Uumbaji 1/2

BIBLIA: “Soma, Elewa, Shuhudia”

MASWALI NA MAJIBU
Mfululizo: Kitabu cha Mwanzo
92A-1.001: Uumbaji 1/2

OMBI: Baba yetu mpendwa tunakushukuru tena kwa nafasi ya uhai siku hii ya leo. Tunaalika Roho Wako atufundishe katika tafakari hii ya kipindi cha Maswali na Majibu katika Biblia. Utusamehe Bwana, ukatutakase na kutuandaa kwa ajili ya ufalme Wako. Ni ombi letu katika jina la Yesu Kristo- Bwana wetu, Amina.


[1] Je, jina la kitabu cha kwanza cha Biblia, yaani “Mwanzo” kina maana gani?

(a) “Kile kilicho cha kwanza, mwanzo, yaani, mwanzo wa tendo, mchakato, au hali ya kuwa” (Zaburi 111:10); (b) Mwanzo, mwanzo wa nyakati (Mwa 1:1) – Dictionary of Biblical Languages with Semantic Domains (DBL).

Mzizi wa neno hili limetumika pia katika Zaburi 111:10, mtunga Zaburi anaposema: “Kumcha Bwana ndio mwanzo wa hekima”

Jina hili lilichukuliwa kutoka katika toleo la Kiyunani la Mwanzo 2:4a: “Hivyo ndivyo vizazi vya mbingu na nchi zilipoumbwa” ambayo inatuelekeza katika tabia ya vizazi katika Mwanzo. Kitabu hiki kinatuelekeza katika “mwanzo” wa uumbaji, “mwanzo” wa mwanadamu, “mwanzo” wa uasi, “mwanzo” wa ibada, “mwanzo” wa wana kumi na wawili wa Israeli, n.k. Kitabu cha Mwanzo kimeweka msingi wa vizazi vilivyoibuka (baadaye) na kuwa taifa la Israeli.

[2] Je, maandiko yanasemaje kuhusu mwanzo wa ulimwengu?

Mwanzo 1:1.
“Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi.”

 

[3] Ni kwa nguvu gani Mungu aliuumba ulimwengu?

Kwa uwezo wa Neno Lake. Zingatia aya zifuatazo:

Mwanzo 1:6, 9.
“6 Mungu akasema, Na liwe anga katikati ya maji, likayatenge maji na maji. 9 Mungu akasema, Maji yaliyo chini ya mbingu na yakusanyike mahali pamoja, ili pakavu paonekane; ikawa hivyo.”

Zaburi 33:6.
“Kwa neno la Bwana mbingu zilifanyika, Na jeshi Lake lote kwa pumzi ya kinywa Chake.”

Zaburi 136:6.
“Yeye aliyeitandaza nchi juu ya maji; Kwa maana fadhili Zake ni za milele.”

Waebrania 1:2
“Tena kwa Yeye (Yesu Kristo) aliufanya Ulimwengu.”

Waebrania 11:3.
“Kwa imani twafahamu ya kuwa ulimwengu uliumbwa kwa neno la Mungu, hata vitu vinavyoonekana havikufanywa kwa vitu vilivyo dhahiri.”

2 Petero 3:5.
“….. Zilikuwako mbingu tangu zamani, na nchi pia, imefanyizwa kutoka katika maji, na ndani ya maji, kwa neno la Mungu.”

 

[4] Je, Mungu Mwana (Yesu Kristo) pia alihusika katika uumbaji wa Ulimwengu?

Yohana 1:1-3
“1 Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. 2 Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu. 3 Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika.”

 

[5] Tunawezaje kujua kwamba Yesu Kristo alikuwa pamoja na Mungu Baba katika uumbaji?

Yohana 1:1.
“Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu.”

Wakolosai 1:15, 16.
“15 Naye (Yesu Kristo) ni mfano wa Mungu asiyeonekana, Mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote. 16 Kwa kuwa katika Yeye vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na vilivyo juu ya nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana; ikiwa ni vitu vya enzi, au usultani, au enzi, au mamlaka; vitu vyote viliumbwa kwa njia Yake, na kwa ajili Yake.”

[6] Je, Mungu Roho (Roho Mtakatifu) pia alihusika katika uumbaji wa Ulimwengu?

Mwanzo 1:2
“Nayo nchi ilikuwa ukiwa, tena utupu, na giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji; Roho ya Mungu ikatulia juu ya uso wa maji.”

Ayubu 26:13
“Hizo mbingu hupambwa kwa Roho Yake; Mkono wake umemchoma nyoka aendaye mbio.”

Ayubu 33:4
“Roho ya Mungu imeniumba, Na pumzi za Mwenyezi hunipa uhai.”

Zaburi 33:6
“Kwa neno la Bwana mbingu zilifanyika, Na jeshi lake lote kwa pumzi ya kinywa Chake”

Zaburi 104:30
“Waipeleka Roho Yako, wanaumbwa, Nawe waufanya upya uso wa nchi.”

 

HITIMISHO:

Wapendwa, Neno la Mungu lina nguvu, nguvu ya uumbaji, nguvu ya kubadilisha mienendo yetu na kutuumbia mioyo mipya, nguvu ya kutupatia uzima wa milele. Wakati Mungu aliumba ulimwengu, alitumia “Neno Lake” kama vile findi seremala atumiavyo mbao, nyundo na misumari kuunda mlango. Mungu huumba, hujenga kwa “neno lake.” Mungu anapoongea, “neno lake” hutumiza matakwa Yake na kamwe “halitanirudia bure.” Neno lake linaudhibiti na kuutegemeza ulimwengu.

Zingatia aya zifuatazo:

Isaya 55:11
“10 Maana kama vile mvua ishukavyo, na theluji, kutoka mbinguni, wala hairudi huko; bali huinywesha ardhi, na kuizalisha na kuichipuza, ikampa mtu apandaye mbegu, na mtu alaye chakula; 11 ndivyo litakavyokuwa Neno Langu, litokalo katika kinywa Changu; halitanirudia bure, bali litatimiza mapenzi Yangu, nalo litafanikiwa katika mambo yale niliyolituma.”

Zaburi 119:89-91
“89 Ee Bwana, neno lako lasimama Imara mbinguni hata milele. 90 Uaminifu wako upo kizazi baada ya kizazi, Umeiweka nchi, nayo inakaa. 91 Kwa hukumu zako vimesimama imara hata leo, Maana vitu vyote ni watumishi wako.”

MWITO:
(Tufanye nini basi na somo hili?)

Zaburi 33:6-9
“6 Kwa neno la Bwana mbingu zilifanyika, Na jeshi lake lote kwa pumzi ya kinywa chake. 7 Hukusanya maji ya bahari chungu chungu, Huviweka vilindi katika ghala. 8 Nchi yote na imwogope Bwana, Wote wakaao duniani na wamche.”

Sauti Ya Injili
{Hebu sikia sauti ya Bwana ikinena nasi tunapofunga kipindi hiki.}

Isaya 40:25-26, 28

25 Mtanifananisha na nani, basi, nipate kuwa sawa naye? Asema yeye aliye Mtakatifu. 26 Inueni macho yenu juu, mkaone; ni nani aliyeziumba hizi; aletaye nje jeshi lao kwa hesabu; aziita zote kwa majina; kwa ukuu wa uweza wake, na kwa kuwa yeye ni hodari kwa nguvu zake; hapana moja isiyokuwapo mahali pake.

28 Je! Wewe hukujua? Hukusikia? Yeye Mungu wa milele, Bwana, Muumba miisho ya dunia, hazimii, wala hachoki; akili zake hazichunguziki.

 

OMBI: Asante Bwana kwa uumbaji Wako. Asante kwa kutuumba kwa namna ya pekee. Tukumbushe kukupenda na kukusifu daima, kwa sababu: “Msaada wetu u katika jina la Bwana, Aliyezifanya mbingu na nchi” (Zaburi 124:8). Jina lako lihimidiwe milele zote, ni katika jina la Yesu Kristo, tumeomba, Amina.

 

Sauti Ya Injili SDA © 2017