Mungu Kama Utatu Kihusiano

72-002 (Kumb. 6:4)/ Fundisho Kuhusu Mungu-Seh 2/ Aya Kuu: “Sikiza, Ee Israeli; Bwana, Mungu wetu, Bwana ndiye mmoja.” (Kumbukumbu 6:4)

Malengo ya Somo: [Kufahamu Utatu].

 1. Kuwasilisha uthibitisho wa Biblia kuhusu uungu wa Baba, Mwana, na Roho
 2. Kuwasilisha uthibitisho wa Biblia kuhusu Mungu kama Utatu kimahusiano
 3. Kuamini kwamba kuna Mungu mmoja katika Nafsi tatu
 4. Kuamini kwamba Yesu Kristo ni Mungu
 5. Kujua kwamba Roho siyo ‘upepo/kiasili,’ bali ni Mungu
 6. Kuthamini zaidi kuhusu Utatu
 7. Kuwa na uwezo wa kujadili, kama siyo kutetea, Utatu.

Maswali ya Moyoni: [1] Kwa jinsi gani Maandiko huthibitisha uungu wa Baba, Mwana, na Roho? [2] Unawezaje kuonesha kutoka Agano la Kale kwamba kuna wingi katika Utatu? [3 Je ni uthibitisho gani wa Biblia uliopo kuhusu Utatu? [4] Unaweza kubainishaje kwenye Maandiko kwamba kila Nafsi katika Utatu huwapenda wengine wawili? [5] Tunajuaje kutokana na lugha ya Kiebrania kwamba ‘Shema’ ya Kumbukumbu 6:4 haimzumzii Mungu katika nafsi ya umoja? Inazungumzia nini, na kwa nini?

UTANGULIZI

“Utatu” ni mojawapo ya mada ngumu zaidi katika teolojia ya Kikristo. Neno ‘Utatu’ halipo kwenye Biblia. Ni istilahi ya kiteolojia. Neno hili halitumiwi kwenye Maandiko. Hata hivyo, ni fundisho salidi la Biblia!

Mungu ni Utatu wa Kimahusiano: “Maandiko humwasilisha Mungu kama Utatu wa kimahusiano, ambapo Nafsi tatu za Uungu zina uzoefu wa upendo wa milele, kiungu, na kufadhiliana, ambapo hulazimu uzoefu wa kutoa na kuchua katika asili yao kama Mungu wa upendo.”

“Mungu ni Mungu wa kimahusiano. Lazima hili lisemwe kabla ya kinginecho, kwa sababu hivyo ndivyo Baba, Mwana, na Roho wameishi pamoja milele. Huu ndio uzoefu ambao wamepitia daima. Huu ndio uzoefu watakaopitia milele.” [Norman R. Gulley, Systematic Theology: God as Trinity, (Berrien Springs, MI: Andrews University Press, 2011), 3].

UTATU NA KISA CHA UUMBAJI

Ili kuelewa utatu tunaanza na kisa cha uumbaji. Mungu ni Muumbaji wa mbingu na dunia.–  “Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi. Nayo nchi ilikuwa ukiwa, tena utupu, na giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji; Roho ya Mungu ikatulia juu ya uso wa maji.” (Mwanzo 1:1–2)

Ushahidi wa Uwingi wa Uungu:Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano Wetu, kwa sura Yetu(Mwanzo 1:26) “G Mungu akasema, hebu Sisi [Baba, Mwana, Roho Mtakatifu] tumfanye mwanadamu katika sura Yetu” (Mwanzo 1:26, AMP)

“Katika uumbaji wa mwanamume na mwanamke katika sura ya Mungu (Mwa. 1:26–27), Nafsi za Utatu zinawakilishwa katika uumoja wa mwanamume na mwanamke kwenye ndoa. Maandiko hubainisha uhalisia wa sura hiyo kuwa ni Roho (Mwa. 1:2; Zab. 104:30; cf. Ayubu 33:4; 26:13) na akiumba kila kupitia Mwana (Kol. 1:15–16; Ebr. 1:2b), na hivyo uhalisia wa sura hiyo ni uumoja katika Nafsi tatu, au Utatu.” [Norman R. Gulley, Systematic Theology: God as Trinity, (Berrien Springs, MI: Andrews University Press, 2011), 24].

“Neno ‘sisi’hudai uwepo wa angalau nafsi mbili zinazoshauriana pamoja. Kauli kwamba mwanadamu aliumba katika mfano “wetu” na aliumbwa katika sura ya ‘Mungu’ hupelekea hitimisho kwamba wale washaurianao lazima wawe nafsi za Uungu uleule.

‘Ukweli huu, uliodokezwa katika AK, katika maandiko kadhaa kama yale yaliyojadiliwa hapa, na Mwa. 3:22; 11:7; Dan. 7:9, 10, 13, 14; nk., umefunuliwa kikamilifu na bayana katika AJ, ambako tunaambiwa kwa kauli dhahiri kwamba Kristo, nafsi ya pili ya Uungu, ilhali akiitwa Mungu na Baba Mwenyewe(Ebr. 1:8), alishiriki na Baba Yake katika kazi ya uumbaji. Maandiko kama Yohana 1:1–3, 14; 1 Kor. 8:6; Kol. 1:16, 17; Ebr. 1:2 hutufundisha siyo tu kwamba Mungu Baba aliumba vitu vyote kupitia Mwanawe, bali pia kwamba uhai wote unadumishwa na Kristo.” [The Seventh-Day Adventist Bible Commentary, 1:215].

YESU: NAFSI YA PILI YA UTATU

Ili kuelewa utatu katika maelezo yafuatayo, tutamwangalia Yesu Kristo. Yapo maswali mawili muhimu: uungu, na ubinadamu wa Yesu.

[1] Je Yesu Kristo alikuwa nafsi? Ndiyo. Alikuwa nafsi–“Kwa sababu Mungu ni mmoja, na mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja, Mwanadamu Kristo Yesu” (1 Timotheo 2:5)

Yesu Kristo alikuwa na hulka: aliwastaajabisha wengi kwa mafundisho Yake (Mathayo 7:28). Mtindo Wake ulikuwa na mguso mahususi (Mathayo 22:16). Alikuwa na nia (Wafilipi 2:5). Alikuwa na utashi (Mathayo 8:7). Alikuwa na hisia (Mathayo 14:14).

[2] Je alikuwa Yesu Kristo Mungu? Ndiyo– “Hapo mwanzo [kabla ya muda wowote] alikuwepo Neno [Kristo], Naye Neno alikuwa kwa Mungu, Naye Neno alikuwa Mungu Mwenyewe.” (Yohana 1:1, AMP) Alikuwepo tangu mwanzo (Yohana 1:1); alikuwa Muumbaji (Yohana 1:3; Wakolosai 1:16); alikuwa ukamilifu wa Mungu (Yohana 1:1; Wakolosai 2:9); aliabudiwa na kupokea ibada (Mathayo 2:2; Yohana 20:28); Naye alisamehe dhambi (Mathayo 9:2).

ROHO MTAKATIFU: NAFSI YA TATU YA UTATU

[1] Roho Mtakatifu ni nafsi

 • Yesu alimwelezea kama paraclete ‘mwingine’ (Yohana 14:16).
  • Paraclete (Kiyunani, parakletos) ni yule ajaye kando ya.
  • Yesu alipomwita kuwa Yeye ni paraclete ‘mwingine,’ hii ilimaanisha kwamba Roho Mtakatifu ni nafsi kama vile tu Yesu alivyo nafsi.
 • Kamwe Roho siyo ‘kitu’ bali “Yeye” (Yohana 16:8, 12–14; Warumi 8:26).
 • Ana hulka (Matendo 5:32). Hivyo ndivyo alivyotambuliwa na mitume.
 • Ana hisia (Waefeso 4:30).
 • Ana utashi (Matendo 16:6–7.)
 • Ana nia (Yohana 3:8; Warumi 8:27).

[2] Roho Mtakatifu ni Mungu.

 • Yeye ni muumbaji (Mwanzo 1:2).
 • Yeye ni wa milele (Waebrania 9:14).
 • Anaitwa Mungu (1 Kor. 12:4–6; 2 Kor. 3:17; Matendo 5:3–4).
 • Anatupatia uhai (Yohana 6:63).
 • Anasadikisha kuhusu dhambi (Yohana 16:8).
 • Anatuombea (Warumi 8:26–27).

UTATU NA AGANO JIPYA

Kile ambacho Agano Jipya hufundisha bayana kama Mungu katika utatu huibuka kwa mdokezo katika Agano la Kale.

[1] Istilahi ya jumla katika Agano la Kale kuhusu Mungu ni Elohimu

 • Neno la Kiebrania ni wingi.
 • Hii kwa sehemu kubwa huzungumzia utaabadi wa Mungu: uwezo Wake na sifa Yake ya kuwa tofauti kabisa
 • Elohimu huumba kwa njia ya Neno na Roho (Mwanzo 1:1–3).

[2] Fundisho hili huwa bayana zaidi katika Mwanzo 1:26: ‘Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano Wetu.’

[3] Kitendo cha uumbaji wa Mungu na utawala Wake vinahusishwa baadaye na Neno lililonasibishwa kama Hekima.

 • Mungu ndiye aijuaye njia yake [ya kupaka Hekima], Naye anajua mahali pake [Hekima iko kwa Mungu pekee]. Maana anatazama hata miisho ya nchi, Na kuona chini ya mbingu nzima. Apate kuufanyia upepo uzito wake; Naam, anayapima maji kwa kipimo. Hapo alipoiwekea mvua amri, Na njia kwa umeme wa radi. Ndipo alipoiona [Hekima] na kuitangaza; Aliithibitisha, naam, na kuichunguza [kwa ajili ya matumizi Yake Mweneyewe, Naye pekee ndiyo huimiliki].” (Ayubu 28:23–27, AMP)
 • Bwana alikuwa nami [Hekima] katika mwanzo wa njia Yake, Kabla ya matendo Yake ya kale.” (Mithali 8:22, AMP)

[4] Roho hutazamwa kama mpaji wa baraka zote na ndiye chanzo cha nguvu, ujasiri, utamaduni na utawala

 • Ndipo Bwana akashuka ndani ya wingu, akanena naye, akatwaa sehemu ya Roho iliyokuwa juu ya Musa, akaitia juu ya wale wazee sabini; ikawa, Roho hiyo ilipowashukia, wakatabiri, lakini hawakufanya hivyo tena.” (Hesabu 11:25)
 • Roho ya Bwana ikamjilia juu yake, naye akawa mwamuzi wa Israeli; akatoka kwenenda vitani, naye Bwana akamtia huyo Kushan-rishathaimu, mfalme wa Mesopotamia, mkononi mwake; na mkono wake ukamshinda Kushan-rishathaimu.” (Waamuzi 3:10)

[5] Roho wa Mungu amepewa nafasi ya juu kuhusu ukombozi na ufunuo, Naye amepangiwa jukumu la kumwimarisha Masihi katika kazi Yake

 • Na Roho ya Bwana atakaa juu Yake; Roho ya hekima na ufahamu, Roho ya shauri na uweza, Roho ya maarifa na ya kumcha Bwana” (Isaya 11:2)
 • Tazama Mtumishi Wangu nimtegemezaye; mteule Wangu, ambaye nafsi Yangu imependezwa Naye; nimetia Roho Yangu juu Yake; Naye atawatolea mataifa hukumu.” (Isaya 42:1)
 • Roho wa Bwana MUNGU i juu Yangu, Kwa sababu BWANA ameniwakfisha Niwahubiri maskini habari njema; Amenituma niwagange waliovunjika moyo, Niwatangazie mateka uhuru, Na kuwafungulia gereza hao waliofungwa” (Isaya 61:1)

[6] Roho angekuwa mfafanuzi wa jibu la imani na utii.

 • Hata Roho itakapomwagwa juu yetu kutoka juu; hata jangwa litakapokuwa shamba lizaalo sana; nalo shamba lizaalo sana litakapohesabiwa kuwa msitu.” (Isaya 32:15)
 • Nami nitawapa ninyi moyo mpya, Nami nitatia Roho mpya ndani yenu, Nami nitatoa moyo wa jiwe uliomo ndani ya mwili wenu, Nami nitawapa moyo wa nyama.” (Ezekieli 36:26)
 • Nami nitatia Roho Yangu ndani yenu, na kuwaendesha katika sheria Zangu, nanyi mtazishika hukumu Zangu, na kuzitenda.” (Ezekieli 36:27)
 • Hata itakuwa, baada ya hayo, ya kwamba nitamimina Roho Yangu juu ya wote wenye mwili; na wana wenu, waume kwa wake, watatabiri, wazee wenu wataota ndoto, na vijana wenu wataona maono.” (Yoeli 2:28)

[7] Manabii wote walizungumza kama walivyofanya kwa sababu Roho Mtakatifu alikuwa ndani yao na katika usemi wao Maana unabii haukuletwa popote kwa mapenzi ya mwanadamu; bali wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu, wakiongozwa na Roho Mtakatifu.” (2 Petro 1:21)

MDOKEZO WA UTATU KATIKA AGANO JIPYA.

Mahubiri ya Yohana Mbatizaji

 • Toba kwa Mungu (Mathayo 3:2, 7–8).
 • Imani katika ujio wa Masihi (Mathayo 3:11).
 • Ubatizo wa Roho Mtakatifu (Mathayo 3:11).

Ubatizo wa Yesu

 • Uwepo wa Yesu Mwenyewe.
 • Sauti ya Baba kutoka mbinguni (Mathayo 3:17).
 • Roho mfano wa huwa (Mathayo 3:16).

Tangazo la kuzaliwa Yesu

 • Utendaji wa Roho katika utahamilisho (Luka 1:35).
 • Yesu angeitwa Mwana wa Mungu (Luka 1:35).
 • Bwana Mungu angempatia enzi ya Daudi babaye (Luka 1:32).

Kanuni ya ubatizo: Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu” (Mathayo 28:19)

Uhusiano katika ya Baba na Mwana

 • Neno alikuwa ‘pamoja’ na Mungu huonesha uhusiano wa Utatu
 • Hakuna aliyemjua Mwana isipokuwa Baba, na kinyume chake (Mathayo 11:27).
 • Baba ‘alimtuma’ Mwana (Yohana 6:44).
 • Baba ‘humpenda’ Mwana (Yohana 5:20).
 • Baba ‘hukasimisha hukumu’ kwa Mwana (Yohana 5:22).

Mahubiri ya Petro (Matendo 2:32–33).

 • Yesu alitukuzwa kwenda mkono wa kuume wa Mungu
 • Yesu alipokea ahadi ya Roho kutoka kwa Baba.

Zingatia baraka zifuatazo za kitume:

 • Neema ya Bwana Yesu Kristo, na pendo la Mungu, na ushirika wa Roho Mtakatifu ukae nanyi nyote.” (2 Wakorintho 13:14)
 • Yohana, kwa yale makanisa saba yaliyoko Asia; Neema na iwe kwenu na amani, zitokazo kwake Yeye aliyeko na aliyekuwako na atakayekuja; na zitokazo kwa Roho saba walioko mbele ya kiti Chake cha enzi; tena zitokazo kwa Yesu Kristo, shahidi aliye mwaminifu, mzaliwa wa kwanza wa waliokufa, na mkuu wa wafalme wa dunia. Yeye atupendaye na kutuosha dhambi zetu katika damu Yake” (Ufunuo 1:4–5)

UHUSIANO KATI YA NAFSI YA UTATU

[1] Wanapeana sifa

 • Baba: humtukuza Mwana (Mathayo 3:17; 17:5; Yohana 5:20–23).
 • Yesu: humwenzi Baba (Yohana 5:19, 30–31; 12:28).
 • Roho: humwenzi Mwana (Yohana 15:26; 16:8–10, 14).

[2] Usiri hubainika kwa Baba

 • Katika uchaguzi wa watu (Yohana 6:37; Efe. 1:4).
 • Katika utendekaji wa matukio (Marko 13:32; Gal. 4:4)
 • Katika harakati na huduma ya Yesu (Yohana 5:16–17, 19, 30).

[3] Uwazi hubainika kwa Mwana

 • Alionekana bayana (1 Yohana 1:1, 14; 20:27).
 • Alibainisha kile ambacho hakikuonekana.
  • Uso wa Baba (Yohana 14:9).
  • Nia ya Baba (Yohana 14:20).
  • Mpango wa Baba (Yohana 19:30).

[4] Ubainishaji huonekana kwa Roho

 • Kusudi la Mwana (Matendo 2).
 • Fundisho la Mwana (Yohana 14:26; 1 Kor. 2:10).
 • Uhakikisho wa wokovu (Warumi 5:5).
 • Roho huleta usahibu kwa Baba (Warumi 8:15).

ZINGATIA: Roho hutuwasilishia ujumbe anaoupokea kutoka kwa Baba —“Lakini Yeye, Roho wa Kweli (Roho aletaye Kweli) atakapokuja, atawaongoza awatie kwenye Kweli yote [ukweli wote mkamilifu]; kwa maana hatanena kwa shauri Lake Mwenyewe [kwa mamlaka Yake], lakini yote atakayoyasikia atayanena [kutoka kwa Baba; atawasilisha ujumbe aliopewa], na mambo yajayo [huko baadaye] atawapasha habari Yake.” (Yohana 16:13)

[5] Maombezi hufanywa na Mwana na Roho kwa ajili yetu

 • Kupitia Roho (Warumi 8:26–27).
 • Kupitia Mwana (Warumi 8:31f; Waebrania 7:25).

[6] Hakuna uhasama katika Utatu. Unaweza kumwomba yeyote miongoni mwa Nafsi za Uungu: Yesu alisema tuombe kwa Baba (Mathayo 6:9); ila maombi huelekezwa kwa Yesu (Luka 23:42; Matendo 7:59).

[7] Utatu na wokovu wa wadhambi: Uhusiano wa nafsi za Utatu juu ya wokovu wa wadhambi unaweza kuhitimishwa hivi:

 • Baba aliufikiria (Waefeso 1:9).
 • Mwana akauleta (1 Wakorintho 6:20).
 • Roho akautekeleza (Yohana 6:63).

HITIMISHO: Fundisho la Utatu ni kiini katika imani ya Ukristo. Fundisho lolote lisiloafiki Utatu ni uzushi. Uzushi ni neno zito; humaanisha fundisho la uongo. Ni bayana kama tulivyoona kwa ufupi, Utatu ni fundisho la Biblia.

“Utatu, kama ilivyobainishwa kwenye Agano la Kale na Agano Jipya, ni Mungu wa upendo. Utatu umeundwa na Nafsi tatu za uungu, za milele, sawa, zenye uishinafsi kama Mungu Mmoja. Zina ushirika wa upendo, Utatu wa kihusiano, pamoja na historia ya ndani ya upendano baina Yao. Kila mmoja humwita mwingine “Mungu” katika Utatu. Shema ya Agano la Kale humzungumzia Mungu kama Mungu mmoja, na wala siyo kama Mungu mkiwa. Mungu wa Biblia ni wa pekee miongoni mwa miungu (1) kama Muumbaji wa yote yaliyopo, (2) kama wingi, (3) kama Utatu wa kihusiano, na (4) kama wote watatu wakishiriki katika mpango wa kuwaokoa wanadamu” [Norman R. Gulley, Systematic Theology: God as Trinity, (Berrien Springs, MI: Andrews University Press, 2011), 32].

HATUA YA MAAMUZI: Ni mwitikio gani unaodhani somo hii ingepaswa kutuhimiza kufanya? “Yesu akamjibu, Ya kwanza ndiyo hii, Sikia, Israeli, Bwana Mungu wetu ni Bwana mmoja; nawe mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote. Na ya pili ndiyo hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Hakuna amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi. Yule mwandishi akamwambia, Hakika, Mwalimu, umesema vema ya kwamba Mungu ni mmoja, wala hakuna mwingine ila Yeye.” (Marko 12:29–32)

Sauti ya Injili/ Mwongozo wa Kujifunza Biblia/ Mafundisho Makuu/ Utatu/ Somo # 2