Zaburi 92: Mwongozo wa Biblia.

ZABURI 92: MWONGOZO WA IBADA.

Ibada Ya Alfajiri/ “Mwongozo wa Ibada” unaoshabihiana na Mpango wa Usomaji wa Biblia wa Leo: Zaburi 92/ Somo: “Wimbo kwa ajili ya Siku ya Sabato” /19-BSG-92A: (Zaburi 92:1-15)/ Wimbo: Ikumbuke kote Sabato ya Bwana (NZK # 84)

UCHUNGUZI: Sabato ni–Kumbukumbu ya daima ya Uumbaji, (Kut. 20:11-12); Ishara ya ukombozi, (Kum. 5:15); Ishara ya utakaso, (Kutoka 31:13; cf. Ezekieli 20:20).

TAFAKARI: “Huu ni wimbo wa sifa kwa Mungu, uliowekwa wakfu kwa sherehe za siku ya Sabato, ambayo ni juu ya Mungu katika uhusiano na upendo Wake kwa wanadamu. Ni zaburi pekee iliyotengwa kwa kusudi hilo. Shairi hili linataja mara saba jina takatifu la BWANA, (Yahweh, BWANA; zaburi nyingine inayofanya hivyo ni Zab. 19), ikipendekeza uhusiano na Sabato ya siku ya saba. Zaburi hii pia inatoa maelezo saba kuhusu waovu (92:6-9) na sifa saba za wenye haki (aya. 12-15). Mwandishi anaonesha shukrani za kina kwa uwepo wa Mungu, kipawa cha uumbaji, uaminifu Wake, na baraka zingine nyingi.” [Jon L. Dybdahl, Ed., Andrews Study Bible Notes, (Berrien Springs, MI: Andrews University Press, 2010), 745].

MAANA YA KIIBADA: “Ni neno jema kumshukuru Bwana, na kuliimbia jina Lako, Ee Uliye Juu.” (Zab. 92:1). Zaburi hii ilitungwa kama wimbo wa Sabato wa sifa kwa Mungu kwa ajili ya nguvu na hekima Yake katika maongozi Yake kwa waovu na wenye haki.

Je, tunawezaje kumsifu na kumshukuru Bwana? Kwa kutangaza upendo Wake usiopimika kila asubuhi na uaminifu Wake kila usiku; Kwa kuimba na kucheza vyombo vya muziki; Kwa kumshukuru Yeye kwa furaha (tukiimba) kwa yale yote aliyo yafanya kwa ajili yetu; Kwa kukiri ubora wa kazi ya uumbaji ya Mungu na mawazo Yake ya kina ambayo ni zaidi ya uelewa wetu (Zab. 92:1-5).

Pili, Jihadhari! Waovu/makafiri ni wapumbavu. Zaburi hii inatoa muhtasari wa mambo makuu matatu kuhusu waovu: Hawaelewi ukweli kuhusu maisha (aya ya 6); Hawaelewi ukweli kuhusu Mungu — kwamba Yeye ndiye Hakimu Mkuu ambaye anatawala milele (aya ya 8); Hawaelewi ukweli kuhusu hukumu ya Mungu ijayo –hawaelewi kwamba kwa sababu ya dhambi zao, ni maadui wa Mungu, na kwamba wataangamia wasipotubu.

Tatu, wenye haki wanapaswa kumsifu Bwana siku ya Sabato! Lakini kwa nini? Kwa sababu ya matendo Yake (uumbaji, aya ya 4). Uwepo wa familia yote ya binadamu ni kwa sababu tu ya tendo la kiungu la uumbaji, kwa hiyo, ingependeza kwa wanadamu wote kumwabudu Bwana siku ya Sabato—kama kumbukumbu ya uumbaji, mbali na mambo (sababu) zingine!

Nne, mwenye haki anapaswa kumsifu Bwana kwa ajili ya utoaji Wake — (a) Nguvu: Bwana atakuza “pembe” yangu (ishara ya uwezo na nguvu, aya ya 10); (b) Ushindi: Mungu ndiye mpiganaji wetu! Tutasikia kushindwa kwa wapinzani wetu (aya ya 11); (c) Usitawi, Ukuaji: Mwenye haki atasitawi kama mtende, Atakua kama mwerezi wa Lebanoni. Waliopandwa katika nyumba ya Bwana watasitawi katika nyua za Mungu wetu. Watazaa matunda hadi wakati wa uzee, Watajaa utomvu, watakuwa na ubichi.” (Zaburi 92:12-14)

HATUA YA MAAMUZI: Ni mwitikio gani unaodhani sura hii ingepaswa kutuhimiza kufanya? [1] Msifu na kumshukuru Bwana Aliye Juu sana; [2] Toa ushuhuda tabithi kwa kazi ya Mungu katika maisha yako – Anakuwezesha; Anamimina mibaraka Yake juu yako; Anakupa ushindi dhidi ya adui zako – kimwili na kiroho (Efeso. 6:10-13); Yeye ndiye akuwezeshaye kusitawi na kukupa nguvu; [3] Tangaza kwamba Mungu ni mnyofu na mwenye haki. Hakika Yeye ndiye mwamba wako. Katika Yeye hakuna uovu wowote (aya ya 15).

SAUTI YA INJILI: Kipengele hiki kimeandikwa kana kwamba Mungu ndiye anaongea nawe, moja kwa moja, kwa sababu hufanya hivyo. Je, Bwana ananiambia nini asubuhi ya leo? Watoto wangu wapendwa, “Hakika mtazishika Sabato Zangu, kwa kuwa ni ishara kati ya Mimi na ninyi katika vizazi vyenu vyote; ili mpate kujua ya kuwa Mimi ndimi Bwana niwatakasaye ninyi.” (Kutoka 31:13). “Mimi ni Bwana, Mungu wenu; endeni katika amri Zangu, mkazishike hukumu Zangu, na kuzitenda; zitakaseni Sabato Zangu; zitakuwa ishara kati ya Mimi na ninyi, mpate kujua ya kuwa Mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.” (Ezekieli 20:19-20)

Mwitikio Wangu: Kwa Neema ya Mungu — Nitamshukuru Bwana, na kuimba sifa kwa Jina Lake takatifu. Nitamwabudu Bwana Mungu siku ya Sabato (Kut. 20:8-12). Nitashirikisha wengine kweli za Biblia kuhusu Sabato.

Uwe na Alfajiri Njema: “Na itakuwa, Mwezi Mpya hata Mwezi Mpya, na Sabato hata Sabato, wanadamu wote watakuja kuabudu mbele zangu, asema Bwana.” (Isaya 66:23).

Sauti ya Injili/ Mwongozo wa Biblia/ Zaburi 1-150/ Ibada/ Zaburi 92/