43-BSG-2 (Yohana 2)

Mwongozo wa Kujifunza Biblia.
Aprili 5, 2018
43-BSG-2 (Yohana 2)

Muhtasari wa Mawazo Makuu
[1] Yesu abadilisha maji kuwa divai kwenye harusi ya Kana, 1-11.
[2] Anaenda Kapernaumu, 12.
[3] Kisha anaenda Yerusalemu, mahali anakowafukuza nje wanunuzi na wauzaji, 13-17.
[4] Anatabiri kifo na ufufuo Wake Mwenyewe kama ushahidi wa mamlaka Yake, 18-22.
[5] Wengi wanamwamini kwa sababu ya miujiza Yake, lakini hawaamini kwa vile “alijua yaliyomo ndani ya mwanadamu,” 23-25.


SEHEMU YA I: MASWALI & MAJIBU

[1] “Na siku ya tatu” (Yohana 2:1). Hii ilikuwa siku gani? Yohana anasimulia matukio ya juma la kwanza la huduma ya Yesu. Hii ni siku mbili baada ya Filipo na Nathanaeli kuitwa (Yohana 1:43–51).

[2] Je, ni mwujiza gani aliotenda Yesu? Kubadilisha maji kuwa divai kwenye karamu ya harusi huko Kana ya Galilaya (Yohana 2:1–11).

[3] Kana iko wapi? Kilikuwa kijiji katikati ya Galilaya, maili tisa kaskazini mwa Nazareti. Kana ulikuwa mji wa makazi ya Nathanaeli kulingana na Yohana 21:2.

[4] Katika aya ya 2 tunasoma: “Yesu naye alikuwa amealikwa arusini pamoja na wanafunzi wake.” (Yohana 2:2). Wakati huu Yesu alikuwa na wanafunzi wangapi? Watano.

“Walikuwepo watano miongoni mwao—Yohana, Andrea, Petro, Filipo, na Nathanaeli (angalia Yohana 1:40–45). Pengine walikuwa marafiki au ndugu wa familia mbili. Vinginevyo walikubali mwaliko wao walipofika Kana kama marafiki wa Yesu. Uwepo wao ulishuhudia ukweli kwamba Yesu alikuwa ameanza kazi Yake kama mwalimu.” (SDA BC 5/ Yohana 2:2)

[5] Wale watumishi walifanya nini kilichoonesha utii na imani yao? (aya ya 7-8)

“Jalizeni mabalasi maji. Nao wakayajaliza hata juu. Akawaambia, Sasa tekeni, mkampelekee mkuu wa meza. Wakapeleka.” (Yohana 2:7–8)

[6] Kuna umuhimu gani wa kutunza divai nzuri hadi mwishoni? (aya ya 10)

“Akamwambia, Kila mtu kwanza huandaa divai iliyo njema; hata watu wakiisha kunywa sana ndipo huleta iliyo dhaifu; wewe umeiweka divai iliyo njema hata sasa.” (Yohana 2:10)

[7] Nini mtazamo wa Yesu juu ya dhambi? (aya ya 14-16)

“Akaona pale hekaluni watu waliokuwa wakiuza ng’ombe na kondoo na njiwa, na wenye kuvunja fedha wameketi. Akafanya kikoto cha kambaa, akawatoa wote katika hekalu, na kondoo na ng’ombe; akamwaga fedha za wenye kuvunja fedha, akazipindua meza zao; akawaambia wale waliokuwa wakiuza njiwa, Yaondoeni haya; msiifanye nyumba ya Baba yangu kuwa nyumba ya biashara.” (Yohana 2:14–16)

[8] Yesu alimaanisha nini waliposema, “Livunjeni hekalu hili, nami katika siku tatu nitalisimamisha”? (aya ya 21) Mauti Yake (angalia ufafanuzi hapa chini)


 

SEHEMU YA II: TAARIFA ZA KUSHANGAZA/UKWELI WA KUAMINI

[1] “Yesu akamwambia, Mama, tuna nini mimi nawe? Saa yangu haijawadia.” (Yohana 2:4)

Mwanamke. “Katika desturi za Mashariki, aina ya mawasiliano ya staha na heshima (sura ya 19:26; linganisha DA 146). Yule alikuwa amewaamuru watu waheshimu wazazi wao (Kut. 20:12; linganisha PP 366) Yeye Mwenyewe alikuwa mfano hai wa kanuni husika. Kwa miaka 30 alikuwa Mwana mwenye upendo, mtiifu, na msikivu (angalia ufafanuzi juu ya Luka 2:51, 52; cf. DA 147).” (SDA BC 5/ Yohana 2:4)

[2] Tuna nini mimi nawe? Kimsingi, “Kitu gani kwako na Kwangu?”

“Maneno haya hudokeza kwamba mtu aliyeambiwa hivyo amevuka mipaka ya kile kinachomhusu hasa (angalia Waamuzi 11:12; 2 Sam. 16:10; 1 Wafalme 17:18; 2 Wafalme 3:13; 2 Nyak. 35:21; Mat. 8:29; Mark 1:24; Luka 8:28; nk.). Kwamba Mariamu hakuelewa jibu la Yesu kama kukataa ni dhahiri kutokana na maelekezo yake kwa watumishi (angalia Yohana 2:5). Mariamu alikuwa ameridhika kwamba Yesu angekidhi mahitaji katika wakati Wake na njia Yake mwafaka. Wakati wote wa maisha Yake ya faragha huko Nazareti, Yesu alikuwa ameheshimu mamlaka ya mama Yake; kwa kweli wakati wote alidumu kuwa Mwana anayefanya wajibu Wake katika mazingira ambapo uhusiano huo uliendelea (angalia Yohana 19:26, 27). Lakini sasa hakuna tena Mtu wa faragha, na Mariamu hakutambua kikamilifu mipaka iliyowekwa katika mamlaka yake juu ya Yesu. Angeweza kujisikia kwamba alikuwa na haki, angalau kwa kiwango fulani, kumwelekeza Yesu katika utume Wake (angalia ufafanuzi wa Mat. 12:46–50). Kwa hiyo, katika maneno haya dhahiri na yenye uungwana Yesu alitafuta kumweleza wazi tofauti katika uhusiano Wake kwa mamaye kakma Mwana wa Adamu na kama Mwana wa Mungu (DA 147). Upendo Wake kwa mamaye haukubadilika, lakini sasa lazima atende kazi siku hadi siku chini ya maelekezo ya Baba wa mbinguni (angalia DA 208; ufafanuzi wa Luka 2:49). (SDA BC 5/ John 2:4)

“Kama ilivyokuwa kwa Mariamu na Yesu, mara nyingi wazazi leo huona ugumu wa kutulia, na hatimaye kuachilia mamlaka kwa watoto wao, ili waweze kupata uzoefu katika kukabiliana na matatizo ya maisha kwa ajili yao wenyewe na kujifunza kukubali wajibu kwa ajili ya maamuzi yao. Ni wenye hekima wazazi na wenye bahati watoto pale mabadilishano haya na mamlaka yanapofanyika vizuri bila ukinzani.” (SDA BC 5/ John 2:4)

[3] “Saa yangu haijawadia.” (Yohana 2:4b)

“Linganisha 7:6, 8, 30; 8:20; nk. Ni dhahiri Mariamu alitumaini kwamba, katika tukio hili, Yesu angejitangaza kuwa Masihi (angalia DA 145), lakini wakati wa tangazo hilo ulikuwa haujawadia (ufafanuzi wa Mark 1:25). Kulikuwa na muda mwafaka ulioteuliwa kwa kila tukio katika maisha Yake (DA 451; ufafanuzi wa Luka 2:49). Ni mpaka mwishoni kabisa wa huduma Yake ndipo Yesu alipojitangaza hadharani kuwa Masihi (ufafanuzi wa Mat. 21:1, 2), na kwa sababu ya dai hili alisulubiwa (Mat. 26:63–65; Luka 23:2; Yohana 19:7; ufafanuzi wa Mat. 27:63–66). Ni hadi usiku wa kusalitiwa ndipo Yesu alisema, “Majira yangu ni karibu” (Mat. 26:18; linganisha 12:23; 13:1; 17:1).” (SDA BC 5/ John 2:4)

[4] “Yesu akawaambia, Jalizeni mabalasi maji. Nao wakayajaliza hata juu.” (Yohana 2:7)

“Yote ambayo nguvu ya mwanadamu ingeweza kutimiza yangepaswa kufanywa kwa mikono ya kibinadamu (angalia uk. 209). Nguvu ya kiungu ilikaribia kudhihirishwa, lakini juhudi makini za kibinadamu zingepaswa kuunganishwa nayo. Kamwe Mungu hawafanyii wanadamu kile ambacho wanaweza kufanya wenyewe, kwa sababu hili lingewafanya wawe wadhaifu wa kiroho. Kama ilivyokuwa kwa Musa (Kut. 4:2), yule majane (2 Wafalme 4:2), na wanafunzi wa Yesu (Mat. 15:34), hatuna budi kutumia kikamilifu rasilimali tulizo nazo mkononi endapo tunatarajia Mungu aongeze baraka Yake.” (SDA BC 5/ John 2:7)

[5] “Mwanzo huo wa ishara Yesu aliufanya huko Kana ya Galilaya, akaudhihirisha utukufu wake, nao wanafunzi wake wakamwamini.” (Yohana 2:11)

Wanafunzi wake wakamwamini. “Muujiza huu uliwapatia wanafunzi wa awali uthibitisho wa kwanza dhahiri juu ya nguvu ya kiungu ikitenda kazi kupitia Kristo, uliwakinga dhidi ya kutoamini na uhasamu wa viongozi wa Kiyahudi, na uliwapatia fursa yao ya kwanza kushuhudia imani yao mpya waliyogundua. Pia, uliheshimu tumaini la Mariamu. Kivitendo, ilielezea moyo wa huruma wa Yesu katika kujihusisha na furaha ya mwanadamu.”

“Hili lilikuwa tukio la Kwanza la Yesu Kutakasa Hekalu, tendo Lake la kwanza la umuhimu wa kitaifa. Kupitia hilo alitangaza haki Yake ya kusimamia masuala ya Hekalu na kutangaza utume Wake kama Masihi.” (SDA BC 5/ John 2:11)

[6] “Akawaambia wale waliokuwa wakiuza njiwa, Yaondoeni haya; msiifanye nyumba ya Baba yangu kuwa nyumba ya biashara.” (Yohana 2:16)

Nyumba ya Baba yangu. “Hekalu lilikuwa makazi ya Mungu miongoni mwa wanadamu (anagalia Kut. 25:8). Tena na tena Wayahudi walimkosoa Yesu kwa kumzungumzia Mungu kama Baba Yake (angalia 5:17, 18; 8:18, 19, 38, 39; 10:30–33). Wao pia walidai kwamba Mungu ni Baba yao (sura ya 8:41), lakini walitambua kwamba Yesu alifanya hivyo akiwa na maana ya juu zaidi. Walitambua kwamba, katika maneno haya, Yesu alitamka madai kamili ya uungu. Katika utakaso wa pili, Yesu alizungumzia Hekalu kama “nyumba yangu” (Mat. 21:13), na pale viongozi walipokataa wito Wake wa mwisho siku iliyofuata aliitaja akisema “nyumba yenu” (Mat. 23:38).” (SDA BC 5/ John 2:16)

Nyumba ya biashara. “Yaani, soko, mahali utendaji wa biashara za kawaida. Wakati wa utakaso wa pili alitumia maneno “pango la wanyang’anyi” (angalia ufafanuzi wa Mat. 21:13). Wale ambao leo hutafuta kwa bidii kuifanya nyumba ya Baba yao iwe “nyumba ya sala” (Mat. 21:13) wataepuka kuifanya mahali pa mawazo, maneno, au matendo ya kawaida. Wataingia kwenye nyumba Yake kwa kicho na ustahivu, wakitambua uwepo Wake mtakatifu, moyo na akili vikiwa vimeinuliwa katika sala na sifa (angalia Yohana 4:23, 24; linganisha Zab. 96:9).” (SDA BC 5/ John 2:16)

[7] “Wanafunzi wake wakakumbuka ya kuwa imeandikwa, Wivu wa nyumba yako utanila.” (Yohana 2:17)

“Yesu alitamani kwa dhati kwamba nyumba ya Baba Yake ingetumiwa kwa kusudi maalum tu ambalo kwalo ilikuwa imewekwa wakfu (angalia ufafanuzi wa Kut. 25:8, 9; Mat. 21:13).” (SDA BC 5/ John 2:17)

[8] “Yesu akajibu, akawaambia, Livunjeni hekalu hili, nami katika siku tatu nitalisimamisha.” (Yohana 2:19)

Livunjeni hekalu hili. Hapa maneno yanayotumiwa kutaja hekalu ni naos, patakatifu halisi (angalia ufafanuzi wa aya ya 14). Katika maneno haya Yesu anadokeza kwa mara ya kwanza hatima iliyokuwa ikimgojea mwishoni mwa safari Yake duniani. Tayari Wayahudi walikuwa wakipanga njama za mauti Yake (angalia DA 164). Wakati wa hukumu Yake, walipotosha kauli hii kuwa dai kwamba alikusudia kulivunja Hekalu, na kulifanya dai hilo kuwa udhuru wa kutimiza unabii wa Kristo (angalia Marko 14:58; angalia ufafanuzi wa Mat. 26:61). (SDA BC 5/ John 2:19)

Mfanano kati ya Hekalu halisi na mwili wa Kristo hauko mbali kama uwezavyo kuonekana mwanzoni. Patakatifu, na baadaye Hekalu, lilikusudiwa kuwa mahali pa makazi ya Mungu duniani (angalia ufafanuzi wa Kut. 25:8, 9). Mahali hapo, juu ya kiti cha rehema, ilionekana Shekina, ishara tukufu ya uwepo wa kudumu wa Mungu (angalia ufafanuzi wa Mwa. 3:24; Kut. 25:17). Lakini, kama ambavyo tayari Yohana alionesha (angalia ufafanuzi wa Yohana 1:14), utukufu huu wa kiungu ulikaa katika mwili wa kibinadamu katika nafsi ya Bwana wetu. Linganisha 1 Kor. 3:16. (SDA BC 5/ John 2:19)

Nitalisimamisha. Yesu alimaanisha ufufuo Wake (angalia ufafanuzi wa sura ya 10:18). Lakini Wayahudi, bila kuelewa kikamilifu umuhimu wa tamko hili, walifikiria jingo la Hekalu halisi. Kwamba hatimaye walitambua maana kamili ya maneno ya Yesu huonekana katika Mat. 27:63, 64. (SDA BC 5/ John 2:19)