5-30-17: Nyota ya Asubuhi mioyoni Mwetu

BIBLIA: “Soma, Elewa, Shuhudia”

MWONGOZO WA KUJIFUNZA BIBLIA
Robo hii: Lisha Kondoo Zangu
Kitabu: 1 Petro & 2 Petro
Somo la (10/13): Unabii na Maandiko

Fungu la Kukariri: “Nasi tuna lile neno la unabii lililo imara zaidi, ambalo, mkiliangalia, kama taa ing’aayo mahali penye giza, mwafanya vyema, mpaka kutakapopambazuka, na nyota ya asubuhi kuzuka mioyoni mwenu”(2 Petro 1:19).

OMBI: Baba yetu mpendwa, asante kwa nafasi nyingine ya tafakari ya Mwongozo wa kujifunza Biblia. Tunaomba Roho Wako atufundishe somo hili. Tusamehe dhambi, uovu, makosa na kasoro zetu zote. Tuandae kwa ajili ya ufalme Wako. Tunaomba haya katika Jina la Yesu Kristo, Bwana wetu, Amina!


NYOTA YA ASUBUHI MIOYONI MWETU

  • Jumanne
    May 30, 2017

“Nasi tuna lile neno la unabii lililo imara zaidi, ambalo, mkiliangalia, kama taa ing’aayo mahali penye giza, mwafanya vyema, mpaka kutakapopambazuka, na nyota ya asubuhi kuzuka mioyoni mwenu.” (2 Petro 1:19).

SWALI # 1: Soma maneno haya kwa uangalifu. Petro anasema nini kilicho muhimu kiasi kile kwetu, hata leo?

Soma jibu na maelezo ya mwandishi, aya ya 1-2-3 hapo chini:

“Hapa, kama ambavyo tunaweza kuona katika sehemu nyingi ndani ya Biblia (Mwanzo 1:4, Yohana 1:5, Isaya 5:20, Waefeso 5:8), mgawanyiko unafanywa baina ya nuru na giza. Kwa Petro Neno la Mungu linang’aa kama nuru katika mahali penye “giza” (baadhi pia hutafsiri giza kama “dhalili,” “chafu”). Hii ndiyo maana yuko wazi sana kuwa tunahitajika “kuiangalia” nuru ile, kulifuata hadi “kutakapopambazuka, na nyota ya asubuhi kuzuka mioyoni [mwetu].” Sisi ni viumbe walioanguka, wanaoishi katika ulimwengu ulioanguka na wenye giza. Tunahitaji uwezo wa Mungu usio wa kibinadamu kutuongoza kutoka katika giza hili kwenda katika nuru, na nuru ile ni Yesu.”

“Petro anawaelekeza wasomaji wake katika lengo. Wengine huamini kuwa maneno “mpaka kutakapopambazuka” humaanisha kuja kwa Yesu mara ya pili. Wazo la “nyota ya asubuhi” kuzuka mioyoni mwenu husikika kuwa ni jambo la mara moja na la mtu binafsi zaidi. Nyota ya asubuhi humaanisha Yesu (Ufunuo 2:28, 22:16). Kuzuka kwake katika mioyo yao huelekea kuwa ni kuhusu kumfahamu Yesu, kumshikilia kikamilifu na kupata uzoefu wa uhakika Kristo aliye hai katika maisha yao binafsi. Yesu hapaswi kuwa ukweli wa kimafundisho tu; yapasa awe kiini cha kuishi kwetu na chimbuko la tumaini na imani yetu. Kwa hiyo Petro anaweka muunganiko wa dhahiri kati ya kujifunza Neno la Mungu na kuwa na uhusiano unaookoa pamoja na Yesu aliye “nyota ya asubuhi.”

Na kwa kweli, nuru ile ikiwa inang’aa mioyoni mwetu, tutaieneza kwa wengine. “Ulimwengu wote ni lazima uangazwe na utukufu wa ukweli wa Mungu. Nuru ile ni lazima ing’ae kwa nchi zote na kwa watu wote. Na ni kutoka kwa wale walioipokea ile nuru ndiyo inapaswa kuangaza. Nyota ya mchana imezuka juu yetu na tunapaswa kuangaza nuru yake katika njia ya wale waliomo gizani.” —Ellen G. White, Christian Experience and Teachings of Ellen G. White, uk. 220.


 

SWALI # 2: Je kujifunza kwako binafsi Neno kunakusaidiaje kumfahamu Yesu vizuri zaidi?

Zaburi 119:128-130
128 Maana nayaona mausia Yako yote kuwa ya adili, Kila njia ya uongo naichukia.
129 Shuhuda Zako ni za ajabu, Ndiyo maana roho yangu imezishika.
130 Kufafanusha maneno Yako kwatia nuru, Na kumfahamisha mjinga.

 

JIBU # 2: Kunasaidia sana, maana Neno linatuelekeza kwa Kristo Yesu, linatupatia upambanuzi wa ndani kuweza kuichukia dhambi, linatuelemisha na kutupatia mwangaza katika maisha ya kila siku.

Anapokaribia kumalizia kitabu chake, mtume Yohana anahitaji tuelewe kinagaubaga kuwa kusudi la Injili ni kumfahamu na kumwamini Yesu Kristo.

Yohana 20:30-31
30 Basi kuna ishara nyingine nyingi alizozifanya Yesu mbele ya wanafunzi wake, zisizoandikwa katika kitabu hiki. 31 Lakini hizi zimeandikwa ili mpate kuamini ya kwamba Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu; na kwa kuamini mwe na uzima kwa jina Lake.

 

UMUHIMU WA NENO LA MUNGU

“Nasi tuna lile neno la unabii lililo imara zaidi, ambalo, mkiliangalia, kama taa ing’aayo mahali penye giza, mwafanya vyema, mpaka kutakapopambazuka, na nyota ya asubuhi kuzuka mioyoni mwenu.” (2 Petro 1:19).

Petro anawaelekeza wasomaji wake kuzingatia kwa makini na “neno la unabii.” Ili kukabiliana na makosa ya hila ya walimu wa uongo, ilikuwa ni muhimu sana wajue na kuzingatia kwa makini NENO (“maandiko”); ili kwamba waweze kukataa na kuyapinga mafundisho ya uongo

 

Zingatia mifano michache katika Biblia:

[1] Daudi- akishuhudia msaada wa Neno.

[2] Apolo, alikuwa hodari katika maandiko, na aliwashinda Wayahudi kwa kufichua mafundisho yao ya uongo.

[3] Yesu Kristo, alimshinda Ibilisi, kwa Neno.

[4] Yesu Kristo –alionya kukusu kupotea kwa wayahudi kwa sababu walikuwa hawajui “maandiko wala uweza wa Mungu.”

[5] Neno la Mungu linatoa maonyo kwetu “sisi, tuliofikiliwa na miisho ya zamani

[6] Neno la Mungu linatutakasa:Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli.” (Yohana 17:17)

[7] Neno la Mungu linatupa ushindi (cf. Waefeso 6:11-17)

(a) Neno la Mungu linatuwezesha kuzipinga hila zote za Shetani
(b) Neno la Mungu ni silaha katika vita ya “ulimwengu wa roho”
(c) Neno la Mungu linatuwezesha “kushindana siku ya uovu”
(d) Neno la Mungu linatuwezesha “kusimama” imara vitani.
(e) Neno la Mungu ni “chapeo ya wokovu”
(f) Neno la Mungu ni “upanga wa Roho”

 

Zaburi 17:4
Mintarafu matendo ya wanadamu; Kwa neno la midomo Yako nimejiepusha na njia za wenye jeuri.

Matendo 18:28
Kwa maana aliwashinda Wayahudi kabisa kabisa mbele ya watu wote, akionyesha kwa maneno ya maandiko ya kuwa Yesu ni Kristo.

Mathayo 4:4
Naye akajibu akasema, Imeandikwa, Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.

Mathayo 22:29
Yesu akajibu, akawaambia, Mwapotea, kwa kuwa hamyajui maandiko wala uweza wa Mungu.

1 Wakorintho 10:11-12
11 Basi mambo hayo yaliwapata wao kwa jinsi ya mifano, yakaandikwa ili kutuonya sisi, tuliofikiliwa na miisho ya zamani. 12 Kwa hiyo anayejidhania kuwa amesimama na aangalie asianguke.

[8] Zingatia umuhimu wa Neno la Mungu kulingana na 2 Timotheo 3:16

  • Kila andiko, lina “pumzi ya Mungu”
  • Lafaa “kwa mafundisho”
  • Lafaa “kwa kuwaonya watu makosa yao”
  • Lafaa “kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki”
  • Lafaa tukamilisha ili tupate “kutenda kila tendo jema”

HITIMISHO

Ili kujenga hoja yake vizuri zaidi, Petro alitoa mfano rahisi, akilinganisha neno la Mungu na ‘taa ing’aayo mahali penye giza.” Kishazi hiki kinatukumbusha maneno ya mtunga Zaburi, “Neno Lako ni taa ya miguu yangu na mwanga wa njia yangu” (Zaburi 119:105; cf. 130; 43:3; Mithali 6:23).

Giza (auchmēros) ni neno la ufafanuzi ambalo chimbuko lake kwa asilia lilikuwa neno, “kavu” au “kiraka,” kisha likatumika kama “chafu”, au “isiyoonekana vyema”. Kishazi “penye giza,” kinaashiria uweusi wa ulimwengu ulioanguka na kuzama dhambini unaozuia watu kuona ukweli mpaka taa ya ufunuo wa kimungu ung’ae kwanza.

Hivyo Petro analinganisha maandiko na taa itoayo mwanga kwa ulimwengu wenye giza na dhambi.

Siku yaja [siku ya Bwana] ambapo kutakuwa na tukio la utukufu, wakati “nyota ya asubuhi” – (Yesu Kristo) atakaporudi katika utukufu Wake mkuu. Siku hiyo aondoa kabisa giza nene la dhambi katika ulimwengu huu na kurejesha mwangaza/ nuru na ufalme Wake wa utukufu (soma: Mathayo 24:30; 25: 31; Tito 2:13; Ufunuo 1:7; Kol 3:4).

NIFANYE NINI BASI NA SOMO HILI?

Gundua kuwa neno la Mungu lina “pumzi ya Mungu” na limekusudiwa kutuelekeza kwa Kristo. Kristo ndiye Neno la Mungu, Kristo ndiye “Sauti ya Injili.” Omba ili Bwana ili azidi kukufunulia neno Lake. Mwamini “Neno” (Kristo Yesu), na kuchunguza maandiko Yake (lile neno la unabii) kila siku.

Yohana 5:38-40
38 Wala neno Lake hamnalo likikaa ndani yenu, kwa kuwa ninyi hammwamini Yule aliyetumwa na Yeye. 39 Mwayachunguza maandiko, kwa sababu mnadhani kwamba ninyi mna uzima wa milele ndani yake; na hayo ndiyo yanayonishuhudia. 40 Wala hamtaki kuja kwangu mpate kuwa na uzima.

SAUTI YA INJILI

[Hebu sikia sauti ya Bwana ikinena nasi tunapofunga kipindi hiki]

Waefeso 6:11,13, 17
11 Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani. 13 Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama. 17 Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni NENO LA MUNGU.

 

OMBI: Asante Bwana kwa kutupa “lile neno la unabii lililo imara zaidi”, asante kwa zawadi ya Yesu Kristo [nyota ya asubuhi] (Ufunuo 2:28); asante kwa utajiri wa Neno Lako. Asante kwa Roho Wako anayetufundisha na kutufunulia hili Neno tena na tena. Tusaidie Bwana, ili tuliangalie sana hili neno la unabii.

Hebu “Neno lako” likapate kuwa “taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu” (Zaburi 119:105). Hebu neno hili liweze kupenyeza katika mioyo yetu kama “taa ing’aayo mahali penye giza” mpaka ile asubuhi njema “kutakapopambazuka” na Nyota ya Asubuhi ataonekana juu mawinguni.

Tusaidie Bwana tuwe watii na “watendaji wa Neno, wala si wasikiaji tu, hali tukijidanganya nafsi zetu”. Tusaidie kuukataa uovu na kukuchagua Wewe daima, “kuweka mbali uchafu wote na ubaya uzidio, na kupokea kwa upole Neno lile lililopandwa ndani, liwezalo kuziokoa roho zetu.” (Yakobo 1:21-22)

Kwa neema ya Bwana, utuandae kuonana na Mfalme wetu. Tumeomba haya katika jina la Yesu Kristo, Amina.


MWISHO

Sauti Ya Injili SDA © 2017

 

Somo hili linapatikana katika:

Tovuti: tgvs.org
Facebook: Sauti Ya Injili SDA
Whats App: Sauti Ya Injili SDA
Mobile App: The Gospel’s Voice