Uwepo wa Shetani.

UWEPO WA SHETANI.

Mwongozo wa Kujifunza Biblia/ Fundisho la Malaika: Shetani/ 76-010 (Mathayo 13:39,)/ Andiko Msingi: “Yule adui aliyeyapanda ni Ibilisi; mavuno ni mwisho wa dunia; na wale wavunao ni malaika.” (Mathayo 13:39)

Maelezo ya Ufunguzi: Shetani ni nani? Baadhi ya watu humfikiria kama kibonzo dufu mwenye mkia uliochongoka na pembe, ilhali wengine humfikiria kuwa ni nguvu fulani, au dhana fulani ya uovu. Biblia hutupatia picha dhahiri kwamba Shetani ni nani, vile alivyo, na malengo na makusudi yake kuhusiana na jamii ya wanadamu. Kifupi, hapo awali Shetani alikuwa malaika mtakatifu, lakini akaanguka kutoka mbinguni kwa sababu ya shauku ya kujitwalia mamlaka ya Mungu, na sasa ni adui wa Mungu anayempinga Yeye, anapinga makusudi Yake, na kuwapinga watu Wake kwa kila chembe ya nguvu yake faradi.

Muhtasari wa Somo:

 1. Uhalisia wa Shetani (Kweli/Uongo)
 2. Uwepo wake hutiliwa mashaka ulimwenguni
 3. Uwepo wake hubainishwa na Biblia

UHALISIA WA SHETANI (KWELI/UONGO)

Shetani ni nani? VILE ASIVYO.

 1. Shetani siyo kisasili—Watu wengi huamini kwamba Shetani ni hadithi tu, kiumbe anayedhaniwa tu kwenye fikra za watu na wala siyo uhalisia, lakini hii ni kinyume cha ufunuo wa Biblia kuhusu Shetani.
 • Shetani siyo ubunifu—Baadhi huamini kwamba Shetani ni uvumbuzi tu wa hila za kikuhani, kwamba makuhani na wachungaji walimvumbua Shetani (na jehanamu) ili kuwaogopesha waumini wao na hivyo kuwashikilia chini yao na kuwatii, lakini hili haliko sahihi Kibiblia.
 • Shetani siyo ushirikina—Wengi huamini kwamba Shetani ni ushirikina, aathari ya imani ya kishirikina ya Zama za Kati, lakini hili ni kinyume cha fundisho la Biblia.
 • Shetani siyo kanuni dhahania ya uovu—Baadhi hufundisha kwamba Mungu ni kanuni dhahania ya wema na kwamba jina la Mungu (God) linapaswa kutajwa kwa kutajwa kwa “o” mbili (good) na kwamba Ibilisi ni kanuni dhahania ya uovu na kwamba jin la Ibilisi (Devil) linapaswa kutajwa bila “d” (evil/uovu), lakini imani hizi ni upotoshaji.
 • Shetani siyo zimwi—Yeye siyo mzuka, zimwi, au nafsi iliyovumbuliwa ili kuwaogofya watoto ili watii na kutenda mema.
 • Shetani siyo jinamizi la ajabu—Yeye siyo, kama aoneshwayo katika michoro na mbao za matangazo kama jinamizi, mwenye pembe, kwato na mikia miwili, suti ya asbesto iliyobana, na uma kubwa. Maelezo haya hutoka katika ushairi wa Zama za Kati uitwao “The Inferno,” ulioandikwa na mshairi Mwitaliano Dante.
 • Shetani siyo mada muwala tu kwa ajili ya utani mzuri—Mamilioni ya wat humtumia kwa namna hii (lakini angalia Yuda 9).

VILE ALIVYO.

 1. Satan ni nafsi: Kiumbe mwenye nafsi ana akili, utambuzi, na utashi (washirika wa Uungu, akidamu/ngazi za malaika, na wanafamilia ya wanadamu wana nafsi.) Kwenye Biblia, Shetani huoneshwa akiwa na hulka tatu. Anafikiria, anajua, anapanga, anabuni, ana shauku, anazungumza, anajaribu, anashutumu, nk. Mambo haya yote yanahusiana na nafsi na wala si kanuni fulani dhahania.
 • Shetani ni nafsi asilifaridi: Yeye ni mtu asiye chini ya sheria za asili maana hana mwili yakinifu, lakini anaweza kujiibuka na kuonekana kwa wanadamu na anaweza kuzungumza nao, Mat. 4:1–11.
 • Shetani ni kiumbe-nafsi wa kawaida: Hakuna mahali popote kwenye Biblia ambapo Shetani anaoneshwa kama nafsi bahau na jinamizi, bali nafsi inayokidhi hali zote za hulka. [Roy E. Gingrich, The History of Satan, (Memphis, TN: Riverside Printing, 2000), 4–5].

UWEPO WAKE HUTILIWA MASHAKA ULIMWENGUNI

1. Kama inavyooneshwa na mfano halisi wa “dhana ya katuni ya Walt Disney” – sehemu kubwa zaidi ulimwengu humsawiri Ibilisi kama kiumbe dufu wa kale na wa kubuni mwenye pembe mbili, mkia mithili ya uma, aliyevalia flani nyekundu, akiwa kwenye harakati za kuchopoa makaa ya mawe na kuyatia kwenye tanuri la kuzimu. Shetani hupuuzwa au kuhafifishwa na ulimwengu.

2. Kama inavyooneshwa na ukanushaji katika mimbari za waliberali– Shetani hupuuzwa au kuhafifishwa kwenye makanisa ya waliberali leo. Waliberali hawa wamkanao Kristo, kwa kweli, kwa muda mrefu wamesambaza dhana kama vile “Ibilisi mzee” na “kuzaliwa upya.” Sasa huacha herufi d katika neno “devil” (Ibilisi) na huongeza o kwenye “God” (Mungu). Ni aibu, lakini maneno mengi kama kuzimu, kuhukumiwa, na Ibilisi hayapatikani kwenye misamiati ya watendakazi viwandani, wanasiasa, watoto mashuleni, wanafunzi vyuoni, na hata wanataaluma. Hayasikiki kwenye mimbari za makanisa ya waliberali—ambako yanapaswa kusikiwa. Makanisa haya ya kiliberali ni maeneo ambako watu wanahitaji kusikia maneno haya. Miaka ya hamsini, gazeti la kidunia la taifa lilifanya utafiti wa takriban wachungaji 5,000 Marekani na kugundua kwamba asilimia 73 walidhihaki dhana ya uwepo halisi wa Ibilisi.

3. Kama inavyooneshwa na ukimya kwenye mimbari za wahafidhina– Shetani hata anapuuzwa au kuhafifishwa miongoni mwa waumini wa Biblia. Inavyoonekana, wachungaji wengi waiaminio Biblia na walei, wamepuuza sana “kumpatia Ibilisi haki yake.” Wakati fulani uliopita, mwandishi huyu aliandika makala iitwayo time ago, “Kama Ningekuwa Ibilisi.” Katika makala hii dondoo zifuatazo zinasisitizwa:

 • Jambo la kwanza ambalo ningefanya ni kukana uwepo wangu. Biblia hutuambia kwamba Mungu anatamani, pengine kuliko vingine vyote, aaminiwe kikamilifu. “Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba Yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao.” (Ebr. 11:6). Lakini hivi sivyo kuhusu Shetani! Kiumbe huyu wa mashaka huonekana kustawi pale anapohafuwazwa, anapopuuzwa au kukanushwa.
 • Chukulia kwamba kuna kanisa liaminilo Biblia ambalo hupitia zahama ya kiroho. Kwa miaka kadhaa hakuna mtu ambayo ametembea kwenye shoroba zake. Mahudhurio na sadaka ziko chini na washiriki wanakoswa utulivu. Wachungaji wote wa Bibia wamepitia uzoefu huu. Hatimaye, katika hali ya kukata tamaa, kamati maalum inateuliwa na kutaniko la waumini ili kugundua chanzo cha ubaridi na ufifiaji huu. Baada ya maombi kadhaa na ufuatiliaji, kamati inawasilisha taarifa. Matokeo ni yapi? Naamini inaweza kuwa salama kudhani kwamba kamati ya kawaida itawalaumu wafuatao: (1) mchungaji; (2) viongozi kadhaa; (3) waumini baridi; au (4) ujirani mgumu.
 • Lakini ni kamati gani itafuatayo ukweli itarejesha mambo yafuatayo? “Tunaamini chanzo kikuu cha maumivu yetu ya moyo kwa miezi kadhaa iliyopita ni Shetani! Tunaamini sababu ya roho kutoongolewa hivi karibuni ni kutokana na mashambulizi makuu ya Ibilisi dhidi ya kanisa! Tunafunga taarifa hii kwa pendekezo kuu kwamba waumini waitishe mkutano maalum, wamkemee Shetani, na kusihi damu ya Kristo na kudai ushindi!”
 • Kama ningekuwa Ibilisi ningekana uwepo wangu ulimwenguni na kuuhafifisha katika kanisa mahalia, hivyo kuniweka huru niendelee na shughuli zangu bila kuzingatiwa, kuzuiwa, wala kupingwa. (The Baptist Bulletin, Dec. 1971, uk. 13)

Ushairi ufuatano wa mwandishi asiyejulikana hubainisha vyema mwenendo wa kuukana uwepo wa Shetani:

 • Ibilisi, watu hawaamini uwepo wa Ibilisi sasa, kama baba zao walivyokuwa wakifanya.

Hufungua mlango kwa ajili ya mafundisho mapana zaidi ili kuruhusu usajifu wake uingie.

Hakuna alama yake miguu iliyopasuka wala mshale wa moto kutoka kwenye upinde wake

Upatikanao duniani popote, maana dunia imepiga kura iwe hivyo.

Lakini nani achanganyaye dawa ya kufisha inayoua moyo na ubongo,

Na kuijaza dunia kila mwaka upitao kwa mauaji mamia kumi elfu?

Nani atiaye maradhi kwenye uoto wa nchi leo kwa pumzi ya moto wa kuzimu?

Endapo Ibilisi hayupo na kamwe hayawepo—hebu mtu fulani tafadhali ainuka na kujibu?

Nani afuatiliaye hatua za muumini ataabikaye na kumchimbia shimo miguu yake?

Nani apandaye magugu kondeni ilhali Mungu akipanda ngano safi,

Lakini Ibilisi amepigiwa kura ya kutowepo—na kwa kweli jambo hilo ni kweli –

Lakini nani atendaye mithili ya kazi anayodhaniwa kuifanya Ibilisi?

Hivi mtu fulani hatajitokeza hivi sasa – na kuanza kuonesha ajilani –

Jinsi gani madanganyo na uhalifu wa siku inavyoibuka – maana hakika tunataka kujua!

Ibilisi alipigiwa kura ya kuondolewa – na kwa kweli Ibilisi ametoweka –

Lakini kiukweli jamani tungependa kujua, nani atekelezaye shughuli hizi?

Hali hii ya jumla ya kutojua Maandiko kuhusu nafsi ya Shetani, vyovyote vile, imechangia sana mojawapo ya maendeleo ya kutisha sana katika miongo ya mwisho ya karne ya ishirini, ambayo ni, ibada ya Shetani.

Josh McDowell anaelezea: Katika sura fulani kuhusu Ushetani leo, William Petersen katika Those Curious New Cults anafafanua kuhusu ukweli kwamba tangu katikati ya miaka ya 1960 Ushetani unazidi kujirudia tena. Anaonesha kichocheo kwa ajili ya ongezeko hili kuwa ni mafanikio makubwa ya Rosemary’s Baby, juu ya filamu hii anasema:

 • “Anton Szandor La Vey, kuhani mkuu aliyejilakibu wa San Francisco’s First Church of Satan na mwandishi wa The Satanic Bible, alicheza katika nafasi ya Ibilisi. Baadaye, aliita filamu hiyo ‘tangazo la Ushetani lenye malipo bora kabisa tangu wakati wa Ufatashi.’ Bila shaka ilikuwa hivyo” (uk. 75).

Watu wengi kutoka nyanja zote za maisha wanazidi kujihusisha katika Ushetani. Wanatofautiana kiumri, kazi na msingi wa elimu. (Handbook of Today’s Religions, uk. 237)

Inasemekana Biblia ya Shetani imeuza zaidi ya nakala 250,000 na sasa iko katika uchapaji awamu ya tatu. Kuhusu fundisho la Ushetani, La Vey anaandika: “Ni dini katili na yenye ubinafsi bayana. Imejengwa katika imani kwamba kiasili mwanadamu ni kiumbe mbinafsi, katili, kwamba maisha ni mapambano ya Udarwini kwa ajili ya utawikaji (usalimivu) wa yule aliye bora zaidi, kwamba dunia itatawaliwa na wale wanaopambana ili kushinda” (Ibid., uk. 238).

UWEPO WAKE HUBAINISHWA KWENYE BIBLIA

[1] Ibilisi ametajwa katika vitabu saba vya Agano la Kale– Mwanzo, 1 Nyakati, Ayubu (mara 12), Zaburi, Isaya, Ezekieli, na Zekaria.

[2] Anapatikana katika vitabu 19 vya Agano Jipya na hurejelewa na kila mwandishi wa Agano Jipya.

[3] Anarejelewa na Bwana wetu Yesu Kristo takriban mara 15– hebu zingatia aya husika chache tu.

 • Katika Mathayo 4, Yesu hahojiani na aina fulani ya nguvu jangwani, bali nafsi ovu mwenye jina la Shetani– “Ndipo Yesu alipomwambia, “Nenda zako, Shetani; kwa maana imeandikwa, Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu Yeye peke yake.” (Mathayo 4:10)
 • Katika Mathayo 16, Yesu alitambua kwamba Shetani alikuwa akimdokeza au kumshawishi Simoni Petro amkemee– “Akageuka, akamwambia Petro, “Akageuka, akamwambia Petro, Nenda nyuma Yangu, Shetani; u kikwazo Kwangu; maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu.” (Mathayo 16:23)
 • Katika Luka 22, Yesu anamsemesha tena Simoni Petro– “Akasema, Simoni, Simoni, tazama, Shetani amewataka ninyi apate kuwapepeta kama vile ngano.” (Luka 22:31)
 • Katika Luka 10, Yesu anazungumzia tukio la kumwona Shetani akianguka – “Akawaambia, Nilimwona Shetani, akianguka kutoka mbinguni kama umeme.(Luka 10:18)
 • Katika Mathayo 25, Yesu anazungumzia makazi ya mwisho ya Shetani pamoja na wafuasi wake (wasiookolewa) – “Ondokeni Kwangu, mliolaaniwa, mwende katika moto wa milele, aliowekewa tayari Ibilisi na malaika Zake.” (Mathayo 25:41)
 • Katika Yohana 8, Yesu analishutumu kundi la Mafarisayo waovu kuwa wanatokana na baba yake, Ibilisi– “Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo.” (Yohana 8:44)
 • Katika Yohana 6, Yesu hudhihirisha kwamba mojawapo wa wanafunzi Wake, mmoja miongoni mwa wale kumi na mbili, alikuwa kwa wakati huo (mapema katika huduma Yake) akishawishiwa na Shetani–baadaye, mtu huyo (Yuda) alitawaliwa na Shetani. “Yesu akawajibu, Je! Mimi sikuwachagua ninyi Thenashara, na mmoja wenu ni Shetani? (Yohana 6:70)

Katika Ufunuo 20, tunaona hatima yake: “Na yule Ibilisi, mwenye kuwadanganya, akatupwa katika ziwa la moto na kiberiti, alimo yule mnyama na yule nabii wa uongo. Nao watateswa mchana na usiku hata milele na milele.” (Ufunuo 20:10)

Wapendwa, Shetani ni halisi yuko hai hasa! Hatuwezi kuiamini Biblia na kukana uwepo wa Shetani. “Endapo mtu huyakubali Maandiko kama ufunuo kutoka kwa Mungu, badala ya rekodi tu ya mawazo ya mwanadamu kuhusu Mungu, basi uhalisia wa Shetani hauwezi kukanwa. Shetani hakuibuka kama kiumbe-nafsi; alikuwepo na alitenda kazi tangu mwanzo kabisa hadi vitabu vya mwisho vya ufunuo wa Mungu. Vitabu saba ya Agano la Kale hufundisha kuhusu uhalisia wake (Mwanzo, 1 Nyakati, Ayubu, Zaburi, Isaya, Ezekieli, Zekaria). Kila mwandishi wa Agano Jipya alithibitisha kuhusu uhalisia na utendaji wake. Fundisho la Kristo pia huafiki na kuthibitisha uwepo na utendaji wa Shetani. Katika aya ishirini na tano kati ya ishirini na tisa katika Injili ambazo humzungumzia Shetani, Bwana wetu anazumgumza. Katika baadhi ya aya hizo hakuna mashaka kwamba Kristo anelekeza fundisho Lake dhidi ya kutojua ama dhana potofu za umati kuhusu Shetani kwa sababu ya imani ya uwili ya Uajemi. Zingatia hususan maandiko kama Mathayo 13:39; Luka 10:18; na 11:18.” [Charles Caldwell Ryrie, Basic Theology: A Popular Systematic Guide to Understanding Biblical Truth, (Chicago, IL: Moody Press, 1999), 156–157].

MAANA YA KIIBADA: Je Shetani yupo?

“Biblia hubainisha wazo kwamba Shetani yupo na kwamba yeye ni adudi yetu (Mwanzo 3:15). Anajulikana kama mshtaki wa ndugu zetu (Ufunuo 12:10), na kwa kweli, jina “Shetani” humaanisha “hasidi.” Hapo awali Shetani alikuwa malaika aitwaye Lusifa, lakini alikuwa mshaufu na alitaka utukufu wa Mungu tu. Alimwasi Mungu Naye alitupwa nje ya mbingu pamoja na theluthi ya malaika walioungana naye (Isaya 14:12–17; Ezekieli 28:11–17).

Kuanzia wakati huo, Shetani amefanya kuwa kusudi lake kuwa mpinzani mchaa wa Mungu, akiwadanganya watu na kuwaongoza kwenye uasi dhidi ya Mungu. Paulo anamtaja kama “mungu wa dunia hii” (2 Wakorintho 4:4) na “mfalme wa uwezo wa anga” (Waefeso 2:2).

Silaha ya msingi ya Shetani ni udanganyifu. Anajaribu kutudanganya kuhusu Mungu, vile alivyo yeye, na vile Mungu asemavyo sisi ni nani. Ndivyo alivyomjaribu Adamu na Hawa ili kutenda dhambi hapo awali katika Bustani ya Edeni (Mwanzo 3:1–6). Alijaribu kumdanganya na kumghilibu Yesu wakati akifunga jangwani (Mathayo 4:1–11), na bado anathubutu kutudanganya leo: “hujigeuza awe mfano wa malaika wa nuru.” (2 Wakorintho 11:14). Kihalisia, Shetani ni “baba wa uongo” na hakuna ukweli katika yeye (Yohana 8:44). Hii ndiyo sababu lazima “tuwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wetu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze.” (1 Petro 5:8).

Yesu alikuja duniani ili kuharibu kazi za Ibilisi (1 Yohana 3:8). Bado dunia ingali chini ya utawala wa Shetani na ndivyo itakavyokuwa hadi Yesu arudipo tena kuanzisha ufalme Wake duniani na hatimaye kuunda mbingu mpya na nchi mpya (Yohana 12:31). Habari njema ni kwamba tunaweza kusalimisha maisha yetu binafsi kwa Yesu na kuyaweka chini ya mamlaka Yake. Tunapoishi kwa ajili ya Yesu Kristo, tunaweza kutumaini kwamba Mungu aishiye ndani yetu lini mkuu zaidi kuliko Shetani na hatuna sababu ya kumhofu au kujishinikwa na mashambulizi yake dhidi yetu (Luka 10:17–20; 1 Yohana 4:4). Kadiri tunavyojisalimisha kwa Mungu, tunaweza kumpinga Ibilisi naye atakimbia (Yakobo 4:7).

Kwa kuisoma Biblia, tunaweza kujifunza siyo tu kwamba Shetani yupo; tunaweza kujifunza vile atendavyo kazi. Nguvu ya Mungu daima itakuwa kubwa zaidi kuliko uwezo wa Shetani, lakini tunapaswa kudumu tukitambua kwamba tuko katika vita vya kiroho ambavyo havitakoma hadi Yesu atakaporejea (Waefeso 6:10–18). Tunaweza kuwa na ujasiri katika ukweli kwamba Yesu alimshinda Shetani mara moja na daima kabisa pale msalabani, na pale hukumu ya mwisho itakapofanyika, mwisho wa milele wa Shetani utakuwa umehakikishwa (Ufunuo 19:20; 20:7–10).” [Compellingtruth.org/does-Satan-exist.html]

Uwe na Siku Yenye Baraka: “Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; Mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele.” (Yohana 10:10)

Sauti ya Injili/ Mwongozo wa Kujifunza Biblia/ Fundisho kuhusu Malaika/ Shetani—mpinzani mkuu wa Mungu/ Somo # 10.