Uumbaji wa Shetani.

UUMBAJI WA SHETANI.

Mwongozo wa Kujifunza Biblia/ Fundisho kuhusu Malaika: Shetani/ 76-011 (Ezekieli 28:14)/ Andiko Msingi: “Wewe ulikuwa kerubi mwenye kutiwa mafuta afunikaye; Nami nalikuweka hata ukawa juu ya mlima mtakatifu wa Mungu, umetembea huko na huko kati ya mawe ya moto.” (Ezekieli 28:14)

Maelezo ya Ufunguzi: Mungu alimwumba malaika mzuri, mkamilifu aitwaye Lusifa. Jina la asili la Shetani lilikuwa “Lusifa” (Isa. 14:12) au, kimsingi, “Nyota ya Asubuhi.” Neno la Kiebrania Hêlel humaanisha “yule ang’aaye,” “mwangavu,” kutokana na halal, “kumulika nuru,” “kuangaza,” “kuwa mwenye mng’ao.” Neno “Lusifa” hutokana na neno la Kilatini, Lusifa, “Mbeba-nuru.”

Shetani hakuumbwa kama malaika mwovu, kama Ibilisi. Mungu alimhuluku kama malaika mkamilifu, mzuri, mwenye hekima na mtukufu. Aliumbwa akiwa mtakatifu, asounajisi (GC 493-4; PP 35) kiumbe asiye na dhambi. (Eze. 28:15) = “Ulikuwa mkamilifu katika njia zako tangu siku ile ulipoumbwa, hata uovu ulipoonekana ndani yako.”

UUMBAJI WA MALAIKA.

[1] Nani aliyewaumba malaika? Yesu Kristo— ZINGATIA: Durusu Somo # kuhusu Uumbaji wa Malaika.

 • Baba alitekeleza kupitia Mwanawe uumbaji wa viumbe wote wa mbinguni. “Kwa kuwa katika Yeye vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na vilivyo juu ya nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana; ikiwa ni vitu vya enzi, au usultani, au enzi, au mamlaka; vitu vyote viliumbwa kwa njia Yake, na kwa ajili Yake.” (Patriarchs and Prophets, 34).
 • Kabla ya uumbaji wa mwanadamu, malaika walikuwepo; maana wakati msingi wa dunia ulipowekwa, “nyota za asubuhi ziliimba pamoja, Na wana wote wa Mungu walipopiga kelele kwa furaha.” Ayubu 38:7. Baada ya anguko la mwanadamu, malaika walitumwa ili kuulinda mti wa uzima, na hapa ni kabla mwanadamu hajafa. Kiasili malaika ni faridi kuliko wanadamu, maana mtunzi wa Zaburi anasema kwamba mwanadamu aliumbwa “punde kuliko malaika.” Zaburi 8:5, NKJV.” (The Great Controversy, 511).
 • Bwana alipowaumba malaika ili kusimamam mbele ya enzi Yake, walikuwa adinati na tukufu. Uzuri wao na utakatifu wao vililingana na hadhi yao iliyotukuka. Walikirimiwa hekima ya Mungu, na kuvishwa deraya ya mbinguni.” (The Signs of the Times, April 14, 1898)

UUMBAJI WA LUSIFA.

[2] Nani aliyemuumba Lusifa (sasa anajulikana kama Shetani)? Aliumbwa na Yesu Kristo.

 • “Lakini kwetu sisi Mungu ni mmoja tu, aliye Baba, ambaye vitu vyote vimetoka Kwake, nasi tunaishi Kwake; yuko na Bwana mmoja Yesu Kristo, ambaye Kwake vitu vyote vimekuwapo, na sisi kwa Yeye huyo.” (1 Wakorintho 8:6) “Kwa kuwa katika Yeye vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na vilivyo juu ya nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana; ikiwa ni vitu vya enzi, au usultani, au enzi, au mamlaka; vitu vyote viliumbwa kwa njia Yake, na kwa ajili Yake. Naye amekuwako kabla ya vitu vyote, na vitu vyote hushikana katika Yeye.” (Wakolosai 1:16–17)
 • Biblia inaelezea mambo mawili muhimu kuhusu Lusifa. Kwanza, yeye ni kiumbe, Mungu anasema, “Nami nalikuweka” (Eze. 28:14). Pili, Mungu alipomuumba alikuwa “mkamilifu/asiye na lawama;” na tatu, uovu haukuonekana ndani yake (Eze. 28:15).
 • Mungu alimwumba (Lusifa) akiwa mwema na mkamilifu, akifanana Naye kadiri iwezekanavyo.” (The Review and Herald, September 24, 1901).
 • Mungu alimwumba (Lusifa) akiwa sharifu, ilhali amemkirimia vipawa tele. Alimpatia wadhifa wa juu wa madaraka. Hakutaka kutoka kwake kitu chochote kisicho mantiki. Alipaswa kutekeleza amana aliyopewa na Mungu katika roho ya unyenyekevu na kicho, akitafuta kuhimiza utukufu wa Mungu, aliyekuwa amempatia utukufu na uzuri na mvuto.” (Sabbath-School Worker, March 1, 1893).
 • Japo Mungu alikuwa amemwumba Lusifa akiwa sharifu na mzuri, na kwamba alikuwa amemtukuza kwa kumpatia heshima ya juu miongoni mwa jeshi la malaika, hata hivyo hakuwa amemweka mbali na uwezekano wa uovu. Ilikuwa katika uwezo wa Shetani (Lusifa), kama angechagua kufanya hivyo, kupotosha karama hizi.” (The Spirit of Prophecy, vol. 4, uk. 317).

[3] Je lini Shetani aliumbwa? Biblia haituambii lini Shetani aliumbwa. Biblia hufundisha kwamba uumbaji wote uliumbwa ukiwa mwema sana na hivyo hali asilia ya Shetani kama malaika ilikuwa sehemu ya uumbaji huo. Malaika wote, pamoja na Shetani, waliumbwa na Mungu Mwenyewe kupitia Kristo (Yohana 1:3; Kol. 1:16–17), kama viumbe watakatifu (Marko 8:38), kabla ya uumbaji wa dunia (Ayubu 38:7), na kwa amri Yake (Zab. 148:2, 5).

Japo hakuna rejea ya wakati iliyobainishwa, wafasiri wengi wa Biblia huielewa Ezekieli 28:11–19 kama rejea kuhusu uumbaji wa Shetani. Ikiwa ndivyo, lazima uumbaji wake ulifanyika kabla ya uwepo wa bustani ya Edeni (Mwa. 2:8) inayozungumziwa na Ezekieli (28:13). [H. Wayne House and Timothy J. Demy, Answers to Common Questions about Angels & Demons, (Grand Rapids, MI: Kregel Publications, 2011), 45–46].

UTAKATIFU WA UUMBAJI WAKE.

[4] Je Biblia inasema nini kuhusu utakatifu wa Lusifa? “Ulikuwa mkamilifu katika njia zako tangu siku ile ulipoumbwa, hata uovu ulipoonekana ndani yako.” (Ezekieli 28:15)

 • Shetani hakuumbwa kama “Shetani” (mpinzani, hasidi) bali kama “Lusifa” (nyota ya alfajiri, mwana wa asubuhi). Baadaye akawa “Shetani” kupitia dhambi yake, kupitia kutumia vibaya uhuru wake aliopewa na Mungu.
 • Lusifa alikuwa kerubi mwenye upako. “Nafasi ya awali ya Shetani inaoneshwa kwa kerubi afunikaye kiti cha rehema katika Hekalu la Kiyahudi. Lusifa, kerubi afunikaye, alisimama katika nuru ya uwepo wa Mungu. Alikuwa mkuu kabisa miongoni mwa viumbe wote, na wa kwanza kabisa katika kudhihirisha makusudi ya Mungu ulimwenguni.” (SDA BC 4:676).
 • Mungu anamwambia Lusifa huyu, “Wewe ulikuwa kerubi mwenye kutiwa mafuta afunikaye; Nami nalikuweka,” …. “ulipoumbwa (Eze. 28:14a; 15a). Kwa maneno mengine, Mungu anamwambia Lusifa huyu: usisahau, Mimi ndiye niliyekuumba. Mimi ndiye niliyekuteua ili kutumika katika hadhi hiyo ya juu.
 • Wapendwa, Mungu alimwumba Lusifa akiwa mkamilifu, na mtakatifu; kisha akamteua ili ahudumu katika Mlima Wake mtakatifu (patakatifu mbinguni). Hivyo, malaika, kama ilivyo kwa wanadamu, uumbaji na utume wao hutoka kwa Mungu na Mungu pekee. Hivi ndivyo Kristo atuambiavyo leo: “Si ninyi mlionichagua Mimi, bali ni Mimi niliyewachagua ninyi; Nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lolote mmwombalo Baba kwa jina Langu awapeni.” (Yohana 15:16)
 • Kristo alimwumba, na Uungu ulimwinua katika wadhifa Wake walimpatia uzuri wake, naye aliishi katikati ya utakatifu na upendo wa Mungu kimahusiano. Alikuwa na kila hamasa ya kufurahia baraka za ajabu alizokirimiwa tele. Inaonekana kwamba Mungu alimpatia vingi sana kiasi kwamba asingekuwa na udhuru wa upinzani ambao Mungu alijua angeanzisha. Ili Shetani aweze kushawishi theluthi ya malaika (Ufu. 12:4a) wawe upande wake lazima ilihusisha mantiki ya hila na subira, na lazima ilihasishwa kwa ahadi yake ya kuboresha hali yao. Maana kwa sababu nyingine watake kuasi? Walikuwa na kila kitu na ni bayana hawakukosa chochote.” [Norman R. Gulley, Systematic Theology: Creation, Christ, Salvation, (Berrien Springs, MI: Andrews University Press, 2012), 136].

NGAZI ZA UUMBAJI WAKE.

Mantiki na Maandiko ya hakika huonesha kwamba uumbaji ulifanyika katika utaratibu ufuatao:

[1] Mbingu ya tatu (mbingu akaapo Mungu) iliumbwa (Zab. 148:4, 5)—Kabla Mungu hajawaumba viumbe Wake, aliumba mahali kwa ajili yao.

[2] Malaika Lusifa (kiumbe aliyeakfishwa kuongoza jeshi la malaika) aliumbwa (Eze. 28:13, 15)—Bila shaka mkuu wa malaika, Eze. 28:14, aliumbwa kabla ya malaika wengine kuumbwa.

[3] Jeshi la malaika waliumbwa (Kol. 1:16)—Hawa wote walikuwa malaika wema hadi pale akisami yao ilipotenda dhambi, 2 Petro 2:4; Yuda 6. ZINGATIA: malaika waliumbwa kila mmoja binafsi, kwa hiyo wao siyo jamaa (kama walivyo wanadamu) bali kundi, Ebr. 12:22.

[4] Mbingu ya pili na jeshi lake la nyota viliumbwa (Zab. 147:4; Zab. 148:3–5)

[5] Angahewa na dunia viliumbwa (Ayubu 38:3–9; Ufu. 10:6)—“Hapo nyota (za mbingu ya pili) za asubuhi zilipoimba pamoja, Na wana wote wa Mungu (malaika wa Mungu) walipopiga kelele kwa furaha,” Ayubu 38:7, wakati Bwana akiumba dunia kuwa maskani ya malaika (na baadaye, kuwa makao ya mwanadamu).

[6] Jamii ya wanadamu iliumbwa (Mwa. 1:27)—Mungu alimwumba Adamu na Hawa, Mwa. 1:27; 5:1, 2, na kutoka kwa Adamu na Hawa ikaja jamii ya wanadamu, Mwa. 1:28. Matendo 17:26. Mwanadamu alikuwa upeo wa mradi wa Mungu wa uumbaji. [Roy E. Gingrich, The History of Satan, (Memphis, TN: Riverside Printing, 2000), 5–6].

MAANA YA KIIBADA: Shetani siyo mwishinafsia; yeye ni kiumbe, siyo Mungu. Shetani aliumbwa akiwa kerubi na mojawapo aliye juu zaidi miongoni mwa malaika. Japo ana uwezo mkuu sana na angali ana uhuru wa muda ulimwenguni, bado yu chini ya utawala wa Mungu na siku moja atahukumiwa milele.

Kabla Dhambi Haijaibuka, Mungu Alikuwa na Mpango:  Yesu Kristo ni “Mwanakondoo (wa Mungu), aliyechinjwa tangu kuwekwa misingi ya dunia.” (Ufunuo 13:8) “Wazo kwamba Mwanakondoo alichinjwa tangu kuwekwa misingi ya dunia linahusiana kikaribu na kauli ya Petro, “…kama ya mwanakondoo asiye na ila…: ambaye hakika aliakifishwasili kabla ya kuwekwa msingi wa ulimwengu (1 Petro 1:19, 20). Uamuzi kwamba Kristo angekufa kwa ajili ya jamii ya wanadamu wenye hatia ulifikiwa kabla ulimwengu huu haujaumbwa, na kuthibitishwa katika wakati ambapo mwanadamu alianguka (angalia PP 63, 64) – (SDA BC 7:819).

“Mungu na Kristo walijua tangu mwanzo, kuhusu uasi wa Shetani na kuhusu anguko la Adamu kupitia nguvu ya udanganyifu wa yule mwasi. Mpango wa wokovu uliandaliwa ili kuikomboa jamii iliyoanguka, ili kuwapatia kipimo kingine. Kristo aliteuliwa katika wadhifa wa Mpatanishi wa uumbaji wa Mungu, aliyewekwa tangu milele kuwa mbadala na mdhamini wetu.” (Selected Messages 1:250).

“Mpango wa ukombozi haukuwa wazohalifi (la kushtukiza), mpango ulioandaliwa baada ya anguko la Adamu. Ulikuwa ufunuo wa “siri iliyokuwa imehifadhiwa katika ukimya kwa nyakati za umilele.” Warumi 16:25. Ulikuwa udhihirisho wa kanuni ambazo kuanzia zama za umilele zimekuwa msingi wa enzi ya Mungu…. Mungu hakuawidhi kwamba dhambi iweze kutokea, bali alitanabihi uwepo wake, na akafanya maandalizi ya kukabili dharura hiyo ya kutisha.” (The Desire of Ages, 22).

SAUTI YA INJILI: Kuepuka Mitego ya Shetani, Sehemu ya 2. Wapendwa, kila siku tunashughulika na kiumbe mwerevu, mlaghari na mwenye chuki kuu aitwaye Ibilisi. Maandiko yanasema kwamba hatuna budi kumzia “Shetani asije akapata nafasi ya kutushinda; maana hatukosi kuzijua hila na makusudi yake.” (2 Wakorintho 2:11, AMP). Lakini tunawezaje kuepuka hila zake, mitego yake? Jibu linapatikana katika 1 Petro — “Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze.” (1 Petro 5:8)

Leo, tutaangalia Sehemu ya 2 ya “Jinsi ya Kuepuka Mitego ya Shetani,” ambayo ni, “Usijishaue.” Maandiko yanasema: “Kiburi hutangulia uangamivu; Na roho yenye kutakabari hutangulia maanguko.” (Mithali 16:18)

Baadhi ya Wakristo hukosa unyenyekevu. Wanatamani sifa na kuheshimiwa na watu, badala ya ukubali wa Mungu: “Walakini hata katika wakuu walikuwamo wengi waliomwamini; lakini kwa sababu ya Mafarisayo hawakumkiri, wasije wakatengwa na sinagogi. Kwa maana walipenda utukufu wa wanadamu kuliko utukufu wa Mungu.” (Yohana 12:42–43)

Yesu, mfano wetu, alikuwa mnyenyekevu. Alitamka kwamba asingeweza kufanya lolote Mwenyewe, bali alimtegemea Baba. Alimpendeza Baba Yake. “Naye aliyenipeleka yu pamoja Nami, hakuniacha peke Yangu; kwa sababu nafanya siku zote yale yampendezayo.” (Yohana 8:29)

Lazima tuwe wanyenyekevu pia. Tunaepuka mitego ya Shetani kwa kufanya mambo yale yampendezayo Mungu na kumpatia nafasi ya kwanza maishani mwetu. “Jidhilini mbele za Bwana, Naye atawakuza.” (Yakobo 4:10)

HATUA YA MAAMUZI: Ni mwitikio gani unaodhani sura hii ingepaswa kutuhimiza kufanya? Jinyenyekeshe mbele ya Bwana! Mkiri Yeye; mtegemee Yeye kikamilifu utashinda vita vinavyochochewa na Ibilisi. “Tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele Yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, Naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu.” (Waebrania 12:2)

Uwe na Siku Yenye Baraka: “Basi mtiini Mungu. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia. Mkaribieni Mungu, Naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu, enyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu, enyi wenye nia mbili.” (Yakobo 4:7–8)

Sauti ya Injili/ Mwongozo wa Kujifunza Biblia/ Fundisho kuhusu Malaika/ Shetani—mpinzani mkuu wa Mungu/ Somo # 11.