Unabii wa Danieli

Muhtasari wa Unabii wa Danieli/ 70-001 (Mathayo 24:15–16, 20)/ Unabii wa Biblia wa Siku za Mwisho: Semina ya Unabii wa Danieli.

UTANGULIZI: Unabii wa Danieli na Ufunuo ni sadifu sana kwa ajili ya wakati wa mwisho. Maneno ya Yesu kipindi akiwaaga wanafunzi Wake ni onyo la kujisomea kitabu cha Danieli sisi wenyewe. “Basi hapo mtakapoliona chukizo la uharibifu, lile lililonenwa na nabii Danieli, limesimama katika patakatifu (asomaye na afahamu), ndipo walio katika Uyahudi na wakimbilie milimani…. Ombeni, ili kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi, wala siku ya Sabato.” (Mathayo 24:15–16, 20)

Kitabu hiki hudhihirisha kwa usahihi wa ajabu miaka 2,500 ya historia ya mwanadamu tangu wakati wa Babeli ya zamani. Yesu aliwaonya watu wa wakati Wake kwamba uangamivu wa Yerusalemu ulikuwa umekaribia sana. Aliwaamuru wasome na kuelewa kitabu cha Danieli. Lakini onyo la Yesu katika Mathayo 24:15 pia linahusika kwa ajili ya wakati wa mwisho kwa sababu ni unabii unaotabiri mwisho wa ulimwengu na Marejeo ya Pili.

ALAMA ZA UNABII

Sehemu nyingi za Danieli na Ufunuo zimeandikwa katika lugha ya taswira. Ili kufasiri kisahihi unabii huu, lazima mtu aelewe maana ya kibiblia ya alama. Mara alama zinapokuwa zimeeleweka, unabii huwa na maana (Angalia Somo # 2: Alama za Unabii wa Biblia)     

Kauli tatu za msingi zinazoongoza somo letu katika Semina hii ya Unabii:

 • Alama za unabii katika Danieli na Ufunuo lazima zifasiriwe kwa kutumia Biblia yenyewe. Ufasiri unaobuniwa na mwanadamu hauna uhalali wowote —“Mkijua neno hili kwanza, ya kwamba hakuna unabii katika maandiko upatao kufasiriwa kama apendavyo mtu fulani tu. Maana unabii haukuletwa popote kwa mapenzi ya mwanadamu; bali wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu, wakiongozwa na Roho Mtakatifu.” (2 Petro 1:20–21). Ili kuelewa unabii vilivyo, lazima turuhusu Biblia iuelezee.
 • Utambuzi sahihi wa unabii wa Danieli na Ufunuo utatupatia ufahamu bayana wa Yesu Kristo. Unabii unaweza kueleweka kisahihi tu kadiri unapojikita na kumwinua Yesu Kristo.
 • Danieli na Ufunuo vina mengi ya kusema kuhusu wakati wa mwisho. Hivyo kiini cha somo letu kitakuwa maandalizi yanayohitajika kwa ajili ya wakati wa mwisho.

MSINGI WA KIHISTORIA

Sura ya 1 – 6: (Historia).

Sehemu hii imejengwa na visa halisi vya ustahimilifu na imani ambayo Danieli na marafiki zake walikabili huko utumwani. Ni visa vya kinabii kwa sababu hutupatia masomo ya msingi kwa ajili ya watu wa Mungu katika siku za mwisho katika sura hizi, Danieli na marafiki zake watatu walipitia mitihani ambayo ni mwonjo wa aina ya masuala yatakayowakumbwa watu wa Mungu katika wakati wa mwisho.

Sura ya 2, 7 – 12: (Unabii).

Sura hizi ni za kinabii kwa sehemu kubwa. Hubaini kuinuka na kuanguka kwa falme kuu tangu wakati wa Danieli hadi mwisho wa historia ya mwanadamu. Kila kundi la unabii hutumika kama mrudio na ukuzaji wa dhima na historia ya sehemu iliyotangulia.

DANIELI: MTU ALIYECHAGULIWA KAMA NABII.

Kitabu cha Danieli hakichukuli kama kitabu cha unabii miongoni mwa Wayahudi kwa sababu hakuyatabiri mambo hayo na masaibu yao ajilani. Unabii wake unaonekana kuwa mambo ya mbali sana katika siku za usoni.

Jina la Danieli humaanisha “Mungu ni mhukumu wangu” au “Mungu hunithibitisha.” Hukumu ni istilahi hababi (pendwa) kwa sababu humaanisha siku moja Mungu atahukumu katika ya mema na mabaya na atawaokoa watu Wake kutoka utumwani.

Kisakidifu, kamwe Danieli hakuona njozi zake zikitimia. Aliona tu mpito (mabadiliko) kutoka Babeli hadi Uajemi lakini hilo lilitabiriwa kwa kina zaidi na Yeremia. Na ni bayana alikuwa akitumia ratiba kutoka kwa Yeremia pale alipotegemea kuanguka haraka kwa Babeli katika Danieli 10. Danieli hakupata umashuhuri wake kwa sababu ya karama ya unabii ila kwa sababu ya karama ya kufasiri ndoto.

Unabii wake wote ulisema kuhusu ukaribu ujao kwamba Babeli ingeangushwa na ufalme wa Uajemi. Lakini unabii mwingine ulisema jambo hilohilo kwa kina zaidi. Hivyo hakuchangia chochote kipya katika uelewa wa anguko la Babeli. Mungu alisema kwamba unabii wa Danieli na kazi yake kama nabii mkuu vingetimia katika wakati wa mwisho. “Lakini [Danieli, ambaye sasa alikuwa na umri wa miaka tisini] enenda zako hata utakapokuwa mwisho ule; maana wewe utastarehe, nawe utasimama katika kura yako mwisho wa siku hizo.” (Danieli 12:13, AMP)

DANIELI: UNABII.

Dhima za kitabu cha Danieli zinatambulishwa katika aya chache za kwanza. Ina sehemu tatu muhimu.

 • Patakatifu: Nebukadneza hushambulia mji na Patakatifu.
 • Watu: Nebukadneza huwachukua watu wa Mungu utumwani.
 • Upotofu wa Kipagani: Nebukadneza anatwaa vyombo vitakatifu vya hekalu la Mungu vilivyowakifishwa kwa ibada ya kweli ya Mungu, na huviweka kwenye hekalu la kipagani.

MFUMO WA UTENDAJI WA KISHETANI.

Mashambulizi ya Nebukadneza dhidi ya watu wa Mungu wa kale ni mfumo wa shambulio la kishetani kupitia Mpinga-Kristo katika historia na hata mwisho hasa wa wakati.

Kwa kurudiarudia, Biblia inaonya kwamba utawala uliotokea kama uasi kanisani utajaribu kuchukua nafasi ya Mungu kanisani na kupotosha na kuwatesa watoto halisi wa Mungu, kama tu alivyofanya Nebukadneza. Utawala huu tayari ulikuwa umeanza katika siku za mitume na utatenda kazi hadi mwisho wa wakati.

Mpinga-Kristo:

 • Hutawala Patakatifu au Hekalu la Mungu
 • Huwadanganya watu na kuwaongoza katika kuvunja sheria
 • Huwadangaya watu na kuwaongoza katika kuvunja sheria
 • Huchukua nafasi ya Mungu na kumwondoa Masihi.

Pembe Ndogo, (Danieli 8: 9-12): Utawala wa pembe ndogo hufanya jambo hilohilo alilofanya Nebukadneza.

 • Hushambulia Patakatifu. Aya ya 11. Huangamiza au kuondoa kirakibu samani zote.
 • Huwashambulia watu wa Mungu na Kristo na kuwaondoa kwenye Patakatifu. Aya ya. 10-12.
 • Ukweli wa patakatifu huangushwa chini na upotofu hutawala. Aya ya 12.

Mfalme wa Kaskazini, (Danieli 11: 31-33): Mfalme wa Kaskazini hufanya jambo hilohilo kama pembe ndogo.

 • Hushambulia Patakatifu. Aya ya 31.
 • Huwapeleka watu wa Mungu utumwani. Aya ya 33.
 • Hukomesha huduma ya patakatifu na kuanzisha laubini (mfano-bandia) wake. Aya ya 31.

Babeli Mkuu: Katika siku za mwisho Babeli Mkuu huwashambulia watu na kujaribu kuangamiza patakatifu pa Mungu na kujenga patakatifu pake. Kwa nini Mungu anatumia alama hizohizo na jina hilohilo? Ufalme wa mwisho ulimwenguni utatenda kama mnyama huyu na ni kiashiria muhimu sana katika siku za mwisho. (Ufunuo 13.)

 • Huwashambulia watu wa Mungu na patakatifu (Ufu. 13:6).
 • Huwapeleka watu wa Mungu utumwani na kuwalazimisha kuabudu mungu wa uongo (Ufu. 13:14-17).
 • Huanzisha agano lake bandia na kubadili amri za Mungu (Ufu. 13:4, 6, 8, 14, 17).

MAANA YA KIIBADA: Kupitia mfano wa Danieli na marafiki zake, tunajifunza pia kwamba Mungu atawalinda watu Wake utumwani na jinsi ambavyo watu Wake wanapaswa kuwa jasiri katika wakati wa mwisho. Danieli na rafiki zake walijisalimisha kwa Mungu, nao walibarikiwa kwa kupewa hekima na ufahamu wa njozi na ndoto. Tunapojisalimisha kwa Mungu Yeye hufunua njozi ili tuweze kuelewa kama ambavyo ameahidi.

“Akasema, Enenda zako, Danieli; maana maneno haya yamefungwa, na kutiwa muhuri, hata wakati wa mwisho. Wengi watajitakasa, na kujifanya weupe, na kusafika; bali wabaya watatenda mabaya; wala hataelewa mtu mbaya awaye yote; bali wao walio na hekima ndio watakaoelewa.” (Danieli 12:9–10)

Kadiri tunapofunga, tutarejea kwenye andiko kuu. Maneno ya Yesu kwa wanafunzi Wake wakati akiwaaga hutumika kama onyo katika usomaji wa kitabu cha Danieli:“Basi hapo mtakapoliona chukizo la uharibifu, lile lililonenwa na nabii Danieli, limesimama katika patakatifu (asomaye na afahamu), ndipo walio katika Uyahudi na wakimbilie milimani.(Mathayo 24:15–16)

“Wakati wa ujio wa Kristo, kukirimiwa (kutiwa mafuta) kwa Roho Mtakatifu, mauti Yake, na kuwasilishwa injili kwa Wamataifa, vilioneshwa bayana. Ilikuwa fanaka ya Wayahudi kuelewa mambo haya ya kinabii, na kutambua utimizwaji wao katika utume wa Yesu. Kristo alihimiza kwa wanafunzi Wake umuhimu wa kujifunza unabii. Ilhali akizungumzia unabii upatikanao katika Danieli kuhusiana na wakati wao, alisema, “Asomaye na afahamu.” Mathayo 24:15. Baada ya ufufuo Wake aliwaelezea wanafunzi Wake katika “manabii wote” “mambo yaliyomhusu Yeye Mwenyewe.” Luka 24:27. Mwokozi alikuwa amezungumza kupitia manabii wote. “Roho wa Kristo aliyekuwa ndani yao” “alishuhudia mateso yatakayompata Kristo, na utukufu utakaokuwako baada ya hayo.” 1 Petro 1:11.

Alikuwa Gabrieli, malaika mwenye cheo baada Mwana wa Mungu, aliyekuja na ujumbe wa kiungu kwa Danieli. Alikuwa Gabrieli, “malaika Wake,” ambaye Kristo alimtuma ili amfunulie Yohana mpendwa Wake kuhusu mambo yajayo; na baraka hutamkwa kwa wale wasomao na kusikiza maneno ya unabii huu, na kushika mambo yaliyoandikwa humo. Ufunuo 1:3.

“Hakika Bwana MUNGU hatafanya neno lolote, bila kuwafunulia watumishi Wake manabii siri Yake.” Ilhali “Mambo ya siri ni ya Bwana, Mungu wetu,” “mambo yaliyofunuliwa ni yetu sisi na watoto wetu milele.” Amosi 3:7; Kumbukumbu 29:29. Mungu ametupatia mambo haya, na baraka Yake itaambatana na usomaji wa kicho na maombi wa maandiko ya kinabii.” [Ellen Gould White, The Desire of Ages, Conflict of the Ages Series, (Pacific Press Publishing Association, 1898), 3:234].

Sauti ya Injili/ Mwongozo wa Kujifunza Biblia/ Unabii/ Semina ya Unabii wa Danieli/ Somo # 1.