Kwa Njia ya Damu ya Kristo

Ibada Ya Alfajiri/ Kumfikia Mungu: KWA NJIA YA DAMU YA KRISTO/ 200A-002 (Efe. 2:12-13)/ Somo la 2/ Aya Kuu: “Lakini sasa, katika Kristo Yesu, ninyi mliokuwa mbali hapo kwanza mmekuwa karibu kwa damu Yake Kristo.” (Waefeso 2:13)

Maswali ya Moyoni: [1] Je, Mungu anapatikana? [2] Ni kwa njia gani tunaweza kumkaribia Mungu wetu? [3] Ni kwa namna gani Kristo anatufanya kuwa karibu na Mungu? [4] Kwa nini ilikuwa lazima kwa Kristo kufa ili kutuleta karibu na Mungu?

Kuna angalau sababu mbili kwa nini Kristo alikukufa kulingana na Aya hii— [1] Mwanadamu alikuwa amefarakana na Mungu: Wapenzi, tulikuwa tumetenda dhambi, tulimkataa na kumuasi Mungu — dhidi ya mapenzi na sharia Yake. Tulikuwa tumetenda uhalifu wa juu mbele za Mungu, na ikumbukwe kuwa, adhabu ya uhaini mkuu ni uhamisho, utengano au adhabu ya kifo. Wapendwa, tulikuwa kwenye mstari wa kifo, unaoitwa “Kifo cha Pili,” (Ufunuo 2:11; 20:6; 20:14; 21:8).

[2] Tulikuwa ulimwenguni pasipo Mungu: bila Mkombozi, bila Mpatanishi, bila Mwombezi. Kwa kifupi, tulikuwa hatuna matumaini! Je, unajua kwamba bila Kristo maisha hayana maana yoyote? Ni kama kuhadithia hadithi/ kisa fulani pasipo kufikia hitimisho. Ni kama kupeperushwa juu na chini katika bahari yenye dhoruba/ tufani kali, ambyo mwisho wake ni kuzama tu. Je, hali hii ilisababishwa na nini? Dhambi. Wapendwa, sisi ndiyo tullitanga mbali na Mungu, si Yeye aliyetuacha. Kumbuka Adamu na Hawa katika anguko la Edeni? (Mwa 3; cf. Isa 59:1-2).

[3] Sababu ya tatu ambayo ilisababisha Kristo afe: Mungu alitaka kuudhirishia ulimwengu mzima jinsi Yeye alitupenda sisi. “Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake.” (Yohana 15:13) Bwana alitaka kutupatia nafasi ya pili: “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.” (Yohana 3:16) Kwa maneno mengine, alikusudia kufuta adhabu ya kifo kilichodaiwa na sheria Yake— “Hakika utakufa.” Wapendwa, hakuna habari njema/ au bora zaidi kuliko hii! Hii ndiyo Injili.

Sasa, sikiliza wapenzi, jambo kuu ninaliliona katika somo la leo ni Upatanisho. Kwa sababu ya damu ya thamani ya Yesu Kristo pale Kalivari, sasa tunaweza kupatanishwa na Mungu. Sasa tunaweza kuletwa karibu na Mungu. Si kwamba sisi ni wastahiki, si kwamba sisi ni wenye haki — lakini kwa sababu ya utakatifu, na haki ya Kristo. Tunashirikishwa Haki ya Kristo, na hivyo sisi pia tunaweza kuletwa karibu na Mungu aliye Mtakatifu.

Bwana asifiwe leo kwa kuwa tuna uhuru usio na ukomo kumfikia Baba yetu wa mbinguni, kwa sababu ya Kristo! Je, ungependa kujongea karibu na Mungu tunapofunga kipindi hiki? Sikiliza maneno ya Wimbo # 495 – Karibu na moyo wa Mungu:

  • “Kuna mahala pa utulivu, karibu na moyo wa Mungu; Mahali ambapo dhambi haiwezi penyeza; karibu na moyo wa Mungu. [Kibwagizo]: Ee Yesu, Mkombozi, uliyetumwa toka kwa moyo wa Mungu, Tushike sasa tunaposubiri mbele Zako; Karibu na moyo wa Mungu.” Amina.

Hatua Ya Maamuzi: Ni mwitikio gani unaodhani somo hili lingepaswa kutuhimiza kufanya? [1] Msifu Mungu kwa ajili ya Yesu. “Yeye asiyejua dhambi alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye” (2 Wakorintho 5:21). [2] Penda adui zako! Kristo alifanya jambo la ziada pale msalabani: Mbali na kutoa maisha Yake kwa ajili ya rafiki Zake (Yoh. 15:13), aliwapenda maadui Zake. Wapendwa hoja ni hii: Sisi hatukuwa “marafiki” wa Mungu wakati huo, yaani, kabla ya Kalivari. Tulikuwa “maadui” kulingana na Warumi 5:10. Tulikuwa “bila nguvu” (Rum 5:6); “Wasiomcha Mungu” (Rum 5:6); na “wadhambi” (Rum. 5:8). Je, mtazamo wako ni upi dhidi ya wadhambi, waovu, na wale waliopoteza matumaini/au kukosa nguvu wakati huu wa janga la kirusi corona? Je, unawajali, Je unawaombea, Je unawapenda maadui zako? [3] Kristo amefanya kila kitu alichohitaji kufanya (kwa ajili yako) pale msalabani– Sasa ni zamu yako! Wapendwa, mlango u wazi kabisa! Ufikiaji kwa Baba sasa upo kwa kila atakayependa! Je, utajongea karibu sasa? Je, utapiga simu mbinguni? Mungu akubariki unapoufanya maamuzi haya—katika jina lake Yesu, tunaomba, Amina.

Alfajiri Njema: “Bali Mungu aonyesha pendo Lake Yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi. Basi zaidi sana tukiisha kuhesabiwa haki katika damu Yake, tutaokolewa na ghadhabu kwa Yeye.” (Rumi 5:8-9).

Sauti Ya Injili/ Mawazo ya Kiibada / Kumfikia Mungu/ Wazo la # 2.