Utangulizi Kwa Bibliolojia.

Utangulizi Kwa Bibliolojia/ 74-001 (2 Timotheo 3:16)/ Mwongozo wa Kujifunza Biblia/ Maandiko/ Utangulizi kwa Bibliolojia (Fundisho Kuhusu Biblia)/ Somo # 1/ Andiko Msingi: “Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu (lililowasilishwa kwa uvuvio), lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki (katika maisha matakatifu, katika kufuata mapenzi ya Mungu katika wazo, kusudi, na tendo)” (2 Timotheo 3:16, AMP)

Teolojia Rakibu wakati mwingine imegawanyika katika makundi kumi ambayo ni:

 • Dibaji ya Bibliolojia (Fundisho kuhusu Biblia)
 • Dibaji ya Teolojia Salihifu (Fundisho kuhusu Mungu)
 • Dibaji ya Kristolojia (Fundisho kuhusu Yesu Kristo)
 • Dibaji ya Numatolojia (Fundisho kuhusu Roho Mtakatifu)
 • Dibaji ya Angilolojia (Fundisho kuhusu Malaika)
 • Dibaji ya Anthropolojia (Fundisho kuhusu Mwanadamu)
 • Dibaji ya Hamatiolojia (Fundisho kuhusu Dhambi)
 • Dibaji ya Soteriolojia (Fundisho kuhusu Wokovu)
 • Dibaji ya Eklesiolojia (Fundisho kuhusu Kanisa)
 • Dibaji ya Eskatolojia (Fundisho kuhusu Mambo ya Mwisho).

Kwa neema ya Mungu, tutaangalia kila mmoja ya mafundisho haya kadiri Bwana atakavyoruhusu. Leo, tunaanza na Muhtasari wa Fundisho kuhusu Biblia (Maandiko). Natumaini kwamba utagundua kwamba mafundisho haya ya Biblia yanavutia na hufaa kujifunza. Ni ombi langu kwamba kila msomaji/msikilizaji ataelewa kikamilifu kile ambacho Roho huyaambia makanisa:

Ili kulijua Neno Lake la kweli (2 Tim. 2:15); kuruhusu Neno likae ndani yao kwa wingi (Kol. 3:16); na kuruhusu Neno Lake lisheheni akilini mwako, hivyo kuleta utii na uaminifu mkubwa zaidi—“kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia.” (Ebr. 10:25), — Amina.

DIBAJI KUHUSU BIBLIOLOJIA (Fundisho kuhusu Biblia)

Maelezo ya Ufunguzi.: Kama Waadventista Wasabato, sisi ni Waprotestanti, ikiwa na maana kwamba tunaamini katika “Sola Scriptura,” Biblia pekee kama msingi mmoja wa mamlaka ya imani na mafundisho yetu. Hii hasa ni sadifu katika siku za mwisho, wakati ambapo, kama ambavyo Ellen G. White alisema, Mungu atakuwa na “watu duniani wanaodumisha Biblia, na Biblia pekee, kama kiwango cha mafundisho yote na msingi wa matengenezo yote”. — The Great Controversy, uk. 595.

MASWALI NA MAJIBU.

[1] Nini maana ya “Sola Scriptura”? Hiki ni kirai cha Kilatini, chenye maana ya “Maandiko pekee,” hubainisha usabilifu kwa Maandiko kama yenye mamlaka pekee katika mafundisho na mwenendo maishani. Hudai ukamilifu wa Maandiko kama mamlaka turufu katika masuala yote ya kiroho. Sola Scriptura humaanisha tu kwamba kweli muhimu kwa ajili ya wokovu na maisha yetu ya kiroho hufundishwa ama dhahiri (bayana) au dhaliri (kimdokezo) katika Maandiko

Maneno Mengine Husiani ya Kilatini:

 • Sola Fide — “imani pekee.”
 • Sola Gratia — “neema pekee.”
 • Soli Deo Gloria — “utukufu kwa Mungu pekee.”
 • Solus Christus – Kristo pekee, ikionesha kwamba wokovu hutimizwa kwa kafara na upatanisho wa Kristo pekee.

“Biblia husimama pekee. Hakuna lolote linaloweza kuongezwa juu yake. Hakuna kinachoweza kuchukuliwa humo. Licha ya kile kinachosemwa au kuandikwa kuhusu kitabu hiki, Biblia haiko chini ya yeyote ila Mungu aliyeivuvia. Mtu yeyote anayehitaji kumjua Mungu na kile anachotamani kwa ajili ya jamii ya mwanadamu lazima aifuate Biblia. Ndilo neno la mwisho.” [Jon L. Dybdahl, Ed., Andrews Study Bible Notes, (Berrien Springs, MI: Andrews University Press, 2010), ix].

[2] Biblia ni nini? Biblia ni Neno la Mungu. Agano la Kale na Agano Jipya huunda Biblia, Neno aliloandika Mungu. Biblia ni uvuvio wa mapenzi ya Mungu usiokuwa na makosa; kiwango cha tabia, kipimo cha uzoefu, na mdhihirishaji mwenye mamlaka wa mafundisho yote, na kumbukumbu sadikifu (tumainifu) ya matendo ya Mungu katika historia.

[3] Je ni virai gani vinavyotumiwa kama rejea kuhusu Biblia?

 • Neno (Yakobo 1:21–23; 1 Pet 2:2).
 • Neno la Mungu (Luka 11:28; Ebr. 4:12).
 • Neno la Kristo (Kol. 3:16).
 • Neno la kweli (Yakobo 1:18).
 • Maandiko Matakatifu (Rum. 1:2; 2 Tim 3:15).
 • Kitabu (Zab. 40:7; Ufu. 22:19).
 • Kitabu cha Bwana (Isa 34:16).
 • Sheria ya Bwana (Zab. 1:2; Isa 30:9).
 • Kitabu cha Sheria (Neh 8:3; Gal 3:10).
 • Mausia ya Mungu (Rum. 3:2; 1 Pet 4:11).
 • Upanga wa Roho (Efe 6:17).
 • Maaandiko ya kweli (Dan 10:21).

[4] Nani aliyeandika Biblia? Biblia iliandikwa na waandishi wengi:

 • Musa aliandika Mwanzo, Kutoka, Walawi, Hesabu, Kumbukumbu, na Zaburi 90.
 • Yoshua aliandika kitabu kinachoitwa kwa jina lake
 • Ayubu huenda aliandika kisa chake mwenyewe.
 • Samweli pengine aliandika Waamuzi, Ruthu, na 1 Samweli.
 • Daudi aliandika Zaburi nyingi (2 Sam. 23:2).
 • Wana wa Kora aliandika Zaburi 42, 44-49, 84-85, 87.
 • Asafu aliandika Zaburi 50, 73-83.
 • Hemani aliandika Zaburi 88.
 • Ethani aliandika Zaburi 89.
 • Hezekia aliandika Zaburi 120-123. 128-130, 132, 134 – 136 (Isa. 38:20).
 • Sulemani aliandika Zaburi 72, 127, Mithali 1 – 29, Mhubiri, Wimbo wa Sulemani.
 • Aguri aliandika Mithali 30.
 • Lemueli aliandika Mithali 31.
 • Yeremia aliandika Yeremia, pengine Maombolezo, na huenda 1 na 2 Wafalme.
 • Ezra aliandika Ezra na pengine 1 na 2 Nyakati na 2 Samweli.
 • Modekai pengine aliandika Esta
 • Luka aliandika Matendo pamoja na Injili ya Luka.
 • Yohana aliandika Injili ya Yohana, 1 Yohana, 2 Yohana, 3 Yohana, na Ufunuo.
 • Paulo aliandika Warumi, 1 & 2 Wakorintho, Wagalatia, Waefeso, Wafilipi, Wakolosai, 1 & 2 Wathesalonike, 1 & 2 Timotheo, Tito, Filemoni, na Waebrania.

ZINGATIA: Vitabu vya unabii wa Agano la Kale viliandikwa na manabii ambao vitabu husika hubeba majina yao. Nyaraka na Injili za Agano Jipya vilipewa majina ya waandishi wao– (mbali na vingine vichache sana).

[5] Ni matukio gani ya Agano la Kale mara nyingi hurejewa katika Agano Jipya?

 • Uumbaji (Mwa. 1:1; Ebr. 11:3)
 • Mwanadamu kuumbwa katika sura ya Mungu (Mwa. 1:26; 1 Kor. 11:7)
 • Mungu akipumzika (Mwa. 2:2-3; Ebr. 4:4)
 • Agizo la ndoa (Mwa. 2:24; Mat. 19:4-6)
 • Anguko (Mwa. 3:6-8; Rum. 5:12-19)
 • Mauti ya Habili (Mwa. 4:8; 1 Yohana 3:12)
 • Kuhamishwa kwa Henoko (Mwa. 5:21-24; Ebr. 11:5)
 • Safina ya Nuhu (Mwa. 6:14-16; 7:1-12; Luke 17:26-27; 2 Pet. 3:6)
 • Kuitwa kwa Ibrahimu (Mwa. 12:1; Ebr. 11:8)
 • Kukutana kwa Ibrahimu na Melkizedeki (Mwa. 14:18-20; Ebr. 7:1-4)
 • Kuangamizwa kwa Sodoma (Mwa. 19; Mat. 11:24; Luka 17:32)
 • Kuzaliwa kwa Isaka (Mwa. 19:26; Gal. 4:23)
 • Kutolewa sadaka kwa Isaka (Mwa. 22:10; Ebr. 11:17-19)
 • Kichaka kinachoungua moto (Kut. 3:2; Luka 20:37; Matendo 7:30)
 • Kutoka (Kut. 12-14; Matendo 7:36; Ebr. 11:29; 1 Kor. 10:1)
 • Kuwasilishwa kwa mana (Kut. 16:15; Yohana 6:31)
 • Kuwasilishwa kwa sheria (Kut. 20; Gal. 3:19)
 • Nyoka wa shaba (Hes. 21:8-9; Yohana 3:14)
 • Eliya na ukame (1 Wafalme 17; Luka 4:25; Yakobo 5:17)
 • Uponyaji wa Naamani (2 Wafalme 5:14; Luka 4:27)
 • Danieli katika tundu la simba (Dan. 6:22; Ebr. 11:33)
 • Yona tumboni mwa samaki (Yn. 1:17; Mat. 12:40; 16:4)

[6] Ni maandiko gani ya Agano la Kale mara nyingi hurejewa katika Agano Jipya?

 • “Iweni watakatifu, kwa kuwa Mimi ni Mtakatifu” (Law. 11:44; 1 Pet. 1:16).
 • “Sitakupungukia wala sitakuacha.” (Yos. 1:5; Ebr. 13:5).
 • “Mwe na hasira, ila msitende dhambi” (Zab. 4:4; Efe. 4:26).
 • ”Hakuna mwenye haki hata mmoja” (Zab. 14:1; Rum. 3:10).
 • “Yeye ambaye Bwana ampenda, humrudi” (Mit. 3:12; Ebr. 12:6).
 • “[Mungu] atafuta kila chozi katika macho yao” (Isa. 25:8; Ufu. 21:4).
 • “Mauti imemezwa kwa kushinda.” (Hos. 13:14; 1 Kor. 15:54).
 • “Nitamimina Roho Yangu juu ya wote wenye mwili” (Yoeli 2:28; Matendo 2:17).
 • “Kila atakayeliitia Jina la Bwana ataokoka” (Yoeli 2:32; Rum. 10:13).
 • “Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana, Dunia na wote wakaao ndani yake” (Zab. 24:1; 1 Kor. 10:26).
 • “Mwanangu, usiyadharau marudia ya Bwana” (Mit. 3:11; Ebr. 12:5).
 • “Na abarikiwe Yeye ajaye kwa jina la Bwana” (Zab. 118:26; Mat. 21:9).
 • “Upendano husitiri wingi wa dhambi.” (Mit. 10:12; 1 Pet. 4:8).
 • “Ni mizuri kama nini miguu yao wahubirio habari ya mema!” (Isa. 52:7; Rum. 10:15).
 • “Dhambi zao sitazikumbuka tena.” (Yer. 31:34; Ebr. 10:17; Ebr. 8:12)

[7] Je Biblia ni muhimu jinsi gani? Mtazamo wetu unapaswa kuwaje kuhusu Biblia?

 • Biblia inapaswa kuwa kiwango cha mafundisho (1 Pet 4:11).
 • Biblia inapaswa kuaminiwa (Yohana 2:22).
 • Biblia inapaswa kufanyiwa wito kwayo (1 Kor. 1:31; 1 Pet 1:16).
 • Biblia inapaswa kusomwa (Kumb. 17:19; Isa 34:16).
 • Biblia inapaswa kusomwa hadharani na wote (Kumb. 31:11–13; Neh 8:3; Yer. 36:6; Matendo 13:15).
 • Biblia inapaswa kujulikana (2 Tim 3:15).
 • Biblia inapaswa kupokelewa kwa upole (Yakobo 1:21).
 • Biblia inapaswa kuchunguzwa (Yohana 5:39; 7:52).
 • Biblia inapaswa kuchunguzwa kila siku (Matendo 17:11).
 • Biblia inapaswa kuhifadhiwa moyoni (Kumb. 6:6; 11:18).
 • Biblia inapaswa kufundishwa kwa watoto (Kumb. 6:7; 11:19; 2 Tim 3:15).
 • Biblia inapaswa kufundishwa kwa wote (2 Nya. 17:7–9; Neh 8:7-8).
 • Biblia inapaswa kuzungumziwa mara kwa mara/daima (Kumb. 6:7).
 • Biblia haipaswi kutumiwa kwa udanganyifu (2 Kor. 4:2).
 • Biblia inapaswa siyo tu kusikiwa bali kufuatwa (Mat 7:24; Luka 11:28; Yakobo 1:22).
 • Biblia inapaswa kutumiwa dhidi ya maadui wa kiroho (Mat 4:4, 7, 10; Efe 6:11, 17).
 • Biblia inapaswa kupokelewa siyo kama neno la wanadamu, bali kama neno la Mungu (1 Thes 2:13).

MAANA YA KIIBADA: Nini umuhimu wa Miongozo hii ya Kujifunza katika mada ya Biblia? “Neno la Mungu ni nuru. Kwa kweli, kitu cha kwanza kabisa Mungu alichoumba ulimwenguni mwetu kwa neno Lake lililotamkwa ilikuwa nuru (Mwa. 1:3). Mtunzi wa Zaburi alisema: “Neno Lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu.” (Zab. 119:105). Kwa kweli, kuna nuru tele kwenye Biblia ambayo ni bayana na rahisi kuelewa. Lakini mwanafunzi wa Biblia yeyote makini anajua kwamba kile ambacho ni dhahiri na rahisi mara nyingi kina kina kikuu. Nuru ya anga dhahiri la samawi huonekana kuwa utando sahili, wenye kupendeza. Lakini tunajua kuwa ni wa kina sana—wa kina kama ulimwengu wenyewe. Kadiri tunavyofuata nuru hiyo kwa kina zaidi, ama ni ulimwenguni au katika Biblia, mara nyingi tunagundua ukweli wa kina zaidi kuhusu Muumbaji wa vitu vyote.” [Jon L. Dybdahl, Ed., Andrews Study Bible Notes, (Berrien Springs, MI: Andrews University Press, 2010), ix].

Wapendwa, Miongozo hii ya Kujifunza Biblia itatusaidia katika safari hiyo. Itatusaidia kumjua na kumwelewa Mungu vyema zaidi. Itatusaidia kuelewa nuru ya Neno Lake, kina cha upendo Wake, na makusudi ya mapenzi Yake yaliyofunuliwa maishani mwetu, na kweli kuu za kiungu zisizo na mwisho zitakazobadili maisha yetu milele, kadiri tunavyongejea marejeo Yake hivi karibuni.

HATUA YA MAAMUZI: Ni mwitikio gani unaodhani sura hii ingepaswa kutuhimiza kufanya? [1] Amini kwamba Maandiko — Agano la Kale na Agano Jipya, ambayo huunda Biblia, ni Neno Mungu lililoandikwa.

[2] Amini kwamba japo Biblia iliandikwa na manabii na mitume, Biblia haikutokana na mapenzi yao, bali kwa mapenzi ya Mungu (2 Pet. 1:20–21). “Kila andiko,” Paulo aliandika, “limetokana na uvuvio wa Mungu” (2 Tim. 3:16).

[3] Amini kwamba mafundisho yake ni matakatifu, kanuni zake zina mamlaka, historia zake ni kweli, na maamuzi yake hayabadiliki.

[4] Amini kwamba Kitabu hiki kina utashi wa Mungu, hali ya mwanadamu, na njia ya wokovu, kiama cha wadhambi, furaha ya waumini, na kweli kuhusu jinsi ya kupokea uzima wa milele.

[5] Amini kwamba Mungu aliupatia ulimwengu Neno Lake hai, Yesu Kristo, na Neno Lake lililoandikwa, Maandiko. Baada ya Yesu (Neno hai la Mungu), kurejea mbinguni, Biblia (Neno la Mungu Lililoandikwa), ilisalia duniani kama mwongozo wa Mungu wa milele kwa ajili ya jamii ya wanadamu. Hapa tunaona mapenzi ya Mungu kwa ajili ya jamii yote ya wanadamu: “Bwana hakawii kuitimiza ahadi Yake, kama wengine wanavyokudhani kukawia, bali huvumilia kwenu, maana hapendi mtu yeyote apotee, bali wote wafikilie toba.” (2 Petro 3:9)

[6] Amini kwamba Kristo ndiye lengo kuu –ndiye kiini cha Biblia; Yeye ndiye ‘Sauti ya Injili’ – (sauti ya Mungu ikizungumza na kila mmoja wetu) – ili kutubu, ‘kuiandaa njia ya Bwana na kunyosha mapito Yake’ kwa sababu anakuja, Naye anataka tuwe tayari.

UAMUZI WANGU LEO:

[1] Nataka kuisoma Biblia; [2] Nataka kumwomba Roho Mtakatifu anifunulie Maandiko; [3] Nataka kujifunza na kuwapasha habari za Biblia wale ninaokutana nao; [4] Nataka kuitii Biblia: “Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu. Kwa sababu mtu akiwa ni msikiaji wa neno tu, wala si mtendaji, mtu huyo ni kama mtu anayejiangalia uso wake katika kioo. Maana hujiangalia, kisha huenda zake, mara akasahau jinsi alivyo.” (Yakobo 1:22–24)

WIMBO WA KUFUNGA: Nipe Biblia – (NZK # 52).

[1] Nipe Biblia nyota ya furaha, wapate nuru wasafirio; Hakuna la kuzuia amani, Kwani Yesu alituokoa.

Nipe Biblia neno takatifu, Nuru yake itaniongoza; Sheria na ahadi na upendo, Hata mwisho vitaendelea.

[2] Nipe Biblia nihuzunikapo ikinijaza moyoni dhambi; Nipe neno zuri la Bwana Yesu, Nimwone Yesu Mwokozi wangu.

[3] Nipe Biblia Biblia nipate kuona, hatari zilizo duniani; Nuru ya neno lake Bwana Yesu, Itaangaza njia ya kweli.

[4] Nipe Biblia taa ya maisha; Mfariji tunapofiliwa; Unionyeshe taa ya mbinguni, Nione utukufu wa Bwana.

Uwe na Siku Yenye Baraka:  Kwa hiyo wekeeni mbali uchafu wote na ubaya uzidio, na kupokea kwa upole neno lile lililopandwa ndani, liwezalo kuziokoa roho zenu.” (Yakobo 1:21)

Sauti ya Injili/ Mwongozo wa Kujifunza Biblia/ Maandiko/ Dibaji kuhusu Bibliolojia (Fundisho kuhusu the Biblia)/ Somo # 1