Wokovu ni Nini?

Wokovu ni Nini?/ 85-001 (1 Timotheo 2:3–4)/ Fundisho Kuhusu Wokovu-Utangulizi (1/3)/ Mwongozo wa Kujifunza Biblia/ Wokovu/ Mambo Muhimu Kuhusu Wokovu/ Aya Kuu:“Tupilieni mbali nanyi makosa yenu yote mliyoyakosa; jifanyieni moyo mpya na roho mpya; mbona mnataka kufa, enyi nyumba ya Israeli? Maana Mimi sikufurahii kufa kwake afaye, asema Bwana MUNGU; basi ghairini, mkaishi. (Ezekieli 18:31–32) “Hili ni zuri, nalo lakubalika mbele za Mungu Mwokozi wetu; ambaye hutaka watu wote waokolewe, na kupata kujua yaliyo kweli.” (1 Timotheo 2:3–4)

Maelezo ya Ufunguzi: “Wokovu ni mojawapo ya jumbe za msingi katika Biblia. Maandiko humdhihirisha Mungu lakini pia hudhihirisha mpango kwa ajili ya jamii ya mwanadamu, ule wa wokovu. Kwa jinsi hiyo, wokovu ni dhima ya AK na AJ. Kwa sababu ya hali endelevu ya ufunuo, mwanadamu huona nyanja tofauti za mpango wa Mungu, lakini kweli ya kina ya wokovu ipo kote katika maandishi ya Biblia nzima. Mungu ni Mungu wa wokovu mwenye shauku kwamba jamii yote ya wanadamu watubu na kuokolewa (Eze. 18:32; 1 Tm 2:3, 4).” [Walter A. Elwell and Barry J. Beitzel, Baker encyclopedia of the Bible, 1988, 2, 1884].

Katika somo hili la utangulizi tunaangalia katika muhtasari wa mada ya wokovu. Tunagusa tu kwa juu mada hii muhimu sana. Vipengele vya kina zaidi vitaongezwa kwenye masomo yajayo.

[1] Wokovu chimbuko lake ni kwa Mungu — “Wokovu una Bwana; Baraka Yako na iwe juu ya watu Wako.” (Zaburi 3:8) “Na wokovu wa wenye haki una Bwana; Yeye ni ngome yao wakati wa taabu.” (Zaburi 37:39) “Ni kweli, msaada haufai unaotazamiwa kutoka milimani, makutano yenye mshindo juu ya milima; ni kweli, wokovu wa Israeli ni katika Bwana, Mungu wetu.” (Yeremia 3:23)

[2] Wokovu ni kusudi la Mungu — [Mungu] “ambaye alituokoa akatuita kwa mwito mtakatifu, si kwa kadiri ya matendo yetu sisi, bali kwa kadiri ya makusudi yake Yeye na neema Yake. Neema hiyo tulipewa katika Kristo Yesu tangu milele” (2 Timotheo 1:9)

[3] Wokovu ni uteuzi wa Mungu — “Kwa kuwa Mungu hakutuweka kwa hasira Yake, bali tupate wokovu, kwa Bwana wetu Yesu Kristo” (1 Wathesalonike 5:9)

[4] Wokovu ni kwa njia ya Kristo — “Katika mateso yao yote Yeye aliteswa, na malaika wa uso Wake akawaokoa; kwa mapenzi Yake, na huruma Zake, aliwakomboa Mwenyewe; akawainua, akawachukua siku zote za kale.” (Isaya 63:9) “Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe, kama Kristo naye ni kichwa cha Kanisa; Naye ni mwokozi wa mwili.” (Waefeso 5:23)

[5] Wokovu ni kupitia Kristo pekee — “Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.” (Matendo 4:12)

[6] Wokovu siyo kwa matendo — “wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu.” (Waefeso 2:9) “Ambaye alituokoa akatuita kwa mwito mtakatifu, si kwa kadiri ya matendo yetu sisi, bali kwa kadiri ya makusudi yake Yeye na neema Yake. Neema hiyo tulipewa katika Kristo Yesu tangu milele” (2 Timotheo 1:9) “Si kwa sababu ya matendo ya haki tuliyoyatenda sisi; bali kwa rehema Yake, kwa kuoshwa kwa kuzaliwa kwa pili na kufanywa upya na Roho Mtakatifu” (Tito 3:5)

[7] Wokovu ni wa neema — “Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu.” (Waefeso 2:8)

[8] Wokovu ni wa upendo — “Bali Mungu aonyesha pendo Lake Yeye Mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi.” (Warumi 5:8) “Katika hili pendo la Mungu lilionekana kwetu, kwamba Mungu amemtuma Mwanawe pekee ulimwenguni, ili tupate uzima kwa Yeye. Hili ndilo pendo, si kwamba sisi tulimpenda Mungu, bali kwamba yeye alitupenda sisi, akamtuma Mwanawe kuwa kipatanisho kwa dhambi zetu.” (1 Yohana 4:9–10)

[9] Wokovu ni wa rehema — “Bwana urudi, uniopoe nafsi Yangu, Uniokoe kwa ajili ya fadhili Zako.” (Zaburi 6:4) “Si kwa sababu ya matendo ya haki tuliyoyatenda sisi; bali kwa rehema Yake [ametuokoa sisi], kwa kuoshwa kwa kuzaliwa kwa pili na kufanywa upya na Roho Mtakatifu” (Tito 3:5)

[10] Wokovu ni wa Mungu mvumilivu — “Nanyi uhesabuni uvumilivu wa Bwana wetu [ugumu Wake katika kupatiliza makosa na kuuhukumu ulimwengu] kuwa ni wokovu, kama vile na ndugu yetu mpenzi Paulo alivyowaandikia kwa hekima aliyopewa” (2 Petro 3:15, AMP)

[11] Wokovu ni kupitia imani katika Kristo — “Mwamini Bwana Yesu, nawe utaokoka pamoja na nyumba yako.” (Matendo 16:31) “Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka.” (Warumi 10:9)

[12] Wokovu ulitangazwa baada ya anguko — “Nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na Uzao wake; Huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino.” (Mwanzo 3:15)

[13] Wokovu wa Israeli ulitabiriwa— “Waambieni walio na moyo wa hofu, Jipeni moyo, msiogope; tazama, Mungu wenu atakuja na kisasi, na malipo ya Mungu; atakuja na kuwaokoa ninyi.” (Isaya 35:4) “Bali Israeli wataokolewa na Bwana kwa wokovu wa milele; ninyi hamtatahayarika, wala kufadhaika, milele na milele.” (Isaya 45:17) “Na Bwana, Mungu wao, atawaokoa siku hiyo, Kama kundi la watu Wake; Kwa maana watakuwa kama vito vya taji, Vikimetameta juu ya nchi Yake.” (Zekaria 9:16) “Hivyo Israeli wote wataokoka; kama ilivyoandikwa, Mwokozi atakuja kutoka Sayuni; Atamtenga Yakobo na maasia yake.” (Warumi 11:26)

[14] Wokovu wa Mataifa ulitabiriwa — “Zaidi ya hayo nitakutoa uwe nuru ya mataifa, upate kuwa wokovu Wangu hata miisho ya dunia.” (Isaya 49:6b) “Bwana ameweka wazi mkono Wake mtakatifu Machoni pa mataifa yote; Na ncha zote za dunia Zitauona wokovu wa Mungu wetu.” (Isaya 52:10) “Niangalieni Mimi, mkaokolewe, enyi ncha zote za dunia; maana Mimi ni Mungu; hapana mwingine.” (Isaya 45:22)

[15] Wokovu hudhihirishwa katika Injili — “Nanyi pia katika huyo mmekwisha kulisikia neno la kweli, habari njema za wokovu wenu; tena mmekwisha kumwamini Yeye, na kutiwa muhuri na Roho yule wa ahadi aliye Mtakatifu.” (Waefeso 1:13) “Na sasa inadhihirishwa kwa kufunuliwa kwake Mwokozi wetu Kristo Yesu; aliyebatili mauti, na kuufunua uzima na kutokuharibika, kwa ile Injili” (2 Timotheo 1:10)

[16] Wokovu ulikuja kwa Mataifa kufuatia anguko la Wayahudi — “Basi nasema, Je! Wamejikwaa hata waanguke kabisa? Hasha! Lakini kwa kosa lao wokovu umewafikilia Mataifa, ili wao wenyewe watiwe wivu.” (Warumi 11:11)

[17] Upatanisho wa Mungu: ahadi ya wokovu — “Kwa maana ikiwa tulipokuwa adui tulipatanishwa na Mungu kwa mauti ya Mwanawe; zaidi sana baada ya kupatanishwa tutaokolewa katika uzima Wake.” (Warumi 5:10)

[18] Kumkiri Kristo ni muhimu kwa wokovu— “Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu.” (Warumi 10:10)

[19] Kuzaliwa upya ni muhimu kwa wokovu— “Yesu akajibu, akamwambia, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu.” (Yohana 3:3)

[20] Ustahimilivu wa siku za mwisho ni muhimu kwa wokovu— “Nanyi mtakuwa mkichukiwa na watu wote kwa ajili ya jina Langu; lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka.” (Mathayo 10:22)

[21] Wokovu: ulichunguzwa na kudhihirishwa na manabii— “Katika habari ya wokovu huo manabii walitafuta-tafuta na kuchunguza-chunguza, ambao walitabiri habari za neema itakayowafikia ninyi” (1 Petro 1:10)

[22] Injili ni uwezo wa Mungu uletao wokovu— “Kwa maana siionei haya Injili; kwa sababu ni uweza wa Mungu uuletao wokovu, kwa kila aaminiye, kwa Myahudi kwanza, na kwa Myunani pia.” (Warumi 1:16) “Kwa sababu neno la msalaba kwao wanaopotea ni upuzi, bali kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu ya Mungu.” (1 Wakorintho 1:18)

[23] Kulihubiri neno ndiyo njia teule ya wokovu— “Kwa maana katika hekima ya Mungu, dunia isipopata kumjua Mungu kwa hekima yake, Mungu alipenda kuwaokoa waaminio kwa upuzi wa lile neno linalohubiriwa.” (1 Wakorintho 1:21)

[24] Maandiko yana uwezo wa kumhekimisha mtu ili apate wokovu— “na ya kuwa tangu utoto umeyajua maandiko matakatifu, ambayo yaweza kukuhekimisha hata upate wokovu kwa imani iliyo katika Kristo Yesu.” (2 Timotheo 3:15) “Kwa hiyo wekeeni mbali uchafu wote na ubaya uzidio, na kupokea kwa upole neno lile lililopandwa ndani, liwezalo kuziokoa roho zenu.” (Yakobo 1:21)

[25] Sasa ndiyo siku ya wokovu— “Bwana asema hivi, Wakati uliokubalika nimekujibu, na siku ya wokovu nimekusaidia; Nami nitakuhifadhi, nitakutoa uwe agano la watu hawa, ili kuiinua nchi hii, na kuwarithisha urithi uliokuwa ukiwa” (Isaya 49:8). “Kwa maana asema, Wakati uliokubalika nalikusikia, Siku ya wokovu nalikusaidia; tazama, wakati uliokubalika ndiyo sasa; tazama siku ya wokovu ni sasa.” (2 Wakorintho 6:2)

[26] Wokovu (kutoka dhambini) unapaswa kutafutwa kwa kuogopa na kutetemeka— “Basi, wapendwa wangu, kama vile mlivyotii siku zote, si wakati mimi nilipokuwapo tu, bali sasa zaidi sana mimi nisipokuwapo, utimizeni wokovu wenu wenyewe kwa kuogopa na kutetemeka.” (Wafilipi 2:12)

MAANA YA KIIBADA: Wapendwa, Mungu yuko radhi kutupatia wokovu—kuokoa jamii ya wanadamu; lakini ni uchaguzi ambao kila mmoja wetu anahitaji kufanya. Sikiza andiko hili: “Hili ni zuri, nalo lakubalika mbele za Mungu Mwokozi wetu; ambaye hutaka watu wote waokolewe, na kupata kujua yaliyo kweli.” (1 Timotheo 2:3–4) “Ukweli kwamba Mungu anataka kila mmoja aokolewe na kuielewa kweli haimaanishi kwamba wote wataokolewa—Biblia huthibitisha kwamba watu wengi humkataa Kristo (Mathayo 25:31–46; Yohana 12:44–50; Waebrania 10:26–29). Lakini shauku ya Mungu ni kwamba watu wote waweze kuokolewa, Naye ametupatia katika Kristo njia ya wokovu. Kwanza Timotheo 4:10 huonesha kwamba uhakikisho wa wokovu unahusika tu kwa wale wanaoupokea.” [Bruce Barton, Philip Comfort, Grant Osborne, Linda K. Taylor, and Dave Veerman, Life Application New Testament Commentary, (Wheaton, IL: Tyndale, 2001), 936].

SAUTI YA INJILI: Wapendwa, tunaokolewa kwa neema kupitia imani: “Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu” (Waefeso 2:8) “ambaye alituokoa akatuita kwa mwito mtakatifu, si kwa kadiri ya matendo yetu sisi, bali kwa kadiri ya makusudi yake Yeye na neema Yake. Neema hiyo tulipewa katika Kristo Yesu tangu milele” (2 Timotheo 1:9)

Pili, “Maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa” (Tito 2:11). Hii ni rejea kuhusu Utahamilisho, Ujio wa Kwanza wa Yesu Kristo, ambaye kuja Kwake duniani ulitoka kwa Mungu mchaa (moja kwa moja) na kwa namna ya pekee. Kwa kuzaliwa Kwake pale Bethlehemu, ilikuwa sahihi kusema kwamba hakika wokovu ulikuwa umeletwa kwa wanadamu wote.

Neema ya Mungu ni nini?Ni “fadhila Yake wasiyoweza kuistahili waovu, wadhambi, ambapo kwayo huwakomboa kutoka kwenye hukumu na mauti. Lakini neema ya Mungu ni zaidi ya hulka ya kiungu; ni Nafsi ya kiungu, Yesu Kristo. Siyo tu kwamba Yesu Kristo alikuwa Mungu mtahamili bali pia alikuwa neema hamilifu. Yeye Mwenyewe hunasifi na kudhihirisha neema ya Mungu, karama ya kiungu turufu, ya milele, na hastalafu (asiyostahili mtu) ya Yule ambaye ametokea, akiwaletea wanadamu wote wokovu.”

“’Imefunuliwa’ hutokana na epiphainō, ambayo hubeba dhana ya kuja kwenye nuru, hususan ile ya kuwa kubainika katika namna ambayo hapo awali ilikuwa haionekani. Yesu alileta kusudi la Mungu la wokovu kana kwamba kutoka kwenye vivuli, hadi katika nuru timilifu. Mungu “alituokoa akatuita kwa mwito mtakatifu.” [John F. MacArthur Jr., Titus, MacArthur New Testament Commentary, (Chicago: Moody Press, 1996), 107].

HATUA YA MAAMUZI: Ni mwitikio gani unaodhani somo hili lingepaswa kutuhimiza kufanya? [1] Jua kwamba Mungu yuko radhi kutupatia wokovu Wake; Je uko tayari kuipokea karama hii? [2] Kuwa mnyenyekevu: wokovu hupatikana kwa imani; “si kwa kadiri ya matendo yetu sisi, bali kwa kadiri ya makusudi yake Yeye na neema Yake.” Hakuna lolote uwezalo kufanya ili kuununua wokovu. Hauizwi! [3] Amini: wokovu ni kupitia imani katika Yesu Kristo.

[4] Kwa sababu Mungu ametuokoa kwa jinsi ya ajabu, njia sahihi ya kuitikia neema Yake ni kuishi maisha matakatifu. Hatuna budi kusema “Hapana” kwa dhambi na tamaa za kilimwengu. Je neema ya Mungu hutufanyia nini? (v. 12) Hutufundisha kuukana udhalimu — “nayo yatufundisha kukataa na kuukana ubaya (mambo yasiyo ya kiimani) na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi (busara, ya kujitawala), na haki, na utauwa (ukamilifu kiroho), katika ulimwengu huu wa sasa (Tito 2:12, AMP) Wapendwa, siyo tu kwamba neema huleta badiliko la awali maishani mwetu (uongofu); hutuwezesha baada ya hapo kuishi kwa ushindi: ushindi dhidi ya dhambi.

NIFANYE NINI? [1] Mwamini Bwana Yesu Kristo: “Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa.” (Marko 16:16) “Wakamwambia, Mwamini Bwana Yesu, nawe utaokoka pamoja na nyumba yako.” (Matendo 16:31)

[2] Mkiri Bwana Yesu: “Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka.” (Warumi 10:9)

Uwe na Siku Yenye Baraka: “Niangalieni Mimi, mkaokolewe, enyi ncha zote za dunia; maana Mimi ni Mungu; hapana mwingine.” (Isaya 45:22)

Sauti ya Injili/ Mwongozo wa Kujifunza Biblia/ Mafundisho Makuu/ Wokovu/ Mambo Muhimu kuhusu Wokovu/ Somo # 1.