Uungu wa Yesu Kristo

78-001 (2 Yohana 1:7)/ Mwongozo wa Kujifunza Biblia/ Utangulizi kuhusu Kristolojia (Fundisho juu ya Yesu Kristo)/ Somo # 1/ Andiko Msingi: “Kwa maana wadanganyifu wengi wametokea duniani, wasiokiri ya kuwa Yesu Kristo yuaja katika mwili. Huyo ndiye yule mdanganyifu na mpinga Kristo.” (2 Yohana 7)

Malengo: Kusudi la somo hili ni kuthibitisha msingi wa Biblia wa imani katika uungu wa Yesu Kristo.

Maelezo ya Ufunguzi: Je Yesu Kristo Mungu? Hili ni swali ambalo wengi wanauliza leo. Wengi hukana ukweli kwamba Yesu Kristo ni Mungu katika mwili. Wengi wamedanganywa. Naam, ni watu wa kidini sana, lakini wamedanganyika. Tunahitaji kunoa upanga wetu katika mada hii. Hivi ni vita vya kiroho! Udanganyifu wa kishetani hutafuta kuhafifisha uungu wa Yesu Kristo na kumtukuza mwanadamu. Leo hata kwa wale wanaoitwa Wakristo wanakana Utahamilisho, Bikra Kuzaa, na Uungu na utukuzwaji wa Kristo. Katika somo hili, tutasimama kwenye ufunuo wa Maandiko katika mada hii muhimu, ikiwa imesheheni rejea za Maandiko. 

Hebu tuanze na kile tukiaminicho: [1] Tunaamini Kristo ni Nafsi ya pili katika Utatu mbinguni—ambapo kuna Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu—ambao wameungana siyo tu katika Ujalali lakini pia katika upaji wa ukombozi. [2] Tunaamini kwamba Kristo ni mmoja na Baba wa milele—mmoja katika asili, anayelingana katika uwezo na mamlaka, Mungu katika maana ya juu zaidi, wa milele na mwishinafsia, mwenye uhai wa asili, usioazimwa, na wala kudihiliwa (kutoholewa). [3] Tunaamini kwamba Kristo alikuwepo tangu milele, akiwa faradi (pekee), mwenye muungano na Baba, akiwa na utukufu uleule, na hulka zote za kiungu.

Maswali ya Moyoni: [1] Kuna ushahidi gani kwamba Yesu Kristo ni Mungu? [2] Alijitazamaje Mwenyewe? [3] Je watu walitambua uungu Wake? [4] Je Yesu hutamka kauli ambazo Mungu pekee ndiye angeweza kuzitamka? [5] Je Yesu ana hulka za uungu? [6] Je majina, vyeo, na lakabu za Mungu huawazwa kwa Yesu? [7] Je Yesu anafanya mambo ambayo Mungu pekee anaweza kufanya? [8] Hivi Biblia inadai bayana na dhahiri kwamba Yesu ni Mungu?

Uungu wa Yesu Kristo – (Mawazo Makuu):

 1. Utambuzi wa Kristo wa Uungu Wake
 2. Cheo cha “Mwana wa Mungu.”
 3. Majina na vyeo kwa ajili ya Uungu pekee
 4. Hulka za Uungu pekee
 5. Kauli zinazoawazwa kwa Uungu tu
 6. Majina, vyeo, na lakabu za Mungu
 7. Yehova wa AK na Yesu wa Agano Jipya
 8. Majukumu, Ibada na Maombi ya Kiungu
 9. Ushahidi wa Kimaandiko
 10. Ushahidi Mwingine
 11. Maana ya Kiibada.

UTAMBUZI WA KUHUSU UUNGU WAKE

Kwanza tunaona utambuzi wa Kristo kuhusu Nafsi na Utume Wake wa kiungu.

 • Akiwa na umri wa miaka kumi na mbili alimtambua Mungu kama Baba Yake (Luka 2:41–52);
 • Akiwa na umri wa miaka thelathini utume Wake wa kiungu ulifunuliwa katika ubatizo Wake (Mat. 3:13–17);
 • Huonekana katika rekodi ya majaribu (Mat. 4:1–11);
 • Huonekana katika wito wa wale kumi na mbili na wengine sabini;
 • Huonekana katika madai ya Hubiri la Mlimani (Mathayo 5 hadi 7).

CHEO CHA “MWANA WA MUNGU.”

Katika sehemu hii tunaona utambuzi wa Kristo Mwenyewe juu ya cheo cha “Mwana wa Mungu.”

 • Wakati Kristo akiwa hapa miongoni mwa wanadamu, alijitambua Mwenyewe kuwa ni Mwana wa Mungu. (Soma Mat. 27:41–43; Yohana 5:23; 9:35–37; 10:36; 17:1).
 • Alithibitisha ushahidi wa wengine kwamba alikuwa Mwana wa Mungu. (Soma Mat. 16:15–17; Yohana 1:32–34, 48, 49; 11:27).
 • Kauli zingine nyingi huthibitisha ukweli kwamba alikuwa vile alivyodai kuwa—Mwana wa Mungu (Soma Mat. 3:16-17; Yohana 19:7; 20:30-31; Matendo 9:20; Rum. 1:1–4; 2 Kor. 1:19; Ebr. 4:14; 2 Petro 1:16-17).

ZINGATIA: Kristo alitumia cheo cha “Mwana wa Mungu” bila simile yoyote, na pamoja na uhuru na uwazi wa juu kabisa. Ni cheo kimojawapo kinachobeba, katika njia ya wazi zaidi, uhusiano Wake wa pekee na Baba.

MAJINA NA VYEO VYA KIUNGU TU

 1. “Mungu” (Yohana 1:1);
 2. “Mungu pamoja nasi” (Mat. 1:23);
 3. “Mungu mkuu” (Tito 2:13);
 4. “Mungu, mwenye kuhimidiwa milele” (Rum. 9:5);
 5. “Mwana wa Mungu” (kadiri ya mara 40);
 6. “Mwana pekee” (mara 5);
 7. “wa kwanza na wa mwisho.” (Ufu. 1:17);
 8. “Alfa na Omega” (Ufu. 22:13);
 9. “wa kwanza na wa mwisho” (Ufu. 22:13);
 10. “Yule Mtakatifu” (Matendo 3:14);
 11. “Bwana” (hutumiwa daima);
 12. “Bwana wa wote” (Matendo 10:36);
 13. “Bwana wa utukufu” (1 Kor. 2:8);
 14. “Mfalme wa utukufu” (Zab. 24:8–10);
 15. “Mshauri wa ajabu.” (Isa. 9:6);
 16. “Baba wa milele” (Isa. 9:6);
 17. “Neno la Mungu.” (Ufu. 19:13);
 18. “Neno” (Yohana 1:1);
 19. “Imanueli.” (Mat. 1:23);
 20. “Mpatanishi” (1 Tim. 2:5); na
 21. “Mfalme wa wafalme na Bwana wa mabwana” (Ufu. 19:16).

HULKA ZA UUNGU TU

Je Kristo anashabihi hulka za Uungu? Ndiyo. Katika maelezo yafuatayo yaliyofupishwa kuhusu Maandiko mbalimbali, tunaona kwamba Yesu Kristo ni Mungu kwa sababu ana hulka za Mungu.

Umilele:

 1. Yeye ni Baba wa milele (Isaya 9:6).
 2. Yeye amekuwepo tangu milele (Mika 5:2).
 3. Alikuwepo “hapo mwanzo,” daima alikuwepo (Yohana 1:1, 2, 14, 15).
 4. Yesu alikuwa na utukufu pamoja na Mungu kabla ya ulimwengu kuumbwa (Yohana 17:5).

Uenevu:

 1. Yuko pamoja nasi daima (Mathayo 28:20).
 2. Yuko kwa kila muumini (Yohana 14:20-23).
 3. Yeye huwajaza wote (Waefeso 1:23; 4:20).
 4. Mahali walipo wawili au watu, Yeye yu kati yao (Mathayo 18:20).

ZINGATIA: Japo uungu Wake una uwezo wa asili wa uenevu, Kristo mtahamili alikuwa amejiwekea mipaka Yeye binafsi katika hali hii. Alikuwa amechagua kuwa Mwenevu kupitia huduma ya Roho Mtakatifu (Yohana 14:16-18).

Uenyezi na Ujalali:

 1. Yeye ni Mwenyezi (Ufunuo 1:8).
 2. Hufanya lolote afanyalo Baba (Yohana 5:19).
 3. Hutegemeza vitu vyote (Wakolosai 1:17; Waebrania 1:3).
 4. Yeye ni mkuu wa utawala na mamlaka yote (Wakolosai 2:10).
 5. Ana uwezo wa kutiisha vitu vyote chini Yake (Wafilipi 3:21).
 6. Ana mamlaka juu ya uhai na mauti Yake (Yohana 10:18).
 7. Yeye ni mtawala wa wafalme wa dunia (Ufunuo 1:5).
 8. Ana uwezo juu ya ulimwengu-asilia (Luka 8:25).
 9. Yeye ni Bwana wa wote (Ufunuo 19:16; 1 Petro 3:22, Wakolosai 1:18; Matendo 10:36).
 10. Atatawala hadi pale atakapowaweka maadui wote chini ya miguu Yake (1 Wakorintho 15:25).
 11. Mamlaka yote, pamoja na jamii yote ya wanadamu amekabidhiwa Yeye (Mathayo 28:18; Yohana 17:2, 3).

Utaalifu:

 1. Anajua mawazo ya watu (Marko 2:8; Luka 6:8; 11:17).
 2. Alijua namna ya kifo Chake (Mathayo 16:21; Yohana 12:33).
 3. Alijua nani angemsaliti (Yohana 6:64, 70-71).
 4. Alijua historia ya mwanamke Msamaria (Yohana 4:29).
 5. Ushuhuda wa wanafunzi (Yohana 16:30; 17:30).
 6. Aliwajua watu wote (Yohana 2:24, 25).
 7. Anajua ujeo (wakati ujao) (Yohana 2:19-22; Yohana 18:4; Yohana 13:19; Mathayo 24:35).
 8. Alimjua Baba (Mathayo 11:27; Mungu pekee ndiye awezaye kujijua—1 Wakorintho 2:11, 16).

Kutobadilika:

 1. Daima na milele atakuwa vilevile (Waebrania 13:8 cf., 1:12, 8, 10).
 2. Maneno Yake hayatapita kamwe (Mathayo 24:35).

Mtakatifu:

 1. Yeye ni mtakatifu (Ufunuo 3:7)
 2. Hakujua dhambi yoyote (2 Wakorintho 5:21).
 3. Hana dhambi (Waebrania 4:15).
 4. Hakutenda dhambi yoyote (Yohana 8:46; 1 Yohana 3:5; 1 Petro 2:22).
 5. Hana ila wala waa (1 Petro 1:19).
 6. Yeye ni mzao mtakatifu atakayeitwa Mwana wa Mungu (Luka 1:35).
 7. Yeye ni mtakatifu, msalihi, na asiyenajisika, na aliyetengwa na wadhambi (Waebrania 7:26).

Kweli:

 1. Amejaa neema na kweli (Yohana 1:14).
 2. Kweli iko katika Yesu (Waefeso 4:21).
 3. Yeye ni kweli (Yohana 14:6).
 4. Yeye ni mwaminifu na mkweli (Ufunuo 19:11).

KAULI ZINAZOAWAZWA KWA MUNGU

Je Kristo alitamka kauli ambazo Mungu pekee angeweza kutamka? Ndiyo.

 1. “Kwa kuwa Mimi sikushuka kutoka mbinguni ili niyafanye mapenzi Yangu, bali mapenzi Yake aliyenipeleka.” (Yohana 6:38)
 2. “Na sasa, Baba, unitukuze Mimi pamoja Nawe, kwa utukufu ule niliokuwa nao pamoja Nawe kabla ya ulimwengu kuwako.” (Yohana 17:5)
 3. “Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambia, Yeye Ibrahimu asijakuwako, Mimi Niko.” (Yohana 8:58)
 4. “Hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani Yangu. Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; Mimi nimeushinda ulimwengu.” (Yohana 16:33)
 5. “Yesu akamwambia, Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye Mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi.” (Yohana 11:25)
 6. “Amin, amin, nawaambia, Yeye alisikiaye neno Langu na kumwamini Yeye aliyenipeleka yuna uzima wa milele; wala haingii hukumuni, bali amepita kutoka mautini kuingia uzimani.” (Yohana 5:24)
 7. “Yesu akamwambia, Mimi ndimi Njia, na Kweli, na Uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya Mimi.” (Yohana 14:6)
 8. Naye anitazamaye Mimi amtazama Yeye aliyenipeleka.” (Yohana 12:45)
 9. “Muda nilipo ulimwenguni, Mimi ni nuru ya ulimwengu. (Yohana 9:5)
 10. “Amwaminiye Mwana yuna uzima wa milele; asiyemwamini Mwana hataona uzima, bali ghadhabu ya Mungu inamkalia.” (Yohana 3:36)
 11. “Ili watu wote wamheshimu Mwana kama vile wanavyomheshimu Baba. Asiyemheshimu Mwana hamheshimu Baba aliyempeleka.” (Yohana 5:23)
 12. “Naye Yesu akapaza sauti, akasema, Yeye aniaminiye Mimi, haniamini Mimi bali Yeye aliyenipeleka. (Yohana 12:44)
 13. “Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani.” (Mathayo 28:18)

Maandiko hayo hapo juu yanaweza tu kufafanuliwa kimantiki kwa msingi wa uungu wa Kristo. Hakuna kiumbe yeyote, hata kama ametukuzwa jinsi gani, ambaye angeweza kimantiki kutamka kauli hizo. Hivi unaweza kumfikiria rais wa Marekani akijitokeza kwenye TV na kujitamkia madai hayo kwa ajili yake mwenyewe? Je unaweza kumfikiria hata malaika aliyetukuka zaidi akifanya hivyo?

STAHIKI ZA UUNGU PEKEE

Yesu Kristo alidai kuwa na nyadhifa/stahiki zifuatazo:

 • Uumbaji wa ulimwengu (Yohana 1:1–3);
 • Uhifadhi wa ulimwengu (Ebr. 1:3);
 • Haki na uwezo wa kusamehe dhambi (Marko 2:5–12);
 • Haki na uwezo wa kuwahukumu wanadamu wote (Matendo 17:31);
 • Mamlaka na haki ya kuwafufua wafu (Yohana 5:28, 29);
 • Mamlaka na haki ya kuibadilisha miili yetu (Flp. 3:21);
 • Mamlaka na uwezo wa kutukirimia uhalidifu/kutokufa (1 Kor. 15:52, 53).

MAJINA, VYEO, NA LAKABU ZA MUNGU.

Je kuna majina, vyeo, na lakabu za Mungu katika AK zinazoawazwa kwa Kristo? Ndiyo.

 1. Mwasisi wa maneno ya milele—Isaya 40:8; Zaburi 119:89 / Mathayo 24:35; Yohana 6:68
 2. Bwanarusi—Isaya 62:5; Hosea 2:16 / Marko 2:19; Ufunuo 21:2
 3. Hukiri kwamba Yeye ni Bwana—Isaya 45:23 (Yehova) / Wafilipi 2:11 (Yesu)
 4. Mtumaji-mwenza wa Roho Mtakatifu—Yohana 14:16 (Baba humtuma) / (Yesu humtuma) Yohana 15:26
 5. Muumbaji wa vitu vyote—Isaya 40:28; Zaburi 148:1-5 / Yohana 1:3; Wakolosai 1:16
 6. Imanueli—Isaya 7:14 / Mathayo 1:23
 7. Mwenye kusamehe dhambi—Yeremia 31:34 / Matendo 5:31
 8. Mungu Mhukumu—Mhubiri 12:14 / 1 Wakorintho 4:5; 2 Wakorintho 5:10; 2 Timotheo 4:1
 9. NIKO—Kutoka 3:14 / Yohana 8:58; Yohana 13:19
 10. Anasabihiwa kama Yehova—Yoeli 2:32; Isaya 45:22 / 1 Wakorintho 1:2
 11. Yehova juu ya wote—Zaburi 97:9 / Yohana 3:31
 12. Yehova haki yetu—Yeremia 23:5, 6 / 1 Wakorintho 1:30
 13. Yehova wa kwanza na wa mwisho—Isaya 44:6; 48:12-16 / Ufunuo 1:8, 17; 22:13
 14. Yehova mjumbe wa agano—Malachi 3:1 / Luka 7:27
 15. Yehova Mchungaji—Isaya 40:11 / Waebrania 13:20
 16. Yehova, ambaye kwa ajili ya utukufu Wake vitu vyote viliumbwa—Mithali 16:4 / Wakolosai 1:16
 17. Mwenza na Mlingani wa Yehova—Zekaria 13:7 / Wafilipi 2:6
 18. Yehova—Zaburi 110:1 / Mathayo 22:42-45
 19. Hakimu wa mataifa—Yoeli 3:12 / Mathayo 25:31-41
 20. Hakimu—Yoeli 3:12 / Mathayo 25:31-46
 21. Mfalme wa Utukufu—Zaburi 24:7, 10 / 1 Wakorintho 2:8; Yohana 17:5
 22. Aliongoza kuwatwaa mateka—Zaburi 68:18 / Waefeso 4:7, 8
 23. Nuru—Zaburi 27:1 / Yohana 1:4-9; 8:12; 1 Yohana 1:5
 24. Bwana wa wote—1 Nyakati 29:11-12 / Matendo 10:36; Warumi 10:11-13
 25. Bwana wa Sabato—Mwanzo 2:3 / Mathayo 12:8
 26. Mfufuaji wa wafu—1 Samweli 2:6; Zaburi 119 (mara 11) / Yohana 11:25; 5:21 w/Luka 7:12-16
 27. Mkombozi—Hosea 13:14; Zaburi 130:7 / Tito 2:13-14; Ufunuo 5:9
 28. Mwamba—Kumbukumbu 32:31; Zaburi 18:2; Isaya 8:14; Zaburi 92:15 / 1 Petro 2:6-8; 1 Wakorintho 10:4
 29. Wokovu kwa kuliitia jina la Bwana—Yoeli 2:32 / Warumi 10:13
 30. Mwokozi—Isaya 43:3; Hosea 13:4 / 2 Petro 1:1, 11; Tito 2:10-13; Matendo 4:12 (cf., Tito 1, 3)
 31. Isaya Alimwona—Isaya 6:1 / Yohana 12:41
 32. Mchungaji—Zaburi 23:1 / Yohana 10:11; Waebrania 13:20
 33. Jiwe la kujikwaa—Isaya 8:13-14 / Warumi 9:32-33; 1 Petro 2:8; Matendo 4:11
 34. Mtegemezaji, Mhifadhi, wa vitu vyote—Nehemia 9:6 / Wakolosai 1:17
 35. Mungu na Muumbaji wa milele—Zaburi 102:24-27 / Waebrania 1:8, 10-12
 36. Wa Kwanza na wa Mwisho—Isaya 41:4; 44:6; 48:12 / Ufunuo 2:8; 22:13
 37. Mungu wa Ujio wa Kwanza—Isaya 40:3 / Mathayo 3:3
 38. Mungu mkuu na Mwokozi—Isaya 43:11-12 / Tito 1:3-4; 2:10, 13; 3:4-6
 39. Mtakatifu—1 Samweli 2:2 / Matendo 3:14
 40. Mhukumu wa watu wote—Zaburi 98:9 / Matendo 17:31
 41. Bwana Mwenyezi—Isaya 6:1-3; 8:13-14 / Yohana 12:41; 1 Petro 2:8
 42. Bwana wa utukufu—Isaya 42:8 / Yohana 17:1-5; 1 Wakorintho 2:8
 43. Mungu Ajaye Mara ya Pili—Zekaria 14:5 / Mathayo 16:27; 24:29-31

UNASIBISHAJI WA YEHOVA WA AK NA YESU WA AJ

Kuna idadi kadhaa ya maandiko ya Agano la Kale yenye jina Yehova ambayo waandishi wa AJ wameyaakisha kwa Yesu Kristo.

Neno “Bwana” (Yehova) katika Zaburi 102:22, na maandiko husiani 25–28, vinaakishwa kwa Yesu katika Waebrania 1:10–12. Jina lilelile la kiungu (Yehova) huonekana katika Habakuki 2:2, 3, na huakishwa kwa Kristo katika Waebrania 10:37.

Matukio mengine matatu ambapo ama Yehova au Elohimu huakishwa/hutumiwa kwa Bwana wetu huweza kuonekana katika yafuatayo:

 • Katika Yeremia 31:31 Yehova linatumiwa, na hurejelea kazi ya Kristo katika Waebrania, sura ya 8 na 10.
 • Rejea kuhusu Yehova katika Hagai 2:6 pia ni la Kimasihi, na huakishwa kwa kazi ya Yesu katika Waebrania 12:26.
 • Jina la kiungu Elohimu katika Zaburi 45:6, 7, huakishwa kwa Mwana wa Mungu katika Waebrania 1:8, 9.

MAJUKUMU, IBADA NA UPOKEAJI IBADA KWA KIUNGU

Kuwafufua watu akiwa duniani:

 • Mathayo 9:25, binti wa mkuu wa Sinagogi;
 • Luka 7:12-16, mwana wa mjane;
 • Yohana 11:44, Lazaro;
 • Yohana 2:19-22, Yeye Mwenyewe.

Ibada kutoka kwa watu:

Ni Mungu pekee ndiye astahiliye ibada (Zaburi 95:6). Siyo watu (Matendo 10:25-26), wala malaika (Ufunuo 19:10) wanaopaswa kupokea ibada; ni Mungu pekee God (Luka 4:8). Yesu Kristo, ihali ni Mungu na Muumbaji, bila kusita alikubali ibada ambayo hata malaika pamoja na watu wema, ilhali ni viumbe, walikataa kwa hofu na utisho kuipokea.

Lakini Yesu alipokea ibada ya wafuatao:

 1. Wenye hekima (Mathayo 2:2, 11);
 2. Mtu aliyezaliwa kipofu (Yohana 9:38);
 3. Wanafunzi (Mathayo 14:33; 28:17);
 4. Kijana mtawala (Mathayo 9:18);
 5. Wanawake (Mathayo 28:9);
 6. Wanafunzi (Mathayo 28:17);
 7. Pepo (Marko 3:11; 5:6);
 8. Kila mmoja (Wafilipi 2:10, 11);
 9. Wazee wanne (Ufunuo 5:14).

Nyadhifa Zingine:

 1. Hufanya kazi za Mungu (Yohana 10:37-39).
 2. Hupelekewa maombi (Matendo 7:59).
 3. Husamehe dhambi (Mathayo 1:21; Marko 2:7).
 4. Uwezo wa kubadili miili ya waumini wote (Wafilipi 3:21).
 5. Kuwafufua wafu kwa ajii ya hukumu (Yohana 5:24-29; Matendo 10:42; Matendo 17:31).
 6. Kumtuma Roho Mtakatifu (kiumbe hawezi kumtuma Mungu; Yohana 16:7; cf. 14:26).
 7. Mpaji wa uzima wa milele pamoja na mamlaka juu ya jamii yote ya wanadamu (Yohana 17:2; Yohana 10:28).
 8. Aliabudiwa na malaika (Zaburi 148:2): God—Waebrania 1:6; Yesu—Luka 4:8.
 9. Kudra na utawala wa milele (Luka 10:22; Yohana 3:35; 17:2; Waefeso 1:2; Wakolosai 1:17; Waebrania 1:3; Ufunuo 1:5).

USHAHIDI WA KIMAANDIKO

Je Maandiko hudai kwa hakika kwamba Kristo ni Mungu? NDIYO. Kana kwamba “uthibitisho kwamba Yesu Kristo ni Mungu” hazitoshi, Maandiko hubainisha wazi kuhusu uungu wa Kristo:

 1. Yohana 1:1, 14, “Naye Neno alikuwa Mungu….  Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu.”
 2. Yohana 1:18, “Mwana pekee aliye katika kifua cha Baba.”
 3. Yohana 20:28, Tomaso alimwambia Yesu “Bwana wangu na Mungu wangu!”
 4. Waebrania 1:8, “Lakini kwa habari za Mwana asema, Kiti Chako cha enzi, Mungu, ni cha milele na milele.”
 5. 2 Petro 1:1, “Mungu wetu, na Mwokozi Yesu Kristo.”
 6. 1 Yohana 5:20, “Yesu Kristo. Huyu ndiye Mungu wa kweli, na uzima wa milele.”
 7. Wakolosai 2:9, “katika Yeye unakaa utimilifu wote wa Mungu, kwa jinsi ya kimwili.”
 8. Isaya 9:6, “Maana kwa ajili yetu Mtoto amezaliwa,… Naye ataitwa jina Lake,… Mungu mwenye nguvu.”
 9. Isaya 7:14; Mathayo 1:23, “Imanueli”—”Mungu pamoja nasi.”
 10. Waebrania 1:1-3, “Yeye kwa kuwa ni mng’ao wa utukufu Wake na chapa ya nafsi Yake….”
 11. Wakolosai 1:15-17, “Naye ni mfano wa Mungu asiyeonekana… katika Yeye vitu vyote viliumbwa.”
 12. Matendo 20:28, Kanisa lilinunuliwa kwa damu ya Mungu.
 13. 2 Wakorintho 4:4, “Kristo aliye sura yake Mungu.”
 14. Warumi 9:5, “[Kristo] Ndiye aliye juu ya mambo yote, Mungu, mwenye kuhimidiwa milele. Amina.”
 15. 1 Wakorintho 1:24, “nguvu ya Mungu, na hekima ya Mungu.”
 16. 2 Wathesalonike 1:12, “Mungu wetu na ya Bwana Yesu Kristo.”
 17. Wafilipi 2:6, “ambaye Yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu.” (Kiyunani huweza kufasiriwa kimsingi kama “akiendelea kujitegemeza katika namna ya Mungu.”)

SHUHUDA ZINGINE

 1. Tomaso: “Bwana wangu na Mungu wangu!” (Yohana 20:28).
 2. Yohana: Yesu Mwenyewe ni “sawa na Mungu” (Yohana 5:18).
 3. Wayahudi: “Wewe uliye mwanadamu wajifanya mwenyewe u Mungu.” (Yohana 10:33).
 4. Kuhani Mkuu: “Mmesikia kufuru Yake” (Marko 14:61-64).
 5. Petro: “Mwana wa Mungu aliye hai.” (Mathayo 16:16; kwa Myahudi, hili lilimfanya awe sawa na Mungu, cf., Yohana 5:18).

MAANA YA KIIBADA: Wakati ule Kristo alipowaambia Wayahudi, “Yeye Ibrahimu asijakuwako, Mimi Niko,” (Yohana 8:58), alikuwa akitamka kuhusu uungu Wake, nao wasikilizaji Wake walitambua maana husika ya maneno Yake, maana “waliokota mawe ili wamtupie”—adhabu ya Kiyahudi dhidi ya kufuru ya kiwango cha juu. Bila shaka alitumia maneno ya Mungu katika Agano la Kale, “MIMI NDIYE NIKO” (Kut. 3:14), ambayo kwa muda mrefu yalitambuliwa kama alama ya uungu, akiasha Kwake Mwenyewe hulka za uishinafsi. Wapendwa, Yesu Kristo ni Mungu hakika.

Pili, utakatifu ni sehemu ya asili Yake. Wakati wa tangazo la kuzaliwa Kwake, malaika alimwambia Mariamu, “Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu.” (Luka 1:35). Machoni pa Yesu, pepo walipaza sauti, “Tuacheni!… Najua Wewe ni nani—Mtakatifu wa Mungu” (Marko 1:24).

Utakatifu (kutokuwa na dhambi) kwa Yesu Kristo ni bayana kulitabiriwa katika Agano la Kale (Zab. 45:7; Isa. 53:9; Yer. 23:5; Zek. 9:9). Alipokuja, aliishi maisha matakatifu—maisha Yake yote miongoni mwa wanadamu.

Yesu Kristo alitangazwa bayana katika Agano Jipya kama:

 1. “Mtakatifu wa Mungu” (Marko 1:24),
 2. “Kitakatifu” (Luka 1:35),
 3. “mtakatifu Yesu” (Matendo 4:27),
 4. “hakutenda lolote lisilofaa” (Luka 23:41),
 5. “wala ndani Yake hamna udhalimu” (Yohana 7:18),
 6. “Mtakatifu, yule Mwenye haki” (Matendo 3:14),
 7. “Yeye asiyejua dhambi” (2 Kor. 5:21),
 8. “asiye na ila” (1 Petro 1:19),
 9. “asiye na waa” (1 Petro 1:19),
 10. “Yeye hakutenda dhambi” (1 Petro 2:22),
 11. “Aliyetengwa na wakosaji” (Ebr. 7:26).

Dokezo moja zaidi hapa: Je angeweza kuanguka? Ndiyo, lakini badala yake, alimtegemea Baba kikamilifu. Katika kitabu cha Waebrania, Roho ana mengi ya kusema kuhusu jinsi Kristo alivyotimilishwa: “Yeye, siku hizo za mwili Wake, alimtolea Yule, awezaye kumwokoa na kumtoa katika mauti, maombi na dua pamoja na kulia sana na machozi, akasikilizwa kwa jinsi alivyokuwa mcha Mungu; na, ingawa ni Mwana, alijifunza kutii kwa mateso hayo yaliyompata; naye alipokwisha kukamilishwa, akawa sababu ya wokovu wa milele kwa watu wote wanaomtii.” (Waebrania 5:7–9)

Naam! Hili hutufikisha kwenye wazo la nne: unyenyekevu wa Kristo. Ilhali Kristo ni Mungu, lazima tukumbuke kwamba katika utahamilisho alikuwa amesalimisha matumizi binafsi ya hulka Zake (Wafilipi 2:6-8; Yohana 5:30). Akiwa mwanadamu kamili, alikuwa mtumishi wa Baba, kama mfano kwetu (Yohana 13:4, 5). Hivyo, wakati akiwa duniani, yalikuwepo baadhi ya mambo ambayo Baba hakumruhusu ajue, na katika ubinadamu Wake hakuwa akijua kila kitu. Hivyo, hakujua wakati wa ujio Wake (Marko 13:32); alienda kuona endapo lilikuwepo tunda kwenye mtini (Marko 11:13) Naye akastaajabia kutoamini (Marko 6:6) na imani (Mathayo 8:10).

HATUA YA MAAMUZI: Ni mwitikio gani unaodhani somo hili ingepaswa kutuhimiza kufanya?  [1] Amini kwamba Yesu Kristo ni Mungu. Amini kwamba Yeye ni wa milele. Isaya alimwita kuwa ni “Baba wa milele” (Isa. 9:6). Mika alimtaja kama Yule “ambaye matokeo Yake yamekuwa tangu zamani za kale, tangu milele.” (Mika 5:2). Paulo alitambua uwepo Wake kuwa ni “kabla ya vitu vyote ” (Kol. 1:17), na Yohana anaafiki: “Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu. Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo Yeye hakikufanyika chochote kilichofanyika.” (Yohana 1:2, 3).

[2] Amini ujumbe wa injili –Utahamilisho, Msalaba, Ufufuo, Kupaa Mbinguni, Ujio wa Pili: “Na bila shaka siri ya utauwa ni kuu. Mungu alidhihirishwa katika mwili, Akajulika kuwa na haki katika roho, Akaonekana na malaika, Akahubiriwa katika mataifa, Akaaminiwa katika ulimwengu, Akachukuliwa juu katika utukufu.” (1 Timotheo 3:16)

MAAMUZI YANGU LEO

Weka tiki kwenye kisanduku sahihi kinachoakisi uamuzi wako leo:

 • Naamini kwamba kweli Yesu Kristo ni Mungu.
 • Kwamba Baba na Mwana ni Mmoja.
 • Kwamba Mwana amekuwepo milele kadimu.
 • Kwamba wokovu hupatikana kupitia Mwana.
 • Kwamba Mwana anakuja tena kutekeleza hukumu
 • Ni shauku yangu kumpokea Yesu Kristo maishani mwangu na kuokolewa.

WIMBO WA KUFUNGA: Nipe Habari za Yesu – (SDAH 152).

Nipe habari za Yesu, Andika moyoni mwangu kila neno. Nisimulie kisa cha thamani sana, Kitamu kilichowahi kusikiwa. Niambie jinsi malaika katika kibwagizo, Waliimbwa wakati wakikaribisha kuzaliwa Kwake. “Atukuzwe Mungu juu mbinguni, Na duniani iwe amani na habari njema kwa watu aliowaridhia.”

Nipe habari za Yesu, Andika moyoni mwangu kila neno. Nisimulie kisa cha thamani sana, Kitamu kilichowahi kusikiwa.

Pale alipofunga pekee jangwani, Nisimulie habari za siku za kale. Jinsi ambavyo kwa ajili ya dhambi zetu alijaribiwa, Lakini akawa mshindi hatimaye. Nisimulie kuhusu miaka ya kazi Zake, Nisimulie kuhusu huzuni aliyobeba. Alidharauliwa na kuteswa, Hakuwa na makazi, alikataliwa na alikuwa maskini.

Nisimulie kuhusu msalaba ambapo aligongomelewa, Akitapatapa kwa uchungu na maumivu. Niambie kuhusu kaburi walimomlaza, Nisimulie jinsi alivyoishi tena. Upendo katika kisa hicho adhimu sana, bayana zaidi kuliko niwezavyo kuona daima. Tulia, hebu nilie wakati ukinong’oneza, Upendo ulinilipia fidia.

Iweni na Siku Yenye Baraka: “Alikuwako ulimwenguni, hata kwa Yeye ulimwengu ulipata kuwako, wala ulimwengu haukumtambua. Alikuja Kwake, wala walio Wake hawakumpokea. Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina Lake:” (Yohana 1:10–12)

Sauti ya Injili/ Mwongozo wa Kujifunza Biblia/ Utangulizi kuhusu Kristolojia (Fundisho juu ya Yesu Kristo)/ Somo # 1