135-001: Malaika kama watumishi wa Mungu

VITA KUU KATI YA KRISTO NA SHETANI

Sehemu ya I: Malaika, Shetani, Mapepo

Mfululizo # 135:001-044

Biblia Takatifu ndio chanzo pekee chenye mamlaka kuhusu fundisho kuhusu “Vita Kuu kati ya Kristo na Shetani.” Katika sehemu ya kwanza ya mfululizo wa masomo haya, kila siku kwa neema ya Mungu, tutajifunza kipengele fulani kinachohusiana na wahusika, yaani Malaika, Shetani, na Mapepo.

Katika sehemu ya pili – kumi tatajifunza matukio mbalimbali yahusuyo “Vita Kuu kati ya Kristo na Shetani”, tangu anguko la Shetani; Vita Kuu katika Edeni; Vita Kuu katika Agano la Kale; Vita Kuu katika Historia ya Falme; Vita Kuu katika maisha, msalaba, ufufuko wa Yesu Kristo; Vita Kuu katika Kanisa la mitume; Vita Kuu katika Historia ya Kanisa, Vita Kuu na Ukengeufu; Vita Kuu na Mapokeo, Vita Kuu na Amri za Mungu; Vita Kuu na Sabato; Vita Kuu na Karne ya 21; Vita Kuu na Siku za Mwisho, Vita Kuu na Kitabu cha Ufunuo; Vita Kuu na Marejeo ya Kristo, Vita Kuu: Ushindi Hatimaye!.


 

Sehemu ya I: Malaika, Shetani, Mapepo

Mada ya Leo: 135-001

MALAIKA KAMA WATUMISHI WA MUNGU.

OMBI: Baba yetu mpendwa, asante kwa zawadi ya neno Lako. Tunaalika Roho wako atuongoze katika tafakari ya somo hili. Tusamehe makosa, uovu, na dhambi. Tuandae kwa ajili ya ufalme wako. Tumeomba haya katika jina la Yesu Kristo-Bwana wetu, Amina.

Muhtasari wa Mawazo Makuu
(1) Uumbaji wao
(2) Wajumbe au watumishi
(3) Wana wa Mungu
(4) Watakatifu
(5) Walinzi
(6) Majeshi ya Mbinguni
(7) “Pepo, watumishi, miali ya moto”
(8) Hitimisho
(9) Sauti Ya Injili

UTANGULIZI

Malaika ni nani? Malaika ni viumbe vya kiroho (spiritual beings) vinavyomsaidia Mungu, hasa katika kazi Yake ya wokovu, kuwasilisha ujumbe wake kwa binadamu na kuhudhuria mahitaji ya watu wa Mungu.

Kimsingi malaika ni wajumbe au watumishi (Heb. malʾāḵ; Gr. ángelos) wa Mungu (k.m., Mwanzo 16:6-7; Kutoka 3:2; Hesabu 22:22 – 35). Vyeo vyao vingine ni pamoja na “wana wa Mungu” (Ayubu 1:6; Zaburi 29: 1), “Watakatifu” (k.m., Zab 89: 7; Danieli 8:13, na “walinzi” (Danieli 4:13, 17, 23). Wakati mwingine kishazi “majeshi ya mbinguni” hutumika pia kumaanisha malaika (1 Wafalme 22:19; 2 Nyakati 18:18; Zaburi 148:2; Nehemia 9:6).

UUMBAJI WAO

Maandiko matakatifu yanaanza na ukweli kuhusu uumbaji wa ulimwengu. “Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi” (Mwanzo 1:1). Ingawa maelezo ya uumbaji yanataja nafsi tatu, yaani, Mungu Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu (Mwanzo 1:2, 26), Agano Jipya linamtaja Mungu Mwana waziwazi kama Muumbaji aliyezungumza na dunia na vyote viijazavyo vikakuwepo (Ebr 1:1 – 3; Yohana 1:1 – 3, 10).

Waebrania 1:1 – 3
1 Mungu, ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi, 2 mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika Mwana, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu.

Yohana 1:1 – 3.
1 Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. 2 Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu. 3 Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika.

Yohana 1:10
Alikuwako ulimwenguni, hata kwa yeye ulimwengu ulipata kuwako, wala ulimwengu haukumtambua.
Katika mjadala huu, mtume Paulo huenda mbele zaidi, akiongelea uumbaji wa ulimwengu kwa ujumla [“cosmos”] anataja wakazi wake kama malaika na viumbe vingine vyenye akili kama vile wanadamu, kwamba wote wameumbwa kwa uwezo wa ubunifu na uumbaji wa Mungu Mwana. “16 Kwa kuwa katika yeye vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na vilivyo juu ya nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana; ikiwa ni vitu vya enzi, au usultani, au enzi, au mamlaka; vitu vyote viliumbwa kwa njia yake, na kwa ajili yake. 17 Naye amekuwako kabla ya vitu vyote, na vitu vyote hushikana katika yeye.” ( Wakolosai 1:16, 17).

Kwa hiyo, malaika wote wameumbwa na Mungu. Ni vuimbe na vinapaswa kutoa ibada kwa Mungu, kama binadamu anavyopaswa.

WAJUMBE AU WATUMISHI

“Malaika wa Bwana” alitumwa kama mjumbe na akamtokea Hagari, Musa, na watakatifu wengine katika agano la kale.

Mwanzo 16:6-7
6 Naye Abramu akamwambia Sarai, Tazama, mjakazi wako yu mkononi mwako, mtendee lililo jema machoni pako. Sarai akamtesa, naye akakimbia kutoka mbele yake. 7 Malaika wa Bwana akamwona kwenye chemchemi ya maji katika jangwa, chemchemi iliyoko katika njia ya kuendea Shuri.

Kutoka 3:2
Malaika wa Bwana akamtokea, katika mwali wa moto uliotoka katikati ya kijiti; akatazama, na kumbe! Kile kijiti kiliwaka moto, nacho kijiti hakikuteketea.

MALAIKA KAMA “WANA WA MUNGU”

Ayubu 1:6
Ilikuwa, siku moja ambayo hao wana wa Mungu walikwenda kujihudhurisha mbele za Bwana, Shetani naye akaenda kati yao.

Zaburi 29:1-2
1 Mpeni Bwana, enyi wana wa Mungu, Mpeni Bwana utukufu na nguvu; 2 Mpeni Bwana utukufu wa jina lake; Mwabuduni Bwana kwa uzuri wa utakatifu.

MALAIKA KAMA “WATAKATIFU”

Zaburi 89:5-8
5 Ee Bwana, mbingu zitayasifu maajabu yako, Uaminifu wako katika kusanyiko la watakatifu. 6 Maana ni nani katika mbingu awezaye kulinganishwa na Bwana? Ni nani afananaye na Bwana miongoni mwa malaika? 7 Mungu huogopwa sana barazani pa watakatifu, Ni wa kuhofiwa kuliko wote wanaomzunguka. 8 Bwana, Mungu wa majeshi, Ni nani aliye hodari kama Wewe, Ee YAHU? Na uaminifu wako unakuzunguka.

Danieli 8:13
Ndipo nikamsikia mtakatifu mmoja akinena, na mtakatifu mwingine akamwuliza huyo aliyenena, Haya maono katika habari ya sadaka ya kuteketezwa ya daima, na lile kosa lifanyalo ukiwa, yataendelea hata lini, kukanyagisha patakatifu na jeshi?

 

MALAIKA KAMA “WALINZI”

Danieli 4:13, 17, 23

13 Nikaona katika njozi za kichwa changu kitandani mwangu, na tazama, mlinzi, naye ni mtakatifu, alishuka kutoka mbinguni.

17 Hukumu hii imekuja kwa agizo la walinzi, na amri hii kwa neno la watakatifu; kusudi walio hai wapate kujua ya kuwa Aliye juu anatawala katika ufalme wa wanadamu, naye humpa amtakaye, tena humtawaza juu yake aliye mnyonge.

23 Tena, kwa kuwa mfalme alimwona mlinzi, naye ni mtakatifu, akishuka kutoka mbinguni, akisema, Ukateni mti huu, mkauangamize; ila kiacheni kisiki cha shina lake katika ardhi, pamoja na pingu ya chuma na shaba, katika majani mororo ya kondeni; kikatiwe maji kwa umande wa mbinguni, na sehemu yake iwe pamoja na wanyama wa kondeni, hata nyakati saba zipite juu yake.

 

MALAIKA KAMA “MAJESHI YA MBINGUNI”

1 Wafalme 22:19
Mikaya akasema, Sikia basi neno la Bwana; Nalimwona Bwana ameketi katika kiti chake cha enzi, na jeshi lote la mbinguni wamesimama upande wa mkono wake wa kuume na wa kushoto.

2 Nyakati 18:18
Mikaya akasema, Sikieni basi neno la Bwana; Nalimwona Bwana ameketi katika kiti chake cha enzi na jeshi lote la mbinguni wamesimama mkono wake wa kuume na wa kushoto.

Zaburi 148:1-2
1 Haleluya. Msifuni Bwana kutoka mbinguni; Msifuni katika mahali palipo juu. 2 Msifuni, enyi malaika wake wote; Msifuni, majeshi yake yote.

Nehemia 9:6
Ezra akasema, Wewe ndiwe Bwana, wewe peke yako; wewe ulifanya mbingu, mbingu za mbingu, pamoja na jeshi lake lote, dunia na vyote vilivyomo, bahari na vitu vyote vilivyomo, nawe unavihifadhi vitu hivi vyote; na jeshi la mbinguni lakusujudu wewe.

 

MALAIKA KAMA “PEPO, WATUMISHI, MIALI YA MOTO”

Waebrania 1:7
Na kwa habari za malaika asema, “Afanyaye malaika Zake kuwa pepo, na watumishi Wake kuwa miali ya moto.”

Dondoo hii (Ebr 1:7) imetolewa katika Zaburi 104:4

Zaburi 104:4
“Huwafanya malaika zake kuwa pepo, Na watumishi wake kuwa moto wa miali.”
“MIALI YA MOTO.”
Malaika ni kama ‘miali ya moto” katika utendaji wa kazi yao. Wanao uwezo wa kuangamiza kabisa. Kishazi hiki kinalandana na kazi waliopewa Makerubi katika bustani ya Edeni, baada ya dhambi kuingia.

Mwanzo 3:24.
23 Kwa hiyo Bwana Mungu akamtoa katika bustani ya Edeni, ailime ardhi ambayo katika hiyo alitwaliwa. 24 Basi akamfukuza huyo mtu, akaweka Makerubi, upande wa mashariki wa bustani ya Edeni, na upanga wa moto uliogeuka huko na huko, kuilinda njia ya mti wa uzima.

PEPO; SPIRITS (NKJV)
Katika lugha asilia neno hili pepo = [ Πνεῦμα (pneuma)] limetumika katika aya mbalimbali katika agano jipya likimaanisha mambo yafuatayo:

(1) Roho Mtakatifu (Marko 1:12);
(2) Roho, kiumbe kisicho na mwili (Yohana 4:24; Matendo 23:8);
(3) Pepo – “Evil spirit” (Matayo 8:16);
(4) Roho – “Ghost” (Luka 24:37, 39);
(5) Utu wa ndani, unaoweza kujibu/ kuwajibika kwa Mungu (Matendo 17:16; Efe 5:9)
(6) Upepo (Yohana 3:8)
(7) Pumzi (2 Thesalonike 2:8)

Kwa lugha rahisi Malaika ni “pepo” = “spirits” (NKJV), kwa sababu hawana nyama na damu, kama binadamu. Malaika ni roho.

Aya hii inatufundisha kuwa Yesu ni bora kuliko malaika kwa sababu ya asili Yake. Katika Waebrania 1:7 Roho Mtakatifu anaonyesha tofauti kuu iliopo kati ya asili ya malaika na ya Mwana (Yesu Kristo). Neno la kigiriki “kufanya” ni poieō (“kuumba/ kuunda” au “kufanya”). Kwa sababu Kristo ndiye aliyeumba malaika, (kulingana na Wakolosai 1:16), ni dhahiri kwamba Yeye ni bora katika cheo, madaraka, kuliko malaika. Si tu kwamba waliumbwa na Yeye, lakini pia, malaika ni milki Yake, ni malaika Wake. Wao ni watumishi wake walioumbwa, ni watumishi Wake, mawaziri wake, ni “watumishi wake kuwa miali ya moto.”


HITIMISHO

Malaika ni watumishi ambao kufurahia kufanya mapenzi ya Mungu. Tangu mwanzo wana sehemu maalum katika mpango wa Mungu na wamehudumu katika nyadhifa nyingi. Baada ya mwanadamu kuanguka dhambini malaika walilinda njia ya mti wa uzima (Mwanzo 3:24). Wakati wa marejeo ya kristo, malaika watakuja pamoja naye, “Hapo atakapokuja Mwana wa Adamu katika utukufu wake, na malaika watakatifu wote pamoja naye, ndipo atakapoketi katika kiti cha utukufu wake” (Mathayo 25: 31), na Kristo atawatuma ” malaika Zake pamoja na sauti kuu ya parapanda, nao watawakusanya wateule Wake toka pepo nne, toka mwisho huu wa mbingu mpaka mwisho huu” (Mathayo 24:31).

Tangu kuumbwa kwa ulimwengu huu, malaika watakatifu wamekuwa walinzi, na watumishi “watumikao, wakitumwa kuwahudumu wale watakaourithi wokovu ” (Waebrania 1:14).

Malaika walionekana mara kwa mara katika huduma ya Kristo duniani, toka tangazo la kwanza la kuzaliwa Kwake hadi wakati wa kupaa Kwake. Ingawa hatuwezi kuwaona maika kwa macho yetu ya kimwili, tunapaswa kuwa na ufahamu wa uwepo wao mara kwa mara katika maisha yetu, tunaweza kujua kwa hakika kwamba daima sisi tu chini ya utunzaji wao upendo.

TUFANYE NINI BASI NA SOMO LA LEO?

Mshukuru Bwana kwa ulinzi wa malaika zake

Zaburi 34:7-9
7 Malaika wa Bwana hufanya kituo, Akiwazungukia wamchao na kuwaokoa.
8 Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu mwema; Heri mtu yule anayemtumaini.
9 Mcheni Bwana, enyi watakatifu wake, Yaani, wamchao hawahitaji kitu.

 

SAUTI YA INJILI

Zaburi 103:20-21
20 Mhimidini Bwana, enyi malaika zake, Ninyi mlio hodari, mtendao neno lake, Mkiisikiliza sauti ya neno lake. 21 Mhimidini Bwana, enyi majeshi yake yote, Ninyi watumishi wake mfanyao mapenzi yake.

MWISHO.


Sauti Ya Injili SDA © 2017

Mfululizo wa masomo haya yanapatikana katika:
(1) Tovuti: www.tgvs.org
(2) Facebook: Sauti Ya Injili SDA
(3) Whats App: Sauti Ya Injili SDA
(4) Mobile App: The Gospel’s Voice