Sabato

MASWALI NA MAJIBU KUHUSU SABATO.

A) Je, madai kwamba Wakristo wanaotunza Jumapili wanavunja Sabato, ni kweli?

Tunachohitaji tu kujua ili kufanya uamuzi sahihi wa swali hili, kwamba ama wanavunja Sabato au la, ni kuchunguza mambo kadhaa yafuatayo:

(1) Je, Sabato ya Biblia ni ipi? Au, kwa maneno mengine, ni siku ipi ambayo Biblia inaagiza kuwa ndiyo siku ya pumziko? “Siku ya saba ni Sabato ya Bwana, Mungu wako” (Kutoka 20:10). “Mtafanya kazi siku sita; lakini siku ya saba ni Sabato ya kustarehe kabisa, kusanyiko takatifu; msifanye kazi ya namna yoyote; ni Sabato kwa Bwana katika makao yenu yote.” Walawi 23:23. “Na siku ile [ya kusulubiwa kwa Kristo Yesu] ilikuwa siku ya Maandalio, na Sabato ikaanza kuingia. Na wale wanawake waliokuja Naye toka Galilaya walifuata, wakaliona kaburi, na jinsi mwili Wake ulivyowekwa. Wakarudi, wakafanya tayari manukato na marhamu. Na siku ya Sabato walistarehe kama ilivyoamriwa.” Luka 23:54-56.

JIBU: Sabato ya Biblia ni siku ya saba ya juma. Hujulikana pia kwa kawaida kama Jumamosi (rejea katika Biblia Habari Njema).

 

(2) Sabato ya Biblia au pumziko la siku ya saba ya juma ilikusudiwa iwe kwa Wayahudi peke yao au wanadamu wote? “[Yesu] Akawaambia, Sabato ilifanyika kwa ajili ya mwanadamu” (Marko 2:27). “Basi, imesalia raha ya Sabato kwa watu wa Mungu” (Waebrania 4:9).

JIBU: Sabato ni baraka na fadhila ya Mungu kwa wanadamu wote. Wakati wa Juma la Uumbaji, Sabato ya siku ya saba ilipoasisiwa na Mungu kwa mara ya kwanza na kukabidhiwa kwa Adamu na Hawa, hawakuwepo Wayahudi duniani. Na, kwa kweli, Wayahudi walitokea zaidi miaka 2,000 baadaye!

 

(3) Yesu alivunja Sabato? “Mkizishika amri Zangu, mtakaa katika pendo Langu; kama vile Mimi nilivyozishika amri za Baba Yangu na kukaa katika pendo Lake.” Yohana 15:10.

JIBU: Kamwe Yesu hakuvunja Sabato. Madai hayo ni visingizio vya uongo na njama za hila ambazo Mafarisayo walizua ili wamshutumu (Yohana 5:16, 18; Mathayo 12:1-8). Ni kweli kwamba agizo la Sabato huzuia kufanya kazi. Lakini utekelezaji wa matendo mema ya huruma kwa wagonjwa na wahitaji kamwe haujazuiwa katika siku hii takatifu. Agizo hili halizuii shughuli za ibada na mambo mengine yenye lengo la kuokoa uhai na kurejesha afya ambazo ni lazima zifanywe (Mathayo 12:1-4; Marko 2:23-28). Pumziko linalozungumziwa katika Sabato siyo tu kwamba ni kukoma kufanya kazi, bali hasa kufanya ushirika wa kina pamoja na Mungu. Sheria ya Sabato inakataza kabisa shughuli za kidunia katika siku ya pumziko ya Bwana; kazi zinazoleta kipato ni lazima zikome; hakuna kazi inayolenga kuleta anasa au faida ya kilimwengu iliyo halali katika siku hiyo. Kazi ya Kristo katika kuwaponya wagonjwa ilikuwa inapatana kabisa na sheria hiyo. Iliiheshimu na kuiadhimisha Sabato.

(4) Je, kitendo cha Yesu kuhudhuria katika masinagogi ya Wayahudi ulikuwa “mkakati tu wa injili kwao,” kwa maana kwamba alijitia “chini ya sheria” ili awakomboe Wayahudi hao toka katika sheria ikiwemo Sabato? “[Yesu] Akaenda Nazareti, hapo alipolelewa; na siku ya Sabato akaingia katika sinagogi kama ilivyokuwa desturi Yake, akasimama ili asome” (Luka 4:16).

JIBU: Kwa bahati mbaya, pamoja na Yesu kuhudhuria katika sinagogi “kama ilivyokuwa desturi Yake,” hakuna hata mara moja anapofundisha kwamba Sabato imekoma na kwamba kungeanzishwa “Sabato Mpya” kwa Wakristo! Lakini hata hivyo tunaona wazi Kwake, Mitume Wake na wafuasi Wake wakiendelea kufundisha na kuitunza Sabato ya siku ya saba (Luka 23:56). Yesu alitembea na wanafunzi Wake kufanya kazi pamoja nao na kuwafundisha kwa muda wa miaka mitatu na nusu, lakini hakudokeza hata kidogo juu ya uwezekano wa badiliko hili la siku ya ibada. Hata hivyo, kulikuwa na haja gani ya kufanya mabadiliko hayo toka katika siku hii takatifu ya Bwana? Naye alipozungumza juu ya sheria za Mungu alitamka waziwazi kuwa hakuja kutangua wala kubadili hata nukta moja ya sheria ya Mungu na kuwa kamwe isingeliweza kubadilika (Mathayo 5:17-19).

(5) Sabato ilipaswa kuendelea hadi lini? Je, ingekomea pale Msalabani (kwa maana kwamba ilimlenga Yesu na kuelekeza Kwake) au ingelidumu milele kama sheria zingine tisa za Amri Kumi? Kwa nini Amri ya Nne ya Sabato ya siku ya saba haikuishia msalabani kama ambavyo Wakristo wengine wengependa tuamini? “Kama vile mbingu mpya na nchi mpya, nitakazofanya, zitakavyokaa mbele Zangu, asema Bwana, ndivyo uzao wenu na jina lenu litakavyokaa. Na itakuwa, mwezi mpya hata mwezi mpya, na Sabato hata Sabato, wanadamu wote watakuja kuabudu mbele Zangu, asema Bwana.” Isaya 66:22, 23.

JIBU: Sabato, kama amri zingine, ni agizo ya milele. Haikuishia msalabani. Isingeweza kuishia msalabani kwa sababu haikuwa miongoni mwa mfumo wa sheria za kafara na ibada za patakatifu zilizoanzishwa ili kushughulikia tatizo la dhambi na ambazo zilikuwa zikielekeza katika ujio wa Kristo.

(6) Je, kuna mahali popote katika Agano Jipya (au hata katika Biblia nzima) ambapo Yesu aliagiza kwamba “Sabato Mpya” ya Wakristo ingekuwa Jumapili, badala ya Jumamosi?

JIBU: Hapana! Kuna aya 8 za Biblia katika Agano Jipya zinazozungumzia Jumapili (Mathayo 28:1; Marko 16:1-2; Marko 16:9; Luka 24:1; Yohana 20:1; Yohana 20:19; na 1 Wakorintho 16:2). Hakuna hata moja miongoni mwa aya hizi inayodokeza juu ya badiliko la ibada toka Sabato ya siku ya saba ya juma hadi Jumapili, siku ya kwanza ya juma.

(7) Je, tuna ushahidi wowote kwamba Wakristo wa awali walitunza Jumapili, siku ya kwanza ya juma, kama siku ya ibada? Ibada ya Jumapili hasa ilianza lini, kwa namna gani?

JIBU: Hakuna ushahidi wowote wa Kimaandiko. Yesu Kristo aliitunza Sabato ya siku ya saba (Luka 4:16; Luka 6; Luka 23:53-56, nk). Alitamka kuwa Yeye ndiye “Bwana wa Sabato” (Marko 2:28). Na wakati akiwaonya wanafunzi Wake juu ya uangamivu wa Yerusalemu uliotokea mnamo mwaka 70 BK, yaani miaka 40 baada ya kupaa Kwake kwenda Mbinguni, aliwatahadharisha waombe ili tukio hilo la maangamizi ya Mji wa Yerusalemu lisiwe katika Sabato: “Ombeni, ili kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi, wala siku ya Sabato” (Mathayo 24:20). Hii ina maana gani? Hii hutuambia dhahiri kwamba Yesu Mwenyewe alitegemea kuwa wanafunzi Wake, na kwa kweli, wafuasi Wake wote, wangekuwa wanaendelea kuitunza siku ya Sabato hata baada ya Yeye kuwa amepaa kwenda Mbinguni! Kwa maneno mengine alitambua uendelevu wa utunzaji wa siku ya Sabato. Kama utunzaji wa Sabato haukuwa na maana ama agizo hili lingekuwa limeishia msalabani, kama wanavyodai wengi, kamwe Kristo asingeliwaonya kwa kuwaambia maneno haya.

Na hii ni hoja ya nguvu zaidi hasa tunapozingatia mambo kadhaa: (1) Jambo la kwanza, hakuna mahali popote katika Maandiko tunapoambiwa juu ya badiliko lolote la Sabato. Kama Yesu angelikusudia kuwa Sabato ya siku ya saba ingekoma, angeweza kuwaambia wanafunzi Wake ambao alitembea na kufanya kazi nao na kuwafundisha kwa muda wa miaka mitatu na nusu. Alipozungumzia juu ya sheria za Mungu alitamka waziwazi kuwa hakuja kutangua wala kubadili hata nukta moja ya sheria ya Mungu na kuwa kamwe isingeliweza kubadilika (Mathayo 5:17-19). (2) Pili, katika Agano Jipya wafuasi wa Yesu, yaani Wakristo, wanaoneshwa wakiendelea kuitunza Sabato ya siku ya Sabato; na hata wale waliomzika hawakuwa tayari kuvunja Sabato ili kuundaa mwili Wake. “Na siku ya Sabato walistarehe kama ilivyoamriwa” (Luka 23:56). Walingojea hadi siku ya kwanza ya juma, Sabato ilipokuwa imepita. Halikadhalika, kwa namna ya uwazi pia, Biblia inamwonesha Mtume Paulo wakati wote akiitunza Sabato na kuabudu katika siku ya Sabato (Matendo 13:14, 42, 44; 15:21; 16:13; 17:2; 18:4; 19:8; 24:14; 25:8). (3) Na mwisho, utunzaji huu wa Sabato uliendelea hadi karne ya tatu BK ndipo ibada ya Jumapili ikapenyezwa taratibu kwa hila na werevu chini ya ushawishi wa yule mwovu na mawakala wake. Kabla ya hapo, Wakristo wote wamekuwa wakiabudu katika siku ya saba ya juma.

(8) Je, asili ya Sabato ya siku ya saba ni nini, na asili ya kafara za wanyama ni nini?

“Basi mbingu na nchi zikamalizika, na jeshi lake lote. Na siku ya saba Mungu alimaliza kazi Yake yote aliyoifanya; akastarehe siku ya saba, akaacha kufanya kazi Yake yote aliyoifanya. Mungu akaibarikia siku ya saba, akaitakasa kwa sababu katika siku hiyo Mungu alistarehe, akaacha kufanya kazi Yake yote aliyoiumba na kuifanya.” Mwanzo 2:1-3.

JIBU: Sabato ya siku ya saba ilianzishwa mara katika Juma la Uumbaji. Dhambi haikuwepo, lakini Sabato ilikuwepo tayari. Ikiwa na maana kwamba kama Anguko la Dhambi lisingetokea, hadi sasa wanadamu wote, tangu kwa Adamu na Hawa, tungelikuwa tunaendelea kuitunza Sabato ya siku ya saba. Lakini, kafara za wanyama, kwa upande mwingine, chanzo chake ni dhambi. Mungu alianzisha mfumo wa kafara na dhabihu kama kielelezo cha kumfundishia na kumwongoza mdhambi katika wokovu upatikanao pekee kwa “Mwanakondoo wa Mungu aichukuaye dhambi ya ulimwengu.” Yohana 1:29. Hivyo badi, dhambi isingeingia ulimwenguni, kusingekuwepo haja ya huduma hizi za kafara. Na pia, zilikusudiwa kuishia pale Msalabani.

Hivyo, kwa kuzingatia maswali haya na majibu, tunaweza kuhitimisha kwa usahihi kwamba Wakristo wanaotunza Jumapili wana hatia ya kuvunja Sabato ya Bwana Mungu.


 

B1) Je, wale wanaosali katika siku ya Jumapili huku wakiivunja Sabato wataenda Jehanamu?

JIBU: Hakuna mvunja-sheria ya Mungu yeyote atakayeokolewa katika Ufalme wa Mungu. “Basi yeye ajuaye kutenda mema, wala hayatendi, kwake huyo ni dhambi” (Yakobo 4:17). “Lakini ukitaka kuingia katika uzima, zishike amri.” Mathayo 19:17.

 

B2) Je, wale wanaodai kuitunza Sabato wanaishika kama ilivyoamriwa? Biblia inaagiza Sabato itunzweje?

JIBU: Walawi 23:3 “Mtafanya kazi siku sita; lakini siku ya saba ni Sabato ya kustarehe kabisa, kusanyiko takatifu; msifanye kazi ya namna yoyote; ni Sabato kwa Bwana katika makao yenu yote.”

(1) Kukoma Kufanya Kazi. Sabato ni wakati wa kukoma kabisa kufanya shughuli zote za kidunia; kazi zinazoleta kipato ni lazima ziepukwe. Huu ni wakati wa kujihusisha katika tafakari takatifu ya kiroho. Masuala ya kibiashara pamoja na starehe, anasa na maburudisho binafsi (mathalani michezo, kuangalia soka, nk.) huepukwa kabisa wakati wa saa za Sabato (Isaya 58:13, 14).

(2) Pumziko Takatifu. Sabato ni siku ya kupumzika kimwili, kiakili na kiroho. “Siku ya saba ni Sabato ya kustarehe kabisa, kusanyiko takatifu” (Walawi 23:3). Ni muda wa ibada ya pekee kwa Mungu. Ni muda bora hasa wa kufanya ushirika wa kina pamoja na Mungu.

(3) Matendo Mema. Ni halali kutenda mema siku ya Sabato, kuokoa roho. “Ni mtu yupi miongoni mwenu mwenye kondoo mmoja, na yule kondoo ametumbukia shimoni siku ya sabato, asiyemshika akamwopoa?” (Mathayo 12:11). Sabato haikukusudiwa kuwa wakati wa kukaa tu bila kufanya kazi yoyote. Sheria ya Sabato hupiga marufuku utendaji wa shughuli za kidunia, za kujipatia mapato. Kama vile ambavyo Mungu aliacha kufanya kazi Yake ya uumbaji na akapumzika katika siku ya Sabato na kuibariki, vivyo hivyo mwanadamu anapaswa kuacha shughuli zake za kila siku za kazi ya kimaisha, na kutenga saa hizo takatifu kwa ajili ya pumziko bora, ibada na kujihusisha katika matendo mema na matakatifu.


 

C) Je, kwa sababu Agano Jipya hukamilisha Agano la Kale, hii humaanisha kwamba mafundisho yake nayo yamebatilika? “Maandiko hayawezi kutanguka [kubatilishwa]” (Yohana 10:35). “[Yesu] Akaanza kutoka Musa na manabii wote, akawaeleza katika Maandiko yote mambo yaliyomhusu Yeye Mwenyewe.” Luka 24:27. Maandiko yanamshuhudia Yesu (Yohana 5:39).

JIBU: Hali ya Agano la Kale kukamilishwa na Agano Jipya kamwe haifanyi Agano la Kale libatilishwe, badala yake huthibitisha kama sehemu ya msingi yenye mamlaka ya kujenga imani na mafundisho ya wokovu. Tangu Edeni ndoa imekuwa ni agano takatifu la kudumu kati ya mke mmoja na mme mmoja, na ndivyo inavyothibitishwa katika Agano Jipya (Mathayo 19:1-9). Halikadhalika fundisho la haki kwa imani katika Kristo (Mwanzo 3:15), nk.


 

D) Yesu aliposema, “Njoni Kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, Nami nitawapumzisha” (Mathayo 11:28), alimaanisha kwamba utunzaji wa Sabato ya siku ya saba ungepaswa kukoma? “Kama ukigeuza mguu wako usihalifu Sabato, usifanye anasa yako siku ya utakatifu Wangu; ukiita Sabato siku ya furaha, na siku takatifu ya Bwana yenye heshima; ukiitukuza, kwa kutokuzifanya njia zako mwenyewe, wala kuyatafuta yakupendezayo, wala kusema maneno yako mwenyewe; ndipo utakapojifurahisha katika Bwana; Nami nitakupandisha mahali pa nchi palipoinuka; nitakulisha urithi wa Yakobo baba yako; kwa maana kinywa cha Bwana kimenena hayo.” Isaya 58:13, 14.

JIBU: Kwa maneno ya Mathayo 11:28, Yesu alikuwa hatangazi kwamba utunzaji wa Sabato ya siku ya saba ungekoma, kwa sababu ishara ya kwamba Mkristo amepumzika katika Kristo ni utunzaji wa kweli wa Sabato takatifu ya Bwana. Hatuwezi kudai kwamba tumepumzika katika Kristo, kwamba tumetua mizigo yetu, wakati huohuo hatupatia fursa, furaha, fadhila, na baraka ya kufanya ushirika na Mungu katika siku Yake aliyoiagiza.


 

E) Je, ni kweli kwamba Yesu alipotoa sheria za afya na vyakula (mathalani katika Walawi 11 na Kumbukumbu 14), alikusudia kwamba baadaye angetumia kielelezo hiki ili kuleta fundisho la kina zaidi la utakatifu? “Kwa kuwa Mimi ni Bwana, Mungu wenu; takaseni nafsi zenu basi; iweni watakatifu, kwa kuwa Mimi ni Mtakatifu; wala msitie uchafu nafsi zenu kwa kitu kitambaacho cha aina yoyote, kiendacho juu ya nchi.” Walawi 11:44. “Nena na mkutano wote wa wana wa Israeli, uwaambie, Mtakuwa watakatifu; kwa kuwa Mimi Bwana, Mungu wenu, ni mtakatifu” (Walawi 19:2). Pia Walawi 11:45; 20:26, nk.

JIBU: Kwa namna ya wazi kabisa, kitabu cha Walawi (na kwingineko katika AK) hufundisha kwa kurudiarudia juu ya utakatifu na usafi wa nafsi na mwili. “Takaseni nafsi zenu basi; iweni watakatifu,” “wala msitie uchafu nafsi zenu…” Dhana kwamba usafi wa Agano la Kale ulikusudiwa na Mungu kuwafundishia watu Wake wa Agano Jipya juu ya utakatifu wa roho, pamoja na kwamba ni nadharia ya kubuni isiyoungwa mkono katika Maandiko, ni upotoshaji dhahiri wa fundisho muhimu la Neno la Mungu.


 

F) Je, Yesu aliposema, “Hakuna kitu kilicho nje ya mtu ambacho kikimwingia chaweza kumtia unajisi, bali vile vimtokavyo, ndivyo vimtiavyo unajisi yule mtu” (Marko 7:15), alikuwa anabatilisha kanuni ya vyakula katika Agano la Kale na hivyo kuhalalisha ulaji wa kila kitu?

JIBU: Biblia haifundishi kwamba Yesu alihalalisha ulaji wa mnyama yoyote au kila kitu! Katika Marko 7:15-23, Yesu hatamki kwamba mtu anaweza kula kitu chochote apendacho. Baadhi ya vitu ambavyo wengi huviita vyakula na vinywaji havistahili kabisa kwa matumizi ya wanadamu na pia vinafisha, na vingine ni hatari kabisa kwa afya. Angalia katika Walawi 11:2-23 na Kumbukumbu 14 kwa ajili ya orodha ya wanyama, ndege, samaki, na wadudu wasiofaa kuliwa.

Anachoelekeza Yesu hapa ni kukanusha imani iliyokuwa imeenea kuwa endapo Myahudi mtauwa (mcha-Mungu kwelikweli) angefuata tu sheria za usafi na taratibu za kidini angekuwa safi kimaadili/kiroho. Kwa upande mwingine, hakuna chakula ambacho kwa chenyewe kinaweza kuinajisi tabia ya mtu. Kinachonajisi ni mawazo maovu (ambayo hujitokeza kwa ndani na kujidhihirisha katika matendo ya nje). Ndiyo maana Biblia inatuambia, “Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo; Maana ndiko zitokako chemchemi za uzima.” Mithali 4:23

Tunapaswa kuwa makini hapa kwa sababu Yesu hasemi kuwa vitu vyote vinaruhusiwa au vinafaa kuliwa. Hapa Yesu hazungumzii wanyama najisi na safi. Mada yake ni juu ya chanzo cha unajisi wa kimaadili/kiroho. Yesu anatumia kielelezo cha vitendo vya nje kama kuosha mikono na kula ili kuweza kutofautisha na hali ya moyoni. Yesu hugeuza mtazamo wa walimu wa sheria: walikuwa wamejikita katika mambo ya nje, wakati Yesu alisisitiza matendo ya ndani ya roho, hali ya kimaadili/kiroho. Kwa wengi, ni rahisi kudumisha hali ya nje ya kuwa Mkristo kwa kile tunachofanya au tusichofanya. Hata hivyo, wakati ambapo wanadamu huangalia nje, Mungu huangalia hadi ndani ya moyo—hupima nia na makusudi yanayosukuma matendo yetu. (Rejea Mwanzo 1:29-30; Matendo 10; 1 Wakorintho 10:31; Mathayo 5 :28, 29).


 

G) Mtume Paulo anaposema kwamba kitendo cha kutahiriwa hakina manufaa yoyote ya wokovu kwa Wakristo wa Agano Jipya baada ya Yesu kuja (Wagalatia 6:15), anasema nini badala yake? “Kutahiriwa si kitu, na kutokutahiriwa si kitu bali kuzihifadhi amri za Mungu” (1 Wakorintho 7:19). “Basi, je! Twaibatilisha sheria kwa imani hiyo? Hasha! Kinyume cha hayo twaithibitisha sheria.” Warumi 3:31.

JIBU: Hata Mtume Paulo katika nyaraka zake, anaonesha wazi kwamba kuna tofauti ya msingi kabisa kati ya sheria za maagizo ambazo zimeishia msalabani (kama vile tohara, nk), na Amri za Mungu, ambazo ni sheria za milele.


 

H) Biblia inaposema, “Basi, mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au sabato; mambo hayo ni kivuli cha mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo” (Wakolosai 2:16, 17), humaanisha nini?

JIBU: Katika Wakolosai 2:16, 17, Mtume Paulo anazungumzia sikukuu na sheria za kafara ambazo zilikomea Msalabani. Kristo alipoangikwa msalabani sharti letu la kutimiza maagizo haya liliondolewa. Mathalani sadaka ya vyakula na vinywaji vilikuwa vikiwasilishwa na Waisraeli hekaluni kwa mujibu wa mfumo wa taratibu za kidini. Kafara za wanyama zilizotolewa katika sherehe au sikukuu mbalimbali, kwenye miandamo ya mwezi, katika Sabato za kila juma, na Sabato za kawaida za kidini zilikuwa ni “vivuli” vilivyokuwa vikielekeza katika wakati ujao kwa dhabihu ile kuu ya Kristo (Wakolosai 2:16-17). Sikukuu mbalimbali: —Pasaka ya Wayahudi, Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, Pentekoste, Siku ya Upatanisho, nk. (Walawi 23:26-32; Hesabu 29:7-11). Miandamo ya Mwezi: siku ya kwanza ya kila mwezi (Hesabu 10:10; 28:11; linganisha 1 Samweli 20:5; Isaya 66:23).

Sabato ya kila juma, Sabato ya siku ya saba, chimbuko lake ni katika tukio la Uumbaji (Mwanzo 2:1-3; Kutoka 20:8-11). Sabato ni kumbukumbu ya mwanzo wa historia ya dunia. Mtume Paulo hazungumzii kukoma kwa wajibu wa kutunza Sabato ya siku ya saba ya Amri ya Nne, bali anazungumzia kukoma kwa siku za mapumziko za mfumo wa kidini zilizotimizwa katika Kristo (Walawi 23:6-8, 15, 16, 21, 24, 25, 27, 28, 37, 38). Sabato ya siku ya saba ni Sheria ya Mungu ya Maadili isiyokuwa na mwisho. Ikiwa kama “Siku ya Kuzaliwa” kwa Sayari Dunia, huthibitisha Utawala wa Muumba (Kutoka 20:8-11; 31:12-17). Pumziko hili lilianzishwa kabla mwanadamu hajatenda dhambi na muda mrefu kabisa kabla taifa la Israeli halijatokea. Kwa hiyo, ni kwa ajili ya wanadamu wote (Marko 2:27) na kamwe isingeliweza kuwa “kivuli cha mambo yajayo” (Wakolosai 2:17).

Kilichoishia Msalabani ni maagizo ya kafara za wanyama, sheria za ukuhani, sikukuu zingine nyingi (Wakolosai 2:14-17; rejea pia Walawi 23:6-8, 15-16, 21, 24-25, 27-28, 37-38; 293:26-32; Hesabu 29:7-11), nk). Hizi ni tofauti kabisa na Amri 10, ambazo ni sheria za milele. Sheria hizi ziliandikwa na Musa kwenye kitabu na kuwekwa KANDO ya Sanduku la Agano (Kumbukumbu la Torati 31:26); wakati Amri Kumi ziliandikwa kwa “chanda cha Mungu mwenyewe” katika Mbao 2 za Mawe na kuwekwa NDANI ya Sanduku la Agano (Kutoka 31:18; 40:3, 20, 21).

Yesu hakuwa na haja ya kufanyia uboreshaji au kuibatilisha Sabato ya siku ya saba kwa sababu haikuanzishwa kama sehemu ya kushughulikia mpango wa moja kwa moja wa ukombozi wa mwanadamu baada ya kuanguka dhambini. Kwa maneno mengine, Sabato, amri ya ibada ya siku ya saba, haikuja baada ya dhambi, bali badala yake, ilikuwepo hata kabla ya dhambi. Sikukuu na sherehe mbalimbali, miandamo ya mwezi pamoja na zile pumziko za sabato zilizoagizwa baada ya dhambi kuingia, kama sehemu ya mpango wa ukombozi wa kushughulikia tatizo la dhambi, zimebainishwa wazi katika Maandiko na kutofautishwa na Sabato ya siku ya saba, na hizi, Biblia inasema, zilikuwa ni “kivuli cha mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo.” Wakolosai 2:17. Kwa maneno mengine, zilitimizwa na kubatilishwa katika mauti ya Yesu Kristo pale msalabani. Yesu aliposema “Imekwisha,” maagizo haya yalipaswa kukoma kuadhimishwa. Ndiyo maana hatushangai kumwona Mtume Paulo katika nyaraka zake mbalimbali akiwaelekeza na kuwaonya Wayahudi, ambao kimsingi hawakuamini juu ya kafara ya Kristo, wasiendelee tena katika utoaji wa kafara na huduma za hekaluni kwa kuwa ni wakati sasa wa kutazama kwa “Mwanakondoo wa Mungu aichukuaye dhambi ya ulimwengu,” katika lile Hekalu au patakatifu pa Mbunguni pasipotengenezwa kwa mikono ya mwanadamu, bali Mungu Mwenyewe.

Hitimisho: Kitendo cha sabato kuwekwa katika kundi moja na sikukuu, mwandamo wa mwezi au vyakula au vinywaji, hutusaidia kutambua ni sheria ipi anayozungumzia Mtume Paulo hapa. Ni wazi kwamba anazungumzia kundi la sheria za kafara na taratibu za ibada ambazo zilielekeza kwa Kristo na zingepaswa kukoma wakati wa ujio Wake. “Mambo hayo,” anasema Paulo, “ni kivuli cha mambo yajayo”—yaani yalilenga kwa Kristo ambaye angekuja baadaye.


 

I) Je, ni kweli kwamba, “Baada ya kanisa kuzaliwa siku ya Pentekoste, Wakristo wote, wakiwemo mitume, walianza ibada zao siku ya kwanza ya juma (mnamo 35 AD), ambayo ndiyo Jumapili kwa kalenda yetu ya Kiarabu”?

JIBU: Hapana! Hakuna ushahidi wowote wa Biblia badiliko la siku ya ibada toka siku ya Sabato kwenda Jumapili, siku ya kwanza ya juma. Badala yake, historia inaonesha wazi kwamba uadhimishaji wa Jumapili kama siku ya ibada ulianzia baadaye mnamo karne ya tatu BK., na kwamba uliingizwa kwa mamlaka ya kibinadamu kama ilivyotabiriwa katika Danieli 7:25. “Siku sasa imebadilika kutoka katika siku ya saba na kuwa siku ya kwanza ya juma. Lakini hatukutani na Maandiko yanayoruhusu mabadiliko hayo, basi tunaweza kusema kuwa yalifanywa na nguvu za Kanisa.”—Explanation of Catechism, (Protestant Episcopal).


 

J) Je, Mfalme Konstantino anahusianaje na uanzishwaji wa ibada ya Jumapili?

JIBU: “Mtawala Kostantino (aliyekufa mwaka 337 BK), mwongofu wa Ukristo, kwa mara ya kwanza alihalalisha kisheria Jumapili katika mwaka 321 BK, alipotangaza kwamba kazi zote zisimamishwe Jumapili, isipokuwa wakulima wangeweza kufanya kazi inapolazimu.”—Encyclopædia Britannica, 2008.

Baada ya Jumapili kufanywa na serikali kuwa siku ya mapumziko kisheria, kanisa Katoliki likafuatia kuifanya siku hiyohiyo kuwa siku ya ibada. Askofu wa kanisa la Kirumi anashuhudia akisema, “Unaweza kusoma Biblia tokea Mwanzo mpaka Ufunuo, na hutapata hata mstari mmoja unaotakasa Jumapili kuwa siku ya ibada. Maandiko yameshuhudia utakaso wa Jumamosi, siku ambayo hatuiadhimishi.”—Cardinal Gobbons, in The Faith of Our Father, edition 1892, uk., 111.

Nukuu nyingine ya Kanisa Katoliki inasema, “Jumapili ni amri ya Katoliki, na kuadhimishwa kwa siku hii kunatokana na amri za Kikatoliki…. Toka mwanzo wa Maandiko mpaka mwisho hakuna mstari wowote unaokubali mabadiliko ya ibada ya siku ya Sabato na kuifanya kuwa siku ya kwanza ya juma.”—Catholica Press (Sydney, Australia) Aug. 25, 1900.


 

K) Je, kuna uthibitisho wowote katika Agano Jipya wa uendelevu wa utunzaji wa Jumamosi, siku ya saba ya juma, kama siku ya ibada?

JIBU: “Karne ya Wakristo wa awali ilipita na hapakuwa na uadhimishaji wa Jumapili na Wakristo hawa, bali Sabato ndiyo iliyotunzwa.”—Sir William Domville, in Examination of Six Texts, sura 8, uk. 291. “Hii haikuwa desturi ya kanisa la Kristo la awali, lakini jambo hili liliendelea polepole kwa njia ya kutojua, siku ile ikabadilishwa.”—Archdeacon Farrar, katika The Voice from Sinai, uk. 167.


 

L) Kuhesabiwa haki kwa neema kwa njia ya imani katika Kristo (Waefeso 2:8; Warumi 5:1) humaanisha kwamba hatupaswi tena kutii sheria? “Tuseme nini basi? Tudumu katika dhambi ili neema izidi kuwa nyingi? Hasha! Sisi tulioifia dhambi tutaishije tena katika dhambi?” (Warumi 6:1, 2). Dhambi ni uasi wa sheria (1 Yohana 3:4). “Katika hili twajua kwamba twawapenda watoto wa Mungu, tumpendapo Mungu, na kuzishika amri Zake. Kwa maana huku ndiko kumpenda Mungu, kwamba tuzishike amri Zake; wala amri Zake si nzito.” 1 Yohana 5:2, 3.

JIBU: Mtume Paulo anadai kwamba uwepo wa neema ya Mungu haumfanyi mwumini kuendelea kutenda dhambi (yaani kuasi sheria za Mungu). Ikiwa na maana kwamba utii wa sheria ni suala la lazima kwa mtu yeyote anayedai kumwamini Kristo. “Mkizishika amri Zangu, mtakaa katika pendo Langu; kama vile Mimi nilivyozishika amri za Baba Yangu na kukaa katika pendo Lake.” Yohana 15:10.


 

M) Je, kitendo cha kusisitiza sana Amri ya Sabato humaanisha kwamba ni bora kuliko amri zingine? “Piga kelele, usiache, Paza sauti yako kama tarumbeta; Uwahubiri watu Wangu kosa lao, Na nyumba ya Yakobo dhambi zao.” Isaya 58:1. “Wala msishirikiane na matendo yasiyozaa ya giza, bali myakemee” (Waefeso 5:11).

JIBU: Kwa mfano, mzazi fulani ana mtoto anayesoma. Mwanaye huyu anafahamu sana Hisabati na masomo mengine. Lakini ana tatizo kubwa la somo la Kiingereza. Ni rahisi kuona jinsi gani mzazi huyu atakavyomkazania na kumsisitizia mwanawe katika eneo lile lenye mapungufu kwake—somo la Kiingereza! Ikitokea umeenda hospitalini na ukadungulika kwamba una ugonjwa wa Malaria, daktari atakuwa kichaa na mwenye wazimu endapo atakupatia dozi ya siku arobaini ya ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB), usiokuwa nao.


 

N) Je, kwa nini katika Amri ya Sabato, kama inavyofundishwa katika Agano Jipya, mkosaji hapaswi kupigwa hadi kufa kama ilivyokuwa ikifanyika katika Agano la Kale (Kutoka 31:14; 31:15; 35:12 na Hesabu 15:32)? Huu si ushahidi kwamba Sabato ni fundisho la kale ambalo Wakristo hawahusiki nalo?

JIBU: Kitendo cha kubadilika kwa namna na aina ya utekelezaji wa adhabu ya wakosaji wa Sabato (au wa amri yoyote ile miongoni mwa Amri za Mungu), haina maana kwamba amri husika imekoma au kubatilishwa. Wahalifu waliotenda makosa ya kufanya ibada ya sanamu, uuaji, zinaa na uvunjaji mwingine wa Amri za Mungu walipigwa kwa mawe hadi kufa. Kwa mfano, Akani na familia yake (Yoshua 7), kwa sababu ya wizi wa nyara za vitani, alipigwa mawe hadi kufa yeye na familia yake. Je, kutotekelezwa kwa adhabu hizi kama ilivyofanyika katika kipindi cha Agano la Kale humaanisha kwamba amri husika imefutwa au imebatilishwa? Hapana! Sheria inayokataza kuua, zinaa, wizi, ibada ya sanamu na kadhalika bado inaendelea hadi leo ijapokuwa namna ya utekelezaji wa adhabu kwa wakosaji umebadilika. Halikadhalika Sabato. Amri hii haijabatilika kwa vile tu jinsi adhabu inavyotekelezwa ni tofauti na vile ilivyofanyika zamani. Kwa kweli hili ni tendo la rehema kwa upande wa Mungu, lakini mdhambi yeyote asiyetubu lazima atakabiliana na Hukumu Kuu ya mwisho ya Mungu. “Kwa sababu hukumu juu ya tendo baya haitekelezwi upesi, mioyo ya wanadamu huthibitishwa ndani yao ili kutenda mabaya. Ajapokuwa mwenye dhambi amefanya maovu mara mia, akazidisha siku zake; lakini hata hivyo najua hakika ya kwamba itakuwa heri kwao wamchao Mungu, wenye kicho mbele Zake; walakini haitakuwa heri kwa mwovu, wala hatazidisha siku zake, zilizo kama kivuli; kwa sababu hana kicho mbele za Mungu.” Mhubiri 8:11-13.


 

O) Kwa nini wanaotunza leo Sabato hawatoi “sadaka ya kondoo wawili, sadaka ya kinywaji na nafaka” (Hesabu 28:9)?

JIBU: Kwa sababu sabato hizi na sikukuu husika zilizoambatana na dhabihu na matoleo haya vilikuwa vielelezo vya mfumo wa sheria za kafara na taratibu za patakatifu, ambavyo vilielekeza kwa Kristo, vyote hivi vilikuwa kivuli cha mambo yajayo—vilikoma pale Yesu alipokuja.


 

P) “Wakati wa Sabato haikutakiwa kutoka nyumbani (Kutoka 16:29). Mbona wa leo wanatoka?” “Angalieni, kwa kuwa Bwana amewapa ninyi hiyo Sabato, kwa sababu hii huwapa siku ya sita chakula cha siku mbili; kaeni kila mtu mahali pake, mtu awaye yote asiondoke mahali pake kwa siku ya saba.” Kutoka 16:29.

JIBU: Agizo hili linatolewa wakati wana wa Israeli wakiwa jangwani, kabla hawajajenga mahali pamoja pa kukutanikia kwa ajili ya ibada. Walikuwa kambini jangwani, hawakuwa na makazi ya kudumu pamoja na hekalu la kuabudia. Hii ililazimu ibada yao kufanyika majumbani. Hakukuwa na sababu ya mtu kusafiri katika siku ya Sabato kwenda mahali fulani pa kuabudia. Amri ya nne inayoagiza utunzaji wa Sabato haikatazi kuondoka nyumbani, bali huzuia kazi yoyote ile ya kawaida, ya kipato na shughuli isiyopatana na moyo wa ibada (Kutoka 20:8-11; Walawi 23:3). Ndiyo maana tunamwona Bwana Yesu, aliyeitunza Sabato kikamilifu, akiwa pamoja na wanafunzi Wake katika shamba la masuke siku ya Sabato (Luka 6:1-5).


 

Q) Je, hivi ni sahihi kudai kwamba mtu mwenye Yesu moyoni hana haja tena ya kuitunza Sabato?

JIBU: Si sahihi hata kidogo. Hii ni sawa na kusema, ukiwa na Yesu moyoni, ukimwamini, basi huna haja ya kufanya lolote. Ni kana kwamba maagizo yote ya Mungu hujitimiza yenyewe bila utendaji au uhusikaji wowote kwa upande wetu. Kama ingalikuwa ndivyo, kwa nini basi Yesu akaagiza akisema, “Mkinipenda, mtazishika amri Zangu” (Yohana 14:15)? Hivi hata unajuaje kwamba Yesu yumo moyoni ikiwa hufuati anachosema? Kinachoonesha kwamba sisi ni watu wa Mungu, kwamba sisi ni wafuasi wa Kristo pale tu tunapofuata mapenzi Yake. Mapenzi ya Mungu ni mafundisho Yake na Amri Zake. “Kuyafanya mapenzi Yako, Ee Mungu wangu, ndiyo furaha yangu; Naam, sheria Yako imo moyoni mwangu.” Zaburi 40:8. Paulo ameandika, “Maana, upendo wa Kristo watubidisha” (2 Wakorintho 5:14). Ili kufanya nini? Kuyatenda mapenzi Yake, kuitekeleza sheria Yake! Imani katika Kristo hutupatia haki ya kuitwa wana na binti za Mungu ambao tunaishi sasa kwa kufuata kanuni takatifu za Ufalme wa Mbinguni—Sheria Yake.

“Kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui juu ya Mungu, kwa maana haitii sheria ya Mungu, wala haiwezi kuitii…. Lakini ikiwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili; bali mwaifuata roho. Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo, huyo si Wake.” Warumi 8:7-9. Ni wazi hapa kwamba wale wanaoongozwa na Roho wa Kristo huitii sheria ya Mungu.

Kifupi, haiwezekani kabisa kudai kwamba mtu awe Yesu moyoni wakati huohuo anahalifu sheria za Mungu. Yesu Mwenyewe ameonya: “Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba Yangu aliye mbinguni.” Mathayo 7:21. “Nao waniabudu bure, Wakifundisha mafundisho Yaliyo maagizo ya wanadamu” (Mathayo 15:9). “Ninyi mwaiacha amri ya Mungu, na kuyashika mapokeo ya wanadamu” (Marko 7:8).


 

R) Ni maana ya “kumwabudu Mungu katika Roho na kweli” (Yohana 4:24)?

JIBU: Kumwabudu Mungu katika roho kunahusisha mwenendo wa akili na makusudio ya moyoni—utu wa ndani. “Na Kristo akiwa ndani yenu, mwili wenu umekufa kwa sababu ya dhambi; bali roho yenu i hai, kwa sababu ya haki” (Warumi 8:10). Kwa upande mwingine, kweli ni ufunuo wa mapenzi na tabia ya Mungu kupitia Neno Lake (Yohana 1:17; 3:34) na matendo ya Yesu (Yohana 8:32, 36); na pia katika huduma endelevu ya Roho Mtakatifu (Yohana 16:13). Haiwezekani kudai kwamba mtu fulani anamwabudu Mungu “katika roho na kweli” huku ukipuuzia waziwazi, kwa makusudi, ufunuo wa mapenzi Yake katika Neno Lake.