23-009: Galilaya ya Mataifa.

BIBLIA: “Soma, Elewa, Shuhudia”

USOMAJI WA BIBLIA KWA MPANGO
http://tgvs.org/archives/2778

Jamii: Biblia Sura kwa Sura
Mfululizo: Kitabu cha Isaya
Somo la leo: Isaya 9A.

Wapendwa sura hii ina mambo mengi sana, kwa hiyo tutaigawa katika sehemumbili A-B.

OMBI: Baba yetu mpendwa, asante kwa nafasi nyingine ya tafakari ya Biblia sura kwa sura. Tunaomba Roho Wako atufundishe somo hili. Tusamehe dhambi, uovu, makosa na kasoro zetu zote. Tuandae kwa ajili ya ufalme Wako. Tunaomba haya katika Jina la Yesu Kristo, Bwana wetu, Amina!

KWA AJILI YETU MTOTO AMEZALIWA

Kitabu cha Isaya kinamejazwa na utabiri yapata 111. Mafungu mengi yanaashiria matukio yatakayotokea baadaye: siku, miaka, na karne nyingi sana za mbeleni. Kwa mfano, utabiri wa Masihi ajaye unaorodheshwa katika aya zifuatazo:

(1) Masihi & mlima wa Bwana (2:2-4).
(2) Masihi: Tawi tukufu (4:2-6).
(3) Kuzaliwa kwa Masihi – “Immanueli” (7:13-14).
(4) Mapambazuko ya siku mpya (9:1-7).
(5) Ukombozi na ushindi wa Masihi (Isa 9:3-5)
(6) Utukufu wa Masihi mtawala (Isa 9:6)
(7) Chipukizi katika shina la Yese (11:1-10).
(8) Uongofu wa Mataifa (19:18-25).
(9) Karamu ya Mwanakondoo (25: 6-8; 26:19).
(10) Huduma ya Masihi (42:1-4).
(11) Mtumishi kama nuru kwa mataifa (49:1-13).
(12) Utii wa hiari wa Mtumishi (50:4-11).
(13) Kafara, ukombozi wa mafanikio ya Mtumishi (52-53)
(14) Yerusalemu mpya (54:9-13; 60:19-22).
(15) Ahadi zilizofanywa kwa Daudi kutimizwa (55:1-5).
(16) Mataifa waliongoka kuwa viongozi wa ibada (66: 19-23).
(17) Mbingu mpya na Nchi mpya (65: 17-25)
MATUMAINI YA ISRAELI.
[Sehemu ya Kwanza] Isaya 9:1-7. Zingatia maswali na majibu yaliyotolewa hapo chini.

Muhtasari wa Mawazo Makuu
(1) Nchi ya Zabuloni na nchi ya Naftali
(2) Nuru Kuu,… Nuru Imewaangaza
(3) Furaha ya ukombozi na Ushindi wa Masihi
(4) Muujiza wa Mtoto ajaye
(5) Majina ya Mtoto ajaye
(6) Utukufu wa Utawala wa Mfalme ajaye
(7) Hitimisho
(8) Sauti Ya Injili
[1] Kwa nini katika ufunguzi wa sura hii, nabii Isaya anataja “nchi ya Zabuloni na nchi ya Naftali?”

Isaya 9:1
Lakini yeye aliyekuwa katika dhiki hatakosa changamko. Hapo kwanza aliiingiza nchi ya Zabuloni na nchi ya Naftali katika hali ya kudharauliwa, lakini zamani za mwisho ameifanya kuwa tukufu, karibu na njia ya bahari; ng’ambo ya Yordani, Galilaya ya mataifa.

Zabuloni na Naftali [katika mpaka wa Kaskazini katika kaskazini mashariki mwa Galilaya, magharibi ya mto Yordani] walikuwa watu wa kwanza kuteseka kutokaa na uvamizi wa mfalme wa Ashuru (2 Wafalme 15:29). Huu ndio ulikuwa mwanzo wa “siku za giza” kwa taifa la Israeli.

2 Wafalme 15:29
“Katika siku za Peka mfalme wa Israeli akaja Tiglath-pileseri mfalme wa Ashuru, akatwaa Iyoni, na Abel-beth-maaka, na Yanoa, na Kedeshi, na Hazori, na Gileadi, na Galilaya, nchi yote ya Naftali; akawahamisha hao watu mpaka Ashuru.”

Mathayo 4:13-16 ananukuu utimilifu wa aya hii katika huduma ya Yesu katika Galilaya.

Mathayo 4:13-16
13 Akatoka Nazareti, akaja akakaa Kapernaumu, mji ulioko pwani, mipakani mwa Zabuloni na Naftali; 14 ili litimie neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, “15 Nchi ya Zabuloni na nchi ya Naftali, Njia ya bahari, ng’ambo ya Yordani, Galilaya ya mataifa, 16 Watu wale waliokaa katika giza Wameona mwanga mkuu, Nao waliokaa katika nchi na uvuli wa mauti Mwanga umewazukia.”
[2] Nuru kwa makabila ya Kaskazini: “Nuru Kuu,… Nuru Imewaangaza” (9:2)

Isaya 9:2
Watu wale waliokwenda katika giza Wameona nuru kuu; Wale waliokaa katika nchi ya uvuli wa mauti, Nuru imewaangaza.”

Ujio wa Masihi hapa unalinganishwa na ujio wa nuru iondoayo giza la dhambi na utumwa.

Angalia aya zifuatazo:

Isaya 42:16
Nitawaleta vipofu kwa njia wasiyoijua; katika mapito wasiyoyajua nitawaongoza; nitafanya giza kuwa nuru mbele yao; na mahali palipopotoka kuwa pamenyoka. Haya nitayatenda, wala sitawaacha.

Isaya 49:6
Naam, asema hivi, Ni neno dogo sana wewe kuwa mtumishi wangu ili kuziinua kabila za Yakobo, na kuwarejeza watu wa Israeli waliohifadhiwa; zaidi ya hayo nitakutoa uwe nuru ya mataifa, upate kuwa wokovu wangu hata miisho ya dunia.

Isaya 58:8
Ndipo nuru yako itakapopambazuka kama asubuhi, na afya yako itatokea mara; na haki yako itakutangulia; utukufu wa Bwana utakufuata nyuma ukulinde.

Isaya 60:1-2
1 Ondoka, uangaze; kwa kuwa nuru yako imekuja, Na utukufu wa Bwana umekuzukia. 2 Maana, tazama, giza litaifunika dunia, Na giza kuu litazifunika kabila za watu; Bali Bwana atakuzukia wewe, Na utukufu wake utaonekana juu yako.
Isaya 60:19-20
19 Jua halitakuwa nuru yako tena wakati wa mchana, Wala mwezi hautakupa nuru kwa mwangaza wake; Bali Bwana atakuwa nuru ya milele kwako, Na Mungu wako atakuwa utukufu wako. 20 Jua lako halitashuka tena, Wala mwezi wako hautajitenga; Kwa kuwa Bwana mwenyewe atakuwa nuru yako ya milele; Na siku za kuomboleza kwako zitakoma.

FURAHA YA UKOMBOZI NA USHINDI WA MASIHI

[3] Je, Bwana angefanya nini kwa Taifa la Israeli? Je, ujio wa Masihi ungewafaidishaje?

Isaya 9:3-5
3 Umeliongeza taifa, umezidisha furaha yao; Wanafurahi mbele zako, Kama furaha ya wakati wa mavuno, Kama watu wafurahivyo wagawanyapo nyara. 4 Kwa maana umeivunja nira ya mzigo wake, na gongo la bega lake, na fimbo yake yeye aliyemwonea, kama katika siku ya Midiani. 5 Maana silaha zote za mtu mwenye silaha wakati wa mshindo, na mavazi yaliyofingirishwa katika damu, yatakuwa tayari kuteketezwa, yatakuwa kuni za kutiwa motoni.

Hatimaye Bwana atawafungua Israeli na kuwaweka kutoka katika utumwa wa Ashuru, Babeli, na kila nguvu za kigeni na dhuluma na manyanyaso yao kwake.
MUUJIZA WA MTOTO AJAYE

Kuzaliwa kwa Mtoto (9:6a): picha ya udhalilishaji Wake
Ofisi ya Mtoto (9:6b): picha ya kuinuliwa Kwake

[4] Nabii Isaya alisema nini kuhusu Kuzaliwa kwa Mtoto (Masihi)? Je, utabiri huu ulitimia vipi katika Agano Jipya?

Isaya 9:6a-b
Maana kwa ajili yetu Mtoto amezaliwa, Tumepewa Mtoto mwanamume

Hapa tunagundua kuwa masihi angekuwa “Mtoto mwanamume”, linganisha aya zifuatazo:

Isaya 7:14 (Imanueli)
Kwa hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara. Tazama, bikira atachukua mimba, atazaa mtoto mwanamume, naye atamwita jina lake Imanueli.

Matayo 1:23 (Mungu pamoja nasi)
Tazama, bikira atachukua mimba, Naye atazaa mwana; Nao watamwita jina lake Imanueli; Yaani, Mungu pamoja nasi.

Luka 2:10-11 (ndiye Kristo Bwana)
10 Malaika akawaambia, Msiogope; kwa kuwa mimi ninawaletea habari njema ya furaha kuu itakayokuwa kwa watu wote; 11 maana leo katika mji wa Daudi amezaliwa, kwa ajili yenu, Mwokozi, ndiye Kristo Bwana.

Luka 1:35 (Mwana wa Mungu)
Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu.
[5] Nabii Isaya alisema nini kuhusu ofisi ya Mtoto (Masihi) ajaye?

Isaya 9:6c
“Na uweza wa kifalme utakuwa begani Mwake”

Zaburi 2:6-12; Zaburi 110:1-4, Yeremia 23:5, 6; Matayo 28:18; Luka 22:29; 1 Wakorintho 15:25; Ufunuo 1:6; 2:27; 19:16.

MAJINA YA MTOTO AJAYE

Isaya 9:6c-g
Naye ataitwa jina Lake, Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme wa amani.

[6] Je, majina haya yanayotajwa katika Isaya 9:6c-g yana maana gani? Je yanatufundisha nini?

{6a} Mshauri wa ajabu (9:6c)

Kristo ni Mshauri wa ajabu. Ukienda Kwake utapata ushauri wa kuaminika, ushauri bora. Lakini zaidi, kishazi hiki kina maana ya “wonder” = jambo fulani la mshangao, kitu fulani kilichoshinda watu kusimulia, au kujua mapana na marefu yake.

Zingatia na linganisha aya zifuatazo:

Isaya 28:29 (shauri la ajabu)
Hayo nayo yatoka kwa Bwana wa majeshi, mwenye shauri la ajabu, apitaye wote kwa hekima Yake.
Waamuzi 13:18 (Jina la ajabu)
Huyo malaika wa Bwana akamwambia, Kwani wewe kuniuliza jina langu, kwa kuwa jina hilo ni la ajabu?

Matayo 21:15 (Maajabu aliyoyafanya)
Lakini wakuu wa makuhani na waandishi walipoyaona maajabu aliyoyafanya, na watoto waliopaza sauti zao hekaluni, wakisema, Hosana, Mwana wa Daudi! Walikasirika

Matendo 2:22 (Miujiza, ajabu, ishara)
Enyi waume wa Israeli, sikilizeni maneno haya: Yesu wa Nazareti, mtu aliyedhihirishwa kwenu na Mungu kwa miujiza na ajabu na ishara, ambazo Mungu alizifanya kwa mkono wake kati yenu, kama ninyi wenyewe mnavyojua;

{6b} Mungu Mwenye Nguvu (9:6 d)

Kishazi hiki kinatuelekeza katika uwezo wa Mungu. Mungu ndiye mpiganaji mkuu, Masihi ajaye angeweza kukamilisha zoezi la kijeshi lililotajwa katika Isaya 9:3-5. Biblia ina mengi ya kusema kuhusu uwezo, nguvu, na ukuu wa Mungu – hilo ni somo lingine. Lakini linganisha aya zifutazo, ili kuelewa vizuri zaidi.

Isaya 10:21
Mabaki, nao ni mabaki ya Yakobo, watamrudia Mungu, aliye mwenye nguvu

Torati 10:17
Kwa maana Bwana, Mungu wenu, Yeye ndiye Mungu wa miungu, na Bwana wa mabwana, Mungu mkuu, mwenye kuogofya, asiyependelea nyuso za watu, wala hakubali rushwa.

Nehemia 9:32a
Basi sasa, Ee Mungu, mkuu, mwenye uweza, Mungu wa kuogofya,

 

{6c} Baba wa milele (9:6e)

Masihi atakuwa Baba kwa watu Wake milele zote. Kama mfalme, Yeye atawahurumia, atawatunza na kuwaadhibu watoto Wake. Wapendwa hii ni tabia ya Mungu, na twapaswa kukumbuka kuwa Kristo Yesu (Masihi) ni Mungu.

Isaya 40:11
Atalilisha kundi lake kama mchungaji, Atawakusanya wana-kondoo mikononi mwake; Na kuwachukua kifuani mwake, Nao wanyonyeshao atawaongoza polepole

Isaya 63:16
Maana wewe ndiwe Baba yetu, ijapokuwa Ibrahimu hatujui, wala Israeli hatukiri; wewe, Bwana, ndiwe Baba yetu, mkombozi wetu tangu milele ndilo jina lako.

Isaya 64: 8
Lakini sasa, Ee Bwana, wewe u baba yetu; sisi tu udongo, nawe u mfinyanzi wetu; sisi sote tu kazi ya mikono yako.

Zaburi 68: 5, 6
5 Baba wa yatima na mwamuzi wa wajane, Mungu katika kao lake takatifu. 6 Mungu huwakalisha wapweke nyumbani; Huwatoa wafungwa wakae hali ya kufanikiwa; Bali wakaidi hukaa katika nchi kavu.

Zaburi 103:13
Kama vile baba awahurumiavyo watoto wake, Ndivyo Bwana anavyowahurumia wamchao.

Mithali 3:12 (Anatuadhibu)
Kwa kuwa Bwana ampendaye humrudi, Kama vile baba mwanawe ampendezaye.

{6d} Mfalme wa amani (9:6f)

Serikali ya Immanuel itakuwa na amani milele, itatetea amani, itarejesha amani kwa watu wake, itarejesha amani kati ya watu Wake na Mungu wao (cf. Msamaha na upatanisho)

Soma aya zifuatazo – (Isaya 2: 4; Isaya 11: 6-9; Mika 4: 3)

Warumi 5:10
Kwa maana ikiwa tulipokuwa adui tulipatanishwa na Mungu kwa mauti ya Mwana wake; zaidi sana baada ya kupatanishwa tutaokolewa katika uzima wake.

Kutakuwa na amani tele Masihi atakaporejesha ufalme Wake, amani itatawala. Hakutakuwa na dhambi wala chembechembe za dhambi, wala mauaji, wala manyanyaso. Zingatia ahadi hii njema katika Isaya 11.

Isaya 11:6-9
6 Mbwa-mwitu atakaa pamoja na mwana-kondoo, na chui atalala pamoja na mwana-mbuzi; ndama na mwana-simba na kinono watakuwa pamoja, na mtoto mdogo atawaongoza. 7 Ng’ombe na dubu watalisha pamoja; watoto wao watalala pamoja; na simba atakula majani kama ng’ombe.

8 Na mtoto anyonyaye atacheza penye tundu la nyoka, na mtoto aliyeachishwa atatia mkono wake katika pango la fira.

9 Hawatadhuru wala hawataharibu katika mlima wangu wote mtakatifu; maana dunia itajawa na kumjua Bwana, kama vile maji yanavyoifunika bahari.

Cha muhumu sana kukumbuka ni kwamba amani hii inapatikana tu, kwa sababu ya kafara ya Yesu Kristo, pale msalabani. Ahadi ya utawala na maisha ya “amani” katika “mlima mtakatifu wa Mungu” (Mbingu na Nchi mpya), unapatikana tu kwa kupitia Kristo Yesu. (cf. Isaya 53:5)

Isaya 53:5.
Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.
UTUKUFU WA UTAWALA WA MFALME AJAYE

Isaya 9:7
Maongeo ya enzi yake na amani Hayatakuwa na mwisho kamwe, Katika kiti cha enzi cha Daudi na ufalme wake; Kuuthibitisha na kuutegemeza Kwa hukumu na kwa haki, Tangu sasa na hata milele. Wivu wa Bwana wa majeshi ndio utakaotenda hayo.

(1) Ufalme Wake utapanuka (9:7a)
(2) Ufalme wa Daudi (9:7b)
(3) Ufalme bora zaidi (9: 7c)
(4) Taarifa ya nyongeza (9:7d)
SAUTI YA INJILI

Yeremia 23:5, 6

5 Tazama siku zinakuja, asema Bwana, nitakapomchipushia Daudi Chipukizi la Haki; naye atamiliki Mfalme, atatenda kwa hekima, Naye atafanya hukumu na haki katika nchi. 6 Katika siku zake Yuda ataokolewa, na Israeli atakaa salama, na Jina Lake atakaloitwa ni hili, BWANA NI HAKI YETU.
Bwana akubariki sana unapoendelea kutafakari sehemu ya kwanza ya Isaya sura ya 9.

MWISHO.

Sauti Ya Injili SDA © 2017