Zaburi 89: Mwongozo wa Biblia.

Ibada Ya Alfajiri/ “Mwongozo wa Ibada” unaoshabihiana na Mpango wa Usomaji wa Biblia wa Leo: Zaburi 89/ Somo: “Kumbuka Agano Lako na Daudi”/ 19-BSG-89A: Wimbo: Yote Namtolea Yesu (NZK # 122)

UCHUNGUZI: Agano la Mungu ni la milele (2 Sam 7:11-16; 23:5; 1 Fal. 2:45; 2 Nyak. 13:5; Zab. 18:50; 89:3-4, 28-29, 35-37; Yer. 33:17)

TAFAKARI: Katika Zaburi 89 tunaona maneno matano: Sifa, Agano, Tatizo, Ombi, na Hitimisho. Kwanza, Sifa: Mtunga zaburi anataka kumsifu Mungu kwa mambo manne — Utu Wake (Zab. 89:1-2, 5-8, 14); Nguvu Zake (Zab. 89:9-13); Utoaji Wake (Zab. 89:15-18); na Ahadi Zake (Zab. 89:3-4, 19-37). Agano: Katika Zab. 89:19-37, mtunga zaburi anaongelea mafunuo matakatifu ambayo Bwana huzindua agano la Daudi. Tatizo: Katika Zaburi 89:38-51, anaomboleza hali ya taabu katika ufalme wa Daudi na kutaka Bwana agairi (asamehe) kwa sababu inaonekana kana kwamba Bwana amewakataa watu Wake. Ombi: Katika Zaburi 89:46 -51, tunaona ombi kwa Mungu kutimiza ahadi Zake na kurejesha neema Yake kwa ufalme. Hitimisho: Aya ya mwisho (Zab 89:52) kuna neno “Amina, Amina” ambalo linahitimisha Kitabu cha Tatu (yaani, Zaburi 73 – 89).

MAANA YA KIIBADA: “Hii ni Zaburi kuu ya Agano. Agano linahusu ofisi ya Daudi ya kifalme, na katika Zaburi hii tumepewa utabiri wa Masihi ajaye, Yesu Kristo” (John G. Butler). Israeli waliteseka sana kwa sababu ya kutotii kwao, hata hivyo, Bwana alisamehe, akaachilia makossa yao na kutimiliza Agano lake na Daudi. Masihi (Yesu Kristo) alitujia kutoka kwenye kwenye mstari (uzao) wa Daudi: “Nami nitamjalia kuwa mzaliwa Wangu wa kwanza, Kuwa juu sana kuliko wafalme wa dunia” (aya ya 27).

Fikiria onyo hili: “Wanawe wakiiacha sheria Yangu, Wasiende katika hukumu Zangu; Wakizihalifu amri Zangu, Wasiyashike maagizo Yangu; Basi, nitawarudi makosa yao kwa fimbo, Na uovu wao kwa mapigo” (Zaburi 89:30-32) Bwana alitoa onyo kali kwa uzao wa Daudi, ili wasiiache sheria Yake. Wapendwa, kuna hatari ya kifo pale tunapoiacha sheria ya Mungu, au kukataa kutii amri Zake. Tunaweza kuteseka sana kwa kutotii na kuadhibiwa na Mungu. Milele kutakuwa na huzuni kuu kuhusu baraka tulizozipoteza kutokana na kutotii kwetu.

SAUTI YA INJILI: Kipengele hiki kimeandikwa kana kwamba Mungu ndiye anaongea nawe, moja kwa moja, kwa sababu hufanya hivyo. Je, Bwana ananiambia nini asubuhi ya leo? Mwanangu, nakupenda sana! Sitaki dhambi yoyote ndani yako. Sitaki uteseke kwa matokeo ya dhambi. Ingekuwa heri kwako endapo ungekubali kutii amri Zangu. Sikilizeni maneno haya: “Kama mkikubali na kutii, mtakula mema ya nchi; bali kama mkikataa na kuasi, mtaangamizwa kwa upanga; maana kinywa cha Bwana kimenena haya.” (Isaya 1:19-20)

MAAMUZI YA LEO: Nitamsifu Bwana kwa upendo Wake usiopunguka, uaminifu, huruma na neema Yake (Zab. 89:1, 2, 5, 8, 14, 24, 28, 33, 49); Nitamwamini Mungu kutimiza ahadi Zake (Zab. 89:19-37); Nitakuwa makini! — Mungu anawakataa wale wanaokataa ahadi Zake, agano Lake (Zab. 89:38-45); Nitamlilia Bwana atimize ahadi Zake kwangu – Tumaini langu Kwake kamwe halitafifia (Zab. 89:46-51); Mwisho, nitapiga kelele za shangwe nikumsifu Bwana milele zote! Na ahimidiwe Bwana milele. Amina na Amina (Zaburi 89:52).

Uwe na Siku Njema:  “Haya, njoni, tusemezane, asema Bwana. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu.” (Isaya 1:18)