5-29-17: Mashahidi Waliouona Utukufu

BIBLIA: “Soma, Elewa, Shuhudia”

MWONGOZO WA KUJIFUNZA BIBLIA

Robo hii: Lisha Kondoo Zangu
Kitabu: 1 Petro & 2 Petro
Somo la (10/13): Unabii na Maandiko

Fungu la Kukariri: “Nasi tuna lile neno la unabii lililo imara zaidi, ambalo, mkiliangalia, kama taa ing’aayo mahali penye giza, mwafanya vyema, mpaka kutakapopambazuka, na nyota ya asubuhi kuzuka mioyoni mwenu” (2 Petro 1:19).

 

OMBI: Baba yetu mpendwa, asante kwa nafasi nyingine ya tafakari ya Mwongozo wa kujifunza Biblia. Tunaomba Roho Wako atufundishe somo hili. Tusamehe dhambi, uovu, makosa na kasoro zetu zote. Tuandae kwa ajili ya ufalme Wako. Tunaomba haya katika Jina la Yesu Kristo, Bwana wetu, Amina!


 

MASHAHIDI WALIOUONA UTUKUFU

  • Jumatatu
    May 29, 2017

SWALI # 1: Soma 2 Petro 1:16–18. Ni shuhuda zipi zingine Petro anasema anazo kwa ajili ya imani yake kwa Yesu?

2 Petro 1:16–18
[a] Anatujulisha nguvu zake Bwana wetu Yesu Kristo
[b] Anashuhudia kuja Kwake katika mwili
[c] Aliuona ukuu Wake. (cf. 1 Yohana 1:1-3)
[d] Anathibitisha ushuhuda wa Mungu Baba kuhusu Kristo Yesu.

Kumbuka Sauti ya Mungu Baba ilisikika kama mara tatu hivi – katika maisha ya Kriso -ikimshuhudia Mwana.

Kwanza, katika Ubatizo wa Yordani; “Na tazama, sauti kutoka mbinguni ikisema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye.” (Matayo 3:17)

Pili, pale Mlimani “uso Wake ukang’aa kama jua, mavazi Yake yakawa meupe kama nuru.” (Matayo 17:1-6)

Tatu, wakati Yesu anatabiri kuhusu kifo Chake msalabani. “27 Sasa roho yangu imefadhaika; nami nisemeje? Baba, uniokoe katika saa hii? Lakini ni kwa ajili ya hayo nilivyoifikia saa hii. 28 Baba, ulitukuze jina lako. Basi ikaja sauti kutoka mbinguni, Nimelitukuza, Nami nitalitukuza tena.” (Yohana 12:27-28)

 

Zingatia Petro anachosema katika aya ya 17.

2 Petro 1:17
“17 Maana alipata kwa Mungu Baba heshima na utukufu, hapo alipoletewa sauti iliyotoka katika utukufu mkuu, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye. 18 Na sauti hiyo sisi tuliisikia ikitoka mbinguni tulipokuwa pamoja Naye katika mlima ule mtakatifu.

 

NYONGEZA: (Maelezo ya mwandishi)

  • “Kando ya neno la unabii, Petro alikuwa shahidi wa moja kwa moja wa mambo yale aliyoyahubiri. Ukristo, alisema, haukujengwa juu ya “hadithi zilizotungwa kwa werevu” (2 Petro 1:16), bali juu ya matukio halisi yaliyotukia katika historia-matukio ambayo yeye binafsi aliyashuhudia. Katika vitabu vya Injili, Petro alikuwapo kuona matukio mengi ya muhimu katika maisha na huduma ya Yesu. Alikuwapo pale wakati wa mahubiri, mafundisho, na miujiza. Tangu muujiza wa mwanzo wa samaki (Luka 5:4-6) hadi kumwona Yesu kule Galilaya baada ya kufufuka kwake (Yohana 21:15), Petro alikuwa ni shahidi wa moja kwa moja wa mambo mengi yaliyotokea.”

SWALI # 2: Katika 2 Petro 1:17, 18, ni tukio gani hasa Petro alijielekeza kwalo kuhusu yale aliyoyaona mwenyewe? Tukio lile lilikuwa na umuhimu gani wa pekee?

  • Petro anasisitiza tukio moja mahususi alilolishuhudia kwa macho: kubadilika sura kwa Yesu. Yesu alikuwa amewachukua Petro, Yakobo, na Yohana pamoja naye kwenda nao juu ya mlima ili kuomba (Luka 9:28). Wakati wakiwa kule pamoja alibadilika sura mbele ya macho yao. Uso wake uling’aa, na mavazi yake yakawa meupe kiasi cha kutia macho kiwi (Mathayo 17:2; Luka 9:29). Musa na Eliya walijiunga naye, na sauti kutoka mbinguni ilisema, “Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye” (Mathayo 17:5).
  • Petro aliona mengi sana katika muda aliokaa pamoja na Yesu; lakini bado, tukio hili linajitokeza kuwa la pekee. Linadhihirisha Yesu kuwa ni Mwana wa Mungu, kwamba maisha yake duniani yalitumika kulingana na mpango wa Mungu, na kwamba alikuwa na uhusiano maalumu sana na Baba. Hata pamoja na yote yale ambayo Petro aliyaona au angeweza kuyaona, tukio hili-ambalo lilijumuisha “sauti hiyo sisi tuliisikia ikitoka mbinguni” (2 Petro 1:18)-lilikuwa ndilo alilolilenga katika barua hii.

TAFAKARI

SWALI # 3: Fikiria ni tukio au matukio gani yamefanya mvuto wa kudumu katika maisha yako ya kiroho na imani. Kilikuwa ni kitu gani, kilikuathiri jinsi gani, na bado kinamaanisha nini leo? Kwa nini unafikiri kilikuwa na athari iliyokuwa nayo? Shiriki majibu yako katika kikosi chako siku ya Sabato.

MWISHO

Sauti Ya Injili SDA © 2017