135-006: Malaika na Ujio wa Masihi

VITA KUU KATI YA KRISTO NA SHETANI

Sehemu ya I: Malaika, Shetani, Mapepo

Mfululizo # 135:001-044

Mada ya Leo: 135-006
MALAIKA NA UJIO WA MASIHI

OMBI: Baba yetu mpendwa, asante kwa zawadi ya neno Lako. Tunaalika Roho wako atuongoze katika tafakari ya somo hili. Tusamehe makosa, uovu, na dhambi. Tuandae kwa ajili ya ufalme wako. Tumeomba haya katika jina la Yesu Kristo, Bwana wetu, Amina.
MALAIKA NA UJIO WA MASIHI

Muhtasari wa Mawazo Makuu
(a) Utabiri: Kuzaliwa kwa Yohana
(b) Utabiri: Kuzaliwa kwa Yesu Kristo
(c) Tangazo la kuzaliwa kwa Yesu Kristo
(d) Tangazo la kufufuka kwa Yesu Kristo
(e) Utabiri wa Marejeo ya Yesu Kristo
(f) Ufunuo wa Injili kwa Mataifa
(g) Unabii wa Siku za Mwisho
(h) Utabiri: Ushindi Hatimaye!

 

MALAIKA ATABIRI KUZALIWA KWA YOHANA MBATIZAJI

Luka 1:11-14
11 Akatokewa na malaika wa Bwana, amesimama upande wa kuume wa madhabahu ya kufukizia. 12 Zakaria alipomwona alifadhaika, hofu ikamwingia. 13 Lakini yule malaika akamwambia, Usiogope, Zakaria, maana dua yako imesikiwa, na mkeo Elisabeti atakuzalia mtoto mwanamume, na jina lake utamwita Yohana. 14 Nawe utakuwa na furaha na shangwe, na watu wengi watakufurahia kuzaliwa kwake.

GABRIELI NDIYE NANI?

Neno Gabrieli linafafanuliwa kama “mtu wa Mungu”; au “Mungu amedhihirisha nguvu zake”

Gabrieli ni “malaika asimamaye mbele za Mungu” (Luka 1:19). Gabrieli ni moja ya malaika wawili waliotajwa kwa jina katika Biblia (mwingine ni Michael – Mikaeli).

Gabrieli alimtokea Danieli katika umbo la kibinadamu ili kumfafanulia maono yake, kumuonyesha nini kingetokea katika siku ya hukumu, na kumpa Daniel “akili upate kufahamu” (Danieli 8:22c). Alimtokea nabii Danieli na kumuelezea unabii wa kondoo na mbuzi (Danieli 8:16 – 26), na kipindi cha unabii wa wiki sabibini (Danieli 9:21 – 27).

Katika Agano Jipya, tunamuona tena Gabrieli akimtokea kuhani Zekaria alipokuwa akihudumu hekaluni. Gabrieli alimfunulia mambo yahusuyo kuzaliwa kwa mtoto wake, yaani Yohana Mbatizaji (Luka 1:11 – 20). Miezi sita baadaye Gabrieli alimtokea Mariamu na kumtaarifu kuwa atakuwa mama mzazi wa Yesu Kristo, Masihi aliyesubiwa toka enzi za Agano la Kale (Luka 1: 26 – 33).

Katika sura hii, tunaona jinsi Mungu alivyotumia malaika wake kuweza kuwasilisha mapenzi yake kwa wanadamu. Malaika (Gabrieli) anamtokea Zakaria na kumwambia mambo sita muhimu sana kuhusu huyu mtoto atakayezaliwa (cf. Luka 1:14-17)

[1] Jina lake litaitwa Yohana
[2] Atakuwa mkuu mbele za Bwana
[3] Hatakunywa divai wala kileo
[4] Atajazwa Roho Mtakatifu
[5] Atawarejeza wengi kwa Bwana Mungu wao
[6] Atatangulia mbele zake katika roho ya Eliya, na nguvu zake

Luka 1:18-19
18 Zakaria akamwambia malaika, Nitajuaje neno hilo? Maana mimi ni mzee, na mke wangu ni mkongwe wa siku nyingi. 19 Malaika akamjibu akamwambia, Mimi ni Gabrieli, nisimamaye mbele za Mungu; nami nimetumwa niseme nawe, na kukupasha habari hizi njema.

Luka 1:20-21
20 Na tazama! Utakuwa bubu, usiweze kusema, mpaka siku ile yatakapotukia hayo, kwa sababu hukuyasadiki maneno yangu; nayo yatatimizwa kwa wakati wake. 21 Na wale watu walikuwa wakimngojea Zakaria, wakastaajabia kukawia kwake mle hekaluni.

 

MALAIKA ATABIRI KUZALIWA KWA YESU KRISTO

Mathayo 1:20-21
26 Mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu kwenda mpaka mji wa Galilaya, jina lake Nazareti, 27 kwa mwanamwali bikira aliyekuwa ameposwa na mtu, jina lake Yusufu, wa mbari ya Daudi; na jina lake bikira huyo ni Mariamu.
Luka 1:26-38
26 Mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu kwenda mpaka mji wa Galilaya, jina lake Nazareti, 27 kwa mwanamwali bikira aliyekuwa ameposwa na mtu, jina lake Yusufu, wa mbari ya Daudi; na jina lake bikira huyo ni Mariamu.

28 Akaingia nyumbani kwake akasema, Salamu, uliyepewa neema, Bwana yu pamoja nawe. 29 Naye akafadhaika sana kwa ajili ya maneno yake, akawaza moyoni, Salamu hii ni ya namna gani?

30 Malaika akamwambia, Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu. 31 Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu.

32 Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake. 33 Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho.

34 Mariamu akamwambia malaika, Litakuwaje neno hili, maana sijui mume?

35 Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu.

36 Tena, tazama, jamaa yako Elisabeti naye amechukua mimba ya mtoto mwanamume katika uzee wake; na mwezi huu ni wa sita kwake yeye aliyeitwa tasa; 37 kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu.

38 Mariamu akasema, Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema. Kisha malaika akaondoka akaenda zake.

 

 

MALAIKA WAKITOA TANGAZO LA KUZALIWA KWA YESU KRISTO

Luka 2:8-12
8 Na katika nchi ile ile walikuwako wachungaji wakikaa makondeni na kulinda kundi lao kwa zamu usiku. 9 Malaika wa Bwana akawatokea ghafula, utukufu wa Bwana ukawang’aria pande zote, wakaingiwa na hofu kuu.

10 Malaika akawaambia, Msiogope; kwa kuwa mimi ninawaletea habari njema ya furaha kuu itakayokuwa kwa watu wote; 11 maana leo katika mji wa Daudi amezaliwa, kwa ajili yenu, Mwokozi, ndiye Kristo Bwana. 12 Na hii ndiyo ishara kwenu; mtamkuta mtoto mchanga amevikwa nguo za kitoto, amelala katika hori ya kulia ng’ombe.

Luka 2:13-14
13 Mara walikuwapo pamoja na huyo malaika, wingi wa jeshi la mbinguni, wakimsifu Mungu, na kusema, 14 Atukuzwe Mungu juu mbinguni, Na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia.
“Tangu Kristo alipoingia ulimwenguni, fitina zote za mashirika ya kishetani yalielekezwa kazini ili kudanganya na kumwangamiza Yeye kama Adamu alivyodanganywa na kuangamizwa…”

“Wakati Kristo anazaliwa Bethlehemu, malaika wa Mungu waliwatokea wachungaji, ambao walikuwa wakiangalia mifugo yao usiku, na kutoa hati za utambulisho za mamlaka ya yule Mtoto mchanga. Shetani alijua kwamba Mmoja amekuja duniani na utume wa kiungu ili kuvuruga mamlaka yake. Alisikia malaika akitangaza: “…. maana leo katika mji wa Daudi amezaliwa, kwa ajili yenu, Mwokozi, ndiye Kristo Bwana” (Luka 2:10, 11). Ellen G. White; God’s Amazing Grace, uk. 162.1

 

 

MALAIKA WAKITOA TANGAZO LA KUFUFUKA KWA YESU KRISTO

Mathayo 28: 5-7
1 Hata sabato ilipokwisha, ikipambazuka siku ya kwanza ya juma, Mariamu Magdalene, na Mariamu yule wa pili, walikwenda kulitazama kaburi.

2 Na tazama, palikuwa na tetemeko kubwa la nchi; kwa sababu malaika wa Bwana alishuka kutoka mbinguni, akaja akalivingirisha lile jiwe akalikalia. 3 Na sura yake ilikuwa kama umeme, na mavazi yake meupe kama theluji. 4 Na kwa kumwogopa, wale walinzi wakatetemeka, wakawa kama wafu.
5 Malaika akajibu, akawaambia wale wanawake, Msiogope ninyi; kwa maana najua ya kuwa mnamtafuta Yesu aliyesulibiwa. 6 Hayupo hapa; kwani amefufuka kama alivyosema. Njoni, mpatazame mahali alipolazwa.

7 Nanyi nendeni upesi, mkawaambie wanafunzi wake, Amefufuka katika wafu. Tazama, awatangulia kwenda Galilaya; ndiko mtakakomwona. Haya, nimekwisha waambia.

AYA ZA NYONGEZA:
(a) Mariko 16:5-7
(b) Luka 24:4-7,23
(c) Yohana 20:10-14

 

MALAIKA NA UTABIRI WA MAREJEO YA YESU KRISTO

Matendo 1:9-11.
9 Akiisha kusema hayo, walipokuwa wakitazama, akainuliwa, wingu likampokea kutoka machoni pao. 10 Walipokuwa wakikaza macho mbinguni, yeye alipokuwa akienda zake, tazama, watu wawili wakasimama karibu nao, wenye nguo nyeupe, 11 wakasema, Enyi watu wa Galilaya, mbona mmesimama mkitazama mbinguni? Huyu Yesu aliyechukuliwa kutoka kwenu kwenda juu mbinguni, atakuja jinsi iyo hiyo mlivyomwona akienda zake mbinguni.

 

MALAIKA NA UFUNUO WA INJILI KWA MATAIFA

Matendo 11:12-14
12 Roho akaniambia nifuatane nao, nisione tashwishi. Ndugu hawa sita nao wakaenda pamoja nami, tukaingia katika nyumba ya mtu yule; 13 akatueleza jinsi alivyomwona malaika aliyesimama nyumbani mwake na kumwambia, Tuma watu kwenda Yafa ukamwite Simoni aitwaye Petro, 14 atakayekuambia maneno ambayo yatakuokoa, wewe na nyumba yako yote.

Matendo 10:1-5
1 Palikuwa na mtu Kaisaria, jina lake Kornelio, akida wa kikosi kilichoitwa Kiitalia, 2 mtu mtauwa, mchaji wa Mungu, yeye na nyumba yake yote, naye alikuwa akiwapa watu sadaka nyingi, na kumwomba Mungu daima.

3 Akaona katika maono waziwazi, kama saa tisa ya mchana, malaika wa Mungu, akimjia na kumwambia, Kornelio!

4 Akamtazama sana, akaogopa akasema, Kuna nini, Bwana? Akamwambia, Sala zako na sadaka zako zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za Mungu. 5 Sasa basi, peleka watu Yafa, ukamwite Simoni, aitwaye Petro.

Matendo 10: 30-33
30 Kornelio akasema, Siku tatu zilizopita, katika saa hii, yaani saa tisa, nilikuwa nikisali nyumbani mwangu; nikamwona mtu amesimama mbele yangu, mwenye nguo zing’arazo, 31 akasema, Kornelio, kuomba kwako kumesikiwa, na sadaka zako zinakumbukwa mbele za Mungu.

Soma Pia:
Ufunuo 14:6-7

 

 

MALAIKA NA UNABII WA SIKU ZA MWISHO

Ufunuo 1:1-3

1 Ufunuo wa Yesu Kristo, aliopewa na Mungu awaonyeshe watumwa wake mambo ambayo kwamba hayana budi kuwako upesi; naye akatuma kwa mkono wa malaika akamwonyesha mtumwa wake Yohana; 2 aliyelishuhudia Neno la Mungu, na ushuhuda wa Yesu Kristo, yaani, mambo yote aliyoyaona. 3 Heri asomaye na wao wayasikiao maneno ya unabii huu, na kuyashika yaliyoandikwa humo; kwa maana wakati u karibu.

Gabrieli ni malaika wa unabii (cf. Danieli 8:16, 9:21-22, 10:11, 21) anayetumwa katika Agano la Kale kwa nabii Danieli. Katika Ufunuo 1:1 – [“naye akatuma kwa mkono wa malaika”] – hajatajwa kwa jina, lakini wanateologia wengi wanafikiri anahusika hapa pia, maana kitabu cha Danieli kina uhusiano wa karibu sana na kitabu cha Ufunuo.

 

 

MALAIKA WAKITOA TANGAZO LA HUKUMU.

Mara tu kabla ya marejeo Ya Kristo, malaika watatu wanaonekane wakiwa na “Ujumbe wa Malaika Watatu”. Wanatoa maonyo ya mwisho kwa walimwengu. Wanaalika watu wote kuungama, kutubu, na kumrudia Mungu wao, “kwa maana saa ya hukumu Yake imekuja”

Ufunuo 14:6-7
[Ujumbe wa Malaika wa Kwanza]

6 Kisha nikaona malaika mwingine, akiruka katikati ya mbingu, mwenye Injili ya milele, awahubiri hao wakaao juu ya nchi, na kila taifa na kabila na lugha na jamaa, 7 akasema kwa sauti kuu, Mcheni Mungu, na kumtukuza, kwa maana saa ya hukumu yake imekuja. Msujudieni yeye aliyezifanya mbingu na nchi na bahari na chemchemi za maji.

Ufunuo 14:8
[Ujumbe wa Malaika wa Pili]

Kisha mwingine, malaika wa pili, akafuata, akisema, Umeanguka, umeanguka Babeli, mji ule ulio mkubwa, maana ndio uliowanywesha mataifa yote mvinyo ya ghadhabu ya uasherati wake.

Ufunuo 14:9-11
[Ujumbe wa Malaika wa Tatu]

9 Na mwingine, malaika wa tatu, akawafuata, akisema kwa sauti kuu, Mtu awaye yote akimsujudu huyo mnyama na sanamu yake, na kuipokea chapa katika kipaji cha uso wake, au katika mkono wake, 10 yeye naye atakunywa katika mvinyo ya ghadhabu ya Mungu iliyotengenezwa, pasipo kuchanganywa na maji, katika kikombe cha hasira yake; naye atateswa kwa moto na kiberiti mbele ya malaika watakatifu, na mbele za Mwana-Kondoo.

11 Na moshi wa maumivu yao hupanda juu hata milele na milele, wala hawana raha mchana wala usiku, hao wamsujuduo huyo mnyama na sanamu yake, na kila aipokeaye chapa ya jina lake.

MWITO WA YESU KRISTO

Ufunuo 14:12
Hapa ndipo penye subira ya watakatifu, hao wazishikao amri za Mungu, na imani ya Yesu.

 

 

MALAIKA NA UTABIRI WA USHINDI HATIMAYE!

Ufunuo 19:9
9 Naye akaniambia, Andika, Heri walioalikwa karamu ya arusi ya Mwana-Kondoo. Akaniambia, Maneno haya ni maneno ya kweli ya Mungu.

Ufunuo 19:11-16
11 Kisha nikaziona mbingu zimefunuka, na tazama, farasi mweupe, na Yeye aliyempanda, aitwaye Mwaminifu na Wa-kweli, naye kwa haki ahukumu na kufanya vita.

12 Na macho yake yalikuwa kama mwali wa moto, na juu ya kichwa chake vilemba vingi; naye ana jina lililoandikwa, asilolijua mtu ila yeye mwenyewe.

13 Naye amevikwa vazi lililochovywa katika damu, na jina lake aitwa, Neno la Mungu.

14 Na majeshi yaliyo mbinguni wakamfuata, wamepanda farasi weupe na kuvikwa kitani nzuri, nyeupe, safi.

Malaika wengi wasiohesabika watamfuata Yesu Kristo. Yesu akiwa Jemedari Mkuu, ataongoza jeshi lake, kufanya vita na kuchukua walteule wake. (soma Mathayo 24:31; 25:31)

15 Na upanga mkali hutoka kinywani mwake ili awapige mataifa kwa huo. Naye atawachunga kwa fimbo ya chuma, naye anakanyaga shinikizo la mvinyo ya ghadhabu ya hasira ya Mungu Mwenyezi.

16 Naye ana jina limeandikwa katika vazi lake na paja lake, MFALME WA WAFALME, NA Bwana WA MABwana.

 

HITIMISHO:

Mungu alitumia malaika zake kutaarifu walimwengu kuhusu ujio wa Masihi mara yake ya kwanza. Malaika walishuhudia kuzaliwa Kwake, kufufuka Kwake, walitabiri marejeo Yake alivyopaa kwenda mbinguni.

Ufunuo wa Yesu Kristo na Unabii wa siku za mwisho (katika kitabu cha Ufunuo) ulitufikia toka kwa Mungu, – kwa Yesu Kristo, – kwa “kwa mkono wa Malaika”, kwa “mtumwa wake Yohana.”

Malaika watakatifu wanatumika hadi leo, katika siku hizi za mwisho, kuwasilisha mapenzi ya Mungu kwa watu wake. Wanatulinda na mabaya ya ulimwengu huu, wako nasi siku zote, na watahusika kwa kiasi kikubwa sana katika marejeo ya Yesu Kristo.

Swali langu kwako ndugu mpendwa!
Je, unaamini kuwa wapo Malaika watakatifu kwa ajili yako? Je, unamshukuru Mungu kwa huduma ya malaika hawa? Je, umezishika “amri za Mungu, na imani ya Yesu?” Je, umejiandaje na marejeo ya Yesu Kristo?

 

SAUTI YA INJILI
{Hebu sikia sauti ya Bwana ikinena nasi tunapofunga somo hili}

Mathayo 24:31
30 Ndipo itakapoonekana ishara yake Mwana wa Adamu mbinguni; ndipo mataifa yote ya ulimwengu watakapoomboleza, nao watamwona Mwana wa Adamu akija juu ya mawingu ya mbinguni pamoja na nguvu na utukufu mwingi.

31 Naye atawatuma malaika zake pamoja na sauti kuu ya parapanda, nao watawakusanya wateule wake toka pepo nne, toka mwisho huu wa mbingu mpaka mwisho huu.

 

Mathayo 25:31
31 Hapo atakapokuja Mwana wa Adamu katika utukufu wake, na malaika watakatifu wote pamoja naye, ndipo atakapoketi katika kiti cha utukufu wake; 32 na mataifa yote watakusanyika mbele zake; naye atawabagua kama vile mchungaji abaguavyo kondoo na mbuzi;

Ufunuo 22:16
Mimi Yesu nimemtuma malaika wangu kuwashuhudia ninyi mambo hayo katika makanisa. Mimi ndimi niliye Shina na Mzao wa Daudi, ile nyota yenye kung’aa ya asubuhi.

Ufunuo 22:6
Kisha akaniambia, Maneno haya ni amini na kweli. Naye Bwana, Mungu wa roho za manabii, alimtuma malaika wake kuwaonyesha watumwa wake mambo ambayo hayana budi kuwako upesi.


 

MWISHO.

Sauti Ya Injili SDA © 2017