Zaburi 91: Mwongozo wa Biblia.

ZABURI 91: MWONGOZO WA IBADA.

Ibada Ya Alfajiri/ “Mwongozo wa Ibada” unaoshabihiana na Mpango wa Usomaji wa Biblia wa Leo: Zaburi 91/ Somo: “Usalama wa Wale wanaomtumaini Bwana”/ 19-BSG-91A: (Zaburi 91:1-16)/ Wimbo: Yote Namtolea Yesu (NZK # 146)

UCHUNGUZI: Matokeo ya kumtumaini Mungu: Amani (Isa 26:3-4); Usalama (Zab. 125:1; Mit. 29:25); Ulinzi dhidi ya hatari (Zab 91:3-10); Uhuru dhidi ya Hofu (Zab 27:1; Zab 23:4)

TAFAKARI: “Zab. 91 ina ujumbe wa faraja kwa wote ambao hupita katika nyakati za shida, na hasa kwa “watu wa Mungu wanaozishika amri” (8T uk. 120) na kwa wale ambao watapitia “wakati wa shida” na hatari ya siku za mwisho” (SDABC 3:843). Kwa nini tunapaswa kumwamini Mungu? Tunawezaje kuwa na uhakika kwamba anaweza kutatua matatizo yetu? Jibu hupatikana katika majina Yake manne kulingana na aya ya 1-2: Yeye ni ALIYE JUU (Elyon); Mwenyezi Mungu (Shaddai); Bwana (Yahweh); Mungu wako (Elohim).

Kwa nini tunapaswa kumkaribia Mungu? Kwa sababu Yeye ndiye usalama wetu katika kila kitu: Yeye ni kimbilio na ngome yetu (aya ya 2). Yeye ndiye hutuokoa kutoka katika “mtego wa mwindaji, na katika tauni iharibuyo” (aya ya 3); Yeye hufunika na kutulinda “chini ya mbawa Zake” (aya ya 4); Yeye hututuliza katika hali zote za kutisha: katika nyakati za ugaidi au kushambuliwa; katika nyakati za ugonjwa/ uharibifu; na katika nyakati za hatari isiyokwepeka (aya ya 5-7). Yeye huhakikisha kwamba sisi tunakwepa na kushuhudia adhabu ya waovu (aya ya 8). Yeye hutufanya sisi kuwa washindi dhidi ya Simba na Nyoka: picha ya Shetani (Zab. 91:13, cf. Mwa. 3:1-24; 2 Cor. 11:3; 1 Pet. 5:8; Ufunuo 12:9; 20:2).

MAANA YA KIIBADA: Wapendwa, siyo siri, Bwana anaweza kufanya mambo haya kwa ajili yetu. Yeye ana uwezo, Yeye yu tayari, Yeye huheshimika pale watoto Wake wanapomlilia kuomba msaada wa haraka! Tunapaswa kumpenda na kumkiri, kwa sababu Yeye ndiye mkombozi, mlinzi, na atukwezaye — Yeye hutuinua “palipo juu” (aya ya 14). Mwisho, tunapaswa kuliita jina Lake na Yeye atajibu. Hebu zingatia hapa kile kitakachotokea tunapomuita: Atakuwa pamoja nasi katika matatizo; Atatukomboa na kutuheshimisha; Atatuzawadia ujira wa maisha marefu; na Atatupa wokovu Wake.

Zingatia: Ahadi nyingi zilizomo katika Zaburi hii ni kwa wale ambao wameamua kutii Amri za Mungu. Ni wale watakaoketi “mahali pa siri pake Aliye Juu,” na kukaa “katika uvuli wake Mwenyezi.” Hawa ndio watakaoweza kusema kwa ujasiri kuwa – “Bwana ndiye kimbilio langu na ngome yangu, Mungu wangu nitakayemtumaini” (aya ya 1-2). Wapendwa, Bwana anaita kila mmoja wetu asubuhi ya leo: kukaa, kudumu katika pendo Lake (Yn. 15:1-4), kutii amzi Zake, kumtumaini na kumtegemea Yeye. Yatupasa kufahamu kwamba Yeye kamwe hatatuacha au kutusahau (Ebr. 13:5)

HATUA YA MAAMUZI: Ni mwitikio gani unaodhani sura hii ingepaswa kutuhimiza kufanya? [1] Sogea karibu na Mungu — ishi katika uwepo Wake; [2] Mwamini Mungu — Anaweza kukulinda; Mwamini Yeye ili akusaidie; [3] Kuwa makini — ulinzi wa Mungu ni wa masharti: lazima ukae ndani Yake, utii amri Zake, uishi katika uwepo Wake, na kufanya uamuzi wa kumfanya Yeye ndiye awe kimbilio lako. (Achana na ushirikina: waganga, wapiga ramli, n.k. hawatakusaidia chochote) [4] Dai ulinzi wa Malaika: “Kwa kuwa atakuagizia malaika Zake wakulinde katika njia zako zote. Mikononi mwao watakuchukua, Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe” (aya ya 11-12); [5] Shikamana na Bwana; Mwite Yeye, Naye atakujibu (aya. 15-16).

SAUTI YA INJILI: Kipengele hiki kimeandikwa kana kwamba Mungu ndiye anaongea nawe, moja kwa moja, kwa sababu hufanya hivyo. Je, Bwana ananiambia nini asubuhi ya leo? Mwanangu, “Kwa kuwa umekaza kunipenda: “Nitakuokoa; Nitakuweka mahali palipo juu.” Kwa kuwa amelijua Jina langu: “Utaniita, Nami nitakuitikia; Nitakuwa pamoja nawe taabuni; Nitakuokoa na kukutukuza.” Ahadi yangu ya mwisho kwako ni hii: “Kwa siku nyingi nitakushibisha, Nami nitakuonesha wokovu Wangu.” (Zab. 91:14-16).

MWITIKIO WANGU: Kwa Neema ya Mungu: Nitaketi mahali pa siri pake Aliye Juu. Nitakaa katika uvuli wake Mwenyezi. Nitasema, Bwana ndiye kimbilio langu na ngome yangu, Mungu wangu nitakayemtumaini.

Uwe na Alfajiri Njema: “Itakuwa utakaposikia sauti ya Bwana, Mungu wako, kwa bidii, kutunza kuyafanya maagizo Yake yote nikuagizayo leo, ndipo Bwana, Mungu wako, atakapokutukuza juu ya mataifa yote ya duniani; na baraka hizi zote zitakujilia na kukupata usikiapo sauti ya Bwana, Mungu wako.” (Torati 28:1-2)