandikwa kwa chanda cha Mungu.” (Kutoka 31:18)
 • “Basi nikageuka nikashuka mle mlimani, mlima ukawaka moto; na zile mbao mbili za agano zilikuwa katika mikono yangu miwili.” (Kumbukumbu 9:15)

[10] Nini umuhimu wa kutembea motoni? Inamaanisha kwamba Lusifa alikuwa mtakatifu, mkamilifu. Shetani alikuwa katika uwepo hasa wa Mungu! Zingatia: Uwepo wa Mungu huteketeza chochote kisicho kitakatifu! “Mungu wetu ni moto ulao.” (Ebr. 12:29).

WADHIFA WA JUU WA LUSIFA.

Hebu tafakari nukuu hizi adhimu kutoka katika Roho ya Unabii:

 • Lusifa huko mbinguni, kabla ya uasi wake, alikuwa malaika mkuu na aliyetukuka, katika heshima akimfuatia Mwana mpendwa wa Mungu. Uso wake, kama ule wa malaika wengine, ulikuwa mwanana na udhihirishao furaha. Paji la uso wake lilikuwa refu na pana, ikionesha akili thabiti. Umbo lake lilikuwa kamilifu; msawazo wake ulikuwa wa pekee na sajifu. Nuru maalum iliang’aa usoni pake na iliangaza kwa uzuri zaidi kumzunguka kuliko ilivyokuwa kuwazunguka malaika wengine; lakini Kristo, Mwana mpendwa wa Mungu, alikuwa na usharifi kuliko jeshi lote la malaika. Alikuwa mmoja na Baba kabla malaika hawajaumbwa.—The Story of Redemption, 13.
 • Lusifa alikuwa kerubi afunikaye, aliyetukuka zaidi miongoni mwa viumbe wa mbinguni; alisimama karibu zaidi na enzi ya Mungu, na alihusiana kwa karibu zaidi na kujinasibisha na utawala wa Mungu, kwa namna maridhawa akiwa amekirimiwa utukufu wa usajifu na uweza.—The Signs of the Times, April 28, 1890.
 • Bwana Mwenyewe alimpatia Shetani utukufu na hekima Yake, na kumfanya awe kerubi afunikaye, mwema, adinasi, na mwenye mvuto sharidi mzuri.—The Signs of the Times, September 18, 1893.
 • Miongoni mwa wakazi wa mbinguni, Shetani alikuwa karibu na Kristo, wakati fulani alikuwa kiumbe wa Mungu aliyepewa heshima kuu zaidi, na alikuwa wa juu zaidi katika mamlaka na utukufu.—The Signs of the Times, July 23, 1902.
 • Lusifa, “mwana wa asubuhi,” katika utukufu upitao malaika wote wanaizungukao enzi, … alikuwa ameungana katika vifungo vya karibu kabisa na Mwana wa Mungu.—The Desire of Ages, 435.
 • Lusifa, “mwana wa asubuhi,” alikuwa wa kwanza miongoni mwa makerubi wafunikao, mtakatifu na asiye na unajisi. Alisimama katika uwepo wa Muumbaji mkuu, na na miali isiyokoma ya utukufu iliyomzunguka Mungu wa milele ilitulia juu yake.—Patriarchs and Prophets, 35.
 • Lusifa alikuwa mkuu zaidi miongoni mwa viumbe wote, naye alikuwa mstari wa mbele kabisa katika kudhihirisha makusudi ya Mungu ulimwenguni.—The Desire of Ages, 758.

MAANA YA KIIBADA: “Ulikuwa mkamilifu katika njia zako tangu siku ile ulipoumbwa, hata uovu ulipoonekana ndani yako. Kwa wingi wa uchuuzi wako watu walikujaza udhalimu ndani yako, nawe umetenda dhambi; kwa sababu hiyo nimekutoa kwa nguvu katika mlima wa Mungu, kama kitu kilicho najisi; Nami nimekuangamiza, Ewe kerubi ufunikaye, utoke katika mawe hayo ya moto. Moyo wako uliinuka kwa sababu ya uzuri wako; umeiharibu hekima yako kwa sababu ya mwangaza wako; nimekutupa chini, nimekulaza mbele ya wafalme, wapate kukutazama.” (Ezekieli 28:15–17)

Hili hapa swali ambalo huulizwa mara nyingi: Kwa vile Mungu ni mtaalifu (hujua vyote), kwa vile alijua kwamba Shetani angeasi na kutenda dhambi, kwa nini alimuumba? Tutajibu swali hili kwa mapana kwenye somo linalofuata. Lakini katika somo hili inatosha kwa sasa kutambua hili: Mungu ni mkamilifu katika njia Zake zote! Alimuumba kiumbe huyu msajifu (wa pekee) aitwaye Lusifa katika utakatifu na ukamilifu wa tabia. Shetani hakuumbwa kama malaika mwovu, kama Ibilisi mwovu. Mungu alimhuluku akiwa kama malaika mkamilifu, mzuri, mwenye hekima na mtukufu. Aliumbwa akiwa kiumbe mtakatifu, asiye na unajisi (GC 493-4; PP 35) asiye na dhambi.

Mungu ni mkamilifu katika utakatifu! Ndiyo maana alimwambia Musa kwenye kichaka kiwakacho moto, “vua viatu vyako miguuni mwako; maana mahali hapo unaposimama ni nchi takatifu” (Kutoka 3:5). Wapendwa, tunapotambua jinsi gani Mungu alivyo mkuu na mtakatifu, tutaelewa jinsi gani tulivyo wadogo.

Sikiza kile Mtume Paulo asemavyo katika Warumi 10: “Kwa maana, wakiwa hawaijui haki ya Mungu, na wakitaka kuithibitisha haki yao wenyewe, hawakujitia chini ya haki ya Mungu.” (Warumi 10:3) Biblia hueleza bayana kwamba watu hawajui utakatifu wa Mungu.

Hatuelewi kwamba “Mungu ni nuru, wala giza lolote wala giza lolote hamna ndani Yake” (1 Yohana 1:5). Yeye ni mkamilifu katika utakatifu. Yakobo 1:13–14 inasema kwamba Mungu hawezi kutenda dhambi. Hawezi hata kujaribiwa kutenda dhambi, na hawezi kumjaribu mtu kutenda dhambi. Wazo tu la dhambi kuwa katika Mungu au kutokana na Mung halifikiriki kwa sababu ya ukamilifu Wake (usalidi).

Nini wazo la msingi hapa? Mungu alimuumba kiumbe mtakatifu, mnyofu, na mkamilifu aitwaye Lusifa. Vilevile, alimuumba mwanadamu (Adamu na Hawa) mkamilifu!

Mungu ni mkamilifu katika yote atendayo! Kazi Yake ya uumbaji ni kamilifu (Kumb. 32:4; Zab. 19:1; 139:14); nia Yake ni kamilifu (Rum. 12:2); sheria Yake ni kamilifu (Zab. 19:7-11); maneno Yake ni makamilifu (Zab. 12:6); na njia Zake ni kamilifu (Zab. 18:30).

HATUA YA MAAMUZI: Ni mwitikio gani unaodhani sura hii ingepaswa kutuhimiza kufanya? Tunapaswa kuuiga ukamilifu wa kimaadili wa Mungu.

[1] Ukamilifu: “Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.” (Mathayo 5:48)

[2] Utakatifu: “Mtakuwa watakatifu; kwa kuwa Mimi Bwana, Mungu wenu, ni mtakatifu.” (Walawi 19:2) “Mtakuwa watakatifu kwa kuwa Mimi ni mtakatifu.” (1 Petro 1:16)

[3] Usajidifu: “Kwa kuwa Mimi ni Bwana, Mungu wenu; takaseni nafsi zenu basi; iweni watakatifu, kwa kuwa Mimi ni Mtakatifu; wala msitie uchafu nafsi zenu kwa kitu kitambaacho cha aina yoyote, kiendacho juu ya nchi. Kwa kuwa Mimi ni Bwana niliyewaleta kutoka nchi ya Misri, ili kwamba niwe Mungu wenu; basi mtakuwa watakatifu, kwa kuwa Mimi ni Mtakatifu.” (Walawi 11:44–45)

[4] Utasbihishaji/Usafishaji: “Basi, wapenzi wangu, kwa kuwa tuna ahadi hizo, na tujitakase nafsi zetu na uchafu wote wa mwili na roho, huku tukitimiza utakatifu katika kumcha Mungu.” (2 Wakorintho 7:1)

Uwe na Siku Yenye Baraka: “Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.” (Warumi 12:2)

Sauti ya Injili/ Mwongozo wa Kujifunza Biblia/ Fundisho kuhusu Malaika/ Shetani/ Somo # 12.