Zaburi 88: Mwongozo wa Biblia.

Ibada Ya Alfajiri/ 19-BSG-88A: MWONGOZO WA IBADA.

Mwongozo wa Ibada unaoshabihiana na Mpango wa Usomaji wa Biblia wa Leo: Zaburi 88/ OMBI LA MSAADA KATIKA SHIDA /19-BSG-88A: (Zaburi 88:1-18)/ Wimbo: Nina haja Nawe, kila saa (NZK )

UCHUNGUZI: Matatizo yanaweza kuwa na manufaa katika kutuongoza sisi kumtafuta Mungu katika maombi (Waam. 4:3; Yer 31:18; Maomb. 2:17-19; Hos. 5:14-15; Yn. 2:1)

TAFAKARI: Zaburi hii inaweza kugawanywa katika sehemu kuu tatu: Kuteseka kwa maombi yasiyojibiwa (aya. 1-2, 13); Kuteseka kwa maumivu yasiyoisha (aya. 3-5, 9, 15); na Kuteseka kutoka katika mateso yasiyostahili (aya. 6-8, 10-12, 14, 16-18). Mtunga Zaburi analia kwa Mungu usiku na mchana (1-2) kwa sababu maisha yake yamejaa shida (3); Yeye yuko hatarini kufa (3-5); Macho yake yamepofusha kwa machozi (9); Anaomba rehema na msaada wa Bwana (9); Anasihi siku kwa siku (13); Amesumbuliwa na mambo haya toka ujanani, (15). Zaidi ya hayo, anahisi kama ghadhabu ya Mungu imemshukia sana (aya ya 6-7, 16); Anahisi kukataliwa kabisa na Mungu (aya ya 14); Inaonekana kwamba yeye yuko karibu na kuzama (17), na hakuna yeyote ambaye yuko karibu kumsaidia (aya ya 18).

MAANA YA KIIBADA: [1] Je, unapaswa kufanya nini unapougua giza la kukata tamaa na maombi yako yanaonekana kutojibiwa? “Mlilie Bwana usiku na mchana, akusaidia!” [2] Je unapaswa kufanya nini wakati maisha yako yamejaa shida, mateso, dhiki? Pale unapojisikia kama mtu mfu (aya ya 4)? Wakati wewe ni dhaifu sana, na bila nguvu yoyote (aya ya 5)? “Mlilie Bwana usiku na mchana, akusaidia!” [3] Je unapaswa kufanya nini wakati unahisi kama Mungu amekusahau au hakujali tena? Pale unapohisi kana kwamba Mungu amekuweka katika shimo la giza la maumivu na kukata tamaa? Wakati hakuna mtu yeyote wa karibu kukusaidia (aya ya 18)? — “Mlilie Bwana usiku na mchana, akusaidia!”

Wapendwa, Mungu peke yake ndiye awezaye kukuokoa. Mungu pekee ndiye awezaye kusikia na kujibu maombi yako. Endelea kuomba, usiipoteze matumaini! Unamwitaji sana aisikilize shida yako. Je, unakumbuka Yusufu (gerezani), Danieli (katika pango la simba), Kristo (katika Gethsemane)? Sikiliza andiko hili kuhusu Kristo Yesu: “Yeye, siku hizo za mwili Wake, alimtolea Yule, awezaye kumwokoa na kumtoa katika mauti, maombi na dua pamoja na kulia sana na machozi, Akasikilizwa kwa jinsi alivyokuwa mcha Mungu” (Ebr. 5:7). Usikate tamaa mpendwa katika janga hili la kirusi-corona. Omba na kulia, kama Yesu alivyoomba. Endelea “kumlilia Bwana usiku na mchana, Naye akusaidia!”Atakupa amani, suluhisho, na nguvu za kuvumilia shida, maradhi, na misukosuko ya maisha. Amina.

SAUTI YA INJILI: Kipengele hiki kimeandikwa kana kwamba Mungu ndiye anaongea moja kwa moja pamoja nawe. Je, Bwana ananiambia nini asubuhi ya leo? Mwanangu, katika saa ya giza: janga, mateso, unyonge, upweke, maradhi (kirusi-corona), n.k, Tafadhali fahamu kwamba MIMI NIPO PAMOJA NAWE! Sikiliza ahadi hii: “Upitapo katika maji mengi, Nitakuwa pamoja nawe; na katika mito, Haitakugharikisha; uendapo katika moto, Hutateketea; wala mwali wa moto, Hautakuunguza. Maana Mimi ni BWANA, MUNGU wako; Mtakatifu wa Israeli, Mwokozi wako.” (Isaya 43:2-3a) Nililie mchana na usiku, nami nitakusaidia!

HATUA YA MMAMUZI: Nitamlilia Bwana ili nipate rehema Zake (aya ya 9); Nitathamini kazi za Bwana (aya ya 10); Nitalisifu Mungu na kutangaza upendo wake na uaminifu wake (mstari wa 10); Nitajitahidi kutangaza haki ya Bwana hata katikati ya majanga, kukataliwa, na mateso, (aya ya 12).

Uwe na Siku Njema: “Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, Sitaogopa mabaya; Kwa maana Wewe upo pamoja nami, Gongo lako na fimbo yako vyanifariji.” (Zaburi 23:4)

Sauti ya Injili/ Mwongozo wa Biblia/ Zaburi 1-150/ Zaburi 88.