Siku ya Sabato ni Ipi?

BIBLIA: “Soma, Elewa, Shuhudia”

MASWALI NA MAJIBU
Mfululizo: Ikumbuke Siku ya Sabato
92S-001: Siku ya Sabato ni Ipi?

OMBI: Baba yetu mpendwa tunakushukuru tena kwa nafasi ya uhai siku hii ya leo. Tunaalika Roho Wako atufundishe katika tafakari hii ya kipindi cha Maswali na Majibu katika Biblia. Utusamehe Bwana, ukatutakase na kutuandaa kwa ajili ya ufalme Wako. Ni ombi letu katika jina la Yesu Kristo- Bwana wetu, Amina.


 

JE, SIKU YA SABATO NI IPI?

Sabato ni lini? Jumamosi, Jumapili au Ijumaa??

Je, ulishawahi kujiuliza kwa nini kuna madhehebu mengi hali Mungu ni mmoja ? Je, ni mpango wa Mungu watu wake wamwabudu kwa namna tofauti ? Kwa nini kuna mivutano ya siku za Ibada ?

 

[1] Je, Mungu aliwaagiza watu waitunze Sabato ?

Jibu : Ndiyo ! Ushahidi wa Biblia.

Mwanzo 2:2-3
“Na siku ya saba Mungu alimaliza kazi yake yote aliyoifanya; akastarehe siku ya saba, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoifanya. Mungu akaibarikia siku ya saba, akaitakasa kwa sababu katika siku hiyo Mungu alistarehe, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoiumba na kuifanya”.

 

[2] Je, Adamu na Ibrahimu waliitunza Sabato?

Jibu : Ndiyo ! Ushahidi wa Biblia
(2a) Mwanzo 2:2-3. Adamu aliitunza Sabato

(2b) Ibrahimu alitunza Amri za Mungu ikiwemo na Sabato(Amri ya Nne). “Kwa sababu Ibrahimu alisikia sauti yangu, akayahifadhi maagizo yangu, na amri zangu, na hukumu zangu, na sheria zangu.” Mwanzo 26:5

 

[3] Je, kuna Amri yoyote inayotuamuru tuitunze Sabato?

Jibu : Ndiyo ! Ushahidi wa Biblia.

Kutoka 20:8-11
“Ikumbuke siku ya Sabato uitakase. Siku sita fanya kazi, utende mambo yako yote; lakini siku ya saba ni Sabato ya Bwana, Mungu wako, siku hiyo usifanye kazi yo yote, wewe, wala mwana wako, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala mjakazi wako, wala mnyama wako wa kufuga, wala mgeni aliye ndani ya malango yako. Maana, kwa siku sita Bwana alifanya mbingu, na nchi, na bahari, na vyote vilivyomo, akastarehe siku ya saba; kwa hiyo Bwana akaibarikia siku ya Sabato akaitakasa.” (linganisha na Mwanzo 2:2-3)

 

[4] Siku ya Sabato ni ipi katika siku saba za Juma?

Jibu: Jumamosi! Ushahidi wa Biblia.

Angalizo: Ndani ya Biblia hakuna majina ya siku ya Jumapili, Jumatatu, Jumanne, n.k. isipokuwa katika Biblia ya Kiswahili cha Kisasa. Ndani ya Biblia Mungu aliziita siku ya kwanza, pili, tatu, n.k (Mwanzo 1…). Kibiblia Yesu alifufuka siku ya Kwanza ya Juma, yaani Jumapili. Fanya hesabu rahisi! Siku ya Saba itakuwa ni lini? Daima ni Jumamosi.

 

[5] Ni nini hasa chimbuko la Majina haya ya siku katika wiku? Je, yalikuwa na maana gani?

Sunday , siku ya Jua, siku ya mungu mume wa Roma ya kale ya kipagani.
Monday, siku ya mwezi, mungu mke wa Roma ya kale ya kipagani.
Tuesday, siku ya mungu tuis wa Roma ya kale ya kipagani.
Wednesday, siku ya mungu wenes wa Roma ya kale ya kipagani.
Thursday, siku ya mungu thrus wa Roma ya kale ya kipagani.
Friday, siku ya mungu frigus wa Roma ya kale ya kipagani.
Saturday, siku ya mungu satun wa Roma ya kale ya kipagani.

 

[6] Je, ufufuko wa Yesu uliathiri utaratibu wa siku saba katika wiki?

Jibu: Hapana.

Uthibitisho wa kibiblia unaonesha kuwa, siku ya Sabato ni Jumamosi kama leo inavyojulikana.

Zingatia aya zifuatazo:

Mathayo 28:1
“Hata sabato ilipokwisha, ikipambazuka siku ya kwanza ya juma, Mariamu Magdalene, na Mariamu yule wa pili, walikwenda kulitazama kaburi.”

Marko 16:2
“Hata alfajiri mapema, siku ya kwanza ya juma, wakaenda kaburini, jua lilipoanza kuchomoza”

Marko 16:9
“Naye alipofufuka alfajiri siku ya kwanza ya juma, alimtokea kwanza Mariamu Magdalene, ambaye kwamba alimtoa pepo saba.”

Luka 24:1
“Hata siku ya kwanza ya juma, ilipoanza kupambazuka, walikwenda kaburini, wakiyaleta manukato waliyoweka tayari.”

Yohana 20:1
“Hata siku ya kwanza ya juma Mariamu Magdalene alikwenda kaburini alfajiri, kungali giza bado; akaliona lile jiwe limeondolewa kaburini.”

Yohana 20:19
“Ikawa jioni, siku ile ya kwanza ya juma, pale walipokuwapo wanafunzi, milango imefungwa kwa hofu ya Wayahudi; akaja Yesu, akasimama katikati, akawaambia, Amani iwe kwenu.”

Yesu alifufuka siku ya Jumapili ambayo Biblia inaiita kuwa ni siku ya kwanza ya Juma. Kama Yesu alifufufuka siku ya kwanza ya juma (Jumapili), Sabato itakuwa lini?

Jibu: Jumamosi

 

[7] Je, katika mafundisho ya Yesu Kristo alifundisha kuishika Sabato?

Jibu: Ndiyo! Yesu ni kielelezo chetu kwa matendo Yake na mwenendo Wake wa maisha. Chochote alichokifanya na kukisema Yesu, ni sharti tukienzi…

Zingatia aya zifuatazo:

Marko 1:21
“Wakashika njia mpaka Kapernaumu, na mara siku ya Sabato akaingia katika sinagogi, akafundisha.”

Marko 6:2
“Na ilipokuwa Sabato, alianza kufundisha katika sinagogi; wengi waliposikia wakashangaa, wakisema, Huyu ameyapata wapi haya? Na, Ni hekima gani hii aliyopewa huyu? Na, ni nini miujiza hii mikubwa inayotendeka kwa mikono Yake?”

Luka 4:16
“Akaenda Nazareti, hapo alipolelewa; na siku ya Sabato akaingia katika sinagogi kama ilivyokuwa desturi Yake, akasimama ili asome.”

Luka 4:31
“Akashuka mpaka Kapernaumu, mji wa Galilaya, akawa akiwafundisha siku ya Sabato”

Luka 13:10
“Siku ya Sabato alikuwa akifundisha katika sinagogi mojawapo.”

Luka 6:6
“Ikawa siku ya Sabato nyingine aliingia katika sinagogi akafundisha; na mlikuwamo mtu ambaye mkono wake wa kuume umepooza.”

 

[8] Je, kanisa la awali (kanisa la mitume) lilikutana siku ya Sabato kuabudu?

Jibu: Ndiyo. Mitume wa Yesu Kristo, na mitume waliowafuata walikutana siku ya Saba ya Juma (Sabato) ili kuabudu.

Zingatia aya zifuatazo:

Matendo 13:14
“Lakini wao wakatoka Perge, wakapita kati ya nchi, wakafika Antiokia, mji wa Pisidia, wakaingia katika sinagogi siku ya Sabato, wakaketi.”

Matendo 13:27
“Kwa maana wakaao Yerusalemu, na wakuu wao, kwa kuwa hawakumjua yeye, wala maneno ya manabii yanayosomwa kila Sabato, wameyatimiza kwa kumhukumu.”

Matendo 13:42
“Na walipokuwa wakitoka, wakawasihi waambiwe maneno haya Sabato ya pili.”

Matendo 13:44
“Hata Sabato ya pili, watu wengi, karibu mji wote, wakakusanyika walisikie neno la Mungu.”

Matendo 15:21
“Kwa maana tangu zamani za kale Musa anao watu wahubirio mambo yake; katika kila mji husomwa kila Sabato katika masinagogi.”

Matendo 16:13
“Hata siku ya Sabato tukatoka nje ya lango, tukaenda kando ya mto, ambapo tukadhani ya kuwa pana mahali pa kusali; tukaketi, tukasema na wanawake waliokutana pale.”

Matendo 17:2
“Na Paulo, kama ilivyokuwa desturi yake, akaingia mle walimo, akahojiana nao kwa maneno ya maandiko Sabato tatu”

Matendo 18:4
“Akatoa hoja zake katika sinagogi kila sabato, akajaribu kuwavuta Wayahudi na Wayunani”

 

[9] Je, kitabu cha Waebrania kinafundisha nini kuhusu Sabato?

Waebrania 4:9
“Basi, imesalia raha ya Sabato kwa watu wa Mungu.”

Waebrania 10:25
“Wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia.”

Angalizo: Tutarudi kwenye kitabu cha Waebrania (siku za usoni) ili kufafanua zaidi maana ya aya hizi katika masomo yatakayofuata.

 

[9] Je, kitabu cha Ufunuo kinafundisha nini kuhusu Sabato?

Katika kitabu cha Ufunuo kuna vidokezo mbalimbali vinavyotuelekeza katika Amri ya Nne, yaani Sabato.

Ufunuo 11:19
“Kisha Hekalu la Mungu lililoko mbinguni likafunguliwa, na Sanduku la Agano Lake likaonekana ndani ya hekalu Lake. Kukawa na umeme, na sauti, na radi, na tetemeko la nchi, na mvua ya mawe nyingi sana.”

Swali: Kulikuwa na nini katika Sanduku la Agano?
Jibu: Mawe mawili, yaani Amri Kumi za Mungu.

Wapendwa, kulingana na kitabu cha Ufunuo, amri za Mungu ziko pale pale, hazibadiliki.

Ufunuo 14:6
“6 Kisha nikaona malaika mwingine, akiruka katikati ya mbingu, mwenye Injili ya milele, awahubiri hao wakaao juu ya nchi, na kila taifa na kabila na lugha na jamaa, 7 akasema kwa sauti kuu, Mcheni Mungu, na kumtukuza, kwa maana saa ya hukumu Yake imekuja. Msujudieni Yeye aliyezifanya mbingu na nchi na bahari na chemchemi za maji.”

(Linganisha aya hii na Kutoka 20:8-11)

Kutoka 20:8-11
“8 Ikumbuke siku ya Sabato uitakase. 9 Siku sita fanya kazi, utende mambo yako yote; 10 Lakini siku ya saba ni Sabato ya Bwana, Mungu wako, siku hiyo usifanye kazi yo yote, wewe, wala mwana wako, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala mjakazi wako, wala mnyama wako wa kufuga, wala mgeni aliye ndani ya malango yako. 11 Maana, kwa siku sita Bwana alifanya mbingu, na nchi, na bahari, na vyote vilivyomo, akastarehe siku ya saba; kwa hiyo Bwana akaibarikia siku ya Sabato akaitakasa.”

 

[10] Je, mapenzi ya Mungu ni yapi katika maisha yetu kuhusu utii wa Amri Zake, ikiwemo Amri ya Nne, yaani “Sabato ya siku ya Saba ya Juma?”

Jibu: Tuitii na kuishika kama amri 9 zingine.

Wapendwa, tukumbuke maonyo ya Yesu Kristo, katika injili ya Mathayo 7:21, anasema: “Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba Yangu aliye mbinguni.”

 

[11] Je, mapenzi ya Baba Yake ni yapi ?

Zaburi 40:8
“Kuyafanya mapenzi yako, Ee Mungu wangu, ndiyo furaha yangu; Naam, sheria Yako imo moyoni Mwangu.”

 

[12] Je, mtu anaweza kumpenda Yesu Kristo bila kuzishika Amri zake zote?

Jibu: La Hasha! Zingatia aya zifuatazo:

Yohana 14:15
“Mkinipenda mtazishika amri Zangu”

Yohana 14:21
“Yeye aliye na amri Zangu, na kuzishika, yeye ndiye anipendaye; naye anipendaye atapendwa na Baba yangu; Nami nitampenda na kujidhihirisha kwake”

Yohana 15:10
“Mkizishika amri Zangu, mtakaa katika pendo Langu; kama vile Mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo Lake.”

 

[13] Je, inawezekana kushika tu baadhi ya amri (kwa mfano: zote tisa, isipokuwa ya Nne –“Sabato”), na kukubalika/ wa na Mungu?

Jibu: La Hasha!!

Yakobo 2:10
“Maana mtu awaye yote atakayeishika sheria yote, ila akajikwaa katika neno moja, amekosa juu ya yote.”

 

[14] Je, twawezaje kujua dhahiri kuwa tunamjua na kumpenda Mungu?

1 Yohana 2:3-5
“Na katika hili twajua ya kuwa tumemjua Yeye, ikiwa tunashika amri Zake. Yeye asemaye, Nimemjua, wala hazishiki amri Zake, ni mwongo, wala kweli haimo ndani yake. Lakini yeye alishikaye neno Lake, katika huyo upendo wa Mungu umekamilika kweli kweli. Katika hili twajua ya kuwa tumo ndani Yake.”

1 Yohana 5:2-3
“Katika hili twajua kwamba twawapenda watoto wa Mungu, tumpendapo Mungu, na kuzishika amri Zake. Kwa maana huku ndiko kumpenda Mungu, kwamba tuzishike amri zake; wala amri zake si nzito.”

 

[15] Je, Sabato itakuwepo mbinguni ?
Jibu : Ndiyo

Nabii Isaya alionyeshwa watakatifu wakienda mbele za Mungu kuabudu siku ya Sabato mbinguni.

 

Isaya 66 :22 Kama vile mbingu mpya na nchi mpya, nitakazofanya, zitakavyokaa mbele zangu, asema Bwana, ndivyo uzao wenu na jina lenu litakavyokaa. 23 Na itakuwa, mwezi mpya hata mwezi mpya, na sabato hata sabato, wanadamu wote watakuja kuabudu mbele zangu, asema Bwana.

Mtume Yohana naye alioneshwa sanduku la Agano (la Amri 10 ikiwemo sabato) liko hekalu la mbinguni.

Ufunuo 11:19
“Kisha Hekalu la Mungu lililoko mbinguni likafunguliwa, na sanduku la agano lake likaonekana ndani ya hekalu lake. Kukawa na umeme, na sauti, na radi, na tetemeko la nchi, na mvua ya mawe nyingi sana.”

 

[16] Je, kuna haja ya kutunza Sabato leo?

Jibu: Ndiyo.

Kuitunza Sabato ya siku ya saba (Jumamosi) ni kumtangaza Mungu kuwa ni Mkuu, Muumbaji na Mweza wa vitu vyote! Shetani anajitahidi sana kufumba uelewa wa watu wasilitambue hili na kuendelea kumwadubu yeye – (mungu wa dunia hii). Tunapoamua kubadilisha au kukubaliana na kosa hili la kubadilisha siku rasmi ya ibada (Kutoka 20:8) tunamkana Mungu kuwa si Muumbaji.

 

HITIMISHO:

Wapendwa, tumechukua muda kuleta somo hili na kujibu maswali kadhaa kwa kutumia Maandiko Matakatifu. Bwana bado anasihi sana watu Wake, aliowaumba kwa mfano Wake, wamtii na kufuata amri Zake zote –ikiwemo Sabato ya siku ya saba ya Juma.

Mpinga Kristo ameibuka na kuleta mafundisho potofu na kinyume cha makusudi ya Mungu. “3 Lakini ikiwa injili yetu imesitirika, imesitirika kwa hao wanaopotea; 4 ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu.” (2 Wakorintho 4:3-4)

Shetani anatumia Manabii, Wachungaji, Walimu, Wanateologia wakuu, Wakuu wa makanisa, n.k., kufundisha watu mapotofu, wakidai “Bwana Mungu alisema hivi…., japo Bwana Mungu hakusema hivyo…”

Katika kitabu cha Ezekieli 22:26, tunaona jinsi makuhani walivyopotosha watu na kuiacha amri ya Bwana.

Ezekieli 22:26
“Makuhani wake wameihalifu sheria Yangu, wametia unajisi vitu Vyangu vitakatifu; hawakuweka tofauti ya vitu vitakatifu na vitu vya kutumiwa sikuzote; wala hawakuwafundisha watu kupambanua vitu vichafu na vitu vilivyo safi, nao wamefumba macho yao, wasiziangalie Sabato zangu, Nami nimetiwa unajisi kati yao.”

Angalia tena sentesi hii: “Makuhani wake wameihalifu sheria Yangu.” (Ezekieli 22:26a).

“Ilikuwa ni kazi maalum ya makuhani kutoa maelekezo kuhusu mahitaji ya kiungu na kuchunguza na kuwafundisha tofauti kati ya mambo matakatifu na yasiyo matakatifu (Walawi 10:10), na kuwafundisha watu katika utunzaji sahihi wa Sabato. Katika haya yote hawakuwa waaminifu.”

“Mashitaka haya yana yanamshangao wa kushangaza na ni sambamba katika zama hizi. Unabii wa Kitabu cha Ufunuo (sura ya 12 – 14) hutangaza kuwa Mungu anatoa mwito wa mageuzi katika kurudi kwenye Sabato ya kweli ya Bwana, siku ya saba ya juma. Matengenezo haya ni kwa ajili ya kuandaa ulimwengu kwa ujio wa pili wa Kristo. Ujumbe umeshatangazwa. Mwitikio wa watu umekuwa sawasawa na siku za Ezekieli. Wanadamu wanaficha nyuso zao kuhusu wajibu wa kuitunza Sabato ya kweli. (SDA BC Vol. 4; uk.)

MWITO: (Tufanye nini basi na somo hili)?

Wapendwa kuna haja ya kuchunguza somo hili kwa makini, tuache ubishi wa kimapokeo, badala yake, tutafute sana kuyatenda mapenzi ya Mungu, ambayo ni kuzishika Amri zake zote.

Shauku yetu ingekuwa kama ya Yesu Kristo: “Kuyafanya mapenzi Yako, Ee Mungu wangu, ndiyofuraha yangu; Naam, sheria Yako imo moyoni mwangu.” (Zaburi 40:8)

SAUTI YA INJILI:
(Hebu Sikia sauti Ya Bwana ikinena nasi tunapofunga kipindi hiki)

1 Yohana 2:3-5
“Na katika hili twajua ya kuwa tumemjua Yeye, ikiwa tunashika amri Zake. Yeye asemaye, Nimemjua, wala hazishiki amri Zake, ni mwongo, wala kweli haimo ndani yake. Lakini yeye alishikaye neno Lake, katika huyo upendo wa Mungu umekamilika kweli kweli. Katika hili twajua ya kuwa tumo ndani Yake.”

OMBI: Baba yetu mpendwa asante kwa somo hili. Hebu Roho Wako akaendelee kutufundisha somo hili tena na tena. Ninaomba sasa kwa ajili ya mtu ye yote ambaye hajakata shauri na kufanya uamuzi kuitii Sabato Yako takatifu; naomba pia kwa hao walio na mwangaza huu, lakini bado wanaendelea kupuuza. Utusamehe sisi sote Bwana, ukatutakase kwa damu Yako, ukatuandae kwa ajili ya ufalme Wako, Bwana. Kaa pamoja nasi hadi tutakapokutana tena katika mfululizo wa masomo haya. Tumeomba haya tukiamini kwamba umesikia na utatenda, sawa sawa na fadhili Zako, ni katika jina la Yesu Kristo-Bwana wetu, Amina.


 

MWISHO:
(Itaendelea tena; Somo litakalofuata: 92S-002)

The Gospel’s Voice © 2017/ Swahili edition.