Kujitolea Kikamilifu Kiroho, 1/2

Kujitolea Kikamilifu Kiroho, Seh. 1/ Ibada ya Usiku/ Tafakari juu ya Maisha ya Kikristo/ 201A-001 (Marko 12:30)/ Aya Kuu: “Sikia, Israeli, Bwana Mungu wetu ni Bwana mmoja; nawe mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote.” (Marko 12:30).

Maswali ya Moyoni: [1] Ni mambo gani matatu ambayo tunapaswa kufanya kama wakristo ambayo yatadhihirisha wakfu wetu kamili wa kiroho kwa Mungu? Upendo, Maisha ya Kila Siku, Kujifunza. [2] Ni nini tunapaswa kufanya na ujumbe huu?

UPENDO: Tunapaswa kumpenda Bwana kwa moyo wetu wote, roho, akili, na nguvu (Marko 12:30). Katika aya hii, “Yesu aliariri maneno ya Shema (Mk 12:29), kisha akajibu swali la mtu mmoja kwa kueleza kile ambacho maneno hayo yalipaswa kumaanisha katika maisha ya kila siku ya wayahudi. Kwa sababu waliamini kwamba kuna Mungu mmoja (kinyume na dini nyingine, kama vile Warumi na Imani yao ya miungu wengi), wanapaswa kumpenda Mungu mmoja wa kweli kwa moyo wao wote. Yesu alinukuu Kumbukumbu la Torati 6:5, “Nawe mpende Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote.” Mathayo, Mariko, na Luka huongeza “kwa akili zako zote.”

“Neno la “mpende” ni agapao, upendo wa kipekee usio na ubinafsi, upendo ambao wanadamu hawawezi kuwa nao pasipo usaidizi wa Roho Mtakatifu. Roho wa Mungu hutusaidia kumpenda kama tunavyopaswa. Mungu anataka upendo na kujitolea kwetu Kwake, sio tu utiifu wetu. Akili ilichukuliwa kama kitovu cha fikra na uelewa, nafsi ilikuwa ni upekee na utu wa mtu, moyo ulikuwa kitovu cha matamanio na upendo, na nguvu iliajumuisha uwezo wa kimwili.” [Bruce B. Barton, Mark, Life Application Bible Commentary, (Wheaton, IL: Tyndale House Publishers, 1994), 354–355]. Wapendwa, tukimpenda Bwana kama vile tunavyopaswa, tutazishika amri Zake zote (Yohana 14:15).

MAISHA YA KILA SIKU: “Akawaambia wote, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate.” (Luka 9:23) Wapendwa, kujitwika misalaba yetu kila siku ni zaidi ya kumpokea Kristo — ni kuishi kwa ajili Yake, kwa kusudi Lake, kila siku!

KUJIFUNZA: Kristo anatualika tujifunze kutoka Kwake – “Jitieni nira Yangu, mjifunze Kwangu; kwa kuwa Mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu; kwa maana nira Yangu ni laini, na mzigo Wangu ni mwepesi” (Mathayo 11:29-30).

Wakristo wote wanapaswa kusoma na kujifunza Neno la Mungu zaidi. Mtume Paulo anatuhimiza kufanya hivyo, akisema “Jitahidi kujionyesha kuwa umekubaliwa na Mungu, mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, ukitumia kwa halali Neno la Kweli” (2 Timotheo 2:15).

Paulo alikuwa na shauku moja tu: Kumjua Bwana Yesu Kristo. Sikiliza maneno haya – “Ili nimjue Yeye, na uweza wa kufufuka Kwake, na ushirika wa mateso Yake, nikifananishwa na kufa Kwake”(Wafilipi 3:10). Mpendwa, imba pamoja nami kibwagizo hiki: “Ombi langu, Ombi langu, Ombi langu; Ombi langu, ni kumjua Bwana.”

Napenda maneno ya Wimbo # 54, “Nataka nimjue Yesu” katika Nyimbo za Kikristo. Mtunzi anaandika hivi— “Nataka nimjue Yesu, na nizidi kumfahamu; Nijue pendo Lake tu, wokovu wake kamili.” [Pambio]: “Zaidi zaidi, nimfahamu Yesu, Nijue upendo Wake, wokovu Wake kamili.” Je mpendwa ni shauku yako kumjua Kristo Yesu na Wokovu wake?

HATUA YA MAAMUZI: Ni mwitikio gani unaodhani somo hili lingepaswa kutuhimiza kufanya? [1] Tunapaswa kujitoa kikamilifu kwa Bwana; [2] Tunapaswa kujikana nafsi; Lazima tuache tamaa za ubinafsi na kujilimbikizia mali za kidunia, badala yake tuwafikirie wengine; [3] Lazima tujifunze kutoka kwa Kristo, kujifunza Neno Lake kila siku, na kujitwika nira Yake.

Usiku Mwema: “Neno moja nimelitaka kwa Bwana, Nalo ndilo nitakalolitafuta — Nikae nyumbani mwa Bwana, siku zote za maisha yangu, Niutazame uzuri wa Bwana, Na kutafakari hekaluni Mwake.” (Zaburi 27:4)

Sauti Ya Injili/ Dondoo za Kiibada/ Tabia na Mwenendo wa Mkristo/ Wazo la 1.