Mithali 28

1 Waovu hukimbia wasipofuatiwa na mtu; Bali wenye haki ni wajasiri kama simba.

2 Kwa sababu ya maasi ya nchi wakuu wake huwa wengi; Bali kwa wenye ufahamu na maarifa hali ya nchi hudumishwa

3 Mtu mhitaji awaoneaye maskini, Ni kama mvua ya dhoruba isiyosaza chakula.

4 Wao waiachao sheria huwasifu waovu; Bali wao waishikao hushindana nao.

5 Watu wabaya hawaelewi na hukumu; Bali wamtafutao Bwana huelewa na yote.

6 Afadhali maskini aendaye katika unyofu wake, Kuliko mpotofu wa njia angawa ni tajiri.

7 Yeye aishikaye sheria ni mwana mwenye hekima; Bali aliye rafiki wa walafi humwaibisha babaye.

8 Yeye azidishaye mali yake kwa riba na faida, Humkusanyia mtu awahurumiaye maskini.

9 Yeye aligeuzaye sikio lake asiisikie sheria, Hata sala yake ni chukizo.

10 Kila mtu awapotezaye wenye haki katika njia mbaya, Ataanguka katika rima lake mwenyewe; Bali wakamilifu watarithi mema.

11 Mtu tajiri ana hekima machoni pake mwenyewe; Bali maskini mwenye ufahamu humchunguza sana.

12 Wenye haki washindapo, uko utukufu mwingi; Bali waovu waondokapo, watu hujificha.

13 Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema.

14 Mwanadamu mwenye kicho yu heri sikuzote; Bali mshupavu wa moyo ataangukia madhara.

15 Kama simba angurumaye, na dubu mwenye njaa; Ndivyo alivyo mtu mbaya awatawalaye maskini.

16 Mkuu aliyepungukiwa na akili huwaonea watu sana; Bali achukiaye kutamani ataongeza siku zake.

17 Aliyelemewa na damu ya mtu Atalikimbilia shimo; wala mtu asimzuie.

18 Aendaye kwa unyofu ataokolewa; Bali mkaidi wa njia zake ataanguka mara.

19 Alimaye shamba lake atakuwa na chakula tele; Bali afuataye mambo ya upuzi atapata umaskini wa kumtosha.

20 Mtu mwaminifu atakuwa na baraka tele; Lakini afanyaye haraka kuwa tajiri hakosi ataadhibiwa.

21 Kupendelea watu si kwema; Wala mtu kuasi kwa ajili ya kipande cha mkate.

22 Mwenye husuda afanya haraka kuwa tajiri; Wala haufikiri uhitaji utakaomjilia.

23 Amkemeaye mwenzake hatimaye atapata kibali; Zaidi ya mtu ajipendekezaye kwa ulimi wake.

24 Aibaye mali ya babaye au mamaye, na kusema, Si kosa; Mwana huyo ni rafiki wa mtu mharibifu.

25 Mwenye nafsi ya kutamani huchochea fitina; Bali amtumainiye Bwana atawandishwa.

26 Mwenye kujitumainia moyo wake ni mjinga; Bali yeye aendaye kwa busara ataokolewa.

27 Mwenye kuwagawia maskini hatahitaji kitu; Bali afichaye macho yake atakuwa na laana nyingi.

28 Wasio haki wainukapo, wanadamu hujificha; Bali waangamiapo, wenye haki huongezeka.