Kwa Njia ya Yesu Kristo

KNjia za Kumfikia Mungu/200A-001 (Yohana 14:5-6)/ Wazo # 1/ Aya Kuu: “Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya Mimi.” (Yohana 14:6)

Maswali Ya Moyoni: [1] Je, Mungu anapatikana kirahisi? [2] Ni kwa njia gani tunaweza kumfikia? [3] Je kuna matakwa yoyote ambayo lazima tuyatimize ili kuweza kumfikia Mungu wetu?

Moja ya maajabu makuu yaliyofunuliwa katika maandiko ni ukweli kwamba Mungu Mtakatifu na Mwenyezi, anaweza kukaribiwa na watu walio dhaifu na wenye dhambi. Hii ndiyo dhana hasa inayowasilishwa na mafundisho ya upatikanaji wa Mungu. Neno kufikika/ upatikanaji humaanisha “urahisi wa kuingia, au kufika sehemu fulani.” Kwa mfano, ikiwa una ufunguo wa nyumba yako au gari lako unaweza ukaingia ndani kwa urahisi wakati wowote na bila shida yoyote. Unapoupoteza ufunguo huo, kamwe hauwezi kuingia.

Katika Yohana 14:5-31, Yesu anazungumza na wanafunzi Wake. Katika tukio hili Kristo hujibu maswali matatu, yaliyoelekezwa Kwake na wanafunzi watatu – Tomaso, Phillipo, na Yuda.  Leo tunashughulika na swali la Tomaso pekee.  Yesu anasema “Nami niendako mwaijua njia.” Tomaso akamwambia, “Bwana, sisi hatujui uendako; nasi twaijuaje njia?” Yesu akamwambia, “Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya Mimi.” (Yohana 14:4-6)

“Jibu la Yesu linaonesha kwamba mwisho wa safari sio mahali pa kimwili bali mtu (Baba), na kwamba njia ya kufikia mwisho wa safari ni mtu mwingine (Mwana). Yesu ndiye Njia ya kwenda kwa Baba; Yesu ndiye Kweli (au uhalisia) wa ahadi za Mungu; na Yesu ndiye Uzima kwa jinsi anavyotupatia maisha Yake ya kiungu, toka sasa na hata milele. Yesu ndiye njia ambayo inaelekeza kwa kweli na uzima.” [Bruce B. Barton, John, Life Application Bible Commentary, (Wheaton, IL: Tyndale House, 1993), 290].

Hatua Ya Maamuzi: Ni mwitikio gani unaodhani somo hili lingepaswa kutuhimiza kufanya? Mpendwa, mwamini Bwana Yesu Kristo. Mungu alimtuma Mwanawe katika ulimwengu wa dhambi ili kwamba wale wanaoamini wasipotee, bali wawe na uzima wa milele. Yesu Kristo atakufikisha salama mwisho wa safari—Mbinguni. Amina.

Alfajiri Njema: “Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya lile neno nililowaambia. Kaeni ndani yangu, Nami ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa peke yake, lisipokaa ndani ya mzabibu; kadhalika nanyi, msipokaa ndani Yangu.” (Yohana 15:3-4)

Sauti Ya Injili/ Mawazo ya Kiibada / Kumfikia Mungu/ Wazo la # 1.