23-011: Chipukizi katika shina la Yese.

BIBLIA: “Soma, Elewa, Shuhudia”

BIBLIA SURA KWA SURA

23-011: Isaya 11
CHIPUKIZI KATIKA SHINA LA YESE

OMBI: Baba yetu wa Mbinguni tunakushukuru kwa zawadi nyingine ya uhai. Leo tunapofungua Neno Lako, tunasihi mwongozo wa Roho Wako. Baba, tusamehe, tusafishe, na kutuandaa kwa ajili ya marejeo Yako. Hebu sura hii ikapate kuwa mbaraka kwetu sote. Tunakushukuru na twaja katika Jina la Kristo, aliye Bwana na Mwokozi wetu, Amina.


MUHTASARI WA SURA

[1] Wahusika:
(a) Masihi, Israeli, Yuda,
(b) Waliosalia – (Remnant of Israel)

[2] Tabia ya Mungu: Haki, Uaminifu, Huruma
[3] Vitu katika Biblia: (Wanyama)
(a) Mbwa-mwitu
(b) Mwana-kondoo
(c) Chui
(d) Mwana-mbuzi;
(e) Ndama na mwana-simba.
(f) Ng’ombe na Dubu
(g) Simba
(h) Mtoto (watoto)

[4] Maneno/ vishazi katika Biblia:
“Mlima wangu wote mtakatifu”

[5] Maeneo katika Biblia: (11:11)
(a) Ashuru, Misri, Pathrosi, Kushi, Elamu, Shinari, Hamathi,
(b) Misri,
(c) Bahari ya Misri
(d) Mto Frati (Euphrates)
(e) Mesopotamia (11:11,16) “Itakuwako njia kuu”

[6] Matukio katika Biblia: (Hakuna)
[7] Fungu Kuu: Isaya 11:1
[8] Msisitizo: Hukumu ya Mungu


MUHTASARI WA MAWAZO MAKUU:
(1) Utu wa Masihi (Utangulizi)
(2) Asili Yake (11:1)
(3) Upako Wake (11:2)
(4) Furaha Yake (11:3a)
(5) Utawala Wake (11:3b-5)
(6) Mafanikio Yake (11:6-16)
(7) Maswali Muhimu
(8) Tufanye Nini Basi?
(9) Sauti Ya Injili


UTANGULIZI
Katika mlango wa 11-12, Isaya anaelezea Mfalme ajaye na ufalme wake na anaandika wimbo wa wokovu wa Israeli. Wimbo huu umegawanywa katika sehemu kuu mbili: Utu wa Masihi (Isaya 11:1-16); na Sifa kwa Masihi (Isaya 12:1-6).

ASILI YAKE (11:1)
Masihi atakuja kutoka ukoo wa Daudi.

Isaya 11:1
Basi litatoka chipukizi katika shina la Yese, na tawi litakalotoka katika mizizi yake litazaa matunda.

UPAKO WAKE (11:2).
Isaya 11:2
Na roho ya Bwana atakaa juu Yake, roho ya hekima na ufahamu, roho ya shauri na uweza, roho ya maarifa na ya kumcha Bwana.

FURAHA YAKE (11:3a).
Isaya 11:3a
Na furaha yake itakuwa katika kumcha Bwana.

UTAWALA WAKE (11:3-5)
Utawala wake utakuwa haki.

Isaya 11:3b-5
Wala hatahukumu kwa kuyafuata ayaonayo kwa macho Yake, wala hataonya kwa kuyafuata ayasikiayo kwa masikio Yake; 4 bali kwa haki atawahukumu maskini, Naye atawaonya wanyenyekevu wa dunia kwa adili; Naye ataipiga dunia kwa fimbo ya kinywa Chake, na kwa pumzi ya midomo Yake atawaua wabaya. 5 Na haki itakuwa mshipi wa viuno vyake, na uaminifu mshipi wa kujifungia.

MAFANIKIO YAKE (11:6-16)
(1) Amani kati ya viumbe vyake
(2) Utukufu wa mlima wake mtakatifu
(3) Dunia itajawa na kumjua Bwana
(4) Mataifa watamtafuta
(5) Mahali pake pa kupumzikia patakuwa na utukufu.
(6) Ajipatie watu wake watakaosalia
(7) Atawakutanisha watu wa israeli waliotupwa
(8) Atawakusanya watu wa yuda waliotawanyika
(9) Wivu kati ya Israeli na Yuda utafikia mwisho.
(10) Hawa wataungana pamoja ili kupigana dhidi ya maadui zao.
(11) Bwana atajenga barabara ya amani kutoka bahari ya Shamu kwa Mto Frati
Isaya 11:6-8
6 Mbwa-mwitu atakaa pamoja na mwana-kondoo, na chui atalala pamoja na mwana-mbuzi; ndama na mwana-simba na kinono watakuwa pamoja, na mtoto mdogo atawaongoza. 7 Ng’ombe na dubu watalisha pamoja; watoto wao watalala pamoja; na simba atakula majani kama ng’ombe. 8 Na mtoto anyonyaye atacheza penye tundu la nyoka, na mtoto aliyeachishwa atatia mkono wake katika pango la fira.

Isaya 11:9-10
9 Hawatadhuru wala hawataharibu katika mlima wangu wote mtakatifu; maana dunia itajawa na kumjua Bwana, kama vile maji yanavyoifunika bahari. 10 Na itakuwa katika siku hiyo, shina la Yese lisimamalo kuwa ishara kwa kabila za watu, Yeye ndiye ambaye mataifa watamtafuta; na mahali pake pa kupumzikia patakuwa na utukufu.

Isaya 11:11-14
11 Na itakuwa katika siku hiyo, Bwana atapeleka mkono Wake mara ya pili, ili ajipatie watu wake watakaosalia, kutoka Ashuru, na kutoka Misri, na kutoka Pathrosi, na kutoka Kushi, na kutoka Elamu, na kutoka Shinari, na kutoka Hamathi, na kutoka visiwa vya bahari. 12 Naye atawatwekea mataifa bendera, atawakutanisha watu wa Israeli waliotupwa, atawakusanya watu wa Yuda waliotawanyika, kutoka ncha nne za dunia. 13 Na wivu wa Efraimu utaondoka, na wale wanaomwudhi Yuda watakatiliwa mbali; Efraimu hatamhusudu Yuda, wala Yuda hatamwudhi Efraimu. 14 Nao watashuka, watalirukia bega la Wafilisti upande wa magharibi; nao pamoja watawateka wana wa mashariki; watanyosha mkono juu ya Edomu na Moabu; na wana wa Amoni watawatii. 15 Na Bwana atauangamiza kabisa ulimi wa bahari ya Misri; na kwa upepo wake uteketezao atatikisa mkono wake juu ya Mto, naye ataupiga, uwe vijito saba, na kuwavusha watu wenye viatu vikavu. 16 Itakuwako njia kuu kwa mabaki ya watu wake watakaobaki, watokao Ashuru, kama vile ilivyokuwako kwa Israeli, katika siku ile waliyotoka katika nchi ya Misri.


 

MASWALI MUHIMU KATIKA SURA HII
{Pitia majibu yaliyowekwa hapo chini}

Je, fundisho kuu ni nini hasa katika sura hii?
Je, kuna dhambi ya kuepukwa/ kutubu hapa?
Je, kuna mtazamo wa kuigwa hapa?
Je, kuna agizo au wajibu wa kufanya hapa?
Je, sura hii inatufundisha nini kuhusu Mungu?
Je, kuna dua/ ombi lolote la kuombwa hapa?
Je, kuna ahadi yoyote kwa ajili yangu hapa?
Je, sura hii ina umuhimu gani katika mpango wa wokovu wetu?


FUNDISHO KUU KATIKA SURA HII

Isaya 11:1
“Basi litatoka chipukizi katika shina la Yese, na tawi litakalotoka katika mizizi yake litazaa matunda.”

YESE: Alikuwa baba yake Daudi. Kupitia ukoo wake (mfalme Daudi) siku moja Mfalme aliye masihi angezaliwa (cf. Ruthu 4:22; 1 Samweli 16:1, 12, 13).

CHIPUKIZI: Hii ni moja ya cheo cha Masihi (Isaya 4:2).

TAWI: Sura iliyotangulia inatoa picha ya hukumu zinazohusisha Assyria na Yuda. Matawi na miti mizuri ya kushamiri ya Yuda yangekatwa kwa sababu ya uovu. Picha hii inafanana na ile ya Danieli 4:10 – 26, ambapo Nebukadreza na ufalme wake unafananishwa na mti uliokatwa kwa hukumu ya Mungu, ikiacha tu kisiki cha mti.

Toka kuanzishwa kwake, Bwana alikuwa na mipango mikubwa sana kwa taifa la Israeli. Ilikuwa kusudi Lake kwamba taifa hili liwe “mjumbe” wa nuru na ukweli kwa ulimwengu, na kwamba ushawishi wake ungeendelea kukua ulimwenguni kote hadi kuleta maisha na amani kwa watu wote. Lakini kwa sababu ya kutotii taifa lilinyenyekezwa na kuchukuliwa mateka.

Hata hivyo, kupitia uzao wa Daudi, Mfalme angetokea na kutimiza kile ambacho Daudi na warithi wake kwenye kiti cha enzi cha Yuda walishindwa kutimiza. Wakati ambapo taifa lilikatwa, na kisiki tu kilibakia, kama ilivyokuwa, kungetokea “mche mwororo,” na “mzizi katika nchi kavu” (Isaya 53:2) – ambao ungesitawi, ungenawiri na kupendeza sana.

Isaya 4:2
Siku hiyo chipukizi la Bwana litakuwa zuri, lenye utukufu, na matunda ya nchi yatakuwa mema sana, na kupendeza, kwa ajili ya Waisraeli wale waliookoka.

Ufunuo 5:5a-b
Na mmojawapo wa wale wazee akaniambia, Usilie; tazama, Simba aliye wa kabila ya Yuda, Shina la Daudi

Ufunuo 22:16
Mimi Yesu nimemtuma malaika wangu kuwashuhudia ninyi mambo hayo katika makanisa. Mimi ndimi niliye Shina na Mzao wa Daudi, ile nyota yenye kung’aa ya asubuhi.


DHAMBI YA KUEPUKWA
“Uasi.” Hebu tujikumbushe tulichosoma kuhusu muhtasari wa dhambi ya Yuda katika Isaya 1.

Isaya 1:4 Ole wake:-
(a) Taifa lenye dhambi,
(b) Watu wanaochukua mzigo wa uovu,
(c) Wazao wa watenda mabaya,
(d) Watoto wanaoharibu;
(e) Wamemwacha Bwana,
(f) Wamemdharau yeye aliye Mtakatifu wa Israeli,
(g) Wamefarakana naye na kurudi nyuma.


 

MTAZAMO WA KUIGWA (11:2)
Hebu tuige Tabia ya Kristo Yesu.

Tumuombe Bwana ili atupatie Roho wake.
(1) Roho Mtakatifu akae juu yetu,
(2) Tuwe na “roho ya hekima na ufahamu”
(3) Tuwe na “roho ya shauri na uweza,”
(4) Tuwe na “roho ya maarifa”
(5) Tuwe na “roho ya kumcha Bwana”


 

AGIZO AU WAJIBU WA KUFANYA KATIKA SURA HII

Tunapaswa kuwatetea wanyonge, na kuhukumu kwa haki kama Kristo alivyohukumu.

Isaya 11:4 a-b
“Bali kwa haki atawahukumu maskini, Naye atawaonya wanyenyekevu wa dunia kwa adili.”

SWALI: Kwa nini aya hii inamzunguzia tabia ya Masihi ya kuhukumu maskini kwa haki?

Waamuzi walikuwa mafisadi, waliwadhulumu maskini na wasiojiweza, matajiri walikuwa wanajitajirisha chini ya wajane na yatima

Isaya 1:23
Wakuu wako ni waasi, na rafiki za wevi; kila mtu hupenda rushwa, hufuata malipo; hawampatii yatima haki yake, wala maneno ya mjane hayawawasilii.

(Soma pia: Isaya 10:1, 2; Yer 5:28; Amosi 2:6; 4:1; 5:10, 11; 8:4 – 6; Zech. 7:10).

Masihi ajaye angehukumu kwa haki, usawa, rehema, na kuzingatia mahitaji ya maskini na wanaonyanyaswa – zingekuwa kanuni za kudumu zinazoongoza ufalme wa Masihi ajaye (cf. Zab 72:2, 3).

Zab 72:2, 3
2 Atawaamua watu wako kwa haki, Na watu wako walioonewa kwa hukumu. 3 Milima itawazalia watu amani, Na vilima navyo kwa haki.


 

JE, SURA HII INATUFUNDISHA NINI KUHUSU MUNGU?

Mungu ni mwaminifu katika kutimiza ahadi zake zote.

Angalia utabiri wa Masihi katika kitabu cha Isaya 11:1 na jinsi kila utabiri ulivyotimia katika utu wa Kristo Yesu. Zingatia mafungu yafuatayo:

“Basi litatoka chipukizi katika shina la Yese, na tawi litakalotoka katika mizizi yake litazaa matunda.” (Isaya 11:1)

[A] Basi Litatoka Chipukizi
Isaya 53:2; Zakaria 6:12; Ufunuo 5:5; 22:16.

[B] Tawi
Isaya 4:2; Zaburi 80:15, 17; Yeremia 23:5, 6; 33:15; Zakaria 3:8; 6:12, 13

[C] Mizizi Yake
Yohana 1:1, 14; Warumi 15:12; Wakolosai 1:17.


 

JE, KUNA DUA/ OMBI LOLOTE LA KUOMBWA HAPA?

Ee Bwana nisamehe makosa, uovu na dhambi zangu ili siku moja nikapate kuingia katika mlima wako mtakatifu. Mahali ambapo wanyama wakali “hawatadhuru wala hawataharibu….”; maana “dunia itajawa na kumjua Bwana, kama vile maji yanavyoifunika bahari” [Isaya 11:9], Amen.


AHADI ZA BWANA KATIKA SURA HII

Katika ufalme wa Masihi (Mbingu mpya na Nchi mpya) kutakuwa na mabadiliko katika mahusiano kati ya wanyama na wanadamu (watakatifu watakao okolewa). Umwagaji damu na ukatili wa wanyama wakali hautakuwepo tena. Hisia ya msingi ya ulimwengu wa wanyama itabadilishwa kabisa. Sheria ya ufalme wa Mungu itakuwa sheria ya uzima na mapendo. “Wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu hayatakuwapo tena; kwa kuwa mambo ya kwanza yamekwisha kupita.” (Ufunuo 21:4b)

Zingatia ahadi za Bwana katika sura hii:

Isaya 11:6-8.
(1) Mbwa-mwitu atakaa pamoja na mwana-kondoo,
(2) Chui atalala pamoja na mwana-mbuzi;
(3) Ndama na mwana-simba
(4) Na kinono watakuwa pamoja,
(5) Na mtoto mdogo atawaongoza.
(6) Ng’ombe na dubu watalisha pamoja;
(7) Watoto wao watalala pamoja;
(8) Simba atakula majani kama ng’ombe.
(9) Mtoto anyonyaye atacheza penye tundu la nyoka
(10) Mtoto aliyeachishwa atatia mkono wake katika pango la fira.

Isaya 11:9
Hawatadhuru wala hawataharibu katika mlima Wangu wote mtakatifu; maana dunia itajawa na kumjua Bwana, kama vile maji yanavyoifunika bahari.

Habakuki 2:14
Kwa maana dunia itajazwa maarifa ya utukufu wa Bwana, kama maji yaifunikavyo bahari.


 

JE, SURA HII INA UMUHIMU GANI KATIKA MPANGO WA WOKOVU WETU?

Hapa Isaya anatupatia picha Masihi anayerudi duniani kwa kusudi la kuwaangamiza maadui wake na kuuchukua ufalme wake. Zingatia ya tatu ya aya ya nne (11:4) “Naye ataipiga dunia kwa fimbo ya kinywa chake, na kwa pumzi ya midomo Yake atawaua wabaya.”
Mada kuu katika aya hii ni Hukumu ya Yesu Kristo. Kwa mfano katika Ufunuo 12:5, maandiko yanamuongelea Masihi yakisema: “Yeye (Masihi) atakayewachunga mataifa yote kwa fimbo ya chuma”. Siku moja Masihi angehukumu kwa “fimbo ya chuma”. Angalia pia aya zifuatazo:

Dan 2:44
Na katika siku za wafalme hao Mungu wa mbinguni atausimamisha ufalme ambao hautaangamizwa milele, wala watu wengine hawataachiwa enzi yake; bali utavunja falme hizi zote vipande vipande na kuziharibu, nao utasimama milele na milele.

Ufunuo 19:11-16
11 Kisha nikaziona mbingu zimefunuka, na tazama, farasi mweupe, na yeye aliyempanda, aitwaye Mwaminifu na Wa-kweli, naye kwa haki ahukumu na kufanya vita. 12 Na macho yake yalikuwa kama mwali wa moto, na juu ya kichwa chake vilemba vingi; naye ana jina lililoandikwa, asilolijua mtu ila Yeye mwenyewe. 13 Naye amevikwa vazi lililochovywa katika damu, na jina lake aitwa, Neno la Mungu. 14 Na majeshi yaliyo mbinguni wakamfuata, wamepanda farasi weupe na kuvikwa kitani nzuri, nyeupe, safi. 15 Na upanga mkali hutoka kinywani mwake ili awapige mataifa kwa huo. Naye atawachunga kwa fimbo ya chuma, naye anakanyaga shinikizo la mvinyo ya ghadhabu ya hasira ya Mungu Mwenyezi. 16 Naye ana jina limeandikwa katika vazi lake na paja lake, MFALME WA WAFALME, na BWANA WA MABWANA.


 

TUFANYE NINI BASI NA SURA HII?

1 Petro 4:5
Nao watatoa hesabu kwake Yeye aliye tayari kuwahukumu walio hai na waliokufa.

HITIMISHO
“Chipukizi katika shina la Yese”, ni Masihi –YESU KRISTO. Tumeona kwa ufupi sana utabiri huu ulivyotimizwa katika Kristo. Katika ujio wake wa kwanza, alikuja kama “mche mwororo, na kama mzizi katika nchi kavu”; lakini katika ujio Wake wa pili atakuja kama “MFALME WA WAFALME, na BWANA WA MABWANA”. Anakuja kama Hakimu, “naye kwa haki ahukumu na kufanya vita”; Na “upanga mkali hutoka kinywani mwake” utawapiga mataifa – Hao wasiomtii. Ingekuwa heri kwetu tukimtii leo na kujinyenyekeza Kwake ili atakaporudi tena, turuhusiwe kuingia katika ufalame wake, Amina.
SAUTI YA INJILI
{Hebu sikia sauti ya Bwana ikinena nasi tunapofunga kipindi hiki}

Mathayo 16:27
Kwa sababu Mwana wa Adamu atakuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika zake; ndipo atakapomlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake.

2 Wakorintho 5:10
Kwa maana imetupasa sisi sote kudhihirishwa mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ili kila mtu apokee ijara ya mambo aliyotenda kwa mwili, kadiri alivyotenda, kwamba ni mema au mabaya.


MWISHO

Sauti Ya Injili SDA © 2017